Arusha: Mahakama yatupa pingamizi la utetezi kesi ya Ole Sabaya

mshale21

JF-Expert Member
Apr 8, 2021
1,323
2,000
Arusha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa utetezi wanaomuwakilisha mshitakiwa wa pili Sylivester Nyegu katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Uamuzi huo umetolewa leo Agosti 23, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo ambaye aliahirisha shauri hilo la jinai namba 105,2021 mwishoni mwa wiki baada ya mawakili Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka kuweka pingamizi.

Mawakili hao walipinga mteja wao asihojiwe kwa maelezo ya awali ambayo hayajapokelewa mahakamani kama kielelezo.

Akitoa uamuzi huo mdogo Hakimu Amworo amesema kwa kuwa maswali ya dodoso huwa na kikomo shahidi ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo anaweza kuulizwa maswali yoyote.

"Kwa kuzingatia kifungu cha 154 cha sheria ya ushahidi shahidi anaweza kuulizwa kwenye hiyo nyaraka hata kama haijatihibitishwa ni ya kweli,"amesema.

Baada ya uamuzi huo Wakili wa Mkuu, Tumaini Kweka aliendelea kumhoji shahidi huyo kwa kutumia nyaraka hiyo.

Agosti 20, 2021 mshitakiwa wa pili Nyegu alikuwa akiendelea kuhojiwa na Mawakili wa Jamhuri mabishano ya kisheria yalitokea baina ya Mawakili wa Upande wa Jamhuri na Mawakili wa Utetezi wakati mshitakiwa huyo akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili Kweka.

Akimuhoji mshitakiwa huyo Wakili Kweka aliiomba mahakama chini kifungu cha 154 cha Sheria ya ushahidi,kumuuliza shahidi maswali kupitia maelezo yake aliyoandika polisi wakati anahojiwa.

Baada ya Wakili Kweka kutoa ombi hilo Wakili Edmund Ngemela anayemtetea Nyegu aliweka pingamizi na kuieleza mahakama kuwa kifungu hicho kinataka ili nyaraka iweze kutumika kumhoji shahidi ni lazima nyaraka hiyo iwe imeandikwa naye na imepokelewa kama kielelezo.

Wakili Ngemela alieleza mahakama kuwa wakati mshitakiwa huyo anatoa ushahidi wake wa msingi mahakamani hapo alidai hajawahi kuhojiwa na hakuna shahidi hata mmoja wa jamhuri aliyefika mahakamani hapo kusema alimhoji shahidi huyo.

Wakili Sylvester Kahunduka ambaye pia anamtetea mshitakiwa huyo wa pili katika shauri hilo alidai mahakamani hapo kuwa kifungu hicho walichotumia jamhuri kumhoji shahidi kwa maelezo hayo hakijafuata matakwa ya kifungu hicho.

"Katika ushahidi wa msingi wa shahidi anasema hakuwahi kuandika maelezo wala kuhojiwa alichokuwa anamuuliza wakili ni particulars zake ambazo mtu yoyote anaweza kuandika, sasa wakili anatoa maelezo anasema ni ya shahidi,"alidai na kuongeza

"Tunaamini kwamba mteja wetu hatatendewa haki kama hicho kinachosemekana ni maelezo kitaumika kumuuliza maswali kwa sababu hana nafasi ya kuthibitisha kama ni yake, maombi haya yatupiliwe mbali."

Akiwasilisha hoja za nyongeza baada ya mawakili hao wa mshitakiwa wa pili, Wakili Kweka aliieleza mahakama siyo takwa la kisheria kutaka maelezo yapokelewe kama kielelezo mahakamani.

"Mheshimiwa Hakimu, mawakili wasomi katika uelewa wa sheria ukisoma kifungu namba 154 ,unaposema 'made by him' haimaanishi lazima wewe uchukue karatasi uandike, inamaanisha ni maelezo yake au yanamhusu yeye yakaandikwa,"alidai.

"Siyo lazima maelezo hayo aonyeshwe, hayo ndiyo matakwa ya kisheria.Tulichonacho sasa hivi kwa hadhi aliyonayo ni shahidi siyo mshitakiwa na suala la ushahidi linaongozwa na Sheria ya Ushahidi Sura ya sita na hata mwenyewe wakati namuuliza nimuite nani aliniambia nimuite shahidi au jina lake,"amesema na kuongeza

"Tunachoomba kimekidhi matakwa ya kifungu cha 154 cha Sheria ya Ushahidi na nilishaanza kumuuliza maswali kuhusu yeye ni nani, ana hadhi gani katika jamii, siyo takwa la kisheria kutaka maelezo yapokelewe kama kielelezo mahakamani na ni kifungu kingine kabisa,"

"Katika muktadha huo na katika kuokoa muda wa mahakama hoja hiyo itupiliwe mbali na upande wa mashtaka turuhusiwe kuendelea kufanya mahojiano kwa shahidi namba mbili kwa upande wa utetezi, kwani unaweza kuhoji kitu chochote ila ukomo wa anga ndo ukomo wako."

Chanzo: Mwananchi
 

EvilSpirit

JF-Expert Member
Jun 15, 2017
6,438
2,000
Naomba mwenye picha ya Odira Amworo aitupie humu tumfahamu. Tunataka tumuone mtu anayemfanya sabaya awe anaachia vijambo visivyo na sauti kwa kutetemeka
 

Janja weed

JF-Expert Member
Nov 20, 2020
1,341
2,000
Odira Omworo atakua mkenya tu hyu mwamba nashangaa amekatizaje hadi kuwa na nafasi kubwa namna hii huku Bongo, hahahaaaaaaaaaaaaaa nacheka utadhani mazuri ukiwa upande wao hakuna shida ila uwe upande mwingine utajuta na majina yako hadi pasipoti utachukuliwa na maelezo utatoa kama yule asikofu aliyemzika Mwendazake
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom