Askofu Ruwaichi, Mei Mosi na Teolojia ya Kazi: Mt. Joseph alikuwa mtu wa haki

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
1620029629308.png

Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam

Tarehe 01 Mei 2021, Kanisa Katoliki Duniani lilisherehekea sikukuu tatu kwa mpigo. Kuna kumbukizi ya miaka 130 ya waraka wa Papa Leo wa XIII uitwao “Mabadiliko ya Kimapinduzi (Rerum novarum),” kumbukizi ya miaka 30 ya waraka wa Papa Yohanne Paul wa II uitwao “Miaka 100 Baada ya Mabadiliko ya Kimapinduzi (Centesmus Anus),” na Sikukuu ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi.

Kwa hapa Tanzania, sikukuu hizi ziliadhimishwa kitaifa kesho yake kwenye kituo cha Hija cha Pugu, katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kupitia ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu Juda Thadeus Ruwaichi.

Ibada hii ilirushwa mbashara kupitia luninga ya TCB1, hili likiwa ni tukio la kuhitimisha mzunguko wa sanamu ya Mtakatifu Joseph kupitia mikono ya Umoja wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Jimbo la Dar es Salaam.

Akihubiri katika misa hiyo, Askofu Ruwaichi alisema kwamba, kazi sio udhalilishaji; kwamba, kazi sio utumwa; na kwamba chimbuko la kazi ni Mungu.

Aliongeza kusema kwamba, Mungu ni mtendakazi kwa sababu ya kazi ya uumbaji aliyoifanya hapo mwanzo; na kwamba, tunapofanya kazi kama Wakristo tunakuwa tunafanya uinjilishaji.

Pia, Askofu Ruwaichi alisema kwamba, “Mtakatifu Joseph alikuwa mtu wa haki.” Kwa sababu hii, alitoa wito kwa kila muumini kuiombea nchi yetu ili raia wake wawe wachapa kazi kama alivyokuwa Mungu na kama alivyokuwa Mtakatifu Joseph.

Wito kuiombea nchi yetu kusudi raia wake wawe wachapa kazi ni wito muhimu sana kwa sababu tano.

Kwanza ni wito unaoanzisha tafakari kuhusu kiwango cha ajira na ukubwa wa tatizo la ajira hapa nchini Tanzania; njia bora za kumaliza tatizo hili; na mgawanyo wa majukumu katika mradi wa kumaliza tatizo hili.

Pili, ni wito unaoanzisha tafakari kuhusu dhana za “mungu wa haki,” “mtu wa haki,” “mfumo wa jamii yenye kutenda haki,” na “mfumo wa kiuchumi wenye kutenda haki.”

Kutenda haki ni kutekeleza majukumu. Kwa hiyo, “mungu wa haki” ni “mungu mwajibikaji” na “mtu wa haki” ni “mtu mwajibikaji.”

Kwa kuwa habari ya “mungu mwajibikaji” ina matatizo yake ya kiteolojia, kwa hapa, nataka kusisitiza habari ya “mtu wa haki,” yaani mtu anayetenda haki kwa kutekeleza majukumu yake.

Na kwa vile ajira ni ajenda ya kiuchumi, napendekeza kufanya tafakari ndogo kuhusu “mfumo wa kiuchumi ambamo haki zinatimizwa na majukumu kutendeka.”

Mfumo wa uchumi ni kitu kama vile mgahawa, duka la kaya, kiwanda, shule, hospitali, benki, na kampuni.

Mifumo hii inafanana katika mambo makuu manne. Kila mfumo una maingizo, mchakato, matokeo, mrejesho, na mpaka unaotenganisha mazingira ya ndani na mazingira ya nje.

Tuchukue mfano wa kiwanda kidogo cha kuzalisha unga lishe chenye mashine iliyosimikwa katika kiwanja namba 5, mtaa wa Mtakuja, Wilaya ya Kinondoni.

Pia tuseme kuwa kiwanda hiki kinapata malighafi ya mahindi kutoka mikoa yote inayozalisha mahindi; na kinauza unga wake katika mikoa yote ya ukanda wa pwani. Katika kiwanda hiki kuna viambata vifuatavyo:

  • maingizo ni mahindi yaliyokaushwa;
  • kuna michakato mikubwa mitatu, yaani kukoboa, kusaga na kupakia unga katika mifuko;
  • kuna matokeo, yaani unga safi kwenye mifuko;
  • mipaka ya kiwanja namba 5, ndio mstari unaotenganisha mazingira ya ndani ya kiwanda na mazingira ya nje;
  • mrejesho ni taarifa za mauzo na maoni ya wateja kuhusu unga unaosambazwa; na
  • mazingira yake ya nje ni mikoa yote inayozalisha mahidni na mikoa yote inayonunua mahindi.
Pale ambapo taarifa kutoka sokoni zinaonyesha kuwa, unga uliozalishwa unahitajika sana sokoni, basi uzalishaji hiongezwa na kinyume chake.

Pia, pale taarifa kutoka sokoni zinaonyesha kuwa, unga una dosari, bidhaa hiyo hufanyiwa maboresho.

Kwa ujumla, mifumo yote ya kiuchumi hupokea maingizo na kuzalisha matokeo baada ya mchakato unaobadilisha maingizo kuwa bidhaa/huduma kwa ajili ya soko la walaji.

Maingizo yanahusisha malighafi, watenda kazi na vitendea kazi. Matokeo ni bidhaa/huduma mbalimbali zinazotakiwa na walaji wa sokoni.

Na mchakato ni utaratibu wa mageuzi unaofanyika ndani ya mfumo wa uzalishaji kwa kufinyanga maingizo-ghafi ili kuzalisha matokeo-safi, kama vile unga lishe.

Kwa hiyo, katika mfumo wa uzalishaji, “mtu wa haki” anapaswa kutupia jicho lake kwenye maeneo manne ya haki na majukumu ya kiuchumi, kama ifuatavyo:

Kuheshimu anatomia ya haki na majukumu katika hatua ya maingizo kunajumuisha mambo yafuatayo, kati ya mengine:

  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika ushiriki (participative justice): Matangazo ya kazi na usaili wa waajiriwa wapya lazima vifanyike ili kuruhusu watenda kazi bora kushiriki katika uzalishaji;
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika mchakato wa ajira (procedural justice): mikataba ya ajira lazima isainiwe kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini.
Kuheshimu anatomia ya haki na majukumu katika hatua ya mchakato wa uzalishaji kunajumuisha mambo yafuatayo, kati ya mengine:
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika kuchangia kapu la mapato ya pamoja (contributive justice): Waajiriwa lazima watekeleze wajibu wao kwa kuchangia juhudu na maarifa katika uzalishaji; waajiri lazima waandae vitendea kazi sahihi, vinavyotosheleza mahitaji ya uzalishaji, na mapema; waajiri lazima wachangie uzalishaji kwa kubadilisha vitendea kazi vitakavyoharibika au kuchoka;
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika mchakato wa kazi (procedural justice): Waajiriwa lazima watekeleze wajibu wao kwa kuzingatia taratibu za kazi zilizokubaliwa kwa pamoja kati yao na waajiri; mwajiri akitaka kumpa adhabu ndogo mwajiriwa lazima azingatie mwongozo wa kisheria; mwajiri akitaka kumfuta kazi mwajiriwa lazima azingatie mwongozo wa kisheria;
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika mabadilishano ya kazi na ujira (commutative justice): Mwajiri lazima amlipe mwajiriwa kulingana na juhudu zake kazini; na mwajiriwa lazima atende kazi kwa bidii kulingana na malipo ya kila mwezi yaliyokubaliwa kwa pamoja.
Kuheshimu anatomia yahaki na majukumu katika hatua ya matokeo kunajumuisha mambo yafuatayo, kati ya mengine:
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika mabadilishano ya kazi na ujira (commutative justice): Waajiriwa lazima walipwe ujira wao kwa mujibu wa mkataba; wanahisa lazima wapate gawio/faida stahiki kulingana na hisa walizowekeza;
  • Haki na majukumu yanayohusiana na usawa wa fursa katika kuchangia kapu la mapato ya pamoja (contributive justice): mwajiri lazima alipe kodi ya serikali; mwajiriwa lazima alipe kodi ya serikali; mwajiri lazima alipe mafao ya pensheni katika mfuko wa jamii; na mwajiriwa lazima alipe mafao ya pensheni katika mfuko wa jamii;
  • Haki na majukumu yanayohusiana na mgawanyo wa keki ya pamoja (distributive justice): makampuni lazima yatimize majukumu yake ya kutoa huduma stahiki kwa jamii inayoyazunguka ili kupunguza makali ya maisha kwa sababu ya miundombini iliyojengwa katika ujirani na jamii.
Na kuna kuheshimu anatomia ya haki katika hatua ya mrejesho (corrective justice) ambako kunajumuisha mambo yafuatayo, kati ya mengine:
  • Pale ambapo kuna dosari katika ngazi ya maingizo, mchakato au matokeo, marekebisho lazima yafanyike ili kuondoa dosari hizo.
  • Mfano, malimbikizo ya mishahara lazima yalipwe, malipo ya pensheni lazima yafanyike, waliofukuzwa kwa bahati mbaya au vinginevyo lazima warudishwe kazini; na kodi sahihi lazima ilipwe.
Kwa vile serikali ni mwajiri mkubwa zaidi, ni wazi kwamba, niliyoyasema hapo juu yanaihusu pia.

Nafahamu kwamba, kwa muda wa mikaka mitano hivi, kuna watu hawajalipwa pensheni zao; kuna watu mikataba yao imevunjwa kinyume cha sheria;

Kuna watu wengi wameajiriwa katika taasisi kadhaa za umma bila hata kufanyiwa usali na kupewa nafasi za umeneja na ukurugenzi. Hili ni tatizo linalohitaji kurekebishwa ili kulinda uhai wa taasisi hizo.

Katika baadhi ya mashirika ya umma kuna watu walijaribu kupinga mikataba yao kuvunjwa kibabe.

Lakini kwa sababu hiyo ama walifunguliwa kesi za uhujumu uchumi au kesi za matumizi mabaya ya madaraka ili kuwanyamazisha. Kesi hizo mpaka leo zipo ama TAKUKURU au polisi au mahakamani.

Mtakatifu Thomas Aquinas alirasimisha mfumo wa maadili asilia na kuufupisha katika maneno mafupi haya: tunawajibika kutenda wema, na kuepuka kutenda ubaya."

Katika ufafanuzi wake anaonyesha kuwa, kutenda wema ni kukuza mema yanayoendana na asili ya binadamu, na kutenda ubaya ni kujeruhi mema yanayoendana na asili ya binadamu.

Kwa hiyo akahitimisha kuwa, kwa mujibu wa maadili asilia, matendo yanayokuza mema yanayoendana na asili ya binadamu ni halali kimaadili, na matendo yanayojeruhi mema yanayoendana na asili ya binadamu ni haramu kimaadili.

Kazi ni mema ya binadamu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kumwezesha kumudu maisha yake kwa kujipatia mahitaji muhimu maishani.

Kwa hiyo, matendo ya ubaguzi, ukatili na uonevu katika sehemu za kazi ni matendo haramu kimaadili kwa kuwa yanajeruhi mema ya binadamu yanayohusiana na ajira.

Kutokana na uzoefu wangu katika sekta ya vyama vya wafanyakazi nafahamu kuwa, sheria zetu za ajira na mahusiano kazini zinakubaliana na mfumo wa maadili asilia kwa sehemu kubwa.

Kimsingi, mfumo wa maadili asilia unasema kuwa, lengo kuu la ustawi wa binadamu linaweza, na linapaswa, kuhalalisha mbinu yoyote halali kwa ajili ya kulifanikisha.

Hii maana yake ni kwamba, kwa mujibu wa mfumo wa maadili asilia, lengo kuu la ustawi wa binadamu linaweza, na linapaswa, kubatilisha mbinu yoyote haramu inayotafutwa ili itumike kama njia ya kufanikisha lengo hili.

Pamoja na ukweli huu, sheria za ajira na mahusiano kazi, katika sekta ya umma na katika sekta binafsi, tayari zimepelekwa likizo isiyo na malipo kwa muda mrefu sasa.

Zinaweza na zinapaswa kurejeshwa kazini kwka ajili ya kulinda utu wa wafanyakazi.

Nawaalika wanachama wa Umoja wa Wanaume Katoliki (UWAKA) na watanzania baki kuzidi kutafakari juu ya maudhui ya waraka wa Papa Leo wa XIII uitwao “Mabadiliko ya Kimapinduzi (Rerum novarum),” pamoja na waraka wa Papa Yohanne Paul wa II uitwao “Miaka 100 Baada ya Mabadiliko ya Kimapinduzi (Centesmus Anus).”

Wito wangu ni kwamba, UWAKA wasisahau kusoma nyaraka hizi pia.

Napenda kuwasilisha, na pia nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
 
Back
Top Bottom