Askofu: Matatizo hayawezi kwisha kwa mabomu, virungu

Mtoboasiri

JF-Expert Member
Aug 6, 2009
5,101
1,946
Awila Silla,Dodoma
na Tumsifu Sanga
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo amesema, matatizo na migogoro inayoikabili Taifa hivi sasa haiwezi kunyamazishwa au kutatuliwa kwa kutumia nguvu za mabomu ya machozi na badala yake serikali itafute muafaka sahihi wa kuyatatua.
Akihuburi jana katika ibada ya maadhimisho ya Jumapili ya Siku ya Matawi katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, pamoja na mambo mengine, askofu huyo alisema muda umefika kwa serikali iliyoko madarakani tangu uhuru na kwa miaka 50 sasa kuleta mabadiliko yatakayokidhi maisha ya sasa na si vinginevyo.

Akifafanua kuhusu maana halisi ya maadhimisho ya Jumapili hiyo, Askofu Mhogolo alieleza kuwa maandamano ni ishara na hatua ya mwisho ya haki ya msingi baada ya haki kupuuzwa na kutosikilizwa.

Aliitaka serikali kutatua kero hizo kwa kuleta ufumbuzi na kuondoa dhana ya kutaka kupora au kupindua serikali madarakani."Mimi nashangaa kwanini serikali hajiamini, mbona tulifunga na kuwaombea ili Mungu awape hekima na busara ya kuiongoza nchi kwanini hamtaki kuitumia fursa hiyo?,alihoji Askofu huyo.

Alisema wananchi wana haki ya kudai wanachotaka kwa kutimiziwa kwa kuwa walioko madarakani wakifanya hivyo watasaidia kudumisha amani ya nchi na jamii na sio kuthubutu kunyamazisha madai hayo kwa virungu na vitisho vya vikosi vya FFU.

"Hili ni taifa letu pekee tunalojivunia na kamwe hakuna lingine ulimwenguni, kwanini tunatumia nguvu na kudharau amani kwa kuchafua na kujaza anga aliyotupa Mungu kwa moshi wa mabomu?

"Juzi nikiwa Ulaya nilisoma kwenye mtandao, nikashangaa sana Tanzania inapoelekea pale nilipoona serikali iliamua kuwapiga watoto wa shule na vyuo kwa virungu na kwa silaha kama wanyan'ganyi, kisa eti wameandamana, huku wakisahau wanalipwa mishahara kupitia kodi zao," alisema Askofu huyo.

Askofu huyo alisikitishwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa kugeuza nchi inayodaiwa ni kisiwa cha amani kuwa ya zomea zomea kwenye mijadala na vikao vya bunge iliyoibuka hivi karibuni na kusema kuwa huo ni mmonyoko wa maadili na kutaka jamii iheshimu na kumurudia Mungu.

Katika hatua nyingine aliwataka viongozi wa dini kuacha tabia ya kuingiza udini kwa lengo la kuisaidia serikali kwa kuwa kufanya hivyo wanaacha misingi na wajibu wa majukumu yao.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka wananchi kuacha unafiki na kuwa majasiri wa kupambana na ufisadi kwa nguvu zao zote.

Askofu Pengo aliyasema hayo jana wakati wa Ibada ya kuadhimisha Dominika ya matawi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph Jijini Dar es Salaam.Alisema ufisadi hautakwisha kama wananchi hawatakuwa jasiri katika kutetea haki na kupiga vita rushwa.

“Tunapiga kelele kwa makundi kusema mafisadi, lakini bado wananchi hawana ujasiri wa kusimama mmoja mmoja kuwaataja mafisadi na wala rushwa."Tunapaswa kuwa na ujasiri katika kutetea haki na si kupindisha haki kwa kupewa rushwa,”alisema Kadinali Pengo.

Alifafanua kwamba watu kama hao wanaopindisha ukweli kwa sababu ya rushwa waliyopokea hawana tofauti na Yuda aliyemsali Yesu kwa kupokea vipande thelathini vya fedha.“Hata mimi sijui, labda akija mtu na Sh500 milioni ili nipindishe haki labda naweza kupokea. Hilo ni swali kwa kila mmoja wetu, tunapaswa kuwa wajasiri katika kusimamia haki na si kukubali kupokea rushwa.


“Siku hizi watu wanapokea rushwa ya Sh5,000 ikizidi sana Sh50,000 ili kupindisha haki halafu tunalalamika mambo yanakwenda vibaya wakati hao wanaofanya hivyo tumewachagua wenyewe,” alisema Kardinali Pengo.


Source: Mwananchi (Jumatatu 18 April 2011)
 
Yep, wacha waseme ukweli na ukweli utuweke huru. Wanaolalamika kwa Dr. Slaa kutaja Majina ya Mafisadi sasa wacha waelezwe vyema na viongozi wa kiroho ili waelewe vyema
 
nakuunga mkono askofu.ni kweli kabisa.tupo kaitka dunia ya kutatua matatizo kwa kutumia hoja na akili zaidi na si mabavu.
 
Back
Top Bottom