Askofu Dkt. Bagonza: Kumnyamazisha anayekemea wizi wa kura ni kujitangaza kuwa mwizi

OKW BOBAN SUNZU

JF-Expert Member
Aug 24, 2011
32,865
2,000
Kuna wanasiasa lakini hawaijui siasa. Wanaitwa wanasiasa kwa sababu wako kwenye nafasi za Kisiasa. Kuna watu si wanasiasa lakini wanaijua siasa. Hawako kwenye nafasi za Kisiasa lakini ni watu muhimu katika kuboresha maisha ya Kisiasa kwa sababu wanaijua siasa.

Pima joto la Kisiasa hapa nchini tangu Sasa mpaka siku ya uchaguzi linalazimisha matumizi ya akili kuliko nguvu. Nashauri yafuatayo yaaminiwe na kuzingatiwa:

1. Matusi kwa mgombea usiyempenda hayaongezi kura kwa unayempenda.

2. Matusi ya mashabiki humuathiri mgombea hata kama hakuwatuma. Kimya cha mgombea kuhusu matusi huchukuliwa kuwa ndiye anawatuma. Wagombea jifunze "kufungia mbwa wenu" maana hawana faini ya kulipa.

3. Double Standards (upendeleo) husababisha huruma za wapiga kura kwa anayeonewa. Usionee wala kupendelea.

4. Udhaifu wa mgombea usiyempenda hujulikana kwa kumpa nafasi ajieleze. Ukimnyima nafasi unamsaidia kuficha udhaifu wake.

5. Hatari ya mgombea kwa jamii hujulikana kwa kumruhusu ajulikane. Ukizuia asijulikane unashiriki kuitumbukiza jamii ichague mtu hatari. Ruhusu vyombo viwatangaze wagombea wote.

6. Uwongo husaidia pale usipogundulika. Teknolojia imeziba mwanya huo. Ukweli unauma lakini unaponya. Teknolojia haisahau lakini wananchi wanasahau upesi. Omba radhi usonge mbele.

7. Wenye dhamana zisizoruhusu itikadi, jifunzeni kuishi na hali msiyoipenda. Wagombea wakishinda au kushindwa kwa haki ni wepesi kusamehe. Visasi ni tabia ya walioshinda kwa hila.

8. Kila mgombea akemee wizi wa kura. Kumnyamazisha anayekemea wizi wa kura ni kujitangaza kuwa mwizi. Haki na uwazi hufunga midomo ya wanaotuhumu ovyo ovyo.

9. Jihadharini na Viongozi wa dini, wawe wa Kiroho au kimwili. Walishirikiana na mkoloni; alipoondoka wakashirikiana na mkombozi. Awamu huja na kupita lakini wao wapo. Walikuwa wajamaa na ujamaa ulipokufa, wakakumbatia ubepari uchwara. Hata ufisadi wana uwezo wa kuubatiza/kuusilimu na kuubariki. Ukitaka kuwatukana FIKIRI mara mbili. Hawa ni watumishi wa nyakati zote. Hujui Nani atakuzika.

10. Kusemasema na kuandika andika kwaweza kuwa uchochezi. Lakini kimya ndio uchozezi wa kiwango cha juu. Kimya kinaua, kinasaliti, kinaunga mkono na kupinga hapo hapo. Tunakoelekea kuna watakaokamatwa kwa kutocheka wakati wengine wanacheka au watakamatwa kwa kununa wakati wengine wanatabasamu
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom