Aziz Ali wa Gerezani na Mtoni Dar es Salaam

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,857
30,205

Wednesday, 4 January 2017

Aziz Ali
Kleist Sykes alikuwa na duka la vyakula Kipata Street sasa mtaa huo umepewa jina lake unaitwa Mtaa wa Kleist. Hizi zilikuwa juhudi za Kitwana Selemani Kondo alipokuwa Meya wa Dar es Salaam kuwaadhimisha watu maarufu wa waliopata kuishi Dar es Salaam na wakaitumikia jamii. Nilipata kumsikia Mzee Kondo akisema, ‘’Hivi vipi litawekwa jina la mtu ambae hana nasaba yoyote na mji wa Dar es Salaam katika mji huu na kuwaacha wenye mji wao?’’ Hakika jambo hilo halikughalis. Mzee Kondo aliendelea na kusema, ‘’Hivi jina la Matola kwa nini lisiwekwe Dodoma lije liwekwe Dar es Salaam na wakati huo huo wakawasahau wazee wetu wa Dar es Salaam?

Turejee kwa Kleist Sykes. Hili duka lilikuwa nyumbani kwake na hapo ndipo ilipokuwa barza ya wazee maarufu wa mjini kukutana jioni inapoingia alasiri kuzungumza. Miaka ile Dar es Salaam kulikuwa na wauza kahawa wanapita mitaani na kahawa zao ndani ya madeli ya shaba yanayong’aa kwa kupigwa braso wakiuza kahawa na wao wenyewe wamevaa nadhifu, kikoi na kizubau na kofia kichwani. Basi baraza ile kila muuza kahawa akipita ataitwa na kuagizwa apige duru kwa wanabarza. Ikawa pale ile barza waungwana wale wanakunywa vikombe na vikombe vya kahawa hadi wanapoagana Maghrib inapoingia.

Mmoja wa wanabarza wa barza hii alikuwa babu yangu Salum Abdallah ambae nyumba aliyokuwa anaishi ilikuwa inatazamana na nyumba ya Kleist. Hawa walikuwa si majirani tu bali hata kazi wanafanya pamoja Tanganyika Railways. Hii ilikuwa miaka ya mwanzo ya 1920.

Kleist akiwa Karani wa Mahesabu na babu yangu Mfua Vyuma kwenye karakana ya Railway iliyokuwa Arab Street sasa Mtaa wa Nkrumah. Mle ndani kulikuwa na king’ora kikipigwa saa moja kamili asubuhi barabara na saa saba mchana. King’ora hiki cha Railway kiliwasaidia sana wakazi wa Kariakoo na Ilala kujua majira.

Mtu mwingine maarufu katika ile barza alikuwa Aziz Ali, Mdigo kutoka Moa Tanga. Huyu Aziz Ali alikuwa mwamba katika miamba ya Dar es Salaam. Alikuwa tajiri ‘’contractor,’’ wa kujenga, majumba, Mwafrika wa kwanza kununua gari na kujenga nyumba ya vigae na vioo Mtoni. Nyumba hii hadi leo ipo na sehemu hiyo katika Kilwa Road inaitwa Mtoni kwa Aziz Ali. Lakini katika sifa hizi sifa yake kubwa sana Aziz Ali ilikuwa ujenzi wa misikiti na kuihudumia misikiti. Hii ilikuwa miaka ya 1930 na hapakuwa na umeme Kariakoo. Misikiti ilikuwa ikitumia karabai kuonea.

Aziz Ali yeye alinunua karabai kwa kila msikiti na ikifika Maghrib mwanae Hamza alikuwa akizitia mafuta na kuziwasha kisha akizipeleka kila msikiti tayari kwa sala ya Maghrib. Inapomalizika sala ya Isha alikuwa anapita tena katika ile misikiti kukusanya karabai zake na kurudi nazo nyumbani kwao Mtaa wa Mbaruku na Kongo. Hii ndiyo ilikuwa kazi yake kila siku. Aziz Ali alipokufa mwaka wa 1951 miaka miwili baada ya kifo cha rafiki yake Kleist gazeti la Tanganyika Standard liliandika kifo chake kwa maneno haya:

‘’Aziz Ali the Builder of Mosques is Dead,’’ yaani, ‘’Aziz Ali Mjenzi wa Misikiti Amekufa.’’ Iko siku nilimtembela Rose Aziz mjukuu wa Aziz Ali, mtoto wa Hamza Aziz. Rose akanionyesha picha katika ukumbi wake ya mtu amevaa tarabushi akanambia, ‘’Mohamed unamuona mume wangu?’’ Nikiwa katika hali ya kushangaa huku nikiikodolea macho ile picha Rose akaendelea, ‘’Huyu babu yangu Aziz Ali.’’

Aziz Ali alikuwa na nyumba nyingi sana Dar es Salaam na ndiyo zilikuwa moja ya utajiri wake. Katika nyumba hizi nyumba ambayo imaecha historia ya pekee ni hii nyumba ya Mtaa wa Mbaruku na Congo kwa sababu nyumba hii ilikuwa moja ya sehemu ambazo harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika zilianza. Nyumba nyingine ilikuwa Mtaa wa Kipata kwa Ally Sykes, hapo zamani lilipokuwa duka la baba yake na barza ya wazee. Nyumba nyingine ilikuwa Stanley Street kwa Abdul Sykes.

Nyumba hii ilikuwa pia ya Kleist na kulikuwa na duka la vifaa vya ujenzi katika uhai wake. Hii ilikuwa mwanzoni mwa mwaka wa 1950. Mambo yalipamba moto sana kuanzia mwaka huo pale vijana wazalendo walipoanza kufanya mipango ya kuunda chama cha siasa halisi kupambana na ukoloni wa Muingereza.

Hizi ndizo zikawa nyumba ambazo Nyerere alikuwa akifika kuanzia mwaka wa 1952 kila anapokuja mjini kutokea Pugu alipokuwa akifundisha. Mama Ali mke wa Aziz Ali bado yu hai, Bi Mkubwa huyu ana mengi katika historia ya nyumba ile ya Mbaruku alipokuwa akiishi na mumewe katika miaka ile ya 1940 na akaendelea kuishi hapo na wanawe baada ya kifo cha mumewe. Hivi sasa Mama Ali anaishi Ilala na ni mtu mzima sana.

Angalia picha:Mohamed Said: AZIZ ALI WA GEREZANI NA MTONI DAR ES SALAAM
 
Kwa hiyo Kleist Sykes ni jina la asili ya Kizulu?

Kuna mchanganyiko wa uzungu humo ndani.
Nadhani huyu alikuwa ana majina yake ya kizulu
Ila Kleist sykes naona moja ni la ki german moja la ki ingereza kabsa

Maana alikuwa anaitwa Keist Sykes Mbuane (kama sikosei pia) nahisi hilo Mbuane ndio limekaa ki Africa

Nadhan mzee Mohamed Said atakuja ku clarify
 
Iceman,
Jina lake alilopewa ni Abdallah lakini kwa kuwa hawa watoto walikuwa ni
watoto wa askari katika jeshi la Wajerumani Tanganyika usajili wao ulikuwa
chini ya Wajerumani na hao ndiyo walitoa jina la Kleist.

Hili ni jina la Kijerumani.
Jina la baba yake lilikuwa Sykes Mbuwane.

Vipi alipata jina la Sykes hakuna ajuaye.

Kleist alikuwa na ndugu yake katika ukoo akiitwa Abdillah lakini Wajerumani
walimpa jina la Schneider.

Humo humo katika uko wao alikuwapo Mashado lakini jina lake ni Ramadhani.
Alikuwapo pia Thomas Saudtz.

Wazulu kutoka Mozambique kijiji cha Kwa Likunyi Imhambane ambao Herman von
Wissman
aliwatia baba zao katika manowari kutoka Laurenco Marquis akajanao
hadi Pangani miaka ya mwisho ya 1800 kuja kupigana na Abushiri bin Salim Al
Harith
na Chief Mkwawa ambae jina lake ni Abdallah.

Watoto wa hawa Wazulu akina Kleist na Schneider wakaja kutiwa katika jeshi la
Wajerumani kupigana na Waingereza chini ya Von Lettow Vorbeck katika Vita ya
Kwanza ya Dunia 1914 - 1918.

Hawa Wazulu baada ya Vita ya Pili 1938 - 1945 kumalizika na Ujerumani kushindwa
wao wakawa mstari wa mbele katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Katika harakati hizi mpya wakaungana na watoto wao kizazi cha pili kuzaliwa Tanganyika
kupambana na ukoloni wa Waingereza.
 
Ahsante nimekuelewa sana hapo Mohamed Said.

Nataka turudi kwa Azizi Ali, je yeye ana uhusiano gani na kupigania uhuru wa Tanganyika!!?
Je aliwahi kujihusisha pia na uongozi wowote wa kisiasa!!?
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom