ATC kwafukuta sakata la mahujaji

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,045
ATC kunahitaji mabadiliko makubwa ya uongozi na pia katika baraza la mawaziri nalo utendaji wake ni wa kukatisha tamaa nalo linahitaji mabadiliko makubwa
ATC kwafukuta sakata la mahujaji

na Salehe Mohamed
Tanzania Daima

SERIKALI inatarajia kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi katika Shirika la Ndege Tanzania (ATC) baada ya kuwapo kwa kile kinachodaiwa ‘uzembe’ wa kiutendaji ndani ya shirika hilo.
Uchunguzi wa Tanzania Daima, umebaini mabadiliko hayo yatatokana na matatizo yaliyotokea wakati wa usafirishaji wa mahujaji wa Tanzania na nchi jirani kwenda Makka, Saudi Arabia, ambao walikuwa watumie ATC kwa safari hizo.

Mabadiliko hayo yanatokana na kuwepo kwa taarifa za ‘uzembe’ wa baadhi watendaji wa shirika hilo, katika kuratibu safari ya mahujaji ambayo ililitia aibu taifa, hali iliyosababisha serikali kuingilia kati na kuwasafirisha na kuwarejesha nchini mahujaji hao.

Chanzo cha kuaminika cha habari hizi kiliiambia Tanzania Daima kuwa pamoja na ATC kutokuwa na uwezo wa kuwasafirisha mahujaji, lakini mipango ya kuratibu safari hiyo haikuwa makini kama ilivyopangwa.

“Hivi sasa ofisi hazikaliki kutokana na kuwapo kwa taarifa za kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya uongozi ATC,” kilitabanaisha chanzo hicho.

Katibu Mkuu wa Miundombinu, Omari Chambo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema liko juu ya uwezo wake, hivyo si rahisi kufahamu mpaka atakapopewa taarifa na viongozi wake.

Alisema kama uchunguzi utafanyika na kugundulika kuna uzembe uliosababishwa na baadhi ya watendaji wa ATC, serikali haitasita kuwawajibisha wahusika.

“Sina taarifa za kufanyika kwa mabadiliko hayo, kama kitu hicho kipo, basi kinafanyika na wakubwa wangu na nitapata taarifa mambo yatakapokamilika, lakini kwa sasa sijui chochote,” alisema Chambo.

Alisema, anachofahamu hivi sasa ni mazungumzo kati ya ATC na kampuni iliyopewa zabuni ya kuwasafirisha mahujaji, Al-Wasam ya Saudi Arabia, ili kurudisha gharama zilizotolewa na serikali.

Alibainisha kuwa, viongozi wa ATC walifanya safari kwenda kwenye shirika hilo kufanya majadiliano hayo ambayo anaamini yatakwenda vizuri.

“Unajua ATC waliingia mkataba wa kibiashara na wale jamaa na nina imani watalipwa haki yao kulingana na mkataba waliowekeana,” alisema.

Kuhusu kiasi cha fedha kilichotumiwa na serikali kuwasafirisha mahujaji hao, Chambo hakuwa tayari kubainisha na kusema ni mapema mno kutaja kiasi hicho.

“Tulichokifanya sisi ni kuhakikisha mahujaji wanakamilisha ibada yao kulingana na taratibu za dini, mambo mengine yatakuja baadaye, lakini kwa sasa kila kitu tuwaachie watu wa ATC,” alisema Chambo.

Aidha, ‘uzembe’ huo unadaiwa kufanyika baada ya Bodi ya Wakurugenzi chini ya Uenyekiti wa Balozi Mustafa Nyang’anyi kushindwa kupata ndege ya uhakika na kwa haraka, kwa ajili ya mahujaji hao.

Hali hiyo ilisababisha mahujaji hao zaidi ya 1,000 kuchelewa kufika Makka kuanza ibada ya hijja ambayo ni moja kati ya nguzo tano za dini ya Kiislamu.

Mahujaji wa Tanzania na wengine kutoka nchi jirani mwishoni mwa mwaka jana, walisota katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa siku kadhaa kutokana na kutopatikana kwa ndege ya kuwasafirisha kwenda Saudia.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya ATC kushindwa kuileta ndege iliyodai kuwa iliikodi kwa ajili ya kuwasafirisha mahujaji hao.

Hali hiyo ilisababisha serikali kuchukua jukumu la kuwasafirisha mahujaji hao na kisha kuunda kamati ya kuwarejesha nchini.

Hata hivyo, ndege iliyokodiwa na serikali kutoka Kampuni ya AL-Wassam, ilishindwa kuhimili safari za mahujaji hao baada ya kuharibika.

Hiyo ilikuwa ni ndege pekee kati ya tatu ambazo zilitafutwa, ambayo ilifanikiwa kupeleka kundi la kwanza la mahujaji 379, lakini ilipokuwa ikiwafuata wengine ilipata hitilafu za kiufundi na jitihada za kuitengeneza zilikwama baada ya kuelezwa kuwa vinahitajika vipuri vingine kutoka Afrika Kusini.

Hata hivyo, katika safari hiyo ya kundi la kwanza, serikali ilijikuta ikilazimika kulipa faini ya dola 6,000 kutokana na ndege hiyo kuchelewa kufika kulingana na ratiba iliyokuwa imepangiwa.

Miongoni mwa mahujaji waliosotea safari hiyo ni baba mkwe wa Rais Jakaya Kikwete, shemeji yake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni na viongozi wengine ambao walichelewa kufika Makka kwa zaidi ya siku saba, baada ya tarehe ya safari, huku wengine wakiahirisha safari hiyo.

Mahujaji hao walianza kurejea nchini Desemba 29 mwaka jana, na mahujaji wa mwisho waliingia nchini mwishoni mwa wiki iliyopita, huku wakiwa wamepata adha ya kubadilishiwa ndege mara kadhaa.
 
Back
Top Bottom