Asemavyo Msekwa juu ya Mwalimu Julius Nyerere ‘Dhamira ya Mwalimu Nyerere...

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
06msekwa4.jpg

Mzee Pius Msekwa



Fidelis Butahe
Monday, 07 November 2011

"NILIPATA bahati ya kulelewa na Mwalimu Julius Nyerere wakati nikiendelea na masomo katika shule ya sekondari ya Pugu, aliujua uwezo wangu darasani ndio maana alipendekeza jina langu ili niende kusoma Chuo Kikuu cha Pune, India".

Hayo ni maneno ya Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara ambaye amewahi kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Aprili, 1994 hadi 2005.


Kabla ya kushika nyidhifa hiyo, Msekwa ambaye amezaliwa Juni 9, 1935 amewahi kuwa katibu msaidizi na baadaye katibu wa bunge kuanzia 1960 hadi 1970.

Baadaye aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Tabora na Kilimanjaro mwaka 1981 hadi 1984, pia alichaguliwa kuwa mbunge wa Ukerewe mwaka 1990, wakati huo alikuwa Naibu Spika wa Bunge.

Msekwa alikuwa pia katika Tume ya Nyalali iliyopewa jukumu la kuangalia uwezekano wa Tanzania kubadilisha mfumo wake wa siasa, kutoka mfumo wa chama kimoja na kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa kazi ambayo ilifanyika mwaka 1991 na kumalizika 1992.

Anamzungumziaje Mwalimu Nyerere
Anasema Nyerere alikuwa kiongozi wa kipekee kwa kuweza kuipatia Uhuru nchi ya Tanganyika bila umwagaji damu kama ilivyotokea kwa nchi nyingine barani Afrika.


"Alikuwa anaweza kujenga hoja…, ndio maana aliweza kujieleza vizuri Umoja wa Mataifa sababu za Tanganyika kudai uhuru na kueleweka," anasema Msekwa.

Anasema kuwa aliweka misingi imara katika utawala wake na kwamba alifanya kazi zake kwa kufuata misingi hiyo na anasisitiza kuwa watanzania wanatakiwa kuifuata misingi hiyo iliyoachwa na Mwalimu Nyerere.

"Msingi wake wa kwanza aliotuachia ni umoja wa taifa letu, katika hili alihakikisha kuwa vikwazo vyote vinavyoweza kuhatarisha umoja huo vinatoweka," anasema.


Anaongeza, "Kikwazo cha kwanza alichokiondoa ni ukabila, katika hilo alitengeneza sheria ya kufuta machifu ili watu wote wajenge imani kwa taifa lao jipya."


Anasema pia Nyerere alisisitiza elimu na kwamba alipoingia madarakani shule za serikali zilikuwa chache na zilizokuwapo zilikuwa zikiendeshwa na madhehebu ya dini na kuamua kuzitaifisha.


"Alikuwa akiona mbali zaidi, aligundua kuwa shule hizi zitakuwa hatari zaidi kwa kuwa watakaosoma wengi watakuwa Wakristo ndio maana aliamua kuzitaifisha…, lengo lake lilikuwa kuondoa kikwazo katika umoja wa Watanganyika," anasema Msekwa.


Anasema kuwa Nyerere alisisitiza suala zima la uchumi na kuwaeleza watu kwamba maendeleo yao yataletwa na wao wenyewe kwa kujitegemea.


Anafafanua, "Ndio maana ikaundwa sheria iliyoeleza kuwa kila mwenye uwezo wa kufanya kazi na afanye,".

Anasema Mwalimu Nyerere alipambana na ujinga, umasikini na maradhi na kwamba kila watanzania wanapokumbuka kifo chake kilichotokea Oktoba 14, 1999 nchini Uingereza, wanatakiwa kumuenzi kwa kuyatenda yale aliyoyaacha na kuyazungumza.

Ukali wa Mwalimu Nyerere
Anasema Mwalimu Nyerere alikuwa mkali kwa watu waliokuwa wakifanya mambo kinyume na utaratibu, hasa katika suala la rushwa.


"Alihakikisha wanaofanya makosa wanafungwa au kuchapwa viboko, ukali wake unahitajika hata kwa viongozi wa sasa kwa kuwa binadamu siku zote ni lazima asimamiwe," anasema Msekwa.


Anasisitiza kuwa mmomonyoko wa maadili kwa viongozi ulikuwepo hata katika utawala wa Mwalimu Nyerere, "Mwalimu Nyerere alisimamia hili kwa umakini, ndio maana hata walimu hukaguliwa na wakaguzi wa elimu, binadamu bila kusimamiwa hatuendi."


"Maadili mema ni wajibu wa kila binadamu, mtu mwizi au mdokozi ni lazima asimamiwe na yule anayehujumu mali ya umma ni ukiukwaji wa maadili ni lazima ashughulikiwe," anasema.


Anasema misingi iliyoachwa na Mwalimu Nyerere ikifuatwa itaiongoza Tanzania zaidi ya miaka 500 ijayo.


Ukaribu wake na Nyerere
Anasema mwanzo wa kukutana na Mwalimu Nyerere ni baada ya kufaulu mtihani wa serikali "Territorial Standard Ten Examination" wakati akisoma shule ya sekondari Nyegezi, na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Pugu, wakati huo ikiitwa St Francis College.

"Ilikuwa ni bahati nilipoanza kulelewa na Mwalimu Nyerere, wakati huo alikuwa mwalimu wangu wa darasani katika shule hiyo, niliutambua upendo wake siku moja aliponiita ofisini kwake na kuniambia kuwa alikuwa amepata habari kwamba serikali ya India ilikuwa imetoa nafasi za masomo katika vyuo vilivyopo nchini humo," anasema Msekwa.


Anasema nafasi hizo zilikuwa kwa wanafunzi waliokuwa wamemaliza darasa la 12 na kufaulu mtihani wa ‘Cambridge School Certificate" na kwamba yeye kipindi hicho alikuwa darasa la 12.


"Alifurahishwa na maendeleo yangu darasani, baadaye nilikuja kugundua kuwa hakuwa amemwambia mwanafunzi mwingine juu ya nafasi hiyo, peke yangu ndiye niliyejaza fomu hizo na kuomba kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha Pune huko India," anasema Msekwa.


Anasema Mwalimu Nyerere aliandika barua ya kumpendekeza kuwa ana uwezo wa kutumia vema nafasi hiyo na baada ya muda aliitwa katika usaili Wizara ya Elimu, alifaulu na kupewa nafasi hiyo.


"Lakini nafasi hiyo sikuitumia kwa kuwa nilikuwa nimeteuliwa kwenda Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, niliamua kwenda Makerere kwa kuwa ilikuwa ni karibu na nyumbani Tanzania," anasema Msekwa.


Anasema kuwa ukaribu wao haukuishia hapo, kwani alipoanza kazi serikalini huku Mwalimu Nyerere akiwa rais na mwenyekiti wa chama tawala, alikuwa akimteua kushika nafasi mbalimbali.


Anasema baada ya kuzaliwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967, aliteuliwa na Mwalimu Nyerere kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na kupewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa azimio hilo kiutendaji upande wa chama.


Anasema aliteuliwa kuwa katibu wa Tume ya watu 20 iliyofanya maandalizi ya kuunganisha Vyama vya TANU na Afro-Shiraz (ASP) kati ya mwaka 1976 na 1977, muungano ambao uliza Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.

"Mwaka 1970 aliniteua kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na kilipozaliwa CCM,aliniteua kuwa Katibu Mtendaji Mkuu mwanzilishi wa chama, yeye alikuwa Mwenyekiti," anasema Msekwa.


Anasema kuwa aliwahi kupewa tuzo ya medali ya heshima na Mwalimu Nyerere mwaka 1985 kabla hajastaafu urais, ilikuwa siku ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Anasema alikuwa akiteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya kuandika Ilani za uchaguzi za CCM kwa kila uchaguzi mkuu uliofanyika kila baada ya miaka mitano, hadi kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Katiba

Msekwa ambaye ana shahada ya sanaa katika somo la historia, shahada ya uzamili ya sayansi ya jamii na mtaalam wa Katiba na masuala ya utawala wa sheria anasema Mwalimu Nyerere ameacha utawala wa Katiba na Sheria na kwamba sheria zinapopitwa na wakati zinatakiwa kubadilishwa ili kwenda na wakati uliopo.

"Mwalimu Nyerere alianza na katiba ya Uhuru ambayo ilimfanya Malkia wa Uingereza kuwa mkuu wa nchi akiwakilishwa na Gavana, kipindi hicho Bunge lilikuwa likipitisha sheria na zinapelekwa kwa Gavana na kusaini sheria hizo kwa niaba ya Malkia."

Anaongeza, "Katika mwaka wa kwanza tangu Tanganyika ipate Uhuru mwalimu Nyerere kila kitu alikuwa akiripoti kwa Malkia wa Uingereza kwa kuwa yeye ndio alikuwa mkuu wa nchi".

Anasema kuwa baadaye katiba hiyo ilibadilishwa na kuja katiba ya Jamhuri, iliyomuondoa Malkia wa Uingereza na Gavana na kumtaja Mwalimu Nyerere kuwa mkuu wa nchi na serikali.


"Tanganyika na Zanzibar zilipoungana ikatengenezwa katiba nyingine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio inayotumika mpaka sasa," anasema Msekwa.


Anafafanua kuwa kuna umuhimu wa kuitizama katiba ya sasa kama inakidhi mahitaji yaliyopo, "Katiba ni ya wananchi wote sio ya serikali na kazi ya kuiandika upya inatakiwa ishirikishe watu wote kama alivyosema rais Jakaya Kikwete, na ndio maana akaunda Tume ya kukusanya maoni kwa wananchi,".


Anasema kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa kuandaa katiba mpya hautakiwi ufanyike katika makongamano, bali wananchi wafuatwe walipo ili waweze kutoa maoni yao.

Viongozi wasio waadilifu
Anasema jukumu la kuwaondoa viongozi wasio waadilifu liko mikononi mwa wananchi waliowachagua.

"Kiongozi yuko madarakani na wananchi wanaona wazi kuwa hawanufaiki chochote wanaweza kumtoa katika wadhifa wake aidha kwa kutomchagua katika uchaguzi au kwa kulitumia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," anasema Msekwa.


Anasema kuwa rais ana uwezo wa kuwaondoa viongozi aliowateua lakini hana uwezo wa kuwavua Ubunge wabunge na kwamba jukumu hilo linaweza kufanywa na wananchi pekee.


"Wananchi wanaweza kuwaondoa viongozi kwa kutowachagua au kwa kuwatumia wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi, Bunge linaweza kuwaondoa madarakani rais na hata Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi," anasema Msekwa.
 
Hiki kizazi cha uongozi kilichomfuata Nyerere mh. Yani kati ya watoto wote waliomfuata baba ni wachache sana.
 
msaada wake kwa nchi hii ni nini haswa. hatutaki kila mtu anadai ni mfuasi wa nyerere huko wakiendelea kufanya madudu
 
Sasa imetosha wewe na mkeo ondokeni madarakani
 
Back
Top Bottom