Attention Bodi Ya Mikopo Ya Elimu Ya Juu Kwa Wanafuzi(HESLB)

Naona serikali wameshamjibu tena mkjj kuhusu ile article yake kuhusu ndege inayopaa. Wamelipia kurasa kadhaa katika magazeti. Naona wameamua ku-invest kwenye kujisafisha kwa kila criticism wanayopewa. Problem ni kuwa hawana kabisa vichwa vilivyotulia; kila statement wakitoa inapwaya mno inakuwa kama imeandikwa na mwanafunzi mwerevu wa drs la saba!

Kitila... wamejibu wapi? nina hamu nao kweli.. hata bibi amechukizwa ati hata mapumzikoni niko busy? hii bongo itavunja ndoa za watu.
 
Tangazo la serikali liko katika gazeti la Uhuru page 21, likiwa limelipiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa na kichwa kisemacho, "Ni kweli Tanzania inapaa kufikia malengo"

Nimeahidiwa kupata makala nzima na nikiipata nitaituma humu haraka iwezekanavyo. Ni matumaini kuwa kama wahusika watakua ofisini muda huu nitaituma leo ama la hadi kesho... Ama kama kuna mtu mwenye nalo atuwekee humu. tujadili
 
Wamechapisha tena tangazo lao katika KULIKONI ya leo.
SOMA PM yako kwa maelezo ya ziada
 
tunaomba utuweke hiyo original article ya mwanakijiji

na pia, majibu ya serikali hapa please mr .. halisi
 
Makala ya Mwanakijiji hii hapa:

Ndege ya Lowassa inayopaa, na abiria walioachwa wameduwaa!

Na M. M. Mwanakijiji

MWALIMU Nyerere katika mojawapo ya maandishi yake ambayo kama leo yangesomwa tena yangewazibua masikio na kuwafumbua macho watawala wetu, alisema hivi kuhusu asili na kiini cha dhana nzima ya maendeleo:

“Ukweli ni kwamba, maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Barabara, majengo, kuongeza uzalishaji wa mazao, na vitu vingine kama hivi siyo maendeleo; hivi vyote ni vyombo tu vya maendeleo… Ongezeko la madarasa katika shule fulani ni maendeleo pale tu majengo hayo yanaweza, na yanatumika kuendeleza uelewa na maarifa ya watu.

“Kuongeza uzalishaji wa ngano, mahindi, au maharage vinakuwa ni maendeleo pale tu vyakula hivi vinawapatia watu chakula bora.

“Vivyo hivyo kuongeza uzalishaji wa pamba, kahawa, au mkonge vitakuwa ni maendeleo pale tu mazao hayo yanapoweza kuuzwa na fedha zinazopatikana kutumika kujipatia vitu vingine ambavyo vitainua maisha ya watu katika afya, maisha mazuri, na kuelewa.
“Maendeleo ambayo si maendeleo ya watu, yanaweza kuwa ni somo kwa wanahistoria wa mwaka 3000.”

Katika maneno hayo ya Mwalimu, kumejaa somo ambalo baadhi ya wanasiasa na viongozi wetu wa leo naona wamelikwepa au limekuwa somo gumu kwao kulifuzu. Miongoni mwa viongozi hao si mwingine bali ni yule kiongozi hodari, shujaa na mahiri, aliyetamba bungeni.

Kwa mara nyingine tena akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake katika kikao cha bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliwatangazia wabunge kwa kutamba, tena na kwa kujidai akionyesha kuwa alikuwa na uhakika wa kile alichokisema.

Akitupilia mbali madai mbalimbali ya vyama vya upinzani kuhusu utekelezaji wa sera za CCM, kiongozi huyo alitamba akitumia mfano wa Rais Mkapa kuielezea Tanzania.
Namnukuu: “Ndege ile (isomeke Tanzania ile) ya Mkapa ilikuwa ni ndege kwenye runway, (hii ya) sasa tumeanza kupaa.

“We are on track, we are on time. Tuko timamu, na tuko na wakati… Ndege imeanza kupaa!”

Maneno yake hayo yalisindikizwa na mrindimo wa makofi kutoka kwa wabunge wa chama chake ambao alitumia muda huo kuwaasa kuisimamia ilani ya uchaguzi ya CCM.
Ni hili suala la kuifananisha Tanzania na ndege, tena ndege iliyoanza kupaa ndio jambo ambalo limenigusa na kunifanya nijiulize hivi Lowassa na viongozi wenzake wa CCM wanaishi katika ulimwengu upi au Tanzania ipi?

Na hii ndege ambayo wenzetu wanaishangilia kuwa imeanza kupaa, inaruka uwanja gani? Imenichukua karibu wiki mbili tangu Waziri Mkuu ayatamke maneno hayo bungeni kwa mbwembwe zote za mwanasiasa huku kidole chake kikipepewa angani kama onyo kwa mimi kuweza kupata jibu.

Nimegundua kuwa ndege ya Lowassa ambayo mwenzetu ameanza kuiona imeanza kupaa, ni ndege ya nchi ya kufikirika, ambako abiria wake ni yeye anawajua, kwani kwa hakika ndege ya Watanzania wengi, hata kutoka kwenye hanga haijatoka!

Niwape wazo kidogo kuhusu ndege kupaa. Miaka ya mwanzoni mwa themanini nikiishi karibu na Kipawa (maeneo ya Karakata), jijini Dar es Salaam, kabla ya ile bomoabomoa, mimi na wenzangu wachache tulikuwa tunapenda kwenda pale uwanja wa ndege siku za Jumamosi kuona ndege zinavyotua na kupaa.

Kitu kimoja ambacho kilikuwa kwenye mawazo yangu wakati wote huo, ilikuwa ni hisia ya kutobahatika kupanda “pipa” hilo kwenda kokote lilikokwenda.

Nilipokuwa nikiona ndege za Sabena zikitua au KLM na British Airways, wazo la kutamani kuwemo kwenye mojawapo ya misafara hiyo lilikuwa likinijia kila kukicha.
Ilipofika wakati wangu wa kupanda ndege kwa mara ya kwanza, hisia ya hofu na hamasa ilikuwa imechanganyika.

Kitendo cha kuwa angani, nikiwa nimejifunga mkanda kwenye kiti changu, kilikuwa ni kitendo cha kijasiri.

Tulivyokuwa tukipasua anga na uharaka wa safari yenyewe, ilinihakikishia kuwa hakuna usafiri salama na wa haraka kama wa ndege.

Nina uhakika bado kuna watu wetu wengi tu ambao hawajapata nafasi ya kusafiri kwa ndege na hivyo wao kama mimi miaka ile, wamebakia kuangalia angani kila ndege ipitapo na kubakia wakiitamania siku ile na wao wataruka na “mchuma” huo.

Hivyo, Waziri Mkuu anapoiona Tanzania kuwa ni ndege iliyoanza kupaa bila ya shaka ana kila sababu na ushahidi wa kuiona hivyo.

Kwa maoni yangu, hata hivyo Tanzania inayopaa ambayo Waziri Mkuu na wabunge wa CCM walikuwa wanaishangilia ni Tanzania ya watu wachache ambao wamebahatika kupanda ndege hiyo na wanafurahia viti vyao vya daraja la kwanza ambako hakuna bughdha zozote.

Watu hawa ni kina nani hasa ambao wanafurahia ndege iliyopaa huku lile daraja la tatu likiwa tupu na abiria wote wakiwa bado wameachwa Kipawa wakiwa wameduwaa?
Ni kina nani hawa wanaotaka tuamini kuwa nchi yetu si tu imeanza kutambaa na kujiandaa kukimbia, kuwa ati leo hii imeanza kupaa?

Sasa sitaki kueleweka kuwa napinga hakuna mafanikio yoyote ambayo nchi yetu imeyapata mpaka hivi sasa, najua ni mengi na watetezi wake wapo na mifano ipo.
Hata hivyo nimekereka kabisa na mfano wa Waziri Mkuu kuwa Tanzania yetu imeanza kupaa! Mwalimu alisema wazi kuwa “itabidi tukimbie wakati wenzetu wanatembea”.
Ninachosema ni kuwa Tanzania ya Lowassa ina watu wachache ambao kwa hakika hawajui adha ya maisha ya kawaida ya Watanzania, kwani Tanzania yao imezunguka maeneo ya miji yetu mikubwa, lakini hawana wazo hata chembe la maisha ya watu wa vijijini kwetu (zaidi ya kutuonyesha kuwa hata huko kuna simu za mkononi!)
Lakini hawa wanaonufaika na Tanzania hii na ambao wanafurahia kuona Tanzania imeanza kupaa (licha ya ushahidi wote kuwa hata kwenye runway hatujafika) ni kina nani?

Viongozi wa juu wa CCM. Hawa ni watu ambao kwao Tanzania imeanza kupaa.
Viongozi hawa bila ya shaka ndio wa kwanza kuifurahia nchi inayopaa kwani hawana matatizo yoyote na mambo mengine.

Hawako tayari kuona mabadiliko ya kweli ya kisheria yanafanyika ili kupigana na rushwa na ufisadi, wako na haraka ya kwenda kuzoa wanachama wa vyama vingine ili kuwakaribisha airport, hata kama hawatapata nafasi ya kuingia kwenye ndege hiyo, na kila kukicha wanawaza ni jinsi gani wataitumia serikali wanayoiongoza kukinufaisha chama.

Kwa hawa, Tanzania inayopaa haitengani hata chembe na manufaa kwa CCM.
Kwa kadiri ndege ya Tanzania inavyopaa ndivyo chama nacho kinavyozidi kupaa katika anga za siasa za Tanzania.

Watendaji wa serikali wakubwa. Hawa bila ya shaka wanafaidika na CCM inayofurahia kupaa kwa Tanzania.

Watendaji hawa hawana wasiwasi wa kuboronga kwani kwa kadiri ya kwamba wanawanufaisha wakubwa wa chama, basi Tanzania yao nayo inapaa.

Hivi karibuni kuna tuhuma kubwa za ufisadi huko Benki Kuu (BoT), watendaji wetu badala ya kutafuta ukweli na undani wa tuhuma hizo na hasa kwa vile zinamhusisha mtendaji mkuu wa benki hiyo, wanaanza kutafuta ni nani alizitoa tuhuma hizo.
Kwa hawa watendaji, tuhuma zinapotolewa kuwa serikali imewatelekeza wanafunzi Ukraine, badala ya kutafuta ukweli wanawauliza wanaotuhumiwa ukweli wa tuhuma dhidi yao!

Kwa vile serikali ya Lowassa haina nia na mazoea ya kushughulikia ufisadi mkubwa, basi watendaji wa serikali wanajua wameshakata tiketi katika ndege hii ya Lowassa.
Kwa hakika kwa watu hawa ndege yao imepaa, wakati abiria wengi wamepigwa na butwaa!

Wafadhili na wafanyabiashara wakubwa wenye ushabiki wa CCM. Hakuna watu ambao kwa hakika Tanzania yao inapaa kama wale wafanyabiashara ambao biashara zao zimepewa baraka zote za kichama na hivyo hawakumbani na matatizo ya kila siku ya kiutendaji.

Wale Watanzania wachache ambao hawakutaka kukata tiketi za ndege hii ya Lowassa, wamejikuta wakinyanyasika kila kukicha na mambo yao yakiwaendea kombo hadi pale waliporudi “kundini”.

Mfano mzuri ni mfanyabiashara mmoja wa Nyanda za Juu Kusini ambaye alikuwa upinzani na alikuwa amejenga karibu na kituo cha FFU.

Bwana huyu alianza kupatiwa barua za kutakiwa kuhamisha makazi yake kwani eneo alilojenga lilikuwa ni mali ya serikali (Polisi).

Jamaa alipoelewa kuwa ilikuwa ni usumbufu wa kisiasa, aliamua kurudi chamani na kelele zote hizo zikayeyuka kama ukungu alfajiri.

Wapo watu wengi ambao wamegundua kuwa kufanikiwa kweli kibiashara ni lazima uabudu katika altare ya CCM, huku ukiimba mapambio ya nyimbo za sifa za chama huku kasida za kushangilia sera na ilani za CCM zikisika. Vinginevyo ndege yako wewe itaendelea kukaa kama jumba la maonyesho!

Ndege imepaa kwa wawekezaji wa nje. Hawa kwa namna fulani wamegundua kuwa katika Tanzania ya sasa wanaweza kwa haraka kutengeneza mamilioni ya dola kwa haraka labda kuliko sehemu nyingi kweli duniani.

Kwa hawa wamegundua kuwa ndege ya Tanzania inapaa kama helikopta haihitaji kukimbia kwenye runway! Walianza Loliondo, ikaja IPTL, DAWASA, ATC, KIA, TANESCO, Richmond, rada, ndege ya rais, na mikataba ya madini.

Kwa wawekezaji hawa, Lowassa anaposema Tanzania “imeanza kupaa”, ni lazima washangilie kwani wao wako kwenye daraja la kwanza!

Ninaweza kuendelea kuorodhesha ni makundi gani ya watu ambao wanaiona Tanzania imeanza kupaa, hata hivyo kila mtu anajua kabisa kuwa Tanzania inayopaa si ya Watanzania wote.

Ni Tanzania ya watu wachache ambao wamefungamana na chama tawala au na serikali ambao kwa hakika hawana wasiwasi wa wapi watakula au biashara zao zitakwenda vipi.
Ni Tanzania ya watu hawa ambao hawana wasiwasi kama watoto wa wakesha hoi wanalala nje ya ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine au wanaishi kwa kushindia mikate na maji!

Ni Tanzania ya watu hawa ambao wanasifia ujenzi wa vyuo vikuu halafu kesho yake wanashangaa mbona vyuo vinachukua watu wachache!

Ni Tanzania ya watu hawa wachache inayopaa kwa kutoa mikopo ya mamilioni ya fedha kwa viongozi walio madarakani na wanaposhituliwa wanasema “hata watu wasio viongozi wanastahili mikopo hiyo!” Tanzania hiyo bila ya shaka inapaa kwao.

Hata hivyo, kwa mamilioni ya wana wa nchi yetu, Tanzania inayopaa ni ya njozini, ni ile ambayo wote tunaitamani.

Kwa hawa ambao hadi leo bado wanajenga kwa kutumia udongo na nyasi, na kuchota maji mtoni huku wakipeleka watoto wao hospitali kwenye matenga ya maembe, kwa hawa Tanzania haipai! Kwa mamilioni ya watoto wetu ambao licha ya madai kuwa kuna chakula cha kutosha, bado tuna tatizo la utapiamlo katika nchi yetu, yaani tumeshindwa hata kuwalisha watoto wetu chakula bora!

Kwa Watanzania hao, kupaa anakozungumzia Lowassa ni msemo tu wa kisiasa usio na ukweli wa mantiki, ni hadaa ya viongozi ili wapigiwe makofi!

Katika Tanzania ya leo, bado tuna watu wanaohangaika kwenda shule ya msingi na kama habari zilizoripotiwa kwenye gazeti moja zina ukweli, basi kwenye nchi hii inayopaa shule ambayo ina mwalimu mmoja na kaka mkuu ni kaimu, basi Tanzania hiyo haijapaa na haipai!

Tunatamani Tanzania inayopaa, Tanzania ambao watoto wake wote licha ya maeneo wanayotoka, uwezo wao wa kimaisha au vyama wanavyotoka wana nafasi sawa ya kufanikiwa endapo watapewa nafasi. Hiyo itakuwa ni Tanzania inayopaa.

Pale ambapo tutaweza kuhakikisha kuwa vijana wetu hawakatishiwi masomo kwenye vyuo vyetu vikuu kwa uzembe wa Bodi ya Mikopo, Tanzania hiyo itakuwa imeanza kupaa.

Pale ambapo tutachunguza ukweli wa tuhuma dhidi ya mtu yeyote na kuchukua hatua za kisheria inapobidi badala ya kutafuta nani alitoa tuhuma hizo, basi Tanzania itaanza kupaa.

Ni pale ambapo badala ya kuendelea na katiba ambayo imepitwa na wakati na tukaamua kama watu wamoja kufanya mazungumzo ya kikatiba ili tujitengenezee katiba mpya yenye kubeba matarajio na matamanio yetu, basi Tanzania itaanza kupaa.

Tanzania inaweza kupaa, lakini hivi sasa haijaanza kupaa! Tusidanganywe na tusidanganyane.

Tanzania yenye neema inawezekana, maisha ya furaha na mafanikio yanawezekana, mabadiliko ya kweli ya maisha ya watu wetu yenye unafuu na ahueni ya kimaisha yanawezekana.

Hata hivyo, hayo yote yanawezekana pale tutakapokuwa wa kweli kwa nafsi zetu na kwa wale tunaowaongoza.

Porojo za kisiasa ni nzuri wakati wa kampeni, lakini wakati wa kufanya kazi ni lazima tuwe wa kweli.

Hivyo hoja ya Waziri Mkuu kuwa Tanzania imeanza kupaa na kwenda ‘ayeya’, haina msingi, haina ukweli, na imetokana na hisia za kisiasa zaidi kuliko ukweli ardhini!
Ndege hiyo wamepanda vigogo. Sisi abiria wengine ambao ndio wengi zaidi na ambao tumeilipia ndege hiyo, tumebakia Kipawa wakati wenzetu wanapaa, sisi tumebakia tunashangaa huku tumepigwa na butwaa, mbona wametuhadaa?

Siku moja tutatafuta marubani wengine.

Niandike: mwanakijiji@journalist.com
Nisikilize: http://mwanakijiji.podomatic.com
Nitumie ujumbe: +12486862010
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/7/11/makala7.php

Majibu ya serikali yamo thread hii-

http://www.jamboforums.com/showthread.php?t=3866
 
..Mwanakijiji na wenzako kazi nzuri mnafanya maana hata hiyo ya kujibu tuu inaonekana wameshtuka,full speed mbele kwa mbele wajue tuko macho na wataanza kutimuana utasikia as a cover up!
 
..Mwanakijiji na wenzako kazi nzuri mnafanya maana hata hiyo ya kujibu tuu inaonekana wameshtuka,full speed mbele kwa mbele wajue tuko macho na wataanza kutimuana utasikia as a cover up!

Imewapiga sasa pahali pale panapouma kwa hiyop inabidi wajitetee kwa nguvu zote. hata hivyo nafurahia wanapojibu kwa vile inasaidia kuwajua udhaifu wao kiundani zaidi.
 
Majibu yangu kwa Bodi ya mikopo yanapatikana kwenye kulikoni pamoja makala nyingine ya "Tuwaachie Nchi" ambayo itajibu maswali kama wanaweza kuninyamazisha au la. Vinginevyo, ndugu msiwe na wasiwasi nimekuwa kimya kwa masaa kadhaa kwa sababu nilikuwa namalizia majibu yangu kwa ofisi ya Waziri Mkuu. Na zaidi ya yoyote bibi alitaka nikae pembeni kidogo na kupumzika kwani I've been hyped up for the past weekend.
 
Mwanakijiji,

Pole sana, najua ukishaanza kupambana kwa hoja na hawa waheshimiwa itabidi mambo yako mengi yasimame lakini ndio hivyo tena. Hata akina Mwalimu waliachia mambo mengi ili kuendeleza mapambano ya kumng'oa mkoloni.

Ninachokuomba usipandishe jazba na tulia, wajibu ukiwa umetulia. Kama unaona kwasababu moja ama nyingine temperature inapanda, acha kuandika na tulia kwanza. Hoja inayotolewa kwa jazba ni hoja iliyokufa hata kabla ya kumfikia msomaji. Angalia majibu ya ofisi ya Waziri Mkuu, yametolewa na watu ambao wamechukia na matokeo yao ni kujichanganya zaidi.
 
MAJIBU YA MWANAKIJIJI KWA BODI YA MIKOPO, YAMETOKA KATIKA GAZETI LA KULIKONI LA LEO, UKURASA WA 12,13 NA 16

UTETEZI WA BODI YA MIKOPO, MAJIBU YAO YATHIBITISHA UFISADI.

MJENGA HOJA

Kwanza kabisa sina budi kutoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo Bw. George Nyatega kwa kitendo chake cha kujaribu kutoa majibu ya makala yangu niliyoandika wiki iliyopita yenye kichwa cha habari "Twaweza kumuamini Prof. Msolla – Bodi ya mikopo kilele cha ufisadi". Jaribio lake hilo ambalo bila ya shaka liliandikwa kwa uangalifu mkubwa limenigusa moyo na kunionesha kuwa sisi kama Watanzania tunaweza kuwa na mjadala wa wazi katika kujaribu kuisogeza mbele kimaendeleo nchi yetu. Licha ya sehemu chache katika majibu yake ambapo anahoji nia na uzalendo wangu nina uhakika Bw. Nyatega na wenzake wanaelewa kuwa lengo langu siyo kuichafua bodi hiyo au majina ya watu bali kuonesha uchafu wa bodi hiyo na kutaja majina ya watu ambao wanahusika na uchafu huo. Hivyo siyo lengo langu hata kidogo kuwachafua, bali kunyoosha kidole dhidi yao na kusema wamechafuka, wasafishwe. Hata hivyo, kwa vile amehoji nia na kusudi la makala yangu na kwa kukosea amehitimisha kuwa lengo langu ni "kuchafua majina ya watu" ninapenda kutumia nafasi hii kueleza ni kwanini niliandika makala zangu mbili zilizotangulia kuhusu Prof. Msolla na baadaye kuihusu Bodi.

Kwanza kabisa lengo la makala yangu ni kuonesha kuwa kuna tatizo kwenye bodi ya mikopo, tatizo ambalo limechangia kupotea kwa mamilioni ya fedha kutokana na mfumo mbaya wa utoaji mikopo. Mifano niliyotoa (nitaelezea tena baadaye) ilikuwa na lengo la kuonesha kuwa madai ya kuwa bodi ni chafu na ina mfumo mbaya siyo madai ya mtu asiyejua nini kinaendelea bali yanatokana na uchunguzi yakanifu.

Pili, na kubwa zaidi lengo langu ambalo Bw. Nyatega hakujaribu kulikanusha ni kuwa uongozi wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu umeshindwa kabisa kuipa uongozi bodi hii licha ya wao (wizara) kukiri mapungufu mbalimbali (angalia makala yangu ya kwanza). Kinara wa ukosefu wa uongozi huo ni bosi wa Bw. Nyatega yaani Waziri Prof. Peter Msolla. Ni madai yangu kuwa matatizo mengi yanayotokea kwenye bodi leo hii na yaliyotokea hadi sasa yametokana na uzembe wa Prof. Msolla na kiburi cha kutotaka kuyakabili matatizo hayo moja kwa moja. Licha ya kwamba anayajua matatizo ya bodi Prof. Msolla na wasaidizi wake wameshindwa kabisa kutafuta mbinu ya kuyatatua. Tatu na mwisho kabisa, katika kuandika makala yangu nilitaka kuonesha kuwa ni kutokana na uchafu wa bodi na kushindwa kwa Prof. Msolla kuongoza ndio maana leo hii tuna watoto wetu waliokwama Ukraine, kwa kisingizio cha "waliondoka wenyewe". Hili "nitaliibua" tena baadaye.

Hayo ndiyo yalikuwa malengo ya makala zangu zilizotangulia na yanaendelea kuwa malengo ya makala hii ya sasa. Hata hivyo jambo moja limenisikitisha katika majibu ya Bw. Nyatega. Katika majibu yake yote ya ukurasa wa nane, Bw. Nyatega ameshindwa kuonesha uungwana wa kunishukuru kwa kumsaidia kuiangalia kwa ukaribu bodi anayoingoza na kusahihisha makosa au mapungufu niliyoyaonesha. Jinsi alivyoandika ni kana kwamba mimi nina kusudio baya na bodi au nchi yangu na ni yeye ndiye mzalendo pekee aliyebakia. Kwa vile nimewasaidia kutambua makosa na matatizo mengine angeonesha angalau uungwana wa kushukuru badala ya kudhihaki juhudi zangu kwani wakati yeye analipwa kufanya anachofanya mimi nafanya kwa kujitolea. Hata hivyo, kama hamaanishi shukrani hizo, sizihitaji lakini nitaendelea kufafanua mambo mengine bila kutarajia shukrani yoyote kwani walisema waswahili kwa usahihi kabisa kuwa "shukrani ya punda ni mateke". Nina uhakika hata hivyo kuna watu ambao wananishukuru kwa kuthubutu kusema "mfalme hajavaa nguo".

Baada ya kusema hayo, hebu tuangalie majibu ya bodi hii na kama majibu haya yanaweza kuingia akilini mwa mtu yeyote mzima na kama katika majibu yao wamejibu kwa uhakika hoja nilizojenga. Ndugu zangu, majibu ya Bw. Nyatega ni ya mtu aliyekurupushwa, yenye kujikanganya, yasiyo na ukweli na kwa hakika ni majibu yenye lengo la kuipotosha jamii na yenye kujaribu kujisafisha. Ni majibu ya mtu anayejaribu kupaka makaburi rangi za kumeremeta kumbe ndani yake ni mifupu mitupu! Kwa bahati mbaya, wamekosea mtu wa kumjibu kwani wakati wengine wanakubali majibu ya bodi kama walivyokubali majibu ya Hosea, Gesimba, na Balali, sisi wengine majibu yao ndio yanatupa maswali mengi zaidi na ya kina kwani majibu hayo siyo majibu bali ni majaribio ya kujibu maswali magumu. Ni majaribio yaliyoshindwa na nitumie nafasi hii kuonesha ni jinsi gani majibu ya Bw. Nyatega hayana mantiki na yenye kukusudia kuficha kitu.

Kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo (loan allocation & loan disbursement)
Bw. Nyatega katika jaribio lake la kujibu hoja zangu anajaribu bila mafanikio kutumia maneno ya Kiingereza kutofautisha mambo mawili lakini hata hivyo ameshindwa kuonesha uhusiano wa mambo hayo. Je mtu anaweza kutenga kitu ambacho hana? La hasha! Na je mtu anaweza kuwagawia watu kitu ambacho hajakitenga kwa ungalifu? La hasha. Katika kuelezea hili suala Bw. Nyatega amedhihiria udhaifu mkubwa wa bodi, anasema hivi kuhusu suala la kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo, "kupangiwa kupewa mkopo (Loans Allocation) hufanyika mwanzoni mwa mwaka wa masomo, baada ya Bodi kupata matokeo ya udahili kutoka vyuo vya elimu ya juu na pia kutoka kwa Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tanzania Commission for Universities - TCU). Baada ya uchambuzi wa waombaji, kulingana na vigezo, Bodi hupanga mikopo kwa kila mwombaji kwa kila Chuo na taarifa hiyo hutolewa kwa njia ya tovuti ya Bodi ili iwafikie wahusika wote." Na baada ya hapo Bw. Nyatega anasema "Bodi huendelea na uchambuzi zaidi kabla ya kufanya malipo "Disbursements".

Kwa maneno mengine ni kuwa wao wanatumia majina yaliyotumwa na vyuo na TCU kupanga mikopo hiyo na baadaye wakiishayachambua ndio wanagawa hizo fedha. Katika majibu yake hayo bila ya shaka tunakutana na mambo mawili makubwa. Wanapopatiwa majina ya waombaji na wanapokubali kuwatengea fedha kabla ya kuhakikisha waombaji ni kina nani, wamefungulia ghala la ufisadi. Hii inajibu swali la mwanafunzi mmoja aliyeomba vyuo vitatu au vinne kukubaliwa mikopo mara hizo zote. Kwa kitendo cha bodi kutenga fedha hizo kwa kila mwombaji aliyeyedailiwa bila kuhakikisha kama ni "multiple allocations) ina maana fedha hizo zipo na zinatengwa zaidi ya mara moja. Huwezi kutenga fedha au kupanga matumizi ya fedha ambazo hauna. The board does not allocate fanthom money! Hivyo wanapompangia Juma Mdoe (jina la kubuni) aliyeomba mkopo kwenye vyuo vitatu Shs milioni 3 kwenye kila chuo, basi Juma atakuwa ametengewa/amepangiwa/amekuwa "allocated" milioni tisa. Sasa kama Juma ataamua kwenda chuo kimojawapo na siyo vile vingine, basi kuna Shs. Milioni sita ambazo zitakuwa hazikutumika. Swali kubwa ni nini kinafanyika kwa fedha hizi? Ni kutokana na uchunguzi wangu ndio nimeonesha kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 500 ambao kwa mwaka uliopita wa 2006/2007 walitengewa mikopo zaidi ya mara moja.

Hili linatuleta kwenye neno la pili nalo ni "kugawa mikopo" (Loan disbursement). Kwa mujibu wa Bw. Nyatega uchambuzi hufanyika na baadaye wanafunzi wanapewa mikopo hiyo. Na kwa ujasiri mkubwa akaniambia kuwa ningetumia taarifa za waliogawiwa mikopo kuonesha kama wamepewa au la. Kwa kutumia ujanja amejaribu kulifanya jambo la "loan allocation" kuwa ni "non-issue". Jaribio lake hilo lilifanywa pia na Prof. Msolla kwenye jibu lake Bungeni mapema kwenye kikao kinachoendelea sasa Dodoma. Swali kwetu ni kuwa lipi ni jambo kubwa, loan allocation au loan disbursement? Jibu langu ni hilo la kwanza. You can not disburse money you haven't allocated! Ili waweze kugawa pesa ni lazima wawe wamezitenga. Hivyo ufisadi hauanzii kwenye kugawa bali kwenye kutenga. Kwa maneno yake yeye mwenyewe bodi imewalipia watu ambao hawako vyuoni, na waliweza kufanya hivyo baada ya kuwatengea. Ufisadi mkubwa katika bodi hauko kwenye kugawa pesa kwani ni rahisi kugawa fedha kwa mtu wanayemtaka kuliko kuangalia wamemtengea nani fedha. Hivyo tatizo ni zile pesa ambazo ziliombwa kwa mwanafunzi zaidi ya mmoja na zikatengwa lakini hazikutumiwa zilifanyiwa nini? Je, Bw. Nyatega anataka kuwahakikishia Watanzania kuwa hakuna afisa wake hata mmoja ambaye "amejipongeza" kwa mikopo ya wanafunzi? Isipokuwa kama Bw. Nyatega atasema kuwa fedha zinapotengwa haina maana kuwa zipo.

Of course, hawezi kusema hivyo kwani yeye mwenyewe anasema hivi "Bodi inakiri kwamba kutokana na mkanganyiko wa "Double Admissions" katika vyuo vikuu mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa 2006/2007 kulitokea ‘Double Loan Allocations' ambazo hata hivyo yalisahishwa kwa kiwango kikubwa wakati wa kufanya malipo (Loan Disbursements)." Na anasema "yalisahihishwa kwa kiwango kikubwa" kwa maana ya kwamba hayakuondolewa yote. Hivyo kupuuzia tatizo la "double allocation" kana kwamba siyo jambo zito ni ufunguzi wa double payment. Kwa maneno mengine, Mkurugenzi wa bodi anakubaliana na mimi kuwa kuna tatizo la ufisadi kwenye bodi anayoiongoza.

Hata hivyo Bw. Nyatega anajaribu kuelezea chanzo cha tatizo hilo (la double allocation) na anapofanya hivyo anaendelea kuthibitisha maneno yangu kuwa bodi jinsi ilivyo sasa ni "kilele cha ufisadi". Anataja sababu tatu lakini zote ziko nusu nusu. Sababu yake ya kwanza kuwa chanzo cha tatizo ni udahili wa zaidi ya mara moja ni tatizo linaloonesha kuwa bodi haina utaratibu wa kuzuia jambo hilo kutokea tena mwaka huu. Anaposema kuwa bodi ilipata majina baadaye ya wanafunzi halisi anashindwa kutuambia kama walipata majina hayo baada ya kugawa fedha au baada ya wanafunzi kuhamia vyuo vingine? Na kama walishagawa pesa zaidi ya mara moja, wana uhakika gani kuwa fedha hazikuishia mifukoni mwa watu wachache katika bodi yake au vyuo husika?

Chanzo cha pili anachodai ni kuwa tatizo ni muda mfupi wa kuchambua majia ya waombaji. Hili nalo ni uthibitisho wa uzembe wa bodi. Kama bodi haina muda wa kufanya uchambuzi wa kina kwanini basi wakubali kupokea mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania na kuzigawa kama nyugu? Kama hawana muda wa kufanya uchambuzi unaostahili kwanini tuwaamini kuwa majina waliyoyapatia fedha ni majina halali?

Katika chanzo cha tatu Bw. Nyatega analaumu mfumo mbaya wa kutokuwa na namba za kuwatofautisha wanafunzi. Madai kuwa kutokuwepo kwa namba maalum za kutofautisha wanafunzi zimechangia sana kwenye tatizo ni kujaribu kuficha ukweli. Kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita Tanzania anapatiwa namba ya mtihani na kituo alichofayia mtihani; kwanini wasitumie namba hiyo? Je, wasomi wote wizara ya Elimu ya Juu na hapo Bodi wameshindwa kabisa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na matokeo yake wameamua kufanya mambo bila uwezo wa kutofautisha waombaji? Ina maana kwa mamilioni yote ya fedha wanazotengewa na serikali wameshindwa kutafuta program ya kompyuta ambayo inaweza kutoa alama nyekundu pale majina yanafanana au namba zinazofanana zinapojitokeza na hivyo kulazimisha manual oversight? Kama huu siyo ubovu na uchafu tuupe jina gani? Kwa kuwaambia kwamba hapa kuna tatizo kwanini wafikirie lengo langu ni kuchafua jina la mtu? Wiki chache zijazo nitaandika jinsi ya kuiboresha bodi yetu ya mikopo baada ya kuivunja hii ya sasa. Lengo siyo kuonesha uchafu tu bali pia kutoa mawazo ya jinsi ya kuundoa uchafu huo.

Hata hivyo hakuna kitu cha kufurahisha kama maelezo ya Mkurugenzi huyo kwenye kipengele cha 2.2 cha majibu yake. Hapa nitamnukuu neno kwa neno. Bw. Nyatega katika kuelezea jinsi bodi ilivyo makini kuhusu matatizo niliyoyaanisha kwenye makala yangu anasema "Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, imeshachukua hatua ya kubainisha kama kulikuwa na ulipaji hewa wa mikopo ya wanafunzi au "Double Payments" na kazi hii imepewa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Prevention of Corruption Bureau– PCB) ambayo inaendelea na uchunguzi na endapo itagundulika kuwa kweli basi hatua zifaazo zitachuliwa ipasavyo." Kwa hili nawapongeza sana, hata hivyo hatua hii imeanza kuchukuliwa lini? Baada ya makala yangu au kabla? Kama ni kabla ni kitu gani kiliwasababishia kutaka kufanya uchunguzi huo? Kama ni baada ya makala yangu ina maana hoja zangu zilikuwa na uzito na siyo za kuchafua watu! Na kama ilikuwa kabla mbona watanzania hawakuambiwa kuhusu suala hili, kwanini lilifanywa kwa usiri hadi makala yangu ilipotoka ndipo Bodi inakiri kuna uchunguzi?

Maelezo kuwa PCB wameombwa wafanya uchunguzi ni maelezo duni. Watanzania hawaiamini PCB isipokuwa viongozi wa serikali tu. Kama uchunguzi wao wa Richmond, BOT n.k ni ishara yoyote, basi ni rahisi kujua Bw. Hosea atatoka na taarifa ya namna gani. Kwa vile sitaki watanzania wasubiri muda mrefu matokeo ya uchunguzi huo, ngoja niwapatie preview ya maelezo kuhusu ufisadi bodi ya mikopo. PCB itakapotoka na uchunguzi wake watagundua kuwa kulikuwa na matatizo ya kimfumo na kimuundo ya hapa na pale na matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Hata hivyo watagundua kuwa matatizo yote hayo hayana maana ya ufisadi na hivyo watasema kuwa hakukuwa na double payments na hakukuwa na rushwa ya aina yoyote. Vyombo vyetu vya habari vitapiga makofi, Msolla atashingiliwa na yote yataisha kinyemela. Kwa ufupi hakuna atakayewajibishwa kwani hakuna ufisadi bodi ya mikopo. Wakija na jibu tofautina hilo nililosema nitawaomba msamaha.

Mifano niliyotoa na majibu ya bodi
Katika majibu ya bodi nimefurahi kuwa kuna mambo kadhaa ambayo wameyakiri. Kwanza suala la Yesse C Msechu na Allawi R Kihalla. Bodi inakiri kuwa vijana hawa walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 siyo 2006/2007 na bodi inaeleza kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa ni "halali" na kuwaelezea kuwa "kwa mwaka 2006/2007 hao ni wanafunzi wanaoendelea na masomo." Kwa mtu ambaye anaweza kumiss point anaweza kufikiri kuwa wanafunzi hawa ni wa mwaka wa pili. Tatizo ni kuwa wanafunzi hawa wako mwaka wa kwanza. Sasa kama walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 iweje mwaka 2006/2007 wawe wanafunzi wa mwaka wa kwanza? Wanapotafuta jibu wakumbuke kuwa wanafunzi wale wengine waliowakana wapo vyuo hivyo hivyo na wanawahafamu wenzao "walioneemeshwa" na bodi.

Zaidi ya yote, wakati Bw. Nyatega anasema kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa walikubaliwa mkopo mwaka 2005/2006 na sasa wako Ukraine, bodi yake ikamtengea tena Yesse Shs. 840,000 kwa mwaka wa kwanza hapo UDSM katika bajeti ya 2006/2007 (Batch 9). Bila ya shaka atasema hawa ni watu wawili tofauti na wamepiga simu UDSM na kuhakikisha kuwa kuna mwanafunzi mwenye jina hilo yupo. Nawapa changamoto UDSM wamlete hadharani mwanafunzi huyo na nitakiri nimekosea.

Tukibakia kwenye suala hili hili, kama wanafunzi hawa walikubaliwa mwaka 2005/2006 na siyo 2006/2007 na mikopo yao ikaheshimiwa kwanini wanafunzi wenzao waliokuwa nao kwenye batch zile zile wamekataliwa? Bila ya shaka Bw. Nyatega atasema hawa 24 "hawakukamilisha taratibu" fulani. Hata hivyo hadi leo hii siyo yeye, siyo Gesimba wala siyo Msolla ambaye ameweka hadharani taratibu hizo ambazo watoto wetu 24 hawakuzikamilisha. Ni taratibu gani hizo ambazo zilikuwa ngumu kiasi hicho hadi kusababisha vijana wasipewe mkopo na kutelekezwa? Inawezekana kuwa vijana hawa hawakutaka kuomba fedha za nauli toka bodi ili wasijiongezee deni na badala yake wakajitafutia nauli zao wenyewe na hivyo kuwanyima watu ulaji? Na kitendo cha wao kuondoka bila "nauli" za bodi kiliwaudhi kina Mbegu, Ruta, na Temu? Kwa wanafunzi wengi wanaosoma nje ya nchi suala la nauli ni suala ambalo limewapa ulaji mwingi watu wa bodi. Ningekuwa na muda ningeanza kuchambua hilo, ninawawekea kiporo kwa sasa.

Mwanafunzi Adiel Daniel Mushi. Bodi inasema kuwa mwanafunzi huyu yupo UDSM ambako malipo yameshafanyika. Na anasema madai yangu ni "uzushi". Kama hilo ni kweli je mwanafunzi aliyeomba mkopo kwenda kusoma Ukraine na akatengewa milioni 3 (batch 10) ni nani huyo? Kwa vile Bw. Nyatega amesema kuwa COET wamethibitisha mwanafunzi huyo yupo, naomba kutoa changamoto nyepesi kuwa pindi wakisoma makala hii wamlete Adiel Daniel Mushi hadharani na siyo mtu anayejiita hivyo, na ale kiapo kwa kuonesha hati ya kuzaliwa kuwa ni yeye na hajulikani kwa jina jingine mahala kwengine; wakifanya hivyo nitakiri nimekosea. Kama bodi haitafanya hivyo, naomba COeT wamlete mwanafunzi huyo hadharani ndani ya siku tatu tangu kusoma makala yangu. Na zaidi ya yote, Bw. Nyatega anaweza kuelezea iweje mtu huyo huyo atengewe tena fedha nyingine kwenye chuo hicho hicho na kozi hiyo hiyo na hakuna mtu wa bodi aliyeshtuka? Kama huo siyo uzembe na kilele cha ufisadi tuuite jina gani?

Mwanafunzi Davis Dennis Kanyika. Mwenyekiti wa bodi anasema kuwa kijana huyu alikuwa asafiri mapema mwaka jana na ilikuwa kabla ya bajeti mpya. Sasa fedha alizotengewa zilitoka bajeti gani kama siyo ya 2005/2006. Ni kitu gani kilisababisha kijana huyo apewe mkopo wa 2005/2006 mwaka 2006/2007 na wale vijana 24 wanyimwe? Bw. Nyatega una mengi ya kujibu. Kama alikubaliwa 2005/2006 na hakuweza kuanza masomo wakati ule ilikuwaje bodi imlipie kwa mwaka wa 2006/2007

Kina Charles J Temba. Mwenyekiti wa bodi anasema kuna wanafunzi wawili kwenye vyuo viwili tofauti (SUA na MIST) ambao majina yao yanafanana na wote wameshalipiwa fedha zao. Na anasema kuwa kuna mwanafunzi mwingine mwenye jina hilo ambaye alipangwa kusomea Mzumbe ambako alipelekewa fedha. Hata hivyo anakiri kuwa mwanafunzi huyo hakutokea huko Mzumbe na fedha zimerudishwa kwenye Bodi. Je, fedha hizo zimerudishwa baada ya mimi kusema jina lake hadharani au kabla? Mkurugenzi wa bodi anakiri kuwa vyeti vilivyotumika kumdahili Charles Temba wa SUA ndivyo vilivyotumika kumdahili yule wa MIST lakini anasema kama asiye na uhakika wa ufisadi kuwa "Ikibainika kwamba kulikuwa na udanganyifu, hatua za kisheria zitachukuliwa." Je nikimwambia kuwa kuna Charles J. Temba mmoja tu atakataa, kama anabisha naomba amlete yule wa MIST na yule wa SUA hadharani. Akifanya hivyo kwa ushahidi unaoweza kusimama mahakamani nitakubali nimepotoka.

Charles B. Temba wa Arusha. Kwa mujibu wa Bw. Nyatega ni kuwa mwanafunzi huyo ni tofauti na Charles J Temba na anakiri kuwa amelipiwa karibu shilingi milioni 2 huko Arusha. Ninapendekezo jepesi kwa Bw. Nyatega. Wakutanishe wanafunzi hawa watatu hapo MAELEZO. Vinginevyo kiri kuna ufisadi kwenye bodi unayoongoza na wewe na Prof. Msolla hamstahili kuendelea kushikilia usukani.

Mwanafunzi Salim Chadoe aliyetengewa fedha mara mbili wanasema kuwa kwa sasa yuko Algeria. Je, zile fedha alizotengewa UDSM zimetumika vipi? Maelezo ya Chadoe yanalingana na maelezo ya bodi kuhusu wanafunzi Alistidia J. Rupia, Kazinja Patrick E, Ligunda Mary, Sophia Sokoni na Mohamed Matwera. Katika maelezo ya bodi ni kuwa wanafunzi wote hawa wote wako Algeria baada ya kukatisha masomo yao ya Udaktari hapo Tanzania. Wanafunzi waliacha masomo hayo ili waende kusoma "Kifaransa" huko Algeria. Bw. Nyatega bila ya shaka anatuona watanzania ni wavivu wa kufikiri. Nitawaacha wengine watafute hoja za suala hili maana kwangu haliingii akilini kabisa. Ili kutuliza maswali yangu ati anadai wanafunzi hawa watakatwa fedha hizo kwenye malipo yajayo. Sasa wakiwakatia fedha si watawasababishia mapungufu. Nashauri pesa hizo zikatwe kwa maofisa wa bodi hiyo waliozembea hadi kusababisha tatizo hilo, na ili kuonesha mfano wa kwanza awe ni Bw. Nyatega mwenyewe.

Mwanafunzi Exaud Chengule. Kwa ufupi Bw. Nyatega anasema kuwa huyu mtu hayupo na wanatafuta fedha alizokopeshwa zimeenda wapi. Je nikiwaambia kuwa mtu huyo hakuwahi kuwepo isipokuwa katika mawazo ya watu wa bodi atakataa. Na uchunguzi wa kumtafuta ulianza lini? baada ya mimi kuwaripotia au kabla. Je kwa kuwaonesha uchafu na uozo huo nimechafua majina yao au nimewasaidia kuwarahisishia kazi yao? Wajifunze kuonesha shukrani siyo kubeza juhudi za watu wanaowasaidia.

Wanafunzi Emmanuel Richard Kizigha na Emmanuel Richard Kizigha. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa ni wawili tofauti lakini inaonekana kuna mmoja anatumia vyeti vya kufoji. Kama kuna mtu kafoji na wanagundua hilo baada ya mimi kuwatajia majina wanajua ni wangapi wanatumia majina ya kufoji na vyeti vya kufoji ambao sijawataja? Kumbuka nimewaambia ninao 500! Kama nisingewapatia hilo jina wangeweza hata kuanzisha uchunguzi? Kama huo wote sio uzembe na kilele cha ufisadi tuupe jina gani? Next time, kila ninapowapatia majina ya wanafunzi wenye mashaka na wakigundua kuna tatizo itabidi wanilipe! Uzalendo utanishinda na bodi inazo pesa bwelele.

Suala la wanafunzi waliotelekezwa Ukraine na serikali ya Kikwete
Bw. Nyatega kama walivyofanya kina Gesimba, mama Kabaka, na Prof. Msolla amerudia maneno yale yale ya kilaghai kuhusu suala la hawa wanafunzi ili kuzima tuhuma dhidi yao. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa "walichagua kwenda Ukraine kwa taratibu zao wenyewe baada ya kushauriwa kutofanya hivyo. Suala hili limeshatolewa ufafanuzi na serikali na bodi ya mikopo mara kadhaa, hivyo, bodi haina haja ya kutoa maelezo ya ziada". Kwa bahati mbaya sana, haja ya kufanya hivyo bado ipo.

Kama waliweza kuwapa mikopo vijana Yesse Msechu na Alawi Kihalla waliokubaliwa mikopo 2005/2006 kwenye batch zile zile na hawa 24 ni kitu gani kiliwafanya washindwe kuwapa mikopo hawa wengine? Madai ya kuwa vijana hawa 24 hawakutimiza taratibu fulani licha ya kutengewa mikopo, Bw. Nyatega awaambie watanzania ni taratibu gani hizo ambazo hawakuzitimiza?Na wao kama bado walishindwa vipi kuwasaidia vijana hawa kutatua matatizo hayo ili wasipate matatizo?

Kama vijana hawa waliweza kutafuta tiketi zao na hawakutaka kutumia mikopo ya tiketi, je hilo ni kosa kubwa la kusababisha wasipewe mikopo. Kama mimi ningekuwa Nyatega ningewashukuru vijana hawa kwa kuonesha mfano kuwa familia inaweza kupunguza deni la elimu ya juu kwa kuwatafutia vijana wao nauli badala ya kusubiri mkopo wa serikali. Bw. Nyatega, mwaka 2005/2006 mliwatengewa vijana hawa fedha, na baadaye kwa sababu mnazozijua nyinyi mkawanyima baada ya vijana hawa kununua tiketi zao na kwenda kuanza masomo, tunaomba uwaambie watanzania fedha zao mlizowatengea mwaka ule kiasi cha 72,000,000 ziko wapi?

Bodi na serikali imeendelea kudai kuwa vijana hawa "walishauriwa" wasiende huko Ukraine, lakini hadi hivi sasa haijatolewa sababu ya kwanini walishauriwa hivyo. Sababu ya Bilateral Agreement haiwezi kusimama kwani Yesse na Alawi walienda na wako vyuo hivyo hivyoj walivyokubaliwa vijana hawa. Iweje hiyo Bilateral Agreement iwahusu wanafunzi wote wa kitanzania walioko Ukraine isipokuwa hawa 24. Hawa vijana hawajakubaliwa kusoma sayari Zebaki ambako hatuna Bilateral Agreement nao!

Na katika kudai kuwa bodi iliwashauri wasiende hakuna kiongozi hata mmoja aliyetayari kusema ushauri huo ulitolewa lini, wapi, na nani. Namuuliza Bw. Nyatega na Prof. Msolla, ni barua gani waliyopewa wanafunzi hawa kuwa wasiende Ukraine? Ni tangazo gani la habari na kwenye chombo kipi lililowataka wasiondoke? Je yawezekana kuwa ushauri huo ulitolewa kwa mdomo (verbal) na hakuna maandishi yoyote? Kama lililotolewa kwa mdomo bila maandishi kwanini tusiamaini kuwa ahadi ya wao waendelee na safari nayo iliyotolewa kwa mdomo? Nakupa changamoto bw. Nyatega na wenzako wekeni hadharani ushauri huu ulikuwa upi, ulitolewa lini, wapi, na nani na ulitumwa kwa nani.

Suala la malipo yaliyofanyika Ukraine – uthibitisho wa ufisadi
Katika majibu yake Bw. Nyatega anasema vitu hivi kwamba kuna malipo yaliyofanyika kumhusisha Alawi Rajabu Kihalla yaliyofanyika tarehe 18/4/2006 kwa kupitia hundi namba 193426 yenye thamani ya Shs. 87,772,800 na yakihusisha wanafunzi wengine waliotangulia. Hata hivyo Bw. Nyatega anasema tena kuwa kuna malipo mengine yaliyofanyika 22/3/2006 (mwezi mmoja kabla ya yale ya Kihalla) kwa mwanafunzi David Dennis Kanyika (yakihusisha wanafunzi wengine) yenye thamani ya Shs. 87,772,000 kwa kutumia hundi yenye namba 193426. Jumla ya malipo hayo yote ni Shs. 175,544,800. Kwa kuangalia namba hizo tunakutana na matatizo yafuatayo.

- Namba za cheki zilizotumika ni zile zile. Hilo haliwezekani isipokuwa kama kuna mtu anataka kufanya malipo hewa.
- Kiasi cha fedha kilicholipwa kinakaribiana. Tofauti ni Shs. 800 tu.
- Wanaolipwa ni watu wale wale. Inawezekana vipi uandike cheki mbili zenye kiwango sawa na zenye namba sawa kwa wanafunzi wale wale isipokuwa kama unataka kuweka kiasi kingine pembeni?

Kama hiyo haitoshi, Bw. Nyatega anasema pia kuwa tarehe 19/1/2006 malipo yalifanyika yaliyomjumuisha Yesse Msechu (na wanafunzi wengine) kwa kupitia hundi namba 149736 yenye thamani ya Shs. 80,097,600. Kwa maneno mengine ndani ya miezi minne bodi yetu ya mikopo ililipa Shs. 255,642,400 kwa wanafunzi wasiopungua 85. Tukumbuke kuwa malipo haya yanatokana na bajeti ya 2005/2006. Je. Bw. Nyatenga anaweza kutupa orodha ya wanafunzi wote waliokuwa kwenye mgao wa mikopo ya mwaka 2005/2006 kule Ukraine? Je ana uhakika kuwa hakuna fedha zilizoishia mikononi mwa watu ambao siyo wanafunzi.

Tricky tricky!
Namuomba Bw. Nyatega awaeleze watanzania Bw. Francis kutoka Ubalozi wetu Moscow ni nani na anahusika vipi na malipo ya mikopo. Zaidi ya ya yote awaambie watanzania Bw. Constantine Mkami wa Ukraine anahusika vipi katika mchakato mzima wa wanafunzi wanaosoma pale Ukraine. Asipofanya hivyo kwa ukweli na uwazi nitamsaidia.

Suala la Sera.
Bw. Nyatega anasema kuwa Bodi yake haiko tayari kuwasaidia vijana hawa kwa sababu ya sera. Kuwa ni sera ya CCM kutowasaidia vijana hawa wa Kitanzania ambao walishakubaliwa mikopo kama Kihalla, Msechu Na Kanyika. Anasema kuwa ni sera ya CCM kutambua baadhi ya wanafunzi kwenye kwa sababu ya makubaliano ya nchi mbili na kuwakataa wengine kwa vile hawakutaka mikopo ya tiketi zao. Bw. Nyatega anachosema ni kuwa ni sera ya serikali ya Rais Kikwete kuwabagua vijana hawa kwa vile wameonesha manung'uniko yao hadharani na kudai haki yao hadharani. Na jinsi nilivyomuelewa Bw. Nyatega ni kuwa ni sera ya wana CCM na wabunge wao kutowatetea vijana hawa na kuwatafutia haki yao kwa vile tu wapinzani wamejitokeza kuwasaidia.

Ndugu zangu, sera hii ni ya kibaguzi, kibabe, na ya kizandiki. Ni sera ambayo haina budi kupigwa vita na kila mtanzania mwenye kuthamini elimu na mwenye kujali haki za wananchi. Haiwezekani watu wachache waje na sera mbovu kama hii na sisi tukawafumbia macho. Binafsi nasikitika kuwa hadi hivi sasa hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyejitokeza kuwatetea vijana hawa, hakuna mchungaji, askofu, walimu, NGO, n.k ambao wametaka serikali iwatimizie ahadi yao vijana hawa. Inaonekana tumekubali serikali iwabague vijana wetu kwa vile tu "hawakukamalisha taratibu fulani" za kusadikika. Sera hii ya CCM lazima ivunjwe na iondolewe vitabuni vinginevyo chama chetu kitakuwa kimetiwa tope kubwa na watu wa bodi. Nawashauri viongozi wa CCM waikane sera hii na kuwatendea haki vijana wetu. Vinginevyo, wajiandae kulipa gharama kubwa ya kisiasa.

Siwezi kuamini kabisa kuwa Rais Kikwete, Makamu wake na Baraza zima la Mawazirila serikali yetu limevumilia sera hii ambayo ina harufu ya nchi ya kibaguzi. Siwezi kuamini kuwa Rais anayetaka watu wasome elimu ya juu anafumbia macho suala hili na kuwaacha watuhumiwa wa ufisadi kumpa maelezo ya kilaghai ili kutetea unga wao. Kwa mara nyingine tena, natoa wito kwa Prof. Msolla kujiuzulu, Bodi ya Mikopo kuvunjwa mara moja na tume huru kuundwa kuchunguza ufisadi katika bodi hii. Ni wazi kuwa ni vigumu kwa serikali yetu kufanya hivyo lakini nimekunja vidole vyangu nikiamini kuwa kuna mtu mwenye dhamira safi Ikulu ambayo hakubali uonevu au ufisadi. Vijana hawa wanaonewa na wametelekezwa bure na watu wa bodi. Prof. Msolla anajua hivyo, Mama Kabaka na mama Katunzi wanajufa hivyo, Bw. Mbegu anajua hivyo, na Bw. Nyatega anafahamu hivyo. Na hatimaye leo hii, kila mtanzania anafahamu hivyo.

Kwa vile Bw. Nyatega amenitafutia majibu ya majina niliyoyaweka mwanzoni, nimeonelea nimuongezee majina mengine ili ayatolee ufafanuzi. Kila jina moja waweke kwenye akaunti ya wanafunzi wa Ukraine Shs. Milioni moja.

Rabson Mahenge, alitengewa (allocated) shilingi laki 980,000 pale Muhimbili kusomea Pharmacy (batch 12) na akatengewa shilingi 1,665,000 (batch 10) kwenye chuo hicho hicho kwa kusomea Pharmacy hiyo hiyo. Sasa Bw. Nyatega anaweza kutuambia kuwa pesa ililipwa mara moja. Sawa. Kwanini watenge mara mbili, aidha kuna uzembe wa kiutendaji au kuna mtu anataka "chenji"

Sifa Anyimike, ametengewa shilingi 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM (Batch 10), lakini akatengewa 1,320,000 kusoma hapo hapo UDSM (batch 8). Huyo huyo Anyimike wetu, akakubaliwa kiasi kingine cha Shs. 540,000 kusoma chuo hicho hicho tena (Batch 6).

Helena Yomo. Kwa huyo nayo ni yale yale. Katika Batch 10 alitengewa Shs. 1, 320,000 kusomea Elimu hapo UDSM. Kwa vile bodi yetu ina makengeza ikatenga tena kiasi kama hicho kwenye batch 8. Na kama hiyo haikutosha mwanafunzi huyo huyo chuo kile kile akatengewa tena Shs 540,000 (Batch 6). Inawezekana Bodi yetu ya Bw. Nyatega watakuja na kusema hao UDSM kuna wanafunzi watatu wote wanaitwa Helena T Yomo na wote wanasomea Elimu, na bila ya shaka watasema wamezungumza na chuo na kuthibitishiwa kuwa wanafunzi wote watatu wapo.

Upendo V Chubwa. Huyu katika Batch 10 alitengewa na Bodi ya Nyatega Shs 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM na wakati huo huo kwenye mwaka huo huo alitengewa 1,320,000 (batch 8) kusomea elimu hapo hapo UDSM. Na kwa vile kina Nyatega na wenzake hawajui jinsi kuendesha bodi hiyo wakaona hiyo haitoshi wakaamua kumuongezea tena 540,000 kwenye chuo hicho hicho kwenye kozi hiyo hiyo (batch 6).

Hivi kama si uzembe na uvivu unaweza kuelezea vipi kumtengea fedha mtu mmoja mara mbili kwenye batch ile ile huku jina lake likijirudia. Hii imetokea kwa wanafunzi wawili, Hamisi Mganda ambaye alitengewa Shs. 2,640,000 (DUCE) na Mwaveso Mbwana ambaye alitengewa kiasi kama hicho kwenye batch 10. Sasa kama majina mawili yanayofanana hayawashtui, nini kitawashtua?

Arton Kayombo. Huyu katika Bodi yetu hii ametengewa Shs. 1,320,000 hapo DUCE kusomea Elimu (batch 10) na kupitia bodi hiyo hiyo akatengewa tena kiasi hicho hicho kwenye batch 8. Sasa inawezekana kabisa kuwa mfumo wanaotumia ni mbovi kiasi cha kwamba majina yanajirudia rudia kwa bahati mbaya. Kama hili ni kweli ni kitu gani kinazuia watu wachache kujipongeza kwa fedha za umma?

Ndugu zangu bodi ya Mikopo ina matatizo na uongozi wake mzima hadi Waziri ni mbovu na unaohitaji kubadilishwa. Unganeni nami kumtaka Prof. Msolla na Bw. Nyatega na bodi nzima wakiongozwa na Bw. Mkono wajiuzulu kwa kuzoea uzembe, kuvumilia ufisadi, na kushindwa kuiongoza bodi hiyo ipasavyo. Mimi na wenzangu tumeanzisha utiaji sahihi wa ombi la kutaka Prof. Msolla ajiuzulu. Unaweza kuingia kwenye http://www.jamboforums.com kwa maelezo ya kuweza kusaini ukurasa huo wa kwenye mtandao.

Niandikie: mjengahoja@jamboforums.com
Nitumie ujumbe: + 1 248 686 2010
 
MAJIBU YA MWANAKIJIJI KWA BODI YA MIKOPO, YAMETOKA KATIKA GAZETI LA KULIKONI LA LEO, UKURASA WA 12,13 NA 16

UTETEZI WA BODI YA MIKOPO, MAJIBU YAO YATHIBITISHA UFISADI.

MJENGA HOJA

Kwanza kabisa sina budi kutoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo Bw. George Nyatega kwa kitendo chake cha kujaribu kutoa majibu ya makala yangu niliyoandika wiki iliyopita yenye kichwa cha habari “Twaweza kumuamini Prof. Msolla – Bodi ya mikopo kilele cha ufisadi”. Jaribio lake hilo ambalo bila ya shaka liliandikwa kwa uangalifu mkubwa limenigusa moyo na kunionesha kuwa sisi kama Watanzania tunaweza kuwa na mjadala wa wazi katika kujaribu kuisogeza mbele kimaendeleo nchi yetu. Licha ya sehemu chache katika majibu yake ambapo anahoji nia na uzalendo wangu nina uhakika Bw. Nyatega na wenzake wanaelewa kuwa lengo langu siyo kuichafua bodi hiyo au majina ya watu bali kuonesha uchafu wa bodi hiyo na kutaja majina ya watu ambao wanahusika na uchafu huo. Hivyo siyo lengo langu hata kidogo kuwachafua, bali kunyoosha kidole dhidi yao na kusema wamechafuka, wasafishwe. Hata hivyo, kwa vile amehoji nia na kusudi la makala yangu na kwa kukosea amehitimisha kuwa lengo langu ni “kuchafua majina ya watu” ninapenda kutumia nafasi hii kueleza ni kwanini niliandika makala zangu mbili zilizotangulia kuhusu Prof. Msolla na baadaye kuihusu Bodi.

Kwanza kabisa lengo la makala yangu ni kuonesha kuwa kuna tatizo kwenye bodi ya mikopo, tatizo ambalo limechangia kupotea kwa mamilioni ya fedha kutokana na mfumo mbaya wa utoaji mikopo. Mifano niliyotoa (nitaelezea tena baadaye) ilikuwa na lengo la kuonesha kuwa madai ya kuwa bodi ni chafu na ina mfumo mbaya siyo madai ya mtu asiyejua nini kinaendelea bali yanatokana na uchunguzi yakanifu.

Pili, na kubwa zaidi lengo langu ambalo Bw. Nyatega hakujaribu kulikanusha ni kuwa uongozi wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu umeshindwa kabisa kuipa uongozi bodi hii licha ya wao (wizara) kukiri mapungufu mbalimbali (angalia makala yangu ya kwanza). Kinara wa ukosefu wa uongozi huo ni bosi wa Bw. Nyatega yaani Waziri Prof. Peter Msolla. Ni madai yangu kuwa matatizo mengi yanayotokea kwenye bodi leo hii na yaliyotokea hadi sasa yametokana na uzembe wa Prof. Msolla na kiburi cha kutotaka kuyakabili matatizo hayo moja kwa moja. Licha ya kwamba anayajua matatizo ya bodi Prof. Msolla na wasaidizi wake wameshindwa kabisa kutafuta mbinu ya kuyatatua. Tatu na mwisho kabisa, katika kuandika makala yangu nilitaka kuonesha kuwa ni kutokana na uchafu wa bodi na kushindwa kwa Prof. Msolla kuongoza ndio maana leo hii tuna watoto wetu waliokwama Ukraine, kwa kisingizio cha “waliondoka wenyewe”. Hili “nitaliibua” tena baadaye.

Hayo ndiyo yalikuwa malengo ya makala zangu zilizotangulia na yanaendelea kuwa malengo ya makala hii ya sasa. Hata hivyo jambo moja limenisikitisha katika majibu ya Bw. Nyatega. Katika majibu yake yote ya ukurasa wa nane, Bw. Nyatega ameshindwa kuonesha uungwana wa kunishukuru kwa kumsaidia kuiangalia kwa ukaribu bodi anayoingoza na kusahihisha makosa au mapungufu niliyoyaonesha. Jinsi alivyoandika ni kana kwamba mimi nina kusudio baya na bodi au nchi yangu na ni yeye ndiye mzalendo pekee aliyebakia. Kwa vile nimewasaidia kutambua makosa na matatizo mengine angeonesha angalau uungwana wa kushukuru badala ya kudhihaki juhudi zangu kwani wakati yeye analipwa kufanya anachofanya mimi nafanya kwa kujitolea. Hata hivyo, kama hamaanishi shukrani hizo, sizihitaji lakini nitaendelea kufafanua mambo mengine bila kutarajia shukrani yoyote kwani walisema waswahili kwa usahihi kabisa kuwa “shukrani ya punda ni mateke”. Nina uhakika hata hivyo kuna watu ambao wananishukuru kwa kuthubutu kusema “mfalme hajavaa nguo”.

Baada ya kusema hayo, hebu tuangalie majibu ya bodi hii na kama majibu haya yanaweza kuingia akilini mwa mtu yeyote mzima na kama katika majibu yao wamejibu kwa uhakika hoja nilizojenga. Ndugu zangu, majibu ya Bw. Nyatega ni ya mtu aliyekurupushwa, yenye kujikanganya, yasiyo na ukweli na kwa hakika ni majibu yenye lengo la kuipotosha jamii na yenye kujaribu kujisafisha. Ni majibu ya mtu anayejaribu kupaka makaburi rangi za kumeremeta kumbe ndani yake ni mifupu mitupu! Kwa bahati mbaya, wamekosea mtu wa kumjibu kwani wakati wengine wanakubali majibu ya bodi kama walivyokubali majibu ya Hosea, Gesimba, na Balali, sisi wengine majibu yao ndio yanatupa maswali mengi zaidi na ya kina kwani majibu hayo siyo majibu bali ni majaribio ya kujibu maswali magumu. Ni majaribio yaliyoshindwa na nitumie nafasi hii kuonesha ni jinsi gani majibu ya Bw. Nyatega hayana mantiki na yenye kukusudia kuficha kitu.

Kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo (loan allocation & loan disbursement)
Bw. Nyatega katika jaribio lake la kujibu hoja zangu anajaribu bila mafanikio kutumia maneno ya Kiingereza kutofautisha mambo mawili lakini hata hivyo ameshindwa kuonesha uhusiano wa mambo hayo. Je mtu anaweza kutenga kitu ambacho hana? La hasha! Na je mtu anaweza kuwagawia watu kitu ambacho hajakitenga kwa ungalifu? La hasha. Katika kuelezea hili suala Bw. Nyatega amedhihiria udhaifu mkubwa wa bodi, anasema hivi kuhusu suala la kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo, “kupangiwa kupewa mkopo (Loans Allocation) hufanyika mwanzoni mwa mwaka wa masomo, baada ya Bodi kupata matokeo ya udahili kutoka vyuo vya elimu ya juu na pia kutoka kwa Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tanzania Commission for Universities - TCU). Baada ya uchambuzi wa waombaji, kulingana na vigezo, Bodi hupanga mikopo kwa kila mwombaji kwa kila Chuo na taarifa hiyo hutolewa kwa njia ya tovuti ya Bodi ili iwafikie wahusika wote.” Na baada ya hapo Bw. Nyatega anasema “Bodi huendelea na uchambuzi zaidi kabla ya kufanya malipo “Disbursements”.

Kwa maneno mengine ni kuwa wao wanatumia majina yaliyotumwa na vyuo na TCU kupanga mikopo hiyo na baadaye wakiishayachambua ndio wanagawa hizo fedha. Katika majibu yake hayo bila ya shaka tunakutana na mambo mawili makubwa. Wanapopatiwa majina ya waombaji na wanapokubali kuwatengea fedha kabla ya kuhakikisha waombaji ni kina nani, wamefungulia ghala la ufisadi. Hii inajibu swali la mwanafunzi mmoja aliyeomba vyuo vitatu au vinne kukubaliwa mikopo mara hizo zote. Kwa kitendo cha bodi kutenga fedha hizo kwa kila mwombaji aliyeyedailiwa bila kuhakikisha kama ni “multiple allocations) ina maana fedha hizo zipo na zinatengwa zaidi ya mara moja. Huwezi kutenga fedha au kupanga matumizi ya fedha ambazo hauna. The board does not allocate fanthom money! Hivyo wanapompangia Juma Mdoe (jina la kubuni) aliyeomba mkopo kwenye vyuo vitatu Shs milioni 3 kwenye kila chuo, basi Juma atakuwa ametengewa/amepangiwa/amekuwa “allocated” milioni tisa. Sasa kama Juma ataamua kwenda chuo kimojawapo na siyo vile vingine, basi kuna Shs. Milioni sita ambazo zitakuwa hazikutumika. Swali kubwa ni nini kinafanyika kwa fedha hizi? Ni kutokana na uchunguzi wangu ndio nimeonesha kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 500 ambao kwa mwaka uliopita wa 2006/2007 walitengewa mikopo zaidi ya mara moja.

Hili linatuleta kwenye neno la pili nalo ni “kugawa mikopo” (Loan disbursement). Kwa mujibu wa Bw. Nyatega uchambuzi hufanyika na baadaye wanafunzi wanapewa mikopo hiyo. Na kwa ujasiri mkubwa akaniambia kuwa ningetumia taarifa za waliogawiwa mikopo kuonesha kama wamepewa au la. Kwa kutumia ujanja amejaribu kulifanya jambo la “loan allocation” kuwa ni “non-issue”. Jaribio lake hilo lilifanywa pia na Prof. Msolla kwenye jibu lake Bungeni mapema kwenye kikao kinachoendelea sasa Dodoma. Swali kwetu ni kuwa lipi ni jambo kubwa, loan allocation au loan disbursement? Jibu langu ni hilo la kwanza. You can not disburse money you haven’t allocated! Ili waweze kugawa pesa ni lazima wawe wamezitenga. Hivyo ufisadi hauanzii kwenye kugawa bali kwenye kutenga. Kwa maneno yake yeye mwenyewe bodi imewalipia watu ambao hawako vyuoni, na waliweza kufanya hivyo baada ya kuwatengea. Ufisadi mkubwa katika bodi hauko kwenye kugawa pesa kwani ni rahisi kugawa fedha kwa mtu wanayemtaka kuliko kuangalia wamemtengea nani fedha. Hivyo tatizo ni zile pesa ambazo ziliombwa kwa mwanafunzi zaidi ya mmoja na zikatengwa lakini hazikutumiwa zilifanyiwa nini? Je, Bw. Nyatega anataka kuwahakikishia Watanzania kuwa hakuna afisa wake hata mmoja ambaye “amejipongeza” kwa mikopo ya wanafunzi? Isipokuwa kama Bw. Nyatega atasema kuwa fedha zinapotengwa haina maana kuwa zipo.

Of course, hawezi kusema hivyo kwani yeye mwenyewe anasema hivi “Bodi inakiri kwamba kutokana na mkanganyiko wa “Double Admissions” katika vyuo vikuu mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa 2006/2007 kulitokea ‘Double Loan Allocations’ ambazo hata hivyo yalisahishwa kwa kiwango kikubwa wakati wa kufanya malipo (Loan Disbursements).” Na anasema “yalisahihishwa kwa kiwango kikubwa” kwa maana ya kwamba hayakuondolewa yote. Hivyo kupuuzia tatizo la “double allocation” kana kwamba siyo jambo zito ni ufunguzi wa double payment. Kwa maneno mengine, Mkurugenzi wa bodi anakubaliana na mimi kuwa kuna tatizo la ufisadi kwenye bodi anayoiongoza.

Hata hivyo Bw. Nyatega anajaribu kuelezea chanzo cha tatizo hilo (la double allocation) na anapofanya hivyo anaendelea kuthibitisha maneno yangu kuwa bodi jinsi ilivyo sasa ni “kilele cha ufisadi”. Anataja sababu tatu lakini zote ziko nusu nusu. Sababu yake ya kwanza kuwa chanzo cha tatizo ni udahili wa zaidi ya mara moja ni tatizo linaloonesha kuwa bodi haina utaratibu wa kuzuia jambo hilo kutokea tena mwaka huu. Anaposema kuwa bodi ilipata majina baadaye ya wanafunzi halisi anashindwa kutuambia kama walipata majina hayo baada ya kugawa fedha au baada ya wanafunzi kuhamia vyuo vingine? Na kama walishagawa pesa zaidi ya mara moja, wana uhakika gani kuwa fedha hazikuishia mifukoni mwa watu wachache katika bodi yake au vyuo husika?

Chanzo cha pili anachodai ni kuwa tatizo ni muda mfupi wa kuchambua majia ya waombaji. Hili nalo ni uthibitisho wa uzembe wa bodi. Kama bodi haina muda wa kufanya uchambuzi wa kina kwanini basi wakubali kupokea mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania na kuzigawa kama nyugu? Kama hawana muda wa kufanya uchambuzi unaostahili kwanini tuwaamini kuwa majina waliyoyapatia fedha ni majina halali?

Katika chanzo cha tatu Bw. Nyatega analaumu mfumo mbaya wa kutokuwa na namba za kuwatofautisha wanafunzi. Madai kuwa kutokuwepo kwa namba maalum za kutofautisha wanafunzi zimechangia sana kwenye tatizo ni kujaribu kuficha ukweli. Kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita Tanzania anapatiwa namba ya mtihani na kituo alichofayia mtihani; kwanini wasitumie namba hiyo? Je, wasomi wote wizara ya Elimu ya Juu na hapo Bodi wameshindwa kabisa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na matokeo yake wameamua kufanya mambo bila uwezo wa kutofautisha waombaji? Ina maana kwa mamilioni yote ya fedha wanazotengewa na serikali wameshindwa kutafuta program ya kompyuta ambayo inaweza kutoa alama nyekundu pale majina yanafanana au namba zinazofanana zinapojitokeza na hivyo kulazimisha manual oversight? Kama huu siyo ubovu na uchafu tuupe jina gani? Kwa kuwaambia kwamba hapa kuna tatizo kwanini wafikirie lengo langu ni kuchafua jina la mtu? Wiki chache zijazo nitaandika jinsi ya kuiboresha bodi yetu ya mikopo baada ya kuivunja hii ya sasa. Lengo siyo kuonesha uchafu tu bali pia kutoa mawazo ya jinsi ya kuundoa uchafu huo.

Hata hivyo hakuna kitu cha kufurahisha kama maelezo ya Mkurugenzi huyo kwenye kipengele cha 2.2 cha majibu yake. Hapa nitamnukuu neno kwa neno. Bw. Nyatega katika kuelezea jinsi bodi ilivyo makini kuhusu matatizo niliyoyaanisha kwenye makala yangu anasema “Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, imeshachukua hatua ya kubainisha kama kulikuwa na ulipaji hewa wa mikopo ya wanafunzi au “Double Payments” na kazi hii imepewa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Prevention of Corruption Bureau– PCB) ambayo inaendelea na uchunguzi na endapo itagundulika kuwa kweli basi hatua zifaazo zitachuliwa ipasavyo.” Kwa hili nawapongeza sana, hata hivyo hatua hii imeanza kuchukuliwa lini? Baada ya makala yangu au kabla? Kama ni kabla ni kitu gani kiliwasababishia kutaka kufanya uchunguzi huo? Kama ni baada ya makala yangu ina maana hoja zangu zilikuwa na uzito na siyo za kuchafua watu! Na kama ilikuwa kabla mbona watanzania hawakuambiwa kuhusu suala hili, kwanini lilifanywa kwa usiri hadi makala yangu ilipotoka ndipo Bodi inakiri kuna uchunguzi?

Maelezo kuwa PCB wameombwa wafanya uchunguzi ni maelezo duni. Watanzania hawaiamini PCB isipokuwa viongozi wa serikali tu. Kama uchunguzi wao wa Richmond, BOT n.k ni ishara yoyote, basi ni rahisi kujua Bw. Hosea atatoka na taarifa ya namna gani. Kwa vile sitaki watanzania wasubiri muda mrefu matokeo ya uchunguzi huo, ngoja niwapatie preview ya maelezo kuhusu ufisadi bodi ya mikopo. PCB itakapotoka na uchunguzi wake watagundua kuwa kulikuwa na matatizo ya kimfumo na kimuundo ya hapa na pale na matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Hata hivyo watagundua kuwa matatizo yote hayo hayana maana ya ufisadi na hivyo watasema kuwa hakukuwa na double payments na hakukuwa na rushwa ya aina yoyote. Vyombo vyetu vya habari vitapiga makofi, Msolla atashingiliwa na yote yataisha kinyemela. Kwa ufupi hakuna atakayewajibishwa kwani hakuna ufisadi bodi ya mikopo. Wakija na jibu tofautina hilo nililosema nitawaomba msamaha.

Mifano niliyotoa na majibu ya bodi
Katika majibu ya bodi nimefurahi kuwa kuna mambo kadhaa ambayo wameyakiri. Kwanza suala la Yesse C Msechu na Allawi R Kihalla. Bodi inakiri kuwa vijana hawa walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 siyo 2006/2007 na bodi inaeleza kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa ni “halali” na kuwaelezea kuwa “kwa mwaka 2006/2007 hao ni wanafunzi wanaoendelea na masomo.” Kwa mtu ambaye anaweza kumiss point anaweza kufikiri kuwa wanafunzi hawa ni wa mwaka wa pili. Tatizo ni kuwa wanafunzi hawa wako mwaka wa kwanza. Sasa kama walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 iweje mwaka 2006/2007 wawe wanafunzi wa mwaka wa kwanza? Wanapotafuta jibu wakumbuke kuwa wanafunzi wale wengine waliowakana wapo vyuo hivyo hivyo na wanawahafamu wenzao “walioneemeshwa” na bodi.

Zaidi ya yote, wakati Bw. Nyatega anasema kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa walikubaliwa mkopo mwaka 2005/2006 na sasa wako Ukraine, bodi yake ikamtengea tena Yesse Shs. 840,000 kwa mwaka wa kwanza hapo UDSM katika bajeti ya 2006/2007 (Batch 9). Bila ya shaka atasema hawa ni watu wawili tofauti na wamepiga simu UDSM na kuhakikisha kuwa kuna mwanafunzi mwenye jina hilo yupo. Nawapa changamoto UDSM wamlete hadharani mwanafunzi huyo na nitakiri nimekosea.

Tukibakia kwenye suala hili hili, kama wanafunzi hawa walikubaliwa mwaka 2005/2006 na siyo 2006/2007 na mikopo yao ikaheshimiwa kwanini wanafunzi wenzao waliokuwa nao kwenye batch zile zile wamekataliwa? Bila ya shaka Bw. Nyatega atasema hawa 24 “hawakukamilisha taratibu” fulani. Hata hivyo hadi leo hii siyo yeye, siyo Gesimba wala siyo Msolla ambaye ameweka hadharani taratibu hizo ambazo watoto wetu 24 hawakuzikamilisha. Ni taratibu gani hizo ambazo zilikuwa ngumu kiasi hicho hadi kusababisha vijana wasipewe mkopo na kutelekezwa? Inawezekana kuwa vijana hawa hawakutaka kuomba fedha za nauli toka bodi ili wasijiongezee deni na badala yake wakajitafutia nauli zao wenyewe na hivyo kuwanyima watu ulaji? Na kitendo cha wao kuondoka bila “nauli” za bodi kiliwaudhi kina Mbegu, Ruta, na Temu? Kwa wanafunzi wengi wanaosoma nje ya nchi suala la nauli ni suala ambalo limewapa ulaji mwingi watu wa bodi. Ningekuwa na muda ningeanza kuchambua hilo, ninawawekea kiporo kwa sasa.

Mwanafunzi Adiel Daniel Mushi. Bodi inasema kuwa mwanafunzi huyu yupo UDSM ambako malipo yameshafanyika. Na anasema madai yangu ni “uzushi”. Kama hilo ni kweli je mwanafunzi aliyeomba mkopo kwenda kusoma Ukraine na akatengewa milioni 3 (batch 10) ni nani huyo? Kwa vile Bw. Nyatega amesema kuwa COET wamethibitisha mwanafunzi huyo yupo, naomba kutoa changamoto nyepesi kuwa pindi wakisoma makala hii wamlete Adiel Daniel Mushi hadharani na siyo mtu anayejiita hivyo, na ale kiapo kwa kuonesha hati ya kuzaliwa kuwa ni yeye na hajulikani kwa jina jingine mahala kwengine; wakifanya hivyo nitakiri nimekosea. Kama bodi haitafanya hivyo, naomba COeT wamlete mwanafunzi huyo hadharani ndani ya siku tatu tangu kusoma makala yangu. Na zaidi ya yote, Bw. Nyatega anaweza kuelezea iweje mtu huyo huyo atengewe tena fedha nyingine kwenye chuo hicho hicho na kozi hiyo hiyo na hakuna mtu wa bodi aliyeshtuka? Kama huo siyo uzembe na kilele cha ufisadi tuuite jina gani?

Mwanafunzi Davis Dennis Kanyika. Mwenyekiti wa bodi anasema kuwa kijana huyu alikuwa asafiri mapema mwaka jana na ilikuwa kabla ya bajeti mpya. Sasa fedha alizotengewa zilitoka bajeti gani kama siyo ya 2005/2006. Ni kitu gani kilisababisha kijana huyo apewe mkopo wa 2005/2006 mwaka 2006/2007 na wale vijana 24 wanyimwe? Bw. Nyatega una mengi ya kujibu. Kama alikubaliwa 2005/2006 na hakuweza kuanza masomo wakati ule ilikuwaje bodi imlipie kwa mwaka wa 2006/2007

Kina Charles J Temba. Mwenyekiti wa bodi anasema kuna wanafunzi wawili kwenye vyuo viwili tofauti (SUA na MIST) ambao majina yao yanafanana na wote wameshalipiwa fedha zao. Na anasema kuwa kuna mwanafunzi mwingine mwenye jina hilo ambaye alipangwa kusomea Mzumbe ambako alipelekewa fedha. Hata hivyo anakiri kuwa mwanafunzi huyo hakutokea huko Mzumbe na fedha zimerudishwa kwenye Bodi. Je, fedha hizo zimerudishwa baada ya mimi kusema jina lake hadharani au kabla? Mkurugenzi wa bodi anakiri kuwa vyeti vilivyotumika kumdahili Charles Temba wa SUA ndivyo vilivyotumika kumdahili yule wa MIST lakini anasema kama asiye na uhakika wa ufisadi kuwa “Ikibainika kwamba kulikuwa na udanganyifu, hatua za kisheria zitachukuliwa.” Je nikimwambia kuwa kuna Charles J. Temba mmoja tu atakataa, kama anabisha naomba amlete yule wa MIST na yule wa SUA hadharani. Akifanya hivyo kwa ushahidi unaoweza kusimama mahakamani nitakubali nimepotoka.

Charles B. Temba wa Arusha. Kwa mujibu wa Bw. Nyatega ni kuwa mwanafunzi huyo ni tofauti na Charles J Temba na anakiri kuwa amelipiwa karibu shilingi milioni 2 huko Arusha. Ninapendekezo jepesi kwa Bw. Nyatega. Wakutanishe wanafunzi hawa watatu hapo MAELEZO. Vinginevyo kiri kuna ufisadi kwenye bodi unayoongoza na wewe na Prof. Msolla hamstahili kuendelea kushikilia usukani.

Mwanafunzi Salim Chadoe aliyetengewa fedha mara mbili wanasema kuwa kwa sasa yuko Algeria. Je, zile fedha alizotengewa UDSM zimetumika vipi? Maelezo ya Chadoe yanalingana na maelezo ya bodi kuhusu wanafunzi Alistidia J. Rupia, Kazinja Patrick E, Ligunda Mary, Sophia Sokoni na Mohamed Matwera. Katika maelezo ya bodi ni kuwa wanafunzi wote hawa wote wako Algeria baada ya kukatisha masomo yao ya Udaktari hapo Tanzania. Wanafunzi waliacha masomo hayo ili waende kusoma “Kifaransa” huko Algeria. Bw. Nyatega bila ya shaka anatuona watanzania ni wavivu wa kufikiri. Nitawaacha wengine watafute hoja za suala hili maana kwangu haliingii akilini kabisa. Ili kutuliza maswali yangu ati anadai wanafunzi hawa watakatwa fedha hizo kwenye malipo yajayo. Sasa wakiwakatia fedha si watawasababishia mapungufu. Nashauri pesa hizo zikatwe kwa maofisa wa bodi hiyo waliozembea hadi kusababisha tatizo hilo, na ili kuonesha mfano wa kwanza awe ni Bw. Nyatega mwenyewe.

Mwanafunzi Exaud Chengule. Kwa ufupi Bw. Nyatega anasema kuwa huyu mtu hayupo na wanatafuta fedha alizokopeshwa zimeenda wapi. Je nikiwaambia kuwa mtu huyo hakuwahi kuwepo isipokuwa katika mawazo ya watu wa bodi atakataa. Na uchunguzi wa kumtafuta ulianza lini? baada ya mimi kuwaripotia au kabla. Je kwa kuwaonesha uchafu na uozo huo nimechafua majina yao au nimewasaidia kuwarahisishia kazi yao? Wajifunze kuonesha shukrani siyo kubeza juhudi za watu wanaowasaidia.

Wanafunzi Emmanuel Richard Kizigha na Emmanuel Richard Kizigha. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa ni wawili tofauti lakini inaonekana kuna mmoja anatumia vyeti vya kufoji. Kama kuna mtu kafoji na wanagundua hilo baada ya mimi kuwatajia majina wanajua ni wangapi wanatumia majina ya kufoji na vyeti vya kufoji ambao sijawataja? Kumbuka nimewaambia ninao 500! Kama nisingewapatia hilo jina wangeweza hata kuanzisha uchunguzi? Kama huo wote sio uzembe na kilele cha ufisadi tuupe jina gani? Next time, kila ninapowapatia majina ya wanafunzi wenye mashaka na wakigundua kuna tatizo itabidi wanilipe! Uzalendo utanishinda na bodi inazo pesa bwelele.

Suala la wanafunzi waliotelekezwa Ukraine na serikali ya Kikwete
Bw. Nyatega kama walivyofanya kina Gesimba, mama Kabaka, na Prof. Msolla amerudia maneno yale yale ya kilaghai kuhusu suala la hawa wanafunzi ili kuzima tuhuma dhidi yao. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa “walichagua kwenda Ukraine kwa taratibu zao wenyewe baada ya kushauriwa kutofanya hivyo. Suala hili limeshatolewa ufafanuzi na serikali na bodi ya mikopo mara kadhaa, hivyo, bodi haina haja ya kutoa maelezo ya ziada”. Kwa bahati mbaya sana, haja ya kufanya hivyo bado ipo.

Kama waliweza kuwapa mikopo vijana Yesse Msechu na Alawi Kihalla waliokubaliwa mikopo 2005/2006 kwenye batch zile zile na hawa 24 ni kitu gani kiliwafanya washindwe kuwapa mikopo hawa wengine? Madai ya kuwa vijana hawa 24 hawakutimiza taratibu fulani licha ya kutengewa mikopo, Bw. Nyatega awaambie watanzania ni taratibu gani hizo ambazo hawakuzitimiza?Na wao kama bado walishindwa vipi kuwasaidia vijana hawa kutatua matatizo hayo ili wasipate matatizo?

Kama vijana hawa waliweza kutafuta tiketi zao na hawakutaka kutumia mikopo ya tiketi, je hilo ni kosa kubwa la kusababisha wasipewe mikopo. Kama mimi ningekuwa Nyatega ningewashukuru vijana hawa kwa kuonesha mfano kuwa familia inaweza kupunguza deni la elimu ya juu kwa kuwatafutia vijana wao nauli badala ya kusubiri mkopo wa serikali. Bw. Nyatega, mwaka 2005/2006 mliwatengewa vijana hawa fedha, na baadaye kwa sababu mnazozijua nyinyi mkawanyima baada ya vijana hawa kununua tiketi zao na kwenda kuanza masomo, tunaomba uwaambie watanzania fedha zao mlizowatengea mwaka ule kiasi cha 72,000,000 ziko wapi?

Bodi na serikali imeendelea kudai kuwa vijana hawa “walishauriwa” wasiende huko Ukraine, lakini hadi hivi sasa haijatolewa sababu ya kwanini walishauriwa hivyo. Sababu ya Bilateral Agreement haiwezi kusimama kwani Yesse na Alawi walienda na wako vyuo hivyo hivyoj walivyokubaliwa vijana hawa. Iweje hiyo Bilateral Agreement iwahusu wanafunzi wote wa kitanzania walioko Ukraine isipokuwa hawa 24. Hawa vijana hawajakubaliwa kusoma sayari Zebaki ambako hatuna Bilateral Agreement nao!

Na katika kudai kuwa bodi iliwashauri wasiende hakuna kiongozi hata mmoja aliyetayari kusema ushauri huo ulitolewa lini, wapi, na nani. Namuuliza Bw. Nyatega na Prof. Msolla, ni barua gani waliyopewa wanafunzi hawa kuwa wasiende Ukraine? Ni tangazo gani la habari na kwenye chombo kipi lililowataka wasiondoke? Je yawezekana kuwa ushauri huo ulitolewa kwa mdomo (verbal) na hakuna maandishi yoyote? Kama lililotolewa kwa mdomo bila maandishi kwanini tusiamaini kuwa ahadi ya wao waendelee na safari nayo iliyotolewa kwa mdomo? Nakupa changamoto bw. Nyatega na wenzako wekeni hadharani ushauri huu ulikuwa upi, ulitolewa lini, wapi, na nani na ulitumwa kwa nani.

Suala la malipo yaliyofanyika Ukraine – uthibitisho wa ufisadi
Katika majibu yake Bw. Nyatega anasema vitu hivi kwamba kuna malipo yaliyofanyika kumhusisha Alawi Rajabu Kihalla yaliyofanyika tarehe 18/4/2006 kwa kupitia hundi namba 193426 yenye thamani ya Shs. 87,772,800 na yakihusisha wanafunzi wengine waliotangulia. Hata hivyo Bw. Nyatega anasema tena kuwa kuna malipo mengine yaliyofanyika 22/3/2006 (mwezi mmoja kabla ya yale ya Kihalla) kwa mwanafunzi David Dennis Kanyika (yakihusisha wanafunzi wengine) yenye thamani ya Shs. 87,772,000 kwa kutumia hundi yenye namba 193426. Jumla ya malipo hayo yote ni Shs. 175,544,800. Kwa kuangalia namba hizo tunakutana na matatizo yafuatayo.

- Namba za cheki zilizotumika ni zile zile. Hilo haliwezekani isipokuwa kama kuna mtu anataka kufanya malipo hewa.
- Kiasi cha fedha kilicholipwa kinakaribiana. Tofauti ni Shs. 800 tu.
- Wanaolipwa ni watu wale wale. Inawezekana vipi uandike cheki mbili zenye kiwango sawa na zenye namba sawa kwa wanafunzi wale wale isipokuwa kama unataka kuweka kiasi kingine pembeni?

Kama hiyo haitoshi, Bw. Nyatega anasema pia kuwa tarehe 19/1/2006 malipo yalifanyika yaliyomjumuisha Yesse Msechu (na wanafunzi wengine) kwa kupitia hundi namba 149736 yenye thamani ya Shs. 80,097,600. Kwa maneno mengine ndani ya miezi minne bodi yetu ya mikopo ililipa Shs. 255,642,400 kwa wanafunzi wasiopungua 85. Tukumbuke kuwa malipo haya yanatokana na bajeti ya 2005/2006. Je. Bw. Nyatenga anaweza kutupa orodha ya wanafunzi wote waliokuwa kwenye mgao wa mikopo ya mwaka 2005/2006 kule Ukraine? Je ana uhakika kuwa hakuna fedha zilizoishia mikononi mwa watu ambao siyo wanafunzi.

Tricky tricky!
Namuomba Bw. Nyatega awaeleze watanzania Bw. Francis kutoka Ubalozi wetu Moscow ni nani na anahusika vipi na malipo ya mikopo. Zaidi ya ya yote awaambie watanzania Bw. Constantine Mkami wa Ukraine anahusika vipi katika mchakato mzima wa wanafunzi wanaosoma pale Ukraine. Asipofanya hivyo kwa ukweli na uwazi nitamsaidia.

Suala la Sera.
Bw. Nyatega anasema kuwa Bodi yake haiko tayari kuwasaidia vijana hawa kwa sababu ya sera. Kuwa ni sera ya CCM kutowasaidia vijana hawa wa Kitanzania ambao walishakubaliwa mikopo kama Kihalla, Msechu Na Kanyika. Anasema kuwa ni sera ya CCM kutambua baadhi ya wanafunzi kwenye kwa sababu ya makubaliano ya nchi mbili na kuwakataa wengine kwa vile hawakutaka mikopo ya tiketi zao. Bw. Nyatega anachosema ni kuwa ni sera ya serikali ya Rais Kikwete kuwabagua vijana hawa kwa vile wameonesha manung’uniko yao hadharani na kudai haki yao hadharani. Na jinsi nilivyomuelewa Bw. Nyatega ni kuwa ni sera ya wana CCM na wabunge wao kutowatetea vijana hawa na kuwatafutia haki yao kwa vile tu wapinzani wamejitokeza kuwasaidia.

Ndugu zangu, sera hii ni ya kibaguzi, kibabe, na ya kizandiki. Ni sera ambayo haina budi kupigwa vita na kila mtanzania mwenye kuthamini elimu na mwenye kujali haki za wananchi. Haiwezekani watu wachache waje na sera mbovu kama hii na sisi tukawafumbia macho. Binafsi nasikitika kuwa hadi hivi sasa hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyejitokeza kuwatetea vijana hawa, hakuna mchungaji, askofu, walimu, NGO, n.k ambao wametaka serikali iwatimizie ahadi yao vijana hawa. Inaonekana tumekubali serikali iwabague vijana wetu kwa vile tu “hawakukamalisha taratibu fulani” za kusadikika. Sera hii ya CCM lazima ivunjwe na iondolewe vitabuni vinginevyo chama chetu kitakuwa kimetiwa tope kubwa na watu wa bodi. Nawashauri viongozi wa CCM waikane sera hii na kuwatendea haki vijana wetu. Vinginevyo, wajiandae kulipa gharama kubwa ya kisiasa.

Siwezi kuamini kabisa kuwa Rais Kikwete, Makamu wake na Baraza zima la Mawazirila serikali yetu limevumilia sera hii ambayo ina harufu ya nchi ya kibaguzi. Siwezi kuamini kuwa Rais anayetaka watu wasome elimu ya juu anafumbia macho suala hili na kuwaacha watuhumiwa wa ufisadi kumpa maelezo ya kilaghai ili kutetea unga wao. Kwa mara nyingine tena, natoa wito kwa Prof. Msolla kujiuzulu, Bodi ya Mikopo kuvunjwa mara moja na tume huru kuundwa kuchunguza ufisadi katika bodi hii. Ni wazi kuwa ni vigumu kwa serikali yetu kufanya hivyo lakini nimekunja vidole vyangu nikiamini kuwa kuna mtu mwenye dhamira safi Ikulu ambayo hakubali uonevu au ufisadi. Vijana hawa wanaonewa na wametelekezwa bure na watu wa bodi. Prof. Msolla anajua hivyo, Mama Kabaka na mama Katunzi wanajufa hivyo, Bw. Mbegu anajua hivyo, na Bw. Nyatega anafahamu hivyo. Na hatimaye leo hii, kila mtanzania anafahamu hivyo.

Kwa vile Bw. Nyatega amenitafutia majibu ya majina niliyoyaweka mwanzoni, nimeonelea nimuongezee majina mengine ili ayatolee ufafanuzi. Kila jina moja waweke kwenye akaunti ya wanafunzi wa Ukraine Shs. Milioni moja.

Rabson Mahenge, alitengewa (allocated) shilingi laki 980,000 pale Muhimbili kusomea Pharmacy (batch 12) na akatengewa shilingi 1,665,000 (batch 10) kwenye chuo hicho hicho kwa kusomea Pharmacy hiyo hiyo. Sasa Bw. Nyatega anaweza kutuambia kuwa pesa ililipwa mara moja. Sawa. Kwanini watenge mara mbili, aidha kuna uzembe wa kiutendaji au kuna mtu anataka “chenji”

Sifa Anyimike, ametengewa shilingi 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM (Batch 10), lakini akatengewa 1,320,000 kusoma hapo hapo UDSM (batch 8). Huyo huyo Anyimike wetu, akakubaliwa kiasi kingine cha Shs. 540,000 kusoma chuo hicho hicho tena (Batch 6).

Helena Yomo. Kwa huyo nayo ni yale yale. Katika Batch 10 alitengewa Shs. 1, 320,000 kusomea Elimu hapo UDSM. Kwa vile bodi yetu ina makengeza ikatenga tena kiasi kama hicho kwenye batch 8. Na kama hiyo haikutosha mwanafunzi huyo huyo chuo kile kile akatengewa tena Shs 540,000 (Batch 6). Inawezekana Bodi yetu ya Bw. Nyatega watakuja na kusema hao UDSM kuna wanafunzi watatu wote wanaitwa Helena T Yomo na wote wanasomea Elimu, na bila ya shaka watasema wamezungumza na chuo na kuthibitishiwa kuwa wanafunzi wote watatu wapo.

Upendo V Chubwa. Huyu katika Batch 10 alitengewa na Bodi ya Nyatega Shs 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM na wakati huo huo kwenye mwaka huo huo alitengewa 1,320,000 (batch 8) kusomea elimu hapo hapo UDSM. Na kwa vile kina Nyatega na wenzake hawajui jinsi kuendesha bodi hiyo wakaona hiyo haitoshi wakaamua kumuongezea tena 540,000 kwenye chuo hicho hicho kwenye kozi hiyo hiyo (batch 6).

Hivi kama si uzembe na uvivu unaweza kuelezea vipi kumtengea fedha mtu mmoja mara mbili kwenye batch ile ile huku jina lake likijirudia. Hii imetokea kwa wanafunzi wawili, Hamisi Mganda ambaye alitengewa Shs. 2,640,000 (DUCE) na Mwaveso Mbwana ambaye alitengewa kiasi kama hicho kwenye batch 10. Sasa kama majina mawili yanayofanana hayawashtui, nini kitawashtua?

Arton Kayombo. Huyu katika Bodi yetu hii ametengewa Shs. 1,320,000 hapo DUCE kusomea Elimu (batch 10) na kupitia bodi hiyo hiyo akatengewa tena kiasi hicho hicho kwenye batch 8. Sasa inawezekana kabisa kuwa mfumo wanaotumia ni mbovi kiasi cha kwamba majina yanajirudia rudia kwa bahati mbaya. Kama hili ni kweli ni kitu gani kinazuia watu wachache kujipongeza kwa fedha za umma?

Ndugu zangu bodi ya Mikopo ina matatizo na uongozi wake mzima hadi Waziri ni mbovu na unaohitaji kubadilishwa. Unganeni nami kumtaka Prof. Msolla na Bw. Nyatega na bodi nzima wakiongozwa na Bw. Mkono wajiuzulu kwa kuzoea uzembe, kuvumilia ufisadi, na kushindwa kuiongoza bodi hiyo ipasavyo. Mimi na wenzangu tumeanzisha utiaji sahihi wa ombi la kutaka Prof. Msolla ajiuzulu. Unaweza kuingia kwenye http://www.jamboforums.com kwa maelezo ya kuweza kusaini ukurasa huo wa kwenye mtandao.

Niandikie: mjengahoja@jamboforums.com
Nitumie ujumbe: + 1 248 686 2010
 
Bravo Mjenga Hoja...

Kikubwa kilichonifurahisha ni kwamba kwa serikali kukataa (au kuchelewa??) kuwalipia hawa wanafunzi, sasa TUMEJUA mengi zaidi.

Kama Mwenyekiti wa Bodi ndiye huyo mheshimiwa, na kutokana na masuala ya utata mkubwa yaliyoibuka yakimhusisha, sasa naelewa pia kwa nini bodi hiyo ina matatizo kiasi hicho, na kwa kweli INABIDI IVUNJWE, na KUUNDWA UPYA.

BTW, wanaanza kutapatapa na kudai kuwa wanataka waliokopeshwa na kushindwa (kukataa??) kulipa washtakiwe! Kwa mwendo huu, wataiweza kazi hiyo????
 
Mwanagenzi, do you think it is coincidental wamekuja na makala hiyo na msimamo huo hii leo?

Wasiolipa makopo chuo kikuu sasa kufungwa (title theirs not mine)

Shadrack Sagati, Dodoma
HabariLeo; Tuesday,July 17, 2007 @00:03

WATAKAOSHINDWA kurejesha mikopo ya masomo katika vyuo vikuu sasa wataweza kufungwa, imefahamika.

Kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Sh milioni saba ni adhabu inayopendekezwa katika muswada wa marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya mwaka 2004 uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana.

Katika muswada huo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu sasa itakuwa na uwezo wa kuwapeleka mahakamani watu wote ambao wamefaidika na mkopo, lakini kwa makusudi wakashindwa kulipa.
Katika marekebisho hayo, inapendekezwa pia kuwa mwajiri atakuwa na wajibu wa kutoa taarifa zinazowahusu wafanyakazi walionufaika na mikopo ili kuepuka kushtakiwa.

Pia kuna hatua ambazo zitachukuliwa kuwadhibiti waajiri na wanafunzi walionufaika na mikopo, lakini wakashindwa kutoa taarifa ya namna ya kulipa mkopo huo.

Hatua hizo ni mtu yeyote ambaye amemwajiri aliyefaidika na mkopo wa bodi hiyo, halafu akashindwa kutoa taarifa kwa bodi ili kutoa utaratibu wa kufanya malipo, mtu wa namna hiyo atakuwa amefanya kosa la jinai na anaweza kutozwa faini ya Sh milioni saba au kwenda jela mwaka mmoja.

Na kama mwajiri, ni shirika au kampuni, mtendaji mkuu au mtu yeyote ambaye ni ofisa maduhuli wa shirika husika, ndiye atakayehusika na adhabu hiyo.

Na kwa makusudi ya kifungu hicho ili kiweze kutekelezeka, sheria ya makampuni inayowalinda watendaji wake kushtakiwa binafsi, haitahusika katika suala hilo la mikopo, muswada unaeleza.

Katika muswada huo, pia inapendekezwa kuwa mwajiri ambaye ameajiri mtu aliyesomeshwa kwa fedha za bodi hiyo na akashindwa kutoa taarifa kwa bodi kama sheria inavyomtaka, bodi itakuwa na mamlaka ya kudai shirika hilo kulipa kiasi chote anachodaiwa mkopeshwaji aliyeajiriwa.

Pia inapendekezwa kuwa mtu ambaye atakuwa kikwazo atakayemzuia ofisa wa bodi au wakala wa bodi hiyo ambaye atakuwa ameteuliwa kufanya kazi kwa niaba ya bodi asitekeleze majukumu yake chini ya sheria hiyo mpya, atakuwa ametenda kosa la jinai na atapelekwa mahakamani na akipatikana na hatia, atalipa faini ya Sh milioni saba au kwenda jela si chini ya mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Maofisa wa bodi au mawakala wake watakuwa na mamlaka ya kufanya ukaguzi rekodi zozote kwa taasisi, makampuni, mashirika yanayoajiri kupata taarifa ya watu waliosomeshwa kwa fedha za bodi hiyo.
Katika sheria hiyo, pia bodi itakuwa na uwezo wa kufungua mashitaka mahakamani ndani ya miaka 10 tangu mhusika achukue mkopo kwa bodi hiyo.

Kiasi ambacho mkopaji atatakiwa kulipa baada ya kupata ajira kitapendekezwa na bodi hiyo kutokana na kipato chake, lakini pia kuna kifungu kinachopendekeza kuwa malipo hayo yasizidi theluthi moja ya pato halisi (net) ya mkopaji.

Katika sheria hiyo mpya, bodi ndiyo itakayokuwa inapendekeza kiasi au asilimia ambayo itamkopesha mkopaji na kiasi ambacho mkopaji, mlezi au mzazi atachangia kutokana na ada ya taasisi husika.
Kwa sasa, bodi hiyo inatoa asilimia 60 ya mkopo na mzazi au mlezi analazimika kuchangia asilimia 40.

Kiasi hicho kimelalamikiwa na wanafunzi, wazazi na wanasiasa kuwa ni ukiukwaji wa sheria hiyo.

Wakati fulani vyama vya siasa vya upinzani vilikuwa na mpango wa kufungua kesi mahakamani kupinga utaratibu huo wa serikali kuwa unapingana na sheria husika.

Lakini pia sheria hiyo itaipa mamlaka bodi hiyo, kufuta mkopo na kutaka mkopaji kurejesha fedha ambazo atakuwa amekopeshwa awali katika mkupuo mmoja, itakapobainika kuwa alitoa taarifa za uongo wakati wa kuomba mkopo husika ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashitaka.

Bodi itafanya hivyo chini ya amri ya 35 ya sheria ya mwenendo wa kesi za madai kwa urejeshaji wa mikopo.

Pia inapendekezwa kuwa mwajiri atakuwa na wajibu wa kutoa taarifa zinazowahusu wafanyakazi walionufaika na mikopo kuepuka kushtakiwa Licha ya muswada huo, serikali pia iliwasilisha muswada mpya wa sheria ya utalii wa mwaka 2007 na muswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya utumishi wa umma mwaka 2007 ambayo yote ilisomwa jana kwa mara ya kwanza.
 
Du kweli wewe mwana kijiji kiboko, Jamaa imebidi wa admit though indirectly kwamba wametafuna!!!. Mfano wanasema kasoro zimerekibishwa kwa ''kiwango kikubwa''!!!. sentensi hii ina maanisha mambo mawili. kwanza ni kweli kasoro zilikuwepo kama mwanakijiji alivyosema, pili kasoro hizo hazijarekebishika kwa kiwanngo cha asilimia mia, ila kwa ''kiwango kikubwa''. Kwa maneno mengine, fedha ambazo mwanakijiji anasema zimetafunwa ni kweli zimetafunwa ila wamejaribu kurekebisha kwa kiwango kikubwa. Sasa hizo nyingine kwa maana hiyo haziwezi kupatikana maana watu wameshajengea maghorofa mbezi!! au vipi wadau???. Sasa hii nchi kwa kweli inatuchanganya. Msemo wa General ulimwengu ''kila mtu na ka muogo kake'' yaani wako radhi watoto wafe Ukraine kwa simple maelezo tu ''kasoro zimerekebishwa kwa kiwango kikubwa''!!!!!!!!. that is damned ......!! nitatukana bure ngoja niache
 
Bwana mdogo wengi ndivyo tunavyochukulia mambo hayo. Hivi kama mmjj asingeweka majina hayo hadharani tungejua kuna watu wametokomea na mikopo?
 
Back
Top Bottom