Mara ya kwanza wakati Donald Trump alipogombea urais wa Marekani dhidi ya Hilary Clinton, wanadiplomasia wengi na wataalam wengi wa mambo ya uchumi, waliweka karata yao kwa Hilary Clinton, wakiamini kuwa Hilary alikuwa na uelewa wa kina kuhusu Afrika, na kama Trump angeshinda basi Afrika ingewekwa pembezoni. Hali halisi ya ilichotokea baadaye, ilikuwa sawa na hofu waliyokuwa nayo. Lakini sasa swali lililopo ni kuwa Trump wa sasa atakuwa na mtazamo ule ule kwa Afrika?
Ushindi wa Donald Trump safari haukuwa kitu cha kushangaza sana, na pia hautakuwa kitu kipya duniani. Lakini kinachosubiriwa ni kuona kama kuna chochote huyu Bwana alijifunza katika awamu yake iliyotangulia. Ni wazi kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika wakati wa Trump uliimarika zaidi, na hata tafiti zilizofanywa wakati ule zilionesha kuwa, China kuzitendea nchi za Afrika kwa heshima na usawa, kumefanya nguvu ya ushwawishi ya China barani iendelee kuimarika.
Mwezi Oktoba 2016, taasisi huru ya uchunguzi wa maoni ya raia barani Afrika, ulionesha kuwa, kati ya watu 54,000 kutoka nchi 36 za Afrika waliotoa maoni kuhusu sura ya China barani Afrika, wengi waliona kuwa China imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi zao kupitia shughuli zake za kiuchumi na kisiasa barani Afrika. Wengi walitoa tathmini chanya ya uwekezaji wa China kwenye miundombinu, shughuli zake za biashara na bidhaa zinazotengenezwa China.
Cha ajabu ni kuwa kwenye utafiti huo, Marekani ilikuwa ya kwanza lakini kilichoifanya Marekani kuwa ya kwanza ni nguvu yake ya ushawishi kwenye utamaduni, na sio kwenye maisha ya mtu moja mmoja kama China. Hali hii ilifanya serikali ya Joe Biden, kutafakari na kujaribu kuchukua hatua, na kutuma viongozi wake wengi waandamizi kufanya ziara barani Afrika kutangaza kurudi tena kwa Marekani barani Afrika, na hatimaye Joe Biden mwenyewe kufanya ziara mwishoni mwa urais wake.
Ni wazi kuwa kivitendo kulikuwa na mabadiliko kidogo sana kwenye mtazamo wa Marekani kwa Afrika katika kipindi cha Joe Biden. Inawezekana kuwa lugha yake ilikuwa ya heshima zaidi, lakini sera na mipango aliyotangaza ya kurudi Afrika haijaonesha matokeo makubwa. China kwa upande mwingine, imeendelea kuonesha ushirikiano wa kivitendo, kupitia mpango wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na Baraza la Urafiki kati ya China na Afrika. Kwa hiyo ambacho Marekani imekuwa inakisema mara kwa mara, kuwa nguvu ya ushawishi ya China inazidi kuongeza barani Afrika na hata sehemu nyingine duniani, bado kipo.
Kinachofahamika ni kuwa kwa Trump urais ni sawa na ukuu wa kampuni, anachofikiria zaidi ni faida kwa Marekani. Kwa mtazamo kama huu, ni wazi kabisa kuwa msaada wa Marekani kwa nchi za Afrika unaweza kupungua sana au kufutwa kabisa, kwani atazingatia tu kanuni za soko.
Mwaka 2025 kutakuwa na marekebisho kwenye makubaliano ya ushirikiano wa uchumi kati ya Marekani na Afrika (AGOA) na Shirika la Fedha za maendeleo la Marekani (DFC), na mwaka wa 2026 kutakuwa na mabadiliko kwenye Benki ya Exim ya Marekani, bila shaka mabadiliko hayo yataoneshwa mwelekeo ambao Bwana Trump anataka kufuata katika mkakati wake wa kibiashara kwa Afrika. Lakini tukumbuke pia uwekezaji mkubwa wa serikali ya Marekani wa karibu zaidi barani Afrika, ni ule wa reli ya Ukanda wa Lobito, haijulikani kama Trump ataufuta au la.
Jambo la uhakika ni kuwa, bila kujali Trump atakuja na sera gani, ziwe ni sera rafiki au zisizo rafiki kwa Afrika, ushirikiano kati ya China na Afrika utaendelea kuwa imara. Kama Trump ataleta fursa zozote kwa Afrika bila shaka itakuwa habari njema kwa wote wanaoitakia mema Afrika, lakini hata kama atafanya alivyofanya safari iliyopita na kuiweka Afrika pembeni, bila shaka kwa ushirikiano na marafiki wengine Afrika itaendelea kusonga mbele.