Attention Bodi Ya Mikopo Ya Elimu Ya Juu Kwa Wanafuzi(HESLB)

Mimi nitasema hata wanune.

Elimu inatupa maarifa.
Maarifa yanatuwezesha kukabiriana na matatizo yetu ya kila siku.
Hatahivyo Kuna baadhi ya matatizo tutaendelea kupambana nayo hadi siku ya kufa lakini mengine yana ufumbuzi wa kudumu.
Kwa mfano kila baada ya masaa kadhaa chini ya 6 tunasikia njaa na kwa hiyo tunapata mlo kama hali inaruhusu. kwa hiyo kila baada saa 6 tuna tatizo linalojirudia. Kuleta ufumbuzi wa kudumu inabidi tuwe na akiba ya chakula ya uhakika ndani ya famila jamii na taifa kwa ujumla.
Ili kuongeza mavuno ya chakula tunabadiri namna ya kulima tunaachna na jembe la mkono nakutumia mashine. Pia tunaachna na utegemeziwa mvua tuna zidisha nguvu katika kilimo cha umwagiliaji.
Hata tukiwezakutatua tatizo la ukubwa wa hifadhi ya chakula hatuwezi kutatua tatizo la kuumwa njaa kila baada ya masaa 6.

Siku zote ili kutatua Matatizo haya yenye ufumbuzi wa kudumu ni lazima tuwe na maarifa.
Maarifa hayaji ila kwa kuzingatia Elimu.
Katika Dunia hii ya Utanda wazi elimu ni pana kama ulimwengu wenyewe, Siongelei Dunia naongelea ulimwengu.Dunia ni kipande kidogo tu cha mwamba kinachoelea kwa kasi kulizunguka Jua kikiwa katika seti ya vipande vingine 7. Ulimwengu ni kila kitu kilichowahi kuweko,kilichopo na kitakacho kuwepo. Ulimwengu unajumuisha hata vitu ambavyo akili ya mtu yeyote haijawahi hata kuvifikiria.Kifupi Elimu ni pana sana sana.

Utashangaa kwa nini nchi za ulimwengu wa kwanza zinatumia Mabilioni ya Dola kujenga Space Station, japokuwa mpango mzima wa ujenzi umekuwa ukikumbwa na ajari nyingi za vyombo vya kusafiria kwenda kwenye ulimwengu usiofikika na nchi masikini kama Tanzania.

Kwa nini wanatumia mabilioni ya dola kujenga Space Station?

Utashangaa sana kwa nini wenzetu wanatuma vyombo kwenye sayari nyingine kama Mars kuchunguza mambo lukuki na kinawauma sana wanaposhindwa kupata jibu nini kilitokea huko kwenye dunia nyingine mpaka dunia hizo zikawa kama zilivyo.

Utashanagaa wanavyojitolea muhanga kuzama na vyombo maelfu ya mita chini ya bahari karibu na chemchem za volkeno kuu za bahari kuchunguza maajabu ya viumbe wanaishi katika maji ya joto kali bila mwanga wa jua.

Sasa utashangaa zaidi unaposikia Rais wa nchi Mawaziri wake Bunge na wa tendaji wa serikali ya CCM wanapoimwagia radhi Elimu kwa makalio yao wazi kama wanga.

Ni kweli MH Kikwete anataka kujenga Univeristy mpya huko Dodoma lakini je University ya dar mahali pekee alipo wahi kupatia elimu yake ya juu kabisa anapashughulikia vipi???

Wanafunzi zaidi ya 500 darasa kwenye darasa lililojengwa kukaa wanafunzi 120.
Wanafunzi wa Chuo kikuu wanakaa chini na yeye mkuu wa nchi na Alumina wa UDSM naona ni sifa kubwa sna kwa chuo chake.

Chuo kikuu cha DSM kupanuliwa kwa kuongeza idadi ya Wanafunzi na siyo majengo, walimu na vifaa vya kufundishia na MH Mkuu wa Chuo MH Kikwete anaona hilo ni jambo lakujivunia kabisa.

Kuharibu utaratibu mzima wa Elimu ya sekondari kwa sababu ambazo hata jemadari wa uharibifu mwenyewe MH Mungai hazimwingii.
Mwl Nyerere alimpendekeza MH Mkapa kuwa Rais.Mkapa alishika madaraka kipindi chote cha miaka 5 kwa adabu. Mzee wake alipofariki akawarudisha Manyang'au wote ambao aliyempendekeza alijua hila zao na ukosefu wao wa shukurani kwa Watanzania.

Mfano kuna huyu mtu mjinga sana anaitwa Joseph Mungai, mwizi katika historia yake ya kuwa Waziri mpaka alifukuzwa kazi na mwalimu Nyerere miaka 1978 na pia mjanja wa kuongea na kipofu wa akili. Mtu huyu katika muda aliokaa kuwa waziri wa Elimu ameipa elimu ya msingi na sekondari kilema cha maisha. Mungai alirudia makosa yaliyofanywa na serikali miaka ya 60 ya kufuta baadhi ya mitara ya elimu na lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia na mfumo mzima wa elimu.
Mungai alirudia kosa hili tena kwa sababu yeye hana chochote cha kupoteza au hata kama anacho hajari.
Huu ni mfano mojawapo wa watu hatari ambao wameachiwa kurandaranda kama Fisi Wachoyo ndani ya Corridor za utawala wa CCM. Wanakazi moja tu kuharibu.
Hata hapo alipo sasa hivi anaharibu tu kwani huyu jamaa kila siku kama walivyo watendajiwengiwa serikali ya CCM wanaweka mambo mazuri pembeni na kuongoza kwa hisia na ujanjaujanja.

Hatuweiz kuidharau Elimu hata kidogo kwa sababu elimu haidharauriki.
Ni gharama kubwa mno mno isiyoandikika kwa tarakimu kujaribu kuidharau au kuidharirisha na kuipa makalio elimu.

Watanzania wengi tuna tatizo moja tunashindwa kutofautisha elimu na fedha.
Kwa sababu tunawajua watu wengi pale Tanzania wanye fedha lakini hawana elimu ya kuingia darasani na wengine hata kusoma hawajui; pia tunawajua watu wengi ambao wana elimu kubwa sana lakini hawana fedha ya kutakata na hata mambo yao mazuri wanayo yafanya tunayadharau tunadhani pengine ni bora tukose elimu lakini tupate fedha.

Yule nabii na mfalme wa Uyahudi ya kale Mfalme Solomoni alikaa akaugua akalia kuomba Mungu wake ampe Hekima. Kwa hekika aliyopewa alifanya mambo mengi makuu.
Nijuavyo mimi hekima iko juu ya kila kitu.
Hekima ndiyo imewafanya watu dhaifu kuwa na nguvu na kuyageuza mahusiano yao na dunia inayowazunguka na watu wa jamii nyingine kuwa imara zaidi.
Siku zote mtu anaye itafuta elimu ya kweli ataishia kuwa na hekima.

Labda niseme pengine viongozi wetu hawaidharau elimu ila wanaidharau na kuudharirisha mfumo wa kuwapa elimu watanzania ili kuendeleza tabaka lao la uongozi.
Ni rahisi sana kuwatawala watu waiso na elimu au wenye elimu nusu au wanao dhani wameelimika ipasvyo wakati wamepewa kivuli cha elimu halisi.

Tunajua kabisa huwezi kwenda maeneo yenye wasomi wengi kama uchaggani Uhayani na Unyakyusani na kutoa maamuzi mbuzi kabla hawajakujia juu.
lakini sehemu zote ambazo hazina wasomi na elimu iko chini wananchi mpka leo wanaburuzwa bila huruma kwa maamuzi ya kisiasa na hata pengine ardhi yao kutaifishwa na serikasli na kupewa wageni.

Loliondo imeuzwa kwa muarabu kama vile haina mwenyewe.

Kule zanziba kuna kisiwa wamepewa wauza madawa ya kulevya awanatua na ndege na kuruka kama serikali ya tanzanaia haipo kabisa.

Kule kwa MH Marmo ndugu zake wamenyang'nywa ardhi ili apewe mwarabu kutengeza viwanja vya kucheza polo na mbio za farasi. MH Marmo yupo elimu yake kaifyata sijui yeye dau lake ni Shs ngapi au tu Waarabu wesha mcheza mchezo mbaya.

historically Waarabua wanadai tanganyika yote ni yao nakwa kawaida muarabu ukimpa ardhi anasema ardhi hiyo ni mali yake milele. Wewe hebu fikiria kwa vile utawala wa Ottoman uliteka Spain mpaka leo wandai ni sehemu ya Himaya ya Waarabu na uislamu. hapa naona wanchanganya uarabu na Uislamu nijuavyo mimi si kila muarabu ni muislamu.
Kesho ninyi akina Marmo msishangae kusikia kwamba ardhi yote ya Whadzabe ni mali ya waarabu na Uislamu.

Hawa watu wanafanya mambo yote haya kwa vile wanajua kwamba sisi tuko bussy na vijisenti vya Rushwa. Pesa kidogo tu tunauza ardhi yetu ya asili.

Mimi nikizunguka state zote za marekani sioni kipande cha ardhi cha kuwapa Wahadzabe ambao wananyang'anywa ardhi na serikali yao.
Hata Marmo mwenyewe akija huku na hivyo vipesa vyake sijui kama ataweza kusurvive hata miaka 2.

Kingine hivi hawa waarabu tunawaamini nini leo wakati ni juzi tu wao na wazungu lao lilikuwa moja.
Tunajuaje siku moja watatuletea camp za materorist ndani ya nchi zetu?
Huu ukosefu wa elimu na hikima unatuletea Kiama.

Kuna kitu wazungu hapa Marekani wanakiita " The tragedy of Common".
Kwaumfano uchafuzi wa bahari
Uchafuzi wa hewa yaani anga.
Uchafuzi wa ardhi kumwaga oili kila mahali.
kukata misitu

Wanaita The tragedy of common kwa vile madhara yanakuwa ya kila mtu ikiwa ni pamoja na wewe mtendaji.

Kukosa elimu sahihi na hekima si tatizo la mtu binafsi ni tatizo la jamii nzima.

Kunamengi sana ya kuongea na ningeomba wengine nao wachangie.
 
HIGHER EDUCATION STUDENTS’ LOANS BOARD
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu


TAARIFA YA KWA UMMA KUHUSU SHUTUMA ILIYOTOLEWA NA GAZETI LA KULIKONI LA JULAI 9-15, 2007 YENYE MADA “TWAWEZA KUMUAMINI PROFESA MSOLLA? Uozo wa Bodi ya Mikopo kilele cha ufisadi”.


1.0 UTANGULIZI

Tarehe 09 Julai, 2007 gazeti la Kulikoni la tarehe 9 - 15/07/2007 lilitoa tuhuma kaika ukurasa wa 3 na wa 9 dhidi ya Mhe. Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Peter Msolla na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu likidai kwamba hakuna kinachofanyika na wala hakioni mafanikio yoyote ya Wizara na Bodi, jambo ambalo siyo kweli. Aidha, mwandishi wa gazeti hilo alitoa mifano kadhaa ya majina ya wanafunzi ambao walipangiwa kupewa mikopo katika vyuo tofauti tofauti na kudai kwamba kwa kufanya hivyo tu Bodi na Wizara zimeshindwa kufanya kazi. Kwa sababu zisizoeleweka, mwandishi huyo hakutaka kuendelea na uchunguzi wake kubainisha kama hao wanafunzi waliopangiwa kupewa mikopo, je walipewa hiyo mikopo au la. Pia mwandishi huyo anajaribu kuibua tena suala la wanafunzi 26 waliojipeleka wenyewe Ukraine. Bodi inapenda kutoa maelezo kama ifuatavyo hapa chini:-

2.0 HAJA YA KUTOFAUTISHA KATI YA KUPANGIWA MKOPO ( LOAN ALLOCATION) NA KUPEWA MKOPO (LOAN DISBURSEMENT)


2.1 Kwanza kabisa tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya kupangiwa kupewa mkopo (Loan Allocation) na kupewa mkopo ( Loan Disbursement), vitu ambavyo mwandishi wa gazeti la Kulikoni amevichanganya, ama kwa kutokujua au kwa makusudi, ili akidhi azma yake ya kuchafua majina ya watu.

Bodi ingependa ieleweke kwamba kupangiwa kupewa mkopo (Loans Allocation) hufanyika mwanzoni mwa mwaka wa masomo, baada ya Bodi kupata matokeo ya udahili kutoka vyuo vya elimu ya juu na pia kutoka kwa Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tanzania Commission for Universities - TCU). Baada ya uchambuzi wa waombaji, kulingana na vigezo, Bodi hupanga mikopo kwa kila mwombaji kwa kila Chuo na taarifa hiyo hutolewa kwa njia ya tovuti ya Bodi ili iwafikie wahusika wote. Taarifa kama hizo ambazo ziko katika tovuti ya Bodi ndizo mwandishi wa gazeti la Kulikoni amezitumia kuandaa shutuma zake, jambo ambalo siyo sahihi kwani baada ya kufanya “Loan Allocations”, Bodi huendelea na uchambuzi zaidi kabla ya kufanya malipo “Disbursements”. Mwandishi huyo angeisaidia sana Bodi na Taifa kwa ujumla kama angetumia taarifa za “Disbursements” na siyo hizo za “Allocation” alizotumia. Taarifa za “Loan Disbursements” hazipatikani katika tovuti, hivyo, ni budi mwenye shida nazo awasiliane na Bodi.

Pamoja na maelezo hayo, Bodi inakiri kwamba kutokana na mkanganyiko wa “Double Admissions” katika vyuo vikuu mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa 2006/2007 kulitokea “Double Loan Allocations” ambazo hata hivyo yalisahishwa kwa kiwango kikubwa wakati wa kufanya malipo (Loan Disbursements).

Mapungufu hayo yalitokana na sababu zifuatazo:-

(i) udahili zaidi ya mara moja (Multiple Admission)

Katika mwaka wa masomo 2006/2007 wanafunzi wa mwaka wa kwanza walipewa udahili na vyuo zaidi ya kimoja na wanafunzi hao waliriporti katika vyuo hivyo na baadae kuhamia vingine. Aidha Bodi ilipata majina baadaye kuthibitisha wanafunzi halisi waliopo katika vyuo hivyo.

(ii) Muda mfupi wa kuchambua majina ya waliodahiliwa kabla ya kufunguliwa kwa vyuo.

Vyuo vingi vya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2006/2007 vilitoa orodha ya majina ya wanafunzi waliodahiliwa siku chache kabla ya vyuo kufunguliwa. Hivyo, Bodi haikupata muda wa kutosha wa kufanya uchambuzi wa kina.

(iii) Kutokuwepo kwa namba maalum (Unique Number) ya kutofautisha wanafunzi, hususan pale majina ya waombaji mikopo yanapofanana.


2.2 Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, imeshachukua hatua ya kubainisha kama kulikuwa na ulipaji hewa wa mikopo ya wanafunzi au “Double Payments” na kazi hii imepewa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Prevention of Corruption Bureau– PCB) ambayo inaendelea na uchunguzi na endapo itagundulika kuwa kweli basi hatua zifaazo zitachuliwa ipasavyo.






3.0 UCHAMBUZI WA MIFANO ILIYOTOLEWA NA MWANDISHI WA GAZETI LA KULIKONI

Bodi ya Mikopo inapenda kutoa taarifa ya malipo yaliyofanyika kwa wanafunzi waliotajwa na gazeti la Kulikoni kama ifuatavyo:-

(i) Wanafunzi Yesse Cornelio Msechu na Alawi Rajabu Kihalla wanaosoma Ukraine.

Yesse Cornelio Msechu aliidhinishwa kupata mkopo katika Batch Na 7 ya tarehe 4/12/2005 na kukopeshwa tiketi ya kusafiria ya tarehe 29/12/2005. Malipo yake ya mkopo yalifanyika kwa hundi Na 149739 ya tarehe 19/01/2006 yenye thamani ya Tshs 80,097,600 ambayo pia ilijumuisha malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia.

Mwanafunzi Alawi Rajabu Kihalla aliiidhinishiwa kupata mkopo Batch Na 7 ya tarehe 4/12/2005, na baada ya kutimiza taratibu zote alikopeshwa tiketi ya ndege iliyoonyesha kuwa angesafiri tarehe 21/02/2006. Malipo ya mkopo wake yalifanyika tarehe 18/4/2006 kwa hundi na 193426 yenye thamani ya Tshs 87,772,800 iliyojumuisha pia malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia.

Kwa maelezo haya, ni dhahiri kuwa hawa ni wanafunzi halali waliotimiza masharti yote ya kukopeshwa na Bodi ya Mikopo kwa mwaka 2005/2006, hivyo, kwa mwaka 2006/2007 hao ni wanafunzi wanaoendelea na masomo.

(ii) Mwanafunzi Mushi, Adiel D.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Bodi, mwanafunzi huyu anasoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako malipo yake ya jumla ya Tshs 1,752,175.00 yamefanyika. Hakuna malipo ya mkopo yaliyofanyika kwa jina la mwanafunzi huyo nchini Ukraine kama ilivyodaiwa. Aidha, COET wamethibitisha kuwa huyu ni mwanafunzi wao na yuko chuoni. Hivyo, madai ya mwandishi wa gazeti la Kulikoni kwamba amekopeshwa T.shs 5,640,000/= ni uzushi ambao malengo yake anayaelewa mwandishi mwenyewe.






(iii) Mwanafunzi David Denis Kanyika

Mwandishi wa gazeti la Kulikoni anaituhumu Bodi ya Mikopo kwa kumkopesha David Dennis Kanyika na kumkatalia mkopo Ramadhani Nyello ambaye inadaiwa walikwenda pamoja na Kanyika nchini Ukraine.

Kumbukumbu za Bodi zinaonyesha kuwa David Dennis Kanyika alitakiwa kusafiri kwenda Ukraine tarehe 11/02/2006 na malipo ya mkopo wake yalifanyika tarehe 22/03/2006 kwa hundi Na. 193426 yenye thamani 87,772,000.00 ambayo ilihusisha pia malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia. Kwa maelezo haya David Denis Kanyika ni mwanafunzi anayeendelea na masomo nchini Ukraine na kwa mwaka 2006/2007 amekopeshwa jumla ya Tshs 3,000,000.00.

(iv) Wanafunzi Charles J. Temba na Charles Joseph Temba

Kumbukumbu za Bodi zinaonyesha kuwa Charles J. Temba anayesoma SUA ambako amelipwa jumla ya Tshs 1,549,300.00 ni mwanafunzi tofauti na Charles Joseph Temba anayesoma MIST ambaye naye amekopeshwa jumla ya Tshs 1,995,600.00. Aidha Bodi imefuatilia kwa simu katika vyuo hivi na kuthibitishiwa kuwa wanafunzi hao wawili wapo katika vyuo husika.

Kuhusu Charles J. Temba aliyepangwa kusoma Chuo Kikuu Mzumbe, ni kwamba, mwanafunzi huyo hakufika Chuoni hapo na fedha zilizo pelekwa kwa jina lake Tshs 1,553,000 zimerejeshwa katika Bodi.

Aidha, Bodi inaendelea na uchunguzi kubainisha kama vyeti vilivyotumika kumdahili Charles J. Temba wa SUA ni vilevile vilivyotumika kumdahili Charles Joseph Temba wa MIST au la. Ikibainika kwamba kulikuwa na udanganyifu, hatua za kisheria zitachukuliwa.

(v) Mwanafunzi Charles B. Temba

Kutokana na kumbukumbu za Bodi, mwanafunzi huyu ni tofauti na Charles J. Temba wa SUA na Charles Joseph Temba wa MIST. Huyu mwanafunzi anasoma Chuo Kikuu cha Arusha na amekopeshwa jumla ya Tshs. 1,917,600.00.


(vi) Mwanafunzi Salim J. Chadoe

Mwanafunzi huyu alidahiliwa kwanza mwezi Agosti, 2006 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadae kupata skolashipu ya Serikali (Bilateral Agreement), kwenda kusoma Algeria mwezi Oktoba mwaka 2006. Malipo pekee yaliyofanyika kwa jina la mwanafunzi huyu ni Tshs 3,000,000.00. nchini Algeria. Hivyo, madai kwamba amelipwa mara kadhaa siyo kweli.


(vii) Wanafunzi Alistidia J. Rupia, Kazinja Patrick E, Ligunda Mary, Sophia Sokoni na Mohamed Matwera

Wanafunzi hawa walidahiliwa mwezi Agosti, 2006 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam isipokuwa Sophia Sokoni ambaye alidahiliwa UCLAS na Mohamed Matwera ambaye alidahiliwa MUCHS.

Kumbukumbu za Bodi zinaonyesha kuwa wanafunzi hawa walifika vyuoni na kuanza masomo katika vyuo hivyo ambapo Bodi ya Mikopo iliwakopesha malipo kwa ajili ya Semester I kama ifuatavyo:-

 Alistidia J. Rupia Tshs. 475,000.00
 Kazinja Patrick E Tshs. 535,000.00
 Ligunda Mary Tshs. 535,000.00
 Sophia Sokoni Tshs. 0.00
 Mohamed Matwera Tshs. 295,000.00

Baadae Mwezi Oktoba 2006, wanafunzi hawa walipata skolashipu ya Serikali (Bilateral Agreement) kwenda kusoma kozi mbalimbali nchini Algeria, ambako Bodi iliwakopesha tena kama ifuatavyo:-

 Alistidia J. Rupia Tshs. 2,705,000.00
 Kazinja Patrick Tshs. 2,705,000.00
 Ligunda Mary Tshs. 2,705,000.00
 Sophia Sokoni Tshs. 2,705,000.00
 Mohamed Matwera Tshs. 2,705,000.00

Hatua ya kuwakopesha wanafunzi hawa tena kusoma Algeria baada ya kuwa wamepokea fedha kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilichukuliwa ili kuwezesha nafasi za masomo zilizotolewa na Algeria chini ya Mkataba wa mashirikiano ziweze kutumika. Vinginevyo nafasi hizo zingepotea bure kwa vile mchakato wa kuwapata wanafunzi hao huwa unachukua muda mrefu (wastani wa miezi 4) kabla ya wanafunzi kuondoka.

Aidha, Bodi itakata fedha hizo walizokopeshwa awali wakiwa vyuo vya hapa nchini kutoka katika malipo yatakayofuata mwaka wa masomo wa 2007/2008.

(viii) Mwanafunzi Nyamhanga Msabi Mwita na Mwita Msabi

Kumbukumbu za Bodi zinaonyesha kuwa hawa ni wanafunzi wawili tofauti ambapo Nyamhanga Msabi Mwita anasoma SAUT na amekopeshwa jumla ya Ths 2,382,000.00 wakati Mwita Musabi yuko China kwa skolashipu ya Serikali (Bilateral Agreement) na amekopeshwa jumla ya Tshs 9,247,045.00

(ix) Mwanafunzi Exaud Chengule

Mwanafunzi huyu alidahiliwa DUCE na TUICO, na kulipwa kwa semester I pekee katika Chuo cha DUCE kiasi cha Tshs 954,000.00. na inaelekea ametelekeza masomo yake katika Chuo cha DUCE. Jitihada zinaendelea kumtafuta ili arudishe fedha alizokopeshwa.

(x) Wanafunzi Emmanuel Richard Kizigha na Emmanuel Richard Kizigha

Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa hawa ni wanafunzi wawili tofauti mmoja akiwa anasoma CBE na mwingine yupo UKRAINE. Wanafunzi hawa tayari wamewasilisha fomu za maombi ya mikopo kwa mwaka 2007/2008 zenye picha tofauti. Emmanuel Richard kizigha wa CBE amekopeshwa Tshs 2,133,000.00 wakati yule wa Ukraine amekopeshwa Tshs 3,000,000.00.

Aidha uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mwanafunzi Emmanuel Richard Kizigha anayesoma Ukraine huenda anatumia vyeti visivyo halali kwani index namba ya mtihani wa kidato cha nne na cha sita si sawa na index namba za shule alizodai kuwa amesoma ( Form Four S.0126/0025 kamaliza mwaka 2000 Magamba Secondary, Form six S.0671/0577 kamaliza mwaka 2003 Ubungo Islamic Higher School). Hali halisi inaonyesha kuwa S.0671 ni ya Shule ya Sekondari Pwani na S.0126 ni ya Lutheran Junior Seminary. Uchunguzi unaendelea na ikibainika alidanganya atachukuliwa hatua kali za kisheria.


4.0 MADAI MENGINE YA MWANDISHI WA GAZETI LA KULIKONI

Mwandishi wa Kulikoni anadai kwamba ana orodha ya majina 500 ya “ waliokubaliwa mikopo ya karibu wastani wa shilingi Millioni Sita” kila mmoja. Bila shaka orodha aliyo nayo itakuwa inatokana na orodha ya “Loan Allocations” ambayo siyo “issue” kubwa sana kama anavyotaka ieleweke kwa umma. Kupangiwa kupewa mkopo ni kama “Indicative Allotment” tu kwa waombaji. Hivyo, mtafiti yeyote atakayetumia muda wake mwingi kuchambua taarifa hizo za “allotment” ataishia kutoa “Conclusions” ambazo siyo sahihi, hasa anapotaka kuzionyesha kama ndiyo mikopo iliyotolewa.

5.0 SUALA LA WANAFUNZI 26 WALIOJIPELEKA WENYEWE UKRAINE

Mwandishi wa gazeti la Kulikoni anajaribu kuibua suala la wanafunzi waliojipeleka Ukraine kwa kutoa taarifa za kupotosha kwamba; kwa vile baadhi ya wanafunzi walipangiwa mikopo zaidi ya chuo kimoja na hawakufika katika vyuo hivo, basi, Bodi ya Mikopo na serikali zina fedha za kuweza kuwakopesha wanafunzi 26 waliokwama Ukraine.

Kwa manufaa ya mwandishi wa gazeti la Kulikoni, na Umma kwa ujumla, suala la msingi linalozungumziwa sio tu ukosefu wa fedha za kuwalipia wanafunzi hao 26 walioko Ukraine bali pia ni suala la kisera. Kwa sera zilizopo, Bodi ya Mikopo haikopeshi tena wanafunzi wa elimu ya juu kusoma nje ya nchi, isipokuwa wale wanaokwenda kusoma kutokana na makubaliano ya serikali ya Tanzania na nchi marafiki. Wanafunzi hao 26 walichagua kwenda Ukraine kwa taratibu zao wenyewe baada ya kushauriwa kutofanya hivyo. Suala hili limeshatolewa ufafanuzi na Serikali na Bodi ya Mikopo mara kadhaa, hivyo, Bodi haina haja ya kutoa maelezo ya ziada.


Imetolewa na


Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
 

Attachments

  • hoja ya gazeti la kulikoni final.doc
    81 KB · Views: 136
Nitaichambua ripoti hii vizuri hapo baadaye, lakini ngoja nijibu hili dogo hapa.

iii) Kutokuwepo kwa namba maalum (Unique Number) ya kutofautisha wanafunzi, hususan pale majina ya waombaji mikopo yanapofanana.

Wanafunzi wote wanaomaliza form 6 wana unique examination numbers ambazo huanza na S. kwa nini wasizitumie hizo?
 
jamani niwajibu au niache mtoto mdogo awajibu..?

Watoto wataharibu mtiririko. Wewe wape vidonge vyao tena kwenye gazeti la Kulikoni huko huko.
Shenzi taipu kabisa hawa, allocation na disbursement ndio utumbo gani?
Haya maelezo yanaacha maswali mengi zaidi ya majibu. Kitu cha haraka haraka nilicho note hapo ni kuwa kwa wanafunzi wa Ukraine zimeandikwa cheki tatu. Moja ya tarehe 19/01/2006 namba 149739 thamani 80,097,600. na assume ni tsh. Pili check namba 193426 ya tarehe 22/03/2006 tsh 87,772,000 na mwisho check namba 193426 ya tarehe 18/04/2006 tsh 87,772,000. Jumla hapa ni 255,641,600 ! Je hizi ndizo fedha walizopewa wanafunzi wa Ukraine?
Kama sivyo ni kivipi kuwa na check tatu tofauti kwa watu walewale. Hawawezi kusema kwamba ni check ileile kwanza kwa sababu figure zinatofautiana zile za check mbili na ile nyingine. Pia tarehe za check zinatofautiani kwenye check yenye namba 193426. Iweje check yenye namba moja iandikwe katika tarehe mbili tofauti?
Aliyetoa majibu hayo ajaribu tena hapa bado kabisa hajaeleweka.
 
Watoto wataharibu mtiririko. Wewe wape vidonge vyao tena kwenye gazeti la Kulikoni huko huko.
Shenzi taipu kabisa hawa, allocation na disbursement ndio utumbo gani?
Haya maelezo yanaacha maswali mengi zaidi ya majibu. Kitu cha haraka haraka nilicho note hapo ni kuwa kwa wanafunzi wa Ukraine zimeandikwa cheki tatu. Moja ya tarehe 19/01/2006 namba 149739 thamani 80,097,600. na assume ni tsh. Pili check namba 193426 ya tarehe 22/03/2006 tsh 87,772,000 na mwisho check namba 193426 ya tarehe 18/04/2006 tsh 87,772,000. Jumla hapa ni 255,641,600 ! Je hizi ndizo fedha walizopewa wanafunzi wa Ukraine?
Kama sivyo ni kivipi kuwa na check tatu tofauti kwa watu walewale. Hawawezi kusema kwamba ni check ileile kwanza kwa sababu figure zinatofautiana zile za check mbili na ile nyingine. Pia tarehe za check zinatofautiani kwenye check yenye namba 193426. Iweje check yenye namba moja iandikwe katika tarehe mbili tofauti?
Aliyetoa majibu hayo ajaribu tena hapa bado kabisa hajaeleweka.

jamaa aliyejibu anaweza akaja na excuse ya typing error!
 
hebu someni majibu hayo na nipeni mawazo ya vitu mlivyonoti ambavyo Havi"click" maana two heads are better than one.
 
Unajua tatizo la waswahili bwana wakikamatwa wizi wanajaribu kutumia Kiingereza kujaribu kuwachahganya watu.Hapa umedunda.Hapo bila wasiwasi ni wizi uliofanyika.Wametumia majina ya hao wanafunzi kuomba na kupitisha fungu hilo la mikopo na baada ya kupata fungu hilo wakaamua kuzitafuna hizo pesa."Kuzi-disburse katika matumbo yao.Haya ndo yaleyele Haki elimu wanayoyazungumzia.Wakati utafika tutaanza kuwachoma moto nyie.
 
[QUOTE
3.0 UCHAMBUZI WA MIFANO ILIYOTOLEWA NA MWANDISHI WA GAZETI LA KULIKONI

Bodi ya Mikopo inapenda kutoa taarifa ya malipo yaliyofanyika kwa wanafunzi waliotajwa na gazeti la Kulikoni kama ifuatavyo:-

(i) Wanafunzi Yesse Cornelio Msechu na Alawi Rajabu Kihalla wanaosoma Ukraine.

Yesse Cornelio Msechu aliidhinishwa kupata mkopo katika Batch Na 7 ya tarehe 4/12/2005 na kukopeshwa tiketi ya kusafiria ya tarehe 29/12/2005. Malipo yake ya mkopo yalifanyika kwa hundi Na 149739 ya tarehe 19/01/2006 yenye thamani ya Tshs 80,097,600 ambayo pia ilijumuisha malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia.

Mwanafunzi Alawi Rajabu Kihalla aliiidhinishiwa kupata mkopo Batch Na 7 ya tarehe 4/12/2005, na baada ya kutimiza taratibu zote alikopeshwa tiketi ya ndege iliyoonyesha kuwa angesafiri tarehe 21/02/2006. Malipo ya mkopo wake yalifanyika tarehe 18/4/2006 kwa hundi na 193426 yenye thamani ya Tshs 87,772,800 iliyojumuisha pia malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia.

Kwa maelezo haya, ni dhahiri kuwa hawa ni wanafunzi halali waliotimiza masharti yote ya kukopeshwa na Bodi ya Mikopo kwa mwaka 2005/2006, hivyo, kwa mwaka 2006/2007 hao ni wanafunzi wanaoendelea na masomo.

(iii) Mwanafunzi David Denis Kanyika

Mwandishi wa gazeti la Kulikoni anaituhumu Bodi ya Mikopo kwa kumkopesha David Dennis Kanyika na kumkatalia mkopo Ramadhani Nyello ambaye inadaiwa walikwenda pamoja na Kanyika nchini Ukraine.

Kumbukumbu za Bodi zinaonyesha kuwa David Dennis Kanyika alitakiwa kusafiri kwenda Ukraine tarehe 11/02/2006 na malipo ya mkopo wake yalifanyika tarehe 22/03/2006 kwa hundi Na. 193426 yenye thamani 87,772,000.00 ambayo ilihusisha pia malipo ya wanafunzi wengine waliotangulia. Kwa maelezo haya David Denis Kanyika ni mwanafunzi anayeendelea na masomo nchini Ukraine na kwa mwaka 2006/2007 amekopeshwa jumla ya Tshs 3,000,000.00.

[/QUOTE]

Tatizo langu lipo kwenye bolded sentences hapo juu!
kama hawawezi kuwalipia hawa wanafunzi sababu ya SERA.. haya malipo yaliyofanywa kutokana na utekelezaji wa SERA gani?
Pia hawa wanafunzi waliotangulia ni akina nani?

Kwa hiyo kwenye hundi zote tatu Bodi imeshatumia jumla ya shilingi 80,097,600 + 87,772,800 + 87,772,000 = 255,642,400.00?????

Tangu lini hundi moja ikawa na tarehe mbili tofauti?
 
Mwenye soft copy ya makala ya Kulikoni aiweke ili kesho niisome, halafu niweze kuchangia vizuri.

alamski
 
Mie nimechoka kabisa. Hivi Waziri ameridhia hii statement itoke kwenye vyombo vya habari? Mimi nimeisoma na kwa kweli ni statement ambayo haina uzito wowote na kusema imetoka kwa mkurugenzi what so ever.... ni kuvunja heshima ya wizara husika. Ndio sababu watu wanaiba sana Tanzania huwezi kuandika upuuzi namna hii, hii hadithi ni sawa imeandikwa na form II student I can't believe. Nafikiri sisi hapa JF tuamke zaidi naona tuna matatizo makubwa zaidi kuliko vile tunavyofikiria. I am gutted.
 
Dua, tutawapa somo la kujenga hoja! Haya ni mapambano ya kifikra. Fikra za wale wanaotutaka tukubaliane na lolote serikali inasema alimradi lina muhuri wa ofisi, na fikra za wale wanaotaka kuhoji hadi huo mhuri kama ulipatikana kwa uhalali! Kwa kutoa tamko hili wamejichimbia shimo ambalo hawawezi kujitoa isipokuwa kusalimu amri na kukiri makosa!
 
jamani niwajibu au niache mtoto mdogo awajibu..?

I can see an openning here to expose the rot in some of our institutions for everyone to see. Let's make this a good case study where the little guy proved the mighty can be wrong.
There are so many holes in that statement, it is unbelivable.

Mkjj, usiwe na haraka. Tuichambue taratibu hiyo taarifa, na tutakutumia maoni kwa PM yako uweke vitu sawa.
 
Mwanakijiji Hoja imejibiwa kwa mapungufu makubwa!,Wacha watu waipitie hii Document vizuri halafu watajibiwa na kuonyeshwa UOZO wao!.Sijui nani aliyejibu ile makala,sasa wanajifunga kamba miguuni wenyewe.Kazi nzuri MKJJ tuwasiliane kwenye PM.
 
TWAWEZA KUMUAMINI PROF. MSOLLA? SEHEMU 2

UOZO WA BODI YA MIKOPO KILELE CHA UFISADI
Na. Mjenga Hoja

Wiki iliyopita nilielezea kwa kirefu kwanini Watanzania hatuwezi kumuamini Prof. Msolla ambaye ni Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu. Nikafafanua kwa mifano mbalimbali ni jinsi Waziri huyu wa awamu ya nne ameshindwa kabisa kuongoza Wizara hiyo na hivyo kuendelea kuja matamko mbalimbali ambayo hayatekelezeki na pia yeye mwenyewe kushindwa kabisa kuonesha mfano wa jinsi yanavyopaswa kutekelezeka. Hatuna sababu ya kumuamini Profesa hata chembe licha ya mbwembwe zote za maneno matamu ya asali Bungeni.

Kama hujashawishika, ni lengo langu leo kuonesha mfano dhahiri wa jinsi gani Mhe. Msolla siyo tu hastahili kuendelea na wadhifa huo bali pia ni jinsi amewaacha vijana wetu kuteseka huko Ukraine kutokana na uzembe wa bodi iliyo chini yake. Kwa kuendelea kusema kuwa vijana hawa "waliondoka wenyewe" na ya kuwa walikurupuka kupanda ndege "kwa udhamini binafsi" wakati yeye na watu wote walio chini yake wanajua ukweli kuwa vijana hawa waliondoka baada ya kukubaliwa mikopo (siyo kuomba) na pia kupewa msaada wote na bodi wa kuweza kupata pasi za kusafiria na zaidi ya yote kupata visa za kwenda Ukraine.

Kinachoonesha ni jinsi gani Prof. Msolla siyo msema kweli ni kauli ya wizara yake mapema kwenye kikao cha Bunge linaloendelea wiki chache zilizopita kwamba serikali "haikutoa udhamini wa mwaka wa kwanza kwa mwanafunzi yeyote nje ya nchi" wakati ushahidi upon a unaonesha kwamba serikali hata kama haikutoa, serikali ilitenga kiasi cha fedha kwa wanafunzi wanaosoma huko nje ya nchi. Mfano dhahiri ni kitendo cha serikali kuanza kuwalipia wanafunzi watatu kati ya wale 29 huko Ukraine. Wanafunzi ambao wanalipiwa na serikali na walikuwa kwenye kundi la wale 29 ni Yesse Cornelio Msechu (Shs. 3,000,000), Rajabu Kihalla, na Adiel Daniel Mushi.

Katika hawa watatu, tutamtumia Adiel Daniel Mushi kudhihirisha ni jinsi gani bodi ya mikopo iliyo chini ya Prof. Msolla ina ubovu ambao tiba yake ni kuivunja na kuiunda bodi hiyo baada ya maandalizi ya kitaalam kufanyika na siyo kukurupuka kama ilivyo sasa. Matatizo yaliyowakuta vijana wetu huko Ukraine ni matokeo ya moja kwa moja ya ubovu wa bodi na uzembe wa maafisa wa wizara na ni kielelezo cha ukosefu wa uongozi toka ngazi za juu za wizara.

Adiel Daniel Mushi alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wale 29 na yeye kama wao alichelewa kwenda kuanza masomo Ukraine, na pamoja nao alienda Ukraine kwa malipo yake baada ya kuambiwa mkopo wake utamfuata Ukraine. Pamoja na wenzake wawili tuliowataja hapo juu, Adiel alisubiri kama wale wengine mkopo wake na mwanzoni alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliolalamika kucheleweshewa mikopo yao. Kwa namna ambayo Prof. Msolla na Bw. Nyatega pekee wanajua Adiel alianza kupokea fedha kutoka bodi na hivyo kuendelea na masomo yake kama kawaida na hivyo kujiengua kutoka katika kuni la wale 29. Wenzake wawili nao wakaanza kupatiwa mikopo.

Wizara inaweza kutafuta kisingizio chochote cha kuelezea ilikuwa Adiel na wenzake waanza kupokea mikopo wakati wengine 26 waliokuwa katika mazingira yale yale na vyuo vile vile wasipatiwe mikopo yao? Kama hiyo haitoshi, huyo huyo Adiel Daniel Mushi alitengewa na bodi hiyo hiyo inayomlipia huko Ukraine fedha nyingine kwenye vyuo vya nyumbani kwa mwaka ule ule! Kwenye batch 8 alitengewa Shs. 1,320,000 kwenda kusomea BSc hapo CoET (mwaka wa kwanza), kama vile hiyo haitoshi bodi yetu yenye makengeza ikamkubalia Shs 1,320,000 nyingine kwenye chuo hicho hicho lakini hiyo ikitangazwa kwenye Batch 13! Nilisahau kuwaambia huko Ukraine ametengewa Shs. 3,000,000! Ina maana mtu mmoja alikubaliwa Shs. 5,640,000!

Sasa bila ya shaka Bodi wanaweza kutoa maelezo kuwa ni makosa ya kompyuta, wanaweza kusema haina maana fedha zote zilitolewa kwa mtu mmoja na wanaweza kusema kuwa jina hilo la "Adiel Daniel Mushi" ni la watu watatu tofauti, wawili wakiwa chuo kimoja na wakisomea kitu kile kile! Kama hii ni nasibu, basi inafaa kuingizwa kwenye Guiness Book of Word Records!

Ndugu zangu hili siyo nasibu bali ni mtindo unaoendelea kwenye bodi hii iliyo chini ya Msolla ya watu wachache kujitajirisha kwa kuomba na kutoa mikopo hewa. Uchunguzi wangu umegundua zaidi ya majina ya wanafunzi 500 ambayo wamekubaliwa mikopo ya karibu wastani wa shilingi milioni sita kila mmoja kwenye vyuo zaidi ya kimoja. Jumla ya mikopo ya ile ya ziada (tukichukulia kuwa mwanafunzi huyo alichagua chuo cha gharama zaidi) inakaribia shilingi bilioni moja! Swali kwa Prof. Msolla na maafisa wake, kama wanafunzi hawa hawakutumia hizo bilioni moja kwenye vyuo vilivyowakubali na wakaamua kwenda chuo kimoja tu, zile fedha zilizotengwa zimekwenda wapi? Kama hazikuliwa wanaonaje wakazitumia kuwasomesha vijana wetu huko Ukraine badala ya kukimbilia kuwatumia tiketi ili warudi haraka haraka yaishe kinyemela?

Kwa vile watataka ushahidi kuwa tukio la Adiel Daniel Mushi siyo la pekee na kuwa kweli wapo watu wengine ambao wamekubaliwa mikopo kwenye vyuo zaidi ya kimoja na fedha, ninawapatia hapa tone la majina hayo mia tano, vinginevyo itabidi ninunue kurasa za magazeti na kuzijanza.

Wa kwanza kati ya wanafunzi hawa ambaye nusura anipe ugonjwa wa moyo ni mwanafunzi aitwaye Charles J. Temba. Huyu siyo miongoni mwa wale waliokubaliwa kule Ukraine. Ila kesi yake ni kali zaidi kuliko ya Adiel.

- Charles J. Temba Mwanafunzi huyu (kama kweli yupo) amekatiwa mikopo mara tatu katika vyuo vitatu tofauti, na vyote ni kwa mwaka wa kwanza! Haiwezekani kuwa bodi haikujua kuwa inamkatia mikopo mtu huyo huyo na kama haikujua basi ni sababu tosha ya kuonesha kuwa kuna ubovu, na kama walijua basi ni ushahidi kuwa kuna ubovu zaidi ya tunavyofikiria. Bw. Temba kwa mwaka huo wa 2006/200

Kwa mwaka huo huo 2006/2007
- Yuko Batch 11, Tumaini University - 1,860,000.00
- Yuko Batch 8, Sokoine University - 1,794,800.00
- Yuko Batch 16, Mzumbe University 1,560,000.00
- Yuko Batch 16, MIST – 1,500,000
Kwenye Batch hiyo hiyo 16 kuna mwanafunzi mwingine anayetumia jina la "Charles B. Temba"… inawezekana kuwa ni mtu yule yule? Huyu yupo University of Arusha mwaka wa kwanza na katengewa = 1,560,000 – Jumla ya fedha alizotengewa: 8,274,800!

Wanafunzi wengine waliokubaliwa mikopo mwaka huo huo zaidi ya mara moja na kwenye vyuo tofauti ni:

- Denis David Kanyika: Yeye alitengewa fedha za mwaka wa kwanza kwenda kusoma Ukraine 2006/2007 (Batch 12). Hiyo ni kinyume na madai ya Waziri kuwa hakukuwa na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyedhaminiwa nje ya nchi. Zaidi ya yote, huyo alikuwepo kwenye batch 8 ya mwaka 2005/2006. Batch hiyo ilikuwa na mwanafunzi aliyekwama Ramadhani Nyello. Kanyika alitanganiwa 3,000,000

- Alistidia J. Rupia ambaye yuko: Batch 10 akikubaliwa mkopo mwaka wa kwanza wa shilingi 1,320,000 (UDSM) kwenda kusomea B.A Education na wakati huo huo akikubaliwa mkopo 4,390,400 (batch 14, batch 16) wa kwenda kusoma Kifaransa Algeria. Yote ni mwaka wa kwanza. Jumla: 5,710,000

- Salim J. Chadoe ambaye yuko batch 5 (UDSM) ambaye amekubaliwa mkopo wa kusomea Bcom kiasi cha shilingi 1,760,000 na pia alikubaliwa (batch 14) mkopo wa shilingi milioni 3,000,000 kwenda Poland jina la chuo na alichokubaliwa kusomea hakikuwekwa dhahiri. Jumla: 4,760,000

- Patrick Kazinja ambaye yuko batch 11 (UDSM) ambako alikubaliwa mkopo wa shilingi 1,440,000 kusomea Bcom na wakati huo huo alikubaliwa shilingi milioni 4,390,000 kwenda kusomea Kifaransa mwaka wa Kwanza huko Algeria Batch 14, na 16. Jumla: 5,830,000

- Mary Ligunda ambaye yuko alikubaliwa kwenye batch 4 shilingi 1,320,000 (UDSM) kwenda kusomea Food & Biochemical Engineering. Wakati huo huo na mwaka huo huo na mtu yule yule alikubaliwa shilingi 4,390,000 kwenda kusoma Kifaransa Algeria. 5,710,000

- Sophia Sokoni amb aye yuko Batch 13 ambaye amekubaliwa mkopo wa shilingi 1,440,000 (UCLAS) kusomea BSc in Building Economics na wakati huo huo amekubaliwa 4,390,400 kwenda kusoma Algeria Kifaransa. Jumla: 5,830,000

- Mohammed Matwera ambaye amekubaliwa mkopo (batch 4) wa shilingi 1,700,000 kusomea Udaktari (UDSM) na wakati huo huo akiwa amekubaliwa mkopo wa 4,390,000 kwenda kusomea Kifaransa Algeria (Batch 14, na 16). Jumla: 6,090,000

- Nyamhanga Msabi Mwita: Huyu ni mwanafunzi katika vyuo viwili ambako sehemu zote ametengewa fedha za chakula, ada, vitabu. Ametengewa Shs. 1,910,000 huko SAUT (Batch 11) na pia kuna mtu mwingine naye anaitwa Msabi Mwita ambaye alitengewa Shs. 9,247,045 kwenda kusoma China (Batch 2). Je huyu ni mtu yule yule au ni watu wawili tofauti?

- Exaud Chengula: Huyu ametengewa fedha kwenye vyuo viwili tofauti mwaka ule ule na vyote kwa mwaka wa kwanza. Ametengewa 1,320,000 kusomea Elimu (DUCE – Dar-es-Salaam University College of Education) na pia ametengewa 1,860,000 huko Tumaini University kusomea BA-CAT (Cultural Anthropology and Tourism).

- Emmanuel Richard Kizigha: Huyu alitengewa Shs. 1,707,000 kusomea pale CBE kwa mwaka 2006/2007 (Batch 7). Wakati huo huo hata hivyo alitengewa Shs. 3,000,000 kwa mwaka wa pili kusoma huko Ukraine (Batch 8). Huyo naye alikuwa kwenye batch 8 ya mwaka 2005/2006 ambayo kijana Ramadhani Nyello alikuwamo naye. Kama Bodi inajua huyu yuko mwaka wa pili huko Ukraine, kwanini wamtengee tena fedha hapo CBE?

Hayo ni majina machache tu ya wanafunzi wale kati ya 500 ambao Prof. Msolla na watu wa bodi wameona ni vyema wawatengee mamilioni ya fedha na kuwanyima kabisa wanafunzi wetu 24 (samahani nilisahau kuwaambia kuwa wanafunzi wawili wengine waliondoka Ukraine baada ya kushindwa kuendelea na masomo na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha.

Kwenye suala la wanafunzi hawa kuna maelezo kadhaa yanayoweza kutolewa, kwanza ni kuwa kukubaliwa mkopo haina maana kupata mkopo; kwa hili tunasema kama umekubaliwa mkopo na fedha zako zikatengwa, ni tofauti gani na mtu kupewa mkopo ambao bado hujauchukua? Kama wanafunzi walikubaliwa, je serikali inasema hawakuchukua mikopo hiyo baada ya kujua wamekubaliwa?

Inawezekana wakasema kuwa bodi ya mikopo imefanya makosa kidogo na yatasahihishwa. Makosa ya kutenga karibu bilioni moja kwa wanafunzi hewa, siyo makosa kidogo! Ni makosa ambayo kwenye nchi zenye kuheshimu sheria yanatosha kabisa kufukuzisha watu kazi. Tunachosema ni kuwa fedha hizo zilizotengwa aidha zimeishia mikononi mwa watu wachache au bado zipo. Kama zimeishia mikononi mwa watu wachache watu hao ni lazima wajulikane, kama bado zipo kwanini zisitumike kuwalipia wanafunzi wetu wa udaktari, na uhandishi waliokwama Ukraine?

Na mwisho wanaweza kusema kuwa madai ninayoyatoa hapa hayana msingi. Na sitashangaa serikali yetu tukufu ikaanza kutafuta ni nani aliyeandika jambo hili na kuliweka hadharani badala ya kufanyia kazi madai yangu. Kama suala la BOT ni mfano sitashangaa serikali kukataa kufanya uchunguzi wowote. Lakini kwa vile suala hili ni kubwa na tulichoonesha ni kiduchu basi itakuwa ni kosa kubwa kulifumbia macho kwani itawahakikishia wananchi kuwa serikali ya Rais Kikwete haina ubavu wa kupambana na ufisadi na maneno ya Tanzania yenye neema kwa kila mtanzania ni maneno matupu kwani hawa wanafunzi wetu 24 hawaoni neema yoyote na hiyo Tanzania kwao ni njozi ya nchi ya kusadikika.

Ni matumaini yangu kwa kuyaweka haya hadharani tumewapa zana wawakilishi wetu Bungeni mahali pa kuanzia kumbana Prof. Msolla. Wabunge wetu wamechaguliwa kuwakilisha wananchi. Miongoni mwa wananchi hao ni hawa vijana 24. Itakuwa ni unafiki wa daraja la kwanza kwa wabunge kujifanya wanawatetea watanzania mamilioni wakati hawa 24 wameshindwa kuwatetea. Itakuwa ni aibu ya taifa letu kuendelea kuwakana vijana wetu "on technicalities". Vijana hawa hawaombi kitu chochote kutoka kwa nchi yao isipokuwa nafasi ya kuendelea na masomo. Hadi hivi sasa vyuo vimewaonea huruma na sasa vyuo hivi vinafungwa na hatima ya watoto wetu haijulikani. Wakati umefika Watanzania tuoneshe kuguswa na suala lao na kuwatetea. Tusisubiri hadi tusikie wamekufa ndipo tujifanye tunatuma rambirambi na kuoneshwa kusikitishwa! Tusisubiri hadi janga litokee ndipo tujifanye tunawatetea!

Mimi nimefanya nafasi yangu, wananchi wengine wamefanya nafasi yao, TANLET wamefanya jukumu lao, viongozi wa upinzani wamefanya nafasi yao, wazazi wamefanya nafasi yao. Watu pekee ambao tunatarajia kuwa watafanya nafasi yao ni viongozi wa CCM na wabunge wake. Kwani hawa wakiamua vijana waendelee kusoma wataendelea, ni hawa wakiamua vijana wapatiwe fedha zao za mikopo ya kuendelea na masomo na kulipia deni lao lililoko sasa hivi vyuoni itafanyika. Tumaini la vijana hawa na wazazi wao ni kuwa serikali ya Kikwete itasita angalau kwa sekunde na kusema itakuwaje kuwa tumewaacha vijana hawa sababu ya uzembe wa watu wachache? Natoa wito kwa wananchi tusimame upande wa watoto hawa ili waendelee kusoma. Tusiwaangushe hadi wakakata matumaini na nchi yao. Watoto hawa wangetaka kuikana nchi yao wangefanya hivyo, kama wangetaka kuzamia ugenini wangefanya hivyo, lakini hadi hivi sasa kwa machozi na kwa kutetemeka, wanaiomba nchi yao itimize ahadi yake kwao, na isiwalipizie kisasi kwa makosa ya watu wachache.

Wamekinga mikono kama wanaomba wakisema "tusomesheni". Wanalia kila siku wakijiuliza "tumeikosea nini Tanzania?" Wanajiambia kila kukicha, "laiti ningekuwa na uwezo nisingehangaika hivi". Ndugu zangu, tukiendelea kuwafumbia macho vijana hawa, ina maana kweli Tanzania tumeingiwa na kiza kipya cha ufisadi! Tusikubali kuwaacha, tusikubali warudi bila kuendelea na masomo, na tuhakikishe kuwa ahadi ya Tanzania yenye neema ianze kuwafikia kwani kama ni adhabu wameshapata vya kutosha! Je, Tanzania itasimama upande wao?

Niandikie: bm1280@hotmail.com
Niachie ujumbe: + 1 249 686 2010
 
Back
Top Bottom