Jamani huko Songea kuna mambo!
Atolewa utumbo kwa kugombania mwanamke
Na Joseph Mwambije,Songea
Saturday Apr 26, 2008
MKAZI wa kijiji cha Namanguli wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma ameuawa kikatili kwa kuchomwa kisu tumboni na utumbo mkubwa kutoka nje katika ugomvi wa kugombea mwanamke.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Falhum Mshana amemtaja marehemu kwa jina la Majidu Chowo (60) na kwamba tukio hilo lilitokea Machi 20, mwaka huu katika Kijiji cha Namanguli wilayani humo.
Akifafanua kuhusu tukio hilo Kamanda Mshana alisema marehemu alikuwa na mke aliyekuwa akiishinaye aitwaye Asia Nchimbi (35). Alisema marehemu alizaa watoto kadhaa na mwanamke huyo na kwamba ukatokea ugomvi baina yao na kufikia kutengana. Hata hivyo alisema baada ya kutengana bado walikuwa wakitembeleana.
Alisema baada ya kutengana na mumewe Asia Nchimbi alimpata hawara aitwaye Nasibu Konde (26) ambaye alimwambia hana mume kwani aliyekuwanaye wameachana.
Mshana alisema siku ya tukio majira ya Saa 2:00 Usiku Hawara wa Nchimbi kijana Nasibu Ndonde alimtembelea mpenzi huyo na kumgongea na kufunguliwa mlango na Majidu Chowo na akamuhoji yeye ni nani aliyelala na mpenzi wake na akajibiwa kuwa huyu ni mke wake.
Katika majibizano hayo Kamanda alisema zikatokea ghasia kubwa ambapo Konde akachomoa kisu na kumchoma Chowo tumboni na kusababisha utumbo mkubwa kutoka nje.Mtuhumiwa wa mauaji hayo Nasibu Konde ameshafikishwa Mahakamani.
Source: Gazeti la Maisha