Deogratias Mutungi
Senior Member
- Oct 1, 2019
- 137
- 178
ASKOFU BAGONZA NAULIZA, UPO UPANDE UPI KISIASA?
Na, Deogratias Mutungi
Nianze makala haya kwa kurejea msemo wa wahenga wa kiswahili usemao “Kuuliza si ujinga” aidha mwenye kuuliza ujengwa katika tabaka la udadisi, kwa muktadha huo udadisi si utundu wala ukorofi bali ni uungwana ulio jaa hekima na busara na misingi ya uungwana ni vitendo, kwa dhana hiyo swali la makala haya linajengwa katika wema wa mantiki ya kutaka kupata jibu la msingi na lenye ukweli ndani yake, maana ukweli umuweka mtu huru, na ndio hasa maudhui na kiini cha makala haya na si vinginevyo.
Ni imani ya makala haya kuwa mlengwa wa swali hili hawezi kununa, kufura na kuugua homa za vipindi wala kunungunika juu ya swali hili lenye mantiki pana katika mazingara ya jamii yetu ya kisiasa na mifumo yetu ya kuabudu hasa kwa karne hii ya haki na uhuru wa kuhoji na kutoa maoni, Makala haya yanahoji kizalendo na bila shaka yatajibiwa kizalendo zaidi.
Muktadha wa swali hili unaangukia kwa Dkt. Benson Bagonza Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, swali linanyumbulishwa ndani ya mfumo wetu wa siasa ambao unaegemea katika ulali wa mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992, aidha makala haya yanatambua na kuheshimu haki za kikatiba alizonazo Dkt. Bagonza hasa katika eneo la kujieleza, kutoa maoni yake na kukosoa mamlaka pale inapobidi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, Imani ya makala haya ni kuwa anachokifanya Dkt. Bagonza kipo sahihi kabisa isipokuwa ukosefu wa uhalali wake wa kujitambulisha anasimamia utambulisho wa itikadi ipi ndio nongwa na dukuduku ya swali hili inapoanzia dhidi ya Baba Askofu.
Wapinzani wanatambulika kupitia itikadi za vyama vyao, Mwenyekiti wa Chadema anaongoza falsafa na misimamo kupitia utambulisho wa chama chake na ukisikiliza hoja zake ni lazima utambue hilo, Zitto Kabwe anatambulika kwa itikadi na misimamo ya chama cha ACT-Wazalendo, Mwana CUF utamtambua kwa itikadi ya chama chake, aidha wanaharakati wenye mirengo ya kuipinga na kukosoa harakati za kisiasa pia utawatambua kwa desturi, mifumo na taratibu zao za kupinga utawala kwa kivuli cha demokrasia.
Aidha ieleweke kuwa mantiki kuu na dhana ya swali hili ni kutaka kujua ukweli wa mambo kutoka kwa Baba Askofu mwenyewe badala ya mitandao ya kijamii na watu binafsi kujenga hoja na kutaka kuhitimisha mjadala huu bila upande wa pili kuhojiwa au kuulizwa “natural justice”yaani kutompa nafasi Baba Askofu kujieleza ni kosa la kiufundi na pengine ni dhambi ya makusudi, hivyo basi makala hii imeona ni vyema kuhoji na kuuliza ni upande upi wa siasa Baba Askofu anasimama kati ya X au Y ikiwa na maana X Chama tawala au Y Vyama vya upinzani, bila shaka Baba Askofu ataweka mambo hadharani na taifa linamsubiri kwa hamu kubwa sana kwa maana kuwa ni muda mrefu sasa amekuwa mfuasi wa upande Fulani wa siasa lakini kwake imekuwa ngumu kujitambulisha, Sasa Baba Askofu makala haya yanakuomba kujitambulisha rasmi hasa kwa kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu hapo oktoba kuwa wewe ni chama gani cha siasa.
Hata hivyo sijambo la ajabu viongozi wa dini kukosoa mamlaka zilizopo madarakani katika kujenga taifa imara na lenye demokrasia inayosimamia na kuzingatia haki na usawa wa binadamu ni sehemu ya jukumu lao kufanya hivyo na mataifa mengi duniani yamefanya hivyo, lakini inapoonekana kiongozi wa dini anapotea njia na kusahau mipaka yake katika kukosoa na kujenga hoja hasi na kuonyesha ushabiki wa kuegemea upande Fulani wa kisiasa hasa kwenye taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi ni bora mtu huyo aulizwe na ajulikane ni wa moto au wa baridi kuliko kuwa wa uvuguvugu.
Inawezekana kabisa kukawepo na wasiwasi na sintofahamu kwa wasomaji wa makala haya juu ya swali hili kwa Baba Askofu Dkt. Benson, Makala haya yanawaondoa hofu kwa kujenga hoja yenye afya kuwa mantiki ya swali hili ni matokeo ya misimamo hasi na yenye mrengo wa kukosoa kila kitu kinachofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya JPM inayojengwa na Baba Askofu, Je Baba Askofu hajaweza kuona chochote kizuri kilichofanywa na serikali hii au yeye amechagua eneo moja la kukosoa.
Kwa sababu wapo wanaojenga hoja za kuhukumu misimamo ya Dkt. Benson nadhani si sahihi kuhukumu, isipokuwa usahihi wa mantiki tunaweza kuujenga katika nadharia ya kuhoji badala ya kuhukumu kwa kuuliza swali hili Dkt. Benson ni mwanachama wa chama gani cha siasa? CHADEMA, CUF,ACT-Wazalendo, TLP, NCCR-Mageuzi au CHAUMA.
Makala haya yanataja vyama vya upinzani tu ndani ya swali hili kwa sababu ni fimbo ya aina gani upendelea kuitumia kushambulia wenzake isipokuwa tu aina ya mti ndo haufahamiki kama ni fimbo ya mti gani kwa kuondoa hofu hii ni sharti Baba Askofu aulizwe kwa mantiki ya kutaka kujua ukweli wa aina ya mti anaoutumia kupata fimbo zake, bila shaka hoja ya nadharia ya swali langu inaeleweka kwa msomaji wa makala haya.
Dhana inayojengwa kumuhusisha Dkt. Benson na upinzani ni matokeo ya tabia na hoja, mitizamo na falsafa zake ambazo ujengwa katika nadharia ya upinzani na hivyo kumhalalisha kuwa ni mpinzani mwenye vinasaba vya falsafa za kupinga kila dhana ya chama tawala CCM na serikali yake aidha iwe nzuri au mbaya jukumu ni moja tu kupinga na hilo ndio azimio linalo utambulisha upinzani wa Afrika katika medali za kisiasa kuwa ujengwa katika mifumo ya kupinga tu, Japo dhana ya upinzani si kupinga tu bali kukosoa na kusifia mafanikio ya serikali au chama dola kwa sababu Afrika ukomavu wa kisiasa ni mdogo ni nadra kukutana na chama chenye falsafa na mitizamo ya namna hiyo.s
Kwa sababu Dkt.Benson Bagonza anaangukia kwenye kapu hilo ndo maana anaulizwa yupo upande upi wa siasa? Dkt. Benson Bagonza ni msomi na muungwa bila shaka atajibu swali hili ili kuondoa wasiwasi watanzania wenye uchu wa kujua ni mfuasi wa chama gani cha siasa miongoni mwa vyama vilivyopo hapa nchini, makala haya yanaamini Baba Askofu ni jasiri na shupavu hivyo hawezi kuogopa kutambulisha chama chake.
Ifahamike kuwa si dhambi wala kosa la jinai kwa Dkt. Benson Bagonza kujitambulisha bayana na kwa uwazi ni itikadi gani na mrengo upi anaufata kisiasa kwa kukitambulisha rasmi chama chake cha siasa anachokiamini si busara kwa Baba Askofu kuendelea kukaa na siri hii ni vyema sasa ikatolewa hadharani, aidha inaweza kuwa alama itakayo kumbukwa katika vitabu vya kihistoria kuwa kiongozi wa dini aliyethubutu kusimamia kile kilicho moyoni kwa kuonyesha ni mwanachama gani wa chama cha siasa kwake utakuwa ushujaa na heshima iliyotukuka.
Kwa sababu makala haya yanaamini kuendelea kufanya siasa kwa kutumia kofia ya uaskofu au kivuli cha kanisa bila kujitambulisha rasmi ni jambo ambalo kimantiki linaonyesha udhaifu wa mtu au kikundi cha watu wasivyokuwa na msimamo unaoeleweka katika kusimamia yale wanayoyaamini, ni kheri kabisa na bora kujitokeza hadharani na kujitambulisha kwa wanachama wenzako wakufahamu na kukutumia kimkakati pale utakapo hitajika na huu ndio ukomavu wa siasa za kidemokrasia zenye mfumo wa vyama vingi.
Ni rai ya makala haya kumuomba Baba Askofu ajitokeze na ajibu hoja, aidha ni imani ya makala haya kuwa Baba Askofu hataweza kuwa na woga wala wasiwasi wa kutambulisha chama chake cha siasa kwa watanzania, Kwa mantiki hiyo tunasubiri kwa hamu na bashasha tele kusikia neno kutoka kwa Baba Askofu.
dmutungid@yahoo.com