Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,913
- 30,254
- Thread starter
- #201
Kadoda,shikamoo mzee Mohamed Said.
wakati unaendelea kutuelimisha kuhusu historia isiyo na shaka ya aziz ally, abdulwahid sykes na wazee wengine mashuhuri wa dar es salaam wa wakati huo walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika harakati za kudai uhuru,naomba kufahamu ushiriki wa waswahili waliokuwa na asili ya kinubi toka sudani.
inasimuliwa kwamba wengi wa hawa askari shupavu wa kinubi,waliletwa tanganyika ama na muingereza au mjerumani kusaidia ktk harakati zao za kusambaza ukoloni.
pia inasimuliwa,baada ya miaka mingi kupita wakiwa ktk ardhi ya tanganyika,hawa wanubi walioa wanawake wa kiswahili na kuzaa nao watoto,pia walishiriki kikamilifu ktk vuguvugu la kudai Uhuru.
wengi wao walikuwa na makazi kariakoo na mji wa kilwa.
kama hutojali,naomba kufahamu majina yao na mchango wao ktk kudai Uhuru.
nimewahi simuliwa kuwa,wakati nyerere alipokuwa anatafuta uungwaji mkono miongoni mwa watanganyika ili awaunganishe kudai uhuru,alipokuwa anaenda kilwa,alikuwa anafikia ktk nyumba ya mzee mmoja mashuhuri wa wakati huo mwenye asili ya kinubi,mzee huyo pia alikuwa na makazi ya kudumu kariakoo.naomba kufahamu jina lake na ushiriki wake ktk kudai uhuru.
natanguliza shukrani.
Wanubi walikuja Tanganyika kwa kuletwa na Wajerumani kama askari.
Ibrahim Hamisi mmoja wa waasisi wa African Association baba yake
aliingia Tanganyika kama askari wa Wajerumani akitokea Daffur.
Wakati wa utoto wangu kulikuwa na Wanubi wengi Gerezani na naikumbuka
famili ya Mzee Johari waliokuwa wakikaa Kirk Street sasa Mtaa wa Lindi.
Hawa wakiishi jirani na nyumba ya Bi. Mluguru biti Mussa mama yake Abdul
Sykes.
Kulikuwa na Mwalimu Sakina Arab akiishi Mtaa wa Pemba huyu bi. mkubwa
alikuwa Mnubi na allikuwa na kaka yake akiitwa Mustafa.
Mwalimu Sakina alikuwa ni dada wa kuPpnga wa Abdul Sykes na ni mmoja
wa akina mama wa mwanzo kuiunga mkono TANU.
Yeye alikuwa mwalimu Al Jamiatul Islamiyya Muslim School.
Kulikuwa na koo nyingi za Kinubi Chang'ombe, Dar es Salaam na Dodoma.
Katika kitabu cha Abdul Sykes kuna kisa hiki cha Ahmed Adam Mnubi
aliyeishi Mikindani:
''Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili
Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi.
Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo
uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere.
Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo,
aliyemiliki nyumba moja ya fahari.
Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa.
Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake.
Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka yake
Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza.
Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani.
Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa mwa karne ya kumi na tisa na
Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani
wakati wa vita vya Maji Maji.
Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa
kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo.
Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi
ya Waingereza.
Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza waliitikadi
nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi
itaifishwe.
Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika
na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.
Utawala wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo
wakati ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya
kifungu cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika
katika majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.
Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka alipofariki
na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam.
Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake.
Nyumba hiyo ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani.
Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, usiku Nyerere aliitisha mkutano na wanachama kama
thelathini hivi walihudhuria.
Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya UNO na hali ya siasa kwa
ujumla mjini Dar es Salaam.
Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa
sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.