Askari wa miguu wa burma (the burma infantry) 1942


Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined
Nov 2, 2008
Messages
11,440
Likes
6,851
Points
280
Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined Nov 2, 2008
11,440 6,851 280
BURMA.jpg


Kulia Abdulwahid Sykes na mdogo wake Ally Sykes
wakiwa katika kikosi cha Burma Infantry 1942

Utangulizi

Leo ni siku ya kumbukumbu ya walipoteza maisha yao katika Vita Kuu mbili za Dunia. Waingereza kwao siku hii ni muhimu sana na wanaiadhimisha kwa heshima zote. Nimehamasishwa kuweka hapa kipande hiki kutoka kitabu cha Abdul Sykes na kipindi cha Al Jazeera ‘’The Burma Boys,’’ kuhusu askari kutoka Afrika ambao walipigana katika King’s African Rifles (KAR) katika misitu ya Burma dhidi ya Wajapani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1938 – 1945).

Kipindi hiki kimeeleza historia ya askari kutoka Ghana na Nigeria. Nimeona niweke hapa yale ambayo marehemu Ally Sykes alinieleza kuhusu askari waliotoka Tanganyika kwenda kupigana Burma yeye na kaka yake wakiwa miongoni mwa askari hao.

Lakini kubwa ambalo biinafsi siku zote limekuwa likinigusa ni kuwa ilikuwa wakiwa Burma katika Bataliani ya Sita ndipo askari kutoka Tanganyika wakiongozwa na Abdul Sykes walipoamua kuunda chama cha TANU kuwaondoa Waingereza katika ardhi ya Tanganyika.

Abdulwahid - jina limaanishalo 'Mtumishi wa Allah, Mmoja na Aliye Pweke alikuwa mjukuu wa Sykes Mbuwane, shujaa aliyetoka mbali na kupoteza maisha yake Tanganyika, akipigana katika jeshi la Wajerumani. Shuleni Abdulwahid alikuwa daima anaogoza katika darasa lake.

Alipomaliza masomo yake ya msingi katika Al Jamiatul Muslim School alichaguliwa kuingia shule ya serikali (Dar es Salaam Government School) ambako alifundishwa na Mwalimu Mdachi Shariff. Shariff alikuwa rais wa Tanganyika Territory African Civil Service Association (TTACSA). Abdulwahid alimaliza darasa la kumi na kufanya mtihani wa kuingia Makerere College ambao aliongoza.

Serikali ya kikoloni, kutokana na msimamo wa siasa wa baba yake, ilimfanyia khiyana asiingie Makerere kwa kisingizio kwamba alikuwa na umri mdogo. Wakati huo Abdulwahid alikuwa na umri wa miaka kumi na saba. Ingawa Waingereza waliuonaumrihuu mdogo kuendelea na masomo katika Makerere, lakini Waingereza waliuona kamautoshao kumwandikisha kwenda kupigana vita kama askari katika Kingís African Rifles (KAR)!

Mwaka wa 1941 Abdulwahid, bila ya khiyari yake aliandikishwa katika jeshi la KAR kwenda kupigana katika Vita Vya Pili vya Dunia vilivyokuwa vinaendelea Ulaya na sehemu nyingine za dunia. Hili lilikuwa pigo kubwa kwa Kleist. Mwanaye alikuwa bado yupo katika orodha ya wanafunzi waliokuwa wakitaraji kuingia Makerere College huko Uganda.

Kleist alikuwa na matumaini makubwa kwa mwanae. Kuchukuliwa kwa Abdulwahid kwenda vitani kulikatisha ndoto yake kabisa. Kleist hakuwa na uhakika kama mwanae angenusurika au angerudi jina tu. Mwaka 1933 Kleist aliandika usia ambamo ulionyesha mapenzi aliyokuwa nayo kwa watoto wake.

Aliwaambia katika usia ule kuwa ilikuwa ni mapenzi yake, Mwenyezi Mungu akijaalia, kuwasomesha hadi kufikia kiwango cha juu kabisa, Makerere ama Ulaya. Ikitokea atafariki kabla ya kutekeleza azma hii, aliwataka waitimize nia yake hii wao wenyewe kwa kusaidiana.

Kleist hakuwa mtu wa maneno matupu. Alihakikisha anawaachia watoto wake mali ya kutosha ili kukamilisha haja hiyo. Usia huu uliposomwa baada ya kufa kwake mwaka 1949, hali ya siasa nchini Tanganyika ilikuwa ikibadilika kwa haraka - na vivyo hivyo majaliwa ya Abdulwahid na nduguze.

Askari wa zamani waliopigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza katika ardhi ya Tanganyika wakati wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia kati ya mwaka 1914-1918 walimuunga mkono Hitler, ingawa si wazi wazi kwa kuwa kufanya hivyo kungekuwa usaliti na uhaini dhidi ya Himaya ya Waingereza.

Hata hivyo hilohalikumzuia Schneider Plantan, askari wa Kijerumani wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia, kutembea huku na kule katika mitaa ya Dar es Salaam akiwachochea watu wasimuunge mkono Winston Churchill katika vita vyake dhidi ya Adolf Hitler. Schneider alikamatwa na kuwekwa kizuizini huko Mwanza, na hakufunguliwa hadi mwisho wa vita mwaka 1945.

Wengi wa askari hawa,waliokuwa katika jeshi la Wajerumani katika Vita Kuu ya Pili walikuwa wamepitisha umri wa katikati. Hivi Vita vikuu viwili vilikuwa vimetengana kwa miaka ishirini na nne tu. Askari hawa wa zamani walikuwa na kumbumbu za kile walichokiona kuwa utawala wa haki na uadilifu wa "Wadachi", Kama Wajerumani walivyokuwa wakiitwa na wazee hao wakongwe wa Vita ya Kwanza ya Dunia. Lakini Kleist hakukubaliana na mtazamo huu.

Alikuwa na fikra zake mwenyewe za haki na uadilifu. Alikuwa anavipinga vita hivyo kwa sababu yeye aliifahamu vyema hatma ya vita vile kwa Waafrika wa Tanganyika. Alijua iwangeendelea kutawaliwa tu ingawa safari hii huenda akaja mtawala mwingine.

Baada ya Abdulwahid kupelekwa vitani na Waingereza, pigo jingine lilifuatia. Ally alitoroka nyumbani akaenda kwenye kambi ya jeshi la Waingereza na kujitolea kuwa askari wa KAR Ally akiwa na umri wa miaka kumi na tu. Kituo cha kuandikisha askari kilikuwa Kilwa Road.

Ally alitoroka kwa sababu alijua wazazi wake wasingemruhusu kujiunga na jeshi. Alimuonea gere kaka yake kwa kuwa mbali na nyumbani akiwa huru, tena mwenye kujitegemea, na kuwa na maamuzi yake mwenyewe mbali na amri za baba yao. Kleist alikuwa mkali sana. Aliitawala nyumba yake kama kambi ya jeshi. Hakuwa mtu wa kupenda mchezo ama upuuzi.

Ally alikuwa chini ya umri uliotakiwa kuajiriwa vitani. Kleist alidhania serikali ingetilia maanani umri mdogo wa Ally na hivyo kutompokea katika KAR. Lakini maadam Ally alikuwa amejitolea kwa khiari yake mwenyewe, Waingereza walimpokea kwa mikono miwili. Kama kaka yake, Ally alipelekwa Kabete kwa mafunzo ya kijeshi ili kwenda kupigana Burma.

Ally alipojiunga na KAR Abdulwahid alikuwa tayari ameondoka kwenda Nairobi, Kenya kupata mafunzo ya kijeshi kama askari wa miguu. Ally alipowasili Kabete kwa mafunzo, Abdulwahid alikuwa tayari ameondoka kwenda Ceylon (Sri Lanka) baada ya kupewa likizo ya kurudi nyumbani kuaga wazazi wake. Kleist alisafiri kwenda Nairobi kuonana na Ally kabla ya kuondoka kwake kwenda Ceylon, lakini alizuiwa kuingia kambini kumuaga mwanae.

Misiba miwili ilikuwa imemsibu Kleist alikuwa na watoto wawili vitani wakimpigania adui wake wa zamani, Mwingereza. Kleist hakuwa na ndugu wengine wa damu mbali ya watoto wake watatu. Alijaribu kuwasiliana na ndugu zake nchini Msumbiji lakini bila mafanikio. Kleist alihangaishwa na mawazo. Vipi ikiwa hawa wanawe wawili watafariki... fikra hiyo ilikuwa nzito. Kleist na mkewe Bibi Mruguru Mussa walibakia na kijana mmoja tu Abbas kuwafariji.

Bibi Mruguru, tofauti na mume wake hakuweza kuwa na subira na kuzuia uchungu wake moyoni. Alikuwa ameolewa na Kleist alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu tu na alimzaa mwanae wa kwanza Abdulwahid akiwa na umri wa miaka kumi na tano.

Kwake yeye, wanae kwenda vitani kulimaanisha kifo. Taarifa zilikuwa zikipokelewa mjini Dar es Salaam kila siku toka ng'ambo Kuhusu askari waliokuwa wakipoteza maisha katika mapambano. Bibi Mruguru aliwaona watoto wake kama tayari wameshaaga dunia. Hakuweza kula au kulala na alilia karibu wakati wote, wakati mwingine akijitupa chini kwa uchungu. Majirani na marafiki walimfariji kwa kumuambia: '’Bi Mluguru acha kulia usiwachurie watoto kwani watoto wangali hai na kuwalilia ilikuwa ni sawasawa na kuwachimvia.’’

Kwa woga wa watoto wao kupelekwa vitani, baadhi ya wazazi waliwaficha watoto wao wakubwa uani na kuwakataza kutoka nje. Kwa mila za watu wa pwani uani ni mahali pa wanawake. Wanaume hawakai huko, kwao wao ni barazani. Kleist alistahamili kimya kimya na alikuwa akifanya shughuli zake kama kwamba hakuna jambo lolote lililotokea.

Kleist alikuwa mtu jasiri na ilikuwa nadra kudhihirisha hisia zake. Kila asubuhi Bibi Mruguru alikwenda kwenye kituo cha kuandikisha askari pale Kilwa Road kuulizia habari za wanae.

Abdulwahid na Ally walikwenda ng’ambo kutumika chini ya Military Labour Service. Kikosi hiki kilianzishwa Julai 1940 wakati Italia, chini ya Mussolini, ilipojiunga na vita upande wa Wajerumani. Madhumuni ya kikosi hiki ilikuwa kusaidia majeshi ya washirika kwa kuwaingiza raia katika vita, kuwafundisha mbinu za vita na kuwekwa chini ya nidhamu ya jeshi.

Askari hawa kutoka uraiani walipewa kila kitu sawa na askari wa KAR kuanzia posho, mahali pa kulala, tiba, malipo ya uzeeni na malipo endapo ulemavu au kifo vitatokea. Kambi ya kuwafunza ilijengwa Kabete karibu na Nairobi kwa ajili ya mafunzo ya awali.

Mshahara kamili ulikuwa shilingi kumi na mbili kwa mwezi, posho ya kila siku pamoja na sare. Cheo kikubwa kwa Waafrika kilikuwa sajini, koplo na koplo lansi. Hawa walikuwa wakilipwa mishahara zaidi ya askari wa kawaida.

Askari waliondoka na meli kuelekea vitani kupitia Kilindini, Mombasa. Meli hizo zilisindikizwa na Jeshi la Wanamaji wa Uingereza (Royal Navy) ili kuzilinda na mashambulizi kutoka nyambizi hatari za Wajapani. Waafrika walikuwa wa kwanza kupelekwa Ceylon kwa mafunzo ya vita vya msituni kuunda lile jeshi lililokuja kuwa maarufu la askari wa miguu la Burma (Burma Infantry).

Jeshi hili ndilo lililokuja kupigana na Wajapani. Jeshi hili la askari wa miguu liliundwa na Waafrika kutoka nchi nyingi. Lilikuwa na Waafrika toka Northern Rhodesia (Zambia), Southern Rhodesia (Zimbabwe), Belgian Congo (Zaire), Nigeria, Gold Coast (Ghana), Kenya, Uganda na Tanganyika. Baadhi ya askari hawa waliwahi kupigana Abyssinia, (Ethiopia) na Somaliland (Somalia) ambako Waingereza na Makaburu wa Afrika ya Kusini walipambana na Wataliani.

Kutokana na kampeni iliyofanikiwa ya kikosi hiki nchini Abyssinia, ilionekana kuwa ni muhimu kuunda kikosi kama hiki kwa haraka. Hii ndiyo ilikuwa sababu ya serikali kutoa wito kutaka watu wa kujitolea kujiunga na KAR. Hawa Waafrika waliojitolea katika vita hivi walileta taathira kubwa na kusababisha ushindi wa Waingereza katika vita ile.

Mwaka wa 1943 Ally aliondoka bandari ya Mombasa katika msafara wa meli ukielekea Ceylon huku wakisindikizwa na wanamaji wa Kiingereza. Meli aliyopanda Ally ilikuwa ya abiria ambayo katika siku za amani ilikusudiwa iwachukue Wazungu tu wakati wa likizo. Chombo hicho hakikusudiwa kuwa na abiria Waafrika sembuse askari weusi.

Chombo kile hakikuundwa kuwachukua abiria hata Wazungu mafukara. Ilikuwa meli ya anasa kwa ajili ya Wazungu matajiri. Wakati meli ile inafanya safari zake za kawaida wakati wa amani Mwafrika ambae kwa bahati angekuwa ndani yake angekuwa mtumishi wa kuwahudumia abiria wazungu. Kazi yake ingekuwa kuwapelekea vinywaji, kuwasubiri mabwana wa Kiingereza na wake zao wakila chakula cha jioni huku wakimulikwa na miangaza ya mishumaa.

Waafrika hawa kazi zao nyingine labda ingekuwa kufagia na kusugua sakafu, kutandika vitanda na kusafisha vyoo. Lakini sasa Uingereza ilikuwa ikipigana vita vikali dhidi ya adui wenye nguvu, Ujerumani, Japan na Italia. Uingereza kuendelea kuwepo kama taifa kulikuwa hatarini, achilia mbali kunusurika kwa makoloni yake yaliyotawanyika duniani kote.

Haikuwa katika hali ya kuangalia nani bwana na nani mtwana. Ikiwa ile meli ya abiria iliweza kuwachukua waungwana wa Kiingereza kwenda Carribean kwa likizo kustarehe chini ya vivuli vya minazi, basi ingeweza vilevile kuwachukua Waafrika kwenda vitani kufa kwa ajili ya Mfalme.

Wakati msafara wa Ally ulipokuwa baharini kuelekea Colombo, moja ya meli ilipigwa kombora na nyambizi ya Wajapani. Chombo hicho kilizama na kuwaua askari wote pamoja na maafisa wao Wazungu. Askari mmoja tu kutoka Tanga aliyekuwa akijulikana kama Magembe ndiye aliyenusurika. Askari kwenye meli zingine hawakujulishwa juu ya msiba huu hadi walipowasili Colombo.

Maafisa Wazungu walidhani kuwa kama Waafrika wangejulishwa kuhusu msiba ule wakiwa bado katika bahari wangetaharuki na kuvunjika moyo. Licha yA Waafrika kujitoa muhanga, Wazungu waliwabagua askari weusi. Waafrika walipachikwa jina la ëmilitary labourí (vibarua wa kijeshi), wakati ambapo Wazungu kutoka Marekani na New Zealand walitambulika kama ëalliesí (washirika) ingawa wote walikuwa wanapigana vita moja chini ya amri moja..

Waafrika kwa kupewa nembo kama hizo walihisi kudhalilishwa na kujiona kuwa wao kazi yao kubwa ilikuwa kutafuta ushindi kutokana na nguvu za misuli yao; akili zao hazikuwa na nafasi katika vita vile. Wao walikuwa ni sawa na zana isiyokuwa na fikra, zana ya kutumiwa kukamilisha kazi ngumu. Askari Waafrika waliitwa natives yaani wenyeji.

Hao wenyeji vilevile walibaguliwa kati ya wenyeji wasemao-Kiingereza na wasiosema-Kiingereza. Mshahara wa askari wa Kiingereza ulikuwa wa juu zaidi kuliko wa Mwafrika katika cheo kilekile. Chakula kilitolewa kulingana na taifa la askari. Kulikuwa na chakula cha Mzungu, Muasia na Mwafrika, cha Mwafrika kikiwa ndicho hafifu kuliko vyote. Askari Mwingereza alipewa kile kilichokuwa kikijulikana kama, ‘’family allotment allowance,’’ ili aweze kuikimu familia yake huko kwao. Hakukuwa na ruzuku kama hiyo kwa Waafrika.

Waafrika walipewa mvinyo kama sehemu ya chakula chao wakati ambapo wazungu walipewa brandi, wiski na bia. Ilikuwa tu pale Waafrika walipoanza kuingia katika mapambano na Wajapani ndipo chakula kikawa sawa kwa wote bila kujali rangi au utaifa wa askari. Chakula hiki kwa lugha ya jeshi kilijulikana kama ‘’K’’ ration nacho kilikuwa kikidondoshwa toka juu angani na ndege za Kiingereza (British Royal Air Force).

Gazeti la jeshi lililokuwa likijulikana kama Second Enchelon, lililokuwa likichapwa kila wiki na kusambazwa katika kambi za majeshi ya washirika, lilichapisha jina na nambari ya Ally kwa makosa likidai alikuwa miongoni mwa wale waliokufa baharini. Ally alipofika kwenye kambi ya Kurnegala, nje kidogo ya Colombo, Abdulwahid alikuwa amekaa hapo katika kikosi cha Service Corps kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kikosi chake kilikuwa kikishughulikia usafirishaji na mawasiliano. Abdulwahid alikuwa anasema lugha zote mbili- Kiingereza na Kiarabu- vizuri sana; kwa sababu hii alipandishwa cheo kutoka koplo hadi kuwa sergeant. Abdulwahid alipata habari ya ‘’kifo,’’ cha mdogo wake katika gazeti hilo la jeshi na kumpelekea habari hizo za kuhuzunisha baba yake. Ilikuwa pale tu Ally alipowasili Kurnegala na kuzungumza na Abdulwahid kwa simu ndipo ilipotambulikana kuwa alikuwa yu hai.

Ally anakumbuka ilikuwa jioni alipowasili kwenye kambi hiyo. Amri ya kutotembea usiku tayari ilikuwa imeshaanza kuzingatiwa. Saa hizo hakuna askari aliyeruhusiwa kuwa nje ya kambi. Abdulwahid alikuwa katika kambi nyingine karibu na hiyo aliyofikia ndugu yake. Habari zilipomfikia kuwa mdogo wake amewasili, alipata shauku ya kumuona ndugu yake. Abdulwahid alichukua gari na kutoka kambini bila ya dereva na hali amri ya kutotembea usiku ingalipo.

Wakati ule Abdulwahid alikuwa amepandishwa cheo na kuwa "Quarter Master Sergeant" na sheria za kambi hazikumzuia yeye kutoka nje ya kambi wakati wa usiku. Ingawaje kwa kawaida alikuwa na dereva wa kumuendesha, Abdulwahid aliamua kuendesha mwenyewe jeep yake kwenda kumwona mdogo wake na kupata habari kutoka nyumbani. Majaaliwa ya binadamu yalivyo hayatabiriki, kwani dereva aliyekuwa akimuendesha Abdulwahid Burma,alikuja kushika nafasi ya juu katika Jeshi la Ulinzi la Watu wa Tanzania.

Ally, kama askari asemaye Kiingereza, alikuwa chini ya kikosi kilichojulikana kama Education Corps. Kazi yake ilikuwa kuwafundisha Wazungu Kiswahili ili waweze kuwaamrisha Waafrika hasa wale watokao Afrika ya Mashariki. Vilevile aliwafundisha kusoma na kuandika Waafrika ambao hawakupata bahati ya kupitia shule Kadhalika aliwafundisha jinsi ya kusoma ramani ili waweze kumudu kujua njia ndani ya misitu ile ya Burma ambayo ilikuwa inababaisha sana kwa mtu asiyekuwa na maarifa ya porini.

Ingawa askari kutoka Afrika walikuwa muhimu katika vita vile kama ilivyokwishaelezwa bado walidharauliwa na askari wenzao kutoka Ulaya na kwingineko. Jambo hili liliwafanya askari kutoka Afrika wajitazame upya.

Wakiwa pale Kurnegala, askari Waafrika walipata mafunzo ya kupigana msituni kwa miezi minne na kisha wakaondoka kwenda Burma kupitia Trincomalee. Kutoka hapo wakielekea Chittagong. Wakati wote huo wakiwa katika msafara walisindikizwa na British Royal Navy, meli zao zikienda polepole kwa tahadhari, zikipita njia ambayo walihisi ni shwari kutokana na mashambulizi ya Wajapani.

Ilikuwa hapo Chitagong ambapo askari walipata kwa mara ya kwanza kuonja kile kilichokuwa kikiwangoja. Kulikuwa na kitambo cha takribani kilometa kumi baina ya bandari na kambi. Barabara ilikuwa mbaya na ilikuwa imejaa matope ambayo yalifika kina cha kifundo cha miguu kutokana na mvua kubwa za monsoon. Kambi ilikuwa chafu kwa matope yaliyotapakaa kila mahali.

Askari ilibidi abebe mzigo wake mzito wa vifaa na zana, bunduki na risasi. Vilevile ilibidi wachimbe mahandaki siku hiyo hiyo kwa ajili yao wenyewe na kwa maafisa wao Wazungu. Kambi iiliwapa picha kamili ya kilichokuwa kikiwasubiri hata kabla hawajasikia milio ya bunduki za Wajapani.

Baada ya kufika Chitagong walikaa hapo kwa siku chache kisha wakasafirishwa kwenda Imphal, Burma, kwa malori ya Jeshi la India. Imphal ina umuhimu mkubwa kwa askari wa Burma waliotoka Tanganyika. Ilikuwa ni hapa, siku ya mkesha wa Krismas mwaka 1945, ambapo Abdulwahid na askari wengine, pamoja na mdogo wake Ally na James Mkande, walifanya makubaliano ya kuunda chama cha siasa kudai uhuru wa Tanganyika mara tu watakaporudi nyumbani baada ya vita. Imphal ilikuwa ndiyo "command centre "ya askari wa Burma.

Ilikuwa ukanda wa hatari ambapo Wajapani walikuwa wakipigana hasa na Waingereza. Askari wengi kutoka Afrika waliuawa Burma wakimtumikia Mfalme ili jua lisitue katika Dola ya Waingereza. Watanganyika wengi walipotezea maisha yao huko wakipigania kuiokoa Dola ya Waingereza chini ya Mfalme George. Kulikuwa na mwimbo wa kuisifu dola ya Mwingereza uliokuwa ukiimbwa hasa mashuleni, baadhi ya maneno yake yakiwa haya:

"Dola ya Mwingereza,
Imetuletea uhuru,
Tunamsifu Baba Marehemu Kingi Joji".

Ilikuwa ni pale Anfal ambapo, huku vita vinafikia ukingoni, Abdulwahid na askari wenzake wa Burma walikaa kitako kutafakari mambo yaliyowasibu katika vita na kuufikiria mustakbal wa Tanganyika. Iliamuliwa kuwa askari wa Burma kutoka Tanganyika waliokuwa batalioni ya sita wawe ndio chanzo cha chama cha siasa kupigania uhuru wa Tanganyika kwa kuuhamasisha umma.

Wote waliafiki wazo hilo. Jina lililochaguliwa kukitambulisha chama hicho lilikuwa Tanganyika African National Union (TANU). Ally Sykes anamkumbuka Abdulwahid kiliandika jina la chama hicho kilichokusudiwa ndani ya shajara yake. Hawa askari wa Burma walikuwa wakifahamu vyema kuwa tayari huko nyumbani kulikuwapo na African Association, chama ambacho kilikuwa kikipigania haki za Waafrika.

Abdulwahid alitarajiwa afahamu hili zaidi ya wenzake kwa sababu baba yake ndiye aliyekianzisha chama hicho akiwa katibu wake wa kwanza. Lakini suala la jinsi wangelivyokiunganisha chama hicho kipya cha TANU na kile cha African Association ili kudai uhuru, halikujadiliwa.

Abdulwahid alilitumikia jeshi nchini Kenya, Ceylon, India na Burma. Hata kabla hajafikisha umri wa miaka ishirini na mmoja alikuwa amekwishapanda cheo na kufikia Regimental Sergeant Major. Hiki kilikuwa ndio cheo cha juu kabisa ambacho Mwafrika aliruhusiwa kukifikia. Cheo kingine cha juu ambacho kiliwekewa Mwafrika kilikuwa kile cha Kapteni ambacho Waingereza walimtunukia Kabaka Edward Mutesa wa Buganda na Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Wahehe.

Lakini Kabaka Mutesa na Chifu Adam Sapi Mkwawa walitunukiwa vyeo hivi kwa sababu ya nyadhifa zao kama machifu, wakati Abdulwahid alizipata tepe zake kwa sababu ya ujasiri wake, kipaji chake cha uongozi na umaridadi wake. Vilevile Abdulwahid alivishwa nishani kadhaa, baadhi yake Burma Star na ile ya War Medal.

Baada ya Vita Vya Pili kumalizika, Wazungu waliruhusiwa kuondoka uwanja wa mapambano kurudi makwao kabla ya Waafrika, huku ikidaiwa kuwa wao walikuwa wakihitajika haraka sana huko Ulaya kwa ajili ya ujenzi wa nchi zao zilizoteketea kwa ajili ya vita.

Vikosi vya Waafrika vilipewa ruhusa mwisho. Askari wa KAR kutoka Tanganyika walikusanywa katika kambi moja iliyokuwa ikijulikana kama Kalieni, nje ya Bombay, kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani. Walipokuwa Kalieni Abdulwahid alikutana na rafiki yake toka nyumbani, Ahmed Rashad Ali, Mzanzibari. Ahmed Rashad alikuwa mcheza kandanda mashuhuri na alikwenda India kwa masomo.

Tutakutana na Ahmed Rashad hapo baadaye tutakapojadili harakati za kudai uhuru huko Zanzibar. Askari kutoka Tanganyika walikuwa na morali ya juu walipokuwa baharini wakirudi nyumbani; kitu pekee kilichotawala mazungumzo yao kilikuwa ni jinsi wangevyoweza kuwaondoa Waingereza kutoka ardhi ya Tanganyika.
 
kawombe

kawombe

JF-Expert Member
Joined
Mar 26, 2015
Messages
3,215
Likes
1,687
Points
280
kawombe

kawombe

JF-Expert Member
Joined Mar 26, 2015
3,215 1,687 280
Iko vzr sana mzee wangu
 
bigmind

bigmind

JF-Expert Member
Joined
Oct 28, 2015
Messages
9,535
Likes
8,927
Points
280
bigmind

bigmind

JF-Expert Member
Joined Oct 28, 2015
9,535 8,927 280
Mkuu baba yangu alipigana vita ya pili ya dunia upande wa mwingereza alikuwa Burma nilishatafuta namna ya kujua alivyoshiriki na kutafuta stahiki zake nimeshindwa maana alishakufa...
 
Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined
Nov 2, 2008
Messages
11,440
Likes
6,851
Points
280
Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined Nov 2, 2008
11,440 6,851 280
Mkuu baba yangu alipigana vita ya pili ya dunia upande wa mwingereza alikuwa Burma nilishatafuta namna ya kujua alivyoshiriki na kutafuta stahiki zake nimeshindwa maana alishakufa...
Bigmind,
Pole sana kaka.

Nadhani marehemu baba yetu kenda na mengi ambayo laiti angelikuhadithia
au kuandika mwenyewe tungefaidika sana na kumbukumbu zake.

Laiti kama ninsingeliandika kitabu cha Abdul Sykes haya tusingeyajua.
 
Kobello

Kobello

JF-Expert Member
Joined
Feb 20, 2011
Messages
6,359
Likes
1,400
Points
280
Kobello

Kobello

JF-Expert Member
Joined Feb 20, 2011
6,359 1,400 280
Askari wa zamani waliopigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza katika ardhi ya Tanganyika wakati wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia kati ya mwaka 1914-1918 walimuunga mkono Hitler, ingawa si wazi wazi kwa kuwa kufanya hivyo kungekuwa usaliti na uhaini dhidi ya Himaya ya Waingereza. Hata hivyo hilohalikumzuia Schneider Plantan, askari wa Kijerumani wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia, kutembea huku na kule katika mitaa ya Dar es Salaam akiwachochea watu wasimuunge mkono Winston Churchill katika vita vyake dhidi ya Adolf Hitler. Schneider alikamatwa na kuwekwa kizuizini huko Mwanza, na hakufunguliwa hadi mwisho wa vita mwaka 1945.
Hitler alikuwa Lance Corporal kwenye vita ya kwanza ya dunia. Hakuwa na cheo cha yeye kuungwa mkono.
Au maalim ulikuwa unamaanisha vita kuu ya pili?
 
Powder

Powder

JF-Expert Member
Joined
Jan 6, 2016
Messages
3,246
Likes
3,011
Points
280
Powder

Powder

JF-Expert Member
Joined Jan 6, 2016
3,246 3,011 280
Mkuu baba yangu alipigana vita ya pili ya dunia upande wa mwingereza alikuwa Burma nilishatafuta namna ya kujua alivyoshiriki na kutafuta stahiki zake nimeshindwa maana alishakufa...
Baba yako alikua Mwislam au Mkristu?
 
bigmind

bigmind

JF-Expert Member
Joined
Oct 28, 2015
Messages
9,535
Likes
8,927
Points
280
bigmind

bigmind

JF-Expert Member
Joined Oct 28, 2015
9,535 8,927 280
Bigmind,
Pole sana kaka.

Nadhani marehemu baba yetu kenda na mengi ambayo laiti angelikuhadithia
au kuandika mwenyewe tungefaidika sana na kumbukumbu zake.

Laiti kama ninsingeliandika kitabu cha Abdul Sykes haya tusingeyajua.
Kiukweli ingawa mengi alitusimulia nakumbuka mengi..!
 
A

Augustn

Member
Joined
Oct 23, 2017
Messages
20
Likes
7
Points
5
A

Augustn

Member
Joined Oct 23, 2017
20 7 5
Nafikiri hata hii inaeleza vizuri kwanini akina black mamba kwanini hawakupewa uongozi we juu sana kwanye jeshi la tz . Mbali na juhudi za skykes lkn bado hakuthaminiwa kwa mchango wake jeshin huko burma.
 
Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined
Nov 2, 2008
Messages
11,440
Likes
6,851
Points
280
Mohamed Said

Mohamed Said

Verified Member
Joined Nov 2, 2008
11,440 6,851 280
Hitler alikuwa Lance Corporal kwenye vita ya kwanza ya dunia. Hakuwa na cheo cha yeye kuungwa mkono.
Au maalim ulikuwa unamaanisha vita kuu ya pili?
Kobello,
Soma tena kwa utaratibu utaelewa.
 
Jogoo wa Shamba II

Jogoo wa Shamba II

JF-Expert Member
Joined
Jan 14, 2013
Messages
2,479
Likes
4,211
Points
280
Jogoo wa Shamba II

Jogoo wa Shamba II

JF-Expert Member
Joined Jan 14, 2013
2,479 4,211 280
Makala good
 
black sniper

black sniper

JF-Expert Member
Joined
Dec 10, 2013
Messages
9,464
Likes
6,514
Points
280
black sniper

black sniper

JF-Expert Member
Joined Dec 10, 2013
9,464 6,514 280
Ahsante mzee wangu
Umenikumbusha mbali
My father was one of the soldiers
Alipelekwa Burma na alirudi salama
Alikuwa anasema alipigana vita vya pili upande wa British lakini sina historia ndefu zaidi.
Laiti kungekuwa hata na picha labda ningemjua ingawa alikuwa kijana sana wakati huo.
Asante tena kwa huu uzi
 
KWEZISHO

KWEZISHO

JF-Expert Member
Joined
Jan 29, 2016
Messages
6,869
Likes
5,454
Points
280
KWEZISHO

KWEZISHO

JF-Expert Member
Joined Jan 29, 2016
6,869 5,454 280
Khadithi safi na yenye mafunzo mazuri
 

Forum statistics

Threads 1,237,315
Members 475,533
Posts 29,284,288