MRADI MKUBWA WA KUJENGA TAIFA 2021
Mwaka 2020 umemalizika. Tunaanza mwaka mpya wa 2021.
Ipo miradi mingi mikubwa ya kitaifa inaendelea. Tunamshukuru Mungu miradi mikubwa ya madaraja, reli, barabara, viwanja vya ndege, ndege, vyuo vikuu na kufua umeme inaendelea vizuri na kukamilika kwake kutainua uchumi wa taifa letu.
Tutakumbuka Baba wa Taifa alitumia muda mrefu katika mradi wa kujenga taifa. Awamu zilizofuata zilitumia muda mwingi kujenga uchumi, miundombinu, elimu, afya, mifumo ya kiutumishi, na hata mihimili ya dola. Awamu hii imefanana na awamu ya baba wa taifa kwani imejikita kujenga miradi ya taifa ambayo itainua uchumi wa Taifa la Tanzania. Yote haya ni mazuri kwa ustawi wa taifa letu
Afya ya taifa hivi sasa ni nzuri. Taifa letu limekuwa ni mfano wa kuigwa kwa mataifa ya Afrika na mabara mengine, kwani tumemtegemea Mungu na kumuita naye akatuvusha katika ugonjwa wa COVID-19 uliotaka kushambulia moyo wa taifa, mapafu ya taifa, figo za taifa, miguu ya taifa, midomo ya taifa, na hata macho ya taifa. Mungu ameonekana na kutuondoa kwenye mauti ya ugonjwa huo na hata sasa tuendelee kumuomba Mungu ili aendelee kuliepusha taifa letu na ugonjwa huo.
Kama taifa Mungu ametuonesha kuwa yeye ni msingi wa ustawi wetu, basi 2021 tusimame na Mungu naye atakuwa msingi wa kila jambo la maendeleo yetu.
Ipo haja ya kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa taifa letu kwa umoja pasipo kujaji utofauti wa itikadi za kisiasa. Kwani Taifa halijengwi kwa mawe na matofali. Linajengwa kwa umoja wetu, kusikilizana, kuelewana, kusameheana, kuonyana na kuheshimiana.
Miradi mingi ikijengwa juu ya taifa imara, ni sawa na kujenga nyumba kwenye mwamba. Mafuriko na dhuruba zikija haiwezi kuporomoka. Taifa kama ilivyo nyumba, hulindwa na uimara wa misingi ya umoja. Mungu alilinde taifa letu, aviongoze vikosi kazi vya ulinzi na kuvipa ufanisi wa kulitumikia taifa.
Kwa hekima yote, ninasihi na kuombea miradi ya taifa ifanikiwe. Kwani itajenga uchumi, itachochea amani, italinda madaraja, viwanda, na hata kukaribisha wawekezaji wasio wanyonyaji.
HAYA SHIME WANA NA MABINTI WA MAMA TANZANIA. TUMUOMBE MUNGU ALILINDE TAIFA LETU.