Athari ya kubaka demokrasia kwa kutumia ndiyooo hata kwa mambo yasiyo ya msingi ni janga la kitaifa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Athari ya kubaka demokrasia kwa kutumia ndiyooo hata kwa mambo yasiyo ya msingi ni janga la kitaifa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sammosses, Feb 10, 2012.

 1. sammosses

  sammosses JF-Expert Member

  #1
  Feb 10, 2012
  Joined: Jan 24, 2011
  Messages: 1,205
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Maisha ni safari ndefu ambayo mwisho wake ni kifo,hakuna aliyezaliwa pasipo kuja kuionja ladha ya umauti.Hata jabali kiasi gani ipo siku ujabali wako utaishia kwenye tani saba za udongo.Wako wapi watawala walioitawala dunia hii kwa mbwembwe nyingi lakini waliishia wapi?Kulikowapo wakina Hitler walioitingisha dunia lilipofika swala la wakati walipotea kama punje ya nafaka iliyodondoka kondeni.

  Yalikuwapo mataifa makubwa duniani yaliyo heshimika kwa uchumi lakini yalidondoka na kupoteza himaya zao ,aidha kutokana na kiburi cha ubinadamu.Wapo waliothubutu kujenga pepo zao kushindana na mwenyezi Mungu lakini hawakuweza kuingia ndani ya pepo zao kwa kutwaliwa roho zao.Napata uchungu mwingi sana mpaka kufikia kuandika haya yote kutokana na maisha yetu yanavyochezewa na hawa wanasiasa.Tumekubali kuyaweka maisha yetu rehani na sasa tunalipa deni la usaliti wetu kwa kuuza haki zetu za kuwachagua viongozi wenye nia ya dhati na wenye kuguswa na matatizo ya yanayoikabili nchi yetu tuliyopewa bure na Mungu.


  Nchi yetu imekumbwa na tatizo la kimfumo linalopelekea wananchi wake kuishi maisha yasiyo na mashiko,na kuwa manamba ndani ya nchi yao.Ile hali yakutumikishwa kama ilivyokuwa inafanywa na wakoloni imerudi kwa kishindo.Matabaka yanazidi kuongezeka siku hadi siku.Mwenye nacho anaongezewa,asiye nacho ananyang’anywa hata kile kidogo.Migogoro kila kukicha,nchi inaendeshwa kidharura kiasi kwamba wananchi wamekata taama ya maisha.


  Mfumo duni na ombwe la uongozi ndani ya nchi yetu,imepelekea nchi kuwa na katiba mbovu inayo jali maslahi ya watu wachache.Katiba ni muongozo wa jinsi ya nchi yetu iendeshwe vipi,iwe kisultani,kifalme ama kimangimeza.Katiba yetu ni katiba iliyoandikwa kwa kufuata maoni ya watu wachache walio amini fikra zao ni sahihi zaidi miongoni mwa raia waliokuwepo kipindi hicho.Waasisi wenyewe wa katiba hiyo waliwahi kukiri katiba yetu inamfanya kiongozi atayechaguliwa kuwa diktekta.Tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi tulikuwa kinadharia zaidi kuliko kivitendo ndo maana mpaka leo hii katiba yetu bado ni ile ya mfumo wa chama kimoja,yenye kuwakumbatia wachache.Wamepita watawala kwa awamu nne tangu kupata uhuru wa nchi hii.Haikuwahi kutokea hata siku moja wazo la kuandika katiba mpya itakayoendana na wakati uliopo kutolewa na serikali ya CCM.Huwezi kuwangoza wananchi kiarobaini na saba ilihali tupo kielfu mbili.


  Awamu ya nne ilipoingia madarakani,wananchi walikuwa na imani na kiongozi waliyemchagua wakiamini ni mlalahoi mwenzao mwenye kujua shida zao.Imani ya wananchi ilianza kupotea na kukosa imani na kiongozi wao kwa kuonyesha udhaifu mkubwa kiutendaji.Serikali yake na chama chake waliamini kuwa rais ni msikivu na serikali yake ni makini.Umakini na usikivu wa serikali yake na chama chake umeishiwa wapi?Shughuli za maendeleo zimekwama kiasi cha nakisi iliyoko kwenye bajeti ilyopitishwa na serikali kuifanya serikali isiweze kujiendesha.Matumizi yamekuwa makubwa kuliko mapato.Tunapitisha bajeti ambayo hatuna senti ndani ya hazina yetu,matokeo yake migomo kila sekta,mpaka sekta ya afya imekumbwa na migogoro inayopeleke nchi kupoteza rasilimali watu na nguvu kazi ya taifa.


  Tatizo la mfumo duni linatokana na katiba dhaifu isiyoendana na wakati uliopo.Katiba iliyompa dhamana kubwa rais matokeo yake ni ulevi wa madaraka na hali ya nchi kwenda halijojo.Vyama vyote vya kisiasa tangu kuingia mfumo wa vyama vingi hapa nchini vilikuwa vikidai katiba mpya itakayoendana na wakati uliopo bila mafanikio.Aidha juhudi zao zilikwamishwa kwa migogoro iliyopandikizwa kimakusudi kabisa ndani ya vyama hivyo na kupelekea kukosa mshikamano wa kitaifa kwa kudai katiba mpya.

  Kila jambo lina wakati wake.Katika kipindi cha kwanza cha awamu ya nne kuelekea uchaguzi mkuu nchi ilikumbwa na taharuki kubwa kutokana na nguvu kubwa ya CHADEMA,nguvu hiyo na ahadi zake za kuanza mchakato wa katiba ndani ya siku mia moja ndo ilipelekea serikali ya CCM chini ya mwenyekiti wake na rais JK kurukia hoja ambayo haikua agenda katika ilani yake ya uchaguzi.Vyama vilivyoinadi katiba mpya katika uchaguzi huo vilikuwa CUF,NCCR na CHADEMA.Pia shinikizo la wadau mbalimbali kuhusu katiba mpya kulipelekea rais kutangaza nia ya kuandika katiba mpya bila kujiandaa kwa kuwa kwanza haikuwa agenda ya chama chake,pili watendaji wake walibeza uwezekano wa kuandika katiba hiyo kitendo kilichosababisha muswaada huo wa katiba kupigiwa sana kelele.


  Sipendi niende mbali sana,hekima ya mh. Rais kama ni kweli alitumwa na dhamira yake na sikuudanganya umma ni matokeo ya mgogoro mkubwa utakaoibuka ndani ya siku chache zijazo.ile dhamira ya kweli ya rais imekwenda kinyume kabisa na utekelezaji wake, tena mbele ya bunge lililloaminiwa na wananchi.kama dhamira ya kweli ya rais ilikuwa katiba isitekwe na wanasiasa,iweje leo hii wabunge hao hao wa serikali sikivu wang’ang’anie makada wa vyama ndo wawe waandalizi wa mikutano ya kukusanya maoni ya katiba!Iwe leo mwanasheria mkuu wa serikali kukosa hoja za msingi kuitetea hoja aliyoileta ndani ya bunge kama si mchezo wa kuigiza?Usanii uliochezwa na maigizo yaliyofanyika ndani ya bunge letu tukufu si kwamba ni dosari bali pia umelishushia heshima bunge hili tuliloliamini lipo kwa maslahi ya umma.


  Hali hii inadhihirisha demokrasia kwenye nchi zinazoendelea ni janga la kimataifa,tusingependa gharama ya demokrasia ikawa ni umwagaji wa damu kama walivyofanya wenzetu wa Kenya.Rais kutishiwa na wabunge vilaza kama ilivyokwisha kunukuliwa kwenye vyanzo vya magazeti ya Kiswahili ni ombwe la uongozi katika taifa hili.


  Rais kwa heshima na taadhima,kama kweli ulisukumwa na dhamira ya dhati ya moyo wako ukiwa na timu ya washauri wako,leo wamekuangusha kwa kushindwa kukitetea kile ulichoamini kuwa katiba bora ni zao la amani katika nchi.Kuna haja gani ya kuwa na wataalamu wasioweza kujenga hoja kama walivyoweza kuitetea sheria ya kuunda chombo cha maadili ya kuwasimamia mahakimu.Kitendo cha washauri wako kushindwa kujenga hoja zenye kueleweka ni anguko la serikali yako na kujipunguzia heshima mbele ya marais wenzako.Kama kweli dhamira ni njema wawajibishe watendaji wako kwani wao ndiyo chanzo cha utendaji mbovu wa serikali yako.Hatupendi kuamini kuwa wewe ni raisi kigeugeu,huku unasema hivi na huku unasema hivi japokuwa hutungi sheria lakini ni sehemu ya bunge kwa mujibu wabunge ibara ya 62(1) na 63(1).


  Mwisho,mara nyingi nimekuwa nikisisitiza kuwa serikali yoyote ile duniani huwa madhubuti pale inapotekeleza yale wapiga kura wake waliyoyategemea.Ukiona serikali ina fumba macho hata kwa mambo ya msingi ujue kifo cha serikali hiyo hakipo mbali.Nilianza kwa kusema walikuwapo majabali walitishia dunia hii na dola zao leo hii wako wapi,tusingependa na serikali yetu iignie kwenye mkumbo wa serikali dhalimu kwa kutumia wingi wa wabunge wake kupitisha hata mambo yasiyo na msingi kwa maendeleo ya taifa hili.Tuachie kumbukumbu nzuri angalau tukukumbuke kwa kusimamia mchakato wa katiba kwa dhati ile ya kweli.Mungu ibariki Afrika ,Mungu ibariki Tanzania
   
Loading...