Arusha: Mahakama yamkuta Lengai Ole Sabaya na kesi ya kujibu

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewakuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, na wenzake wawili hivyo wanatakiwa kuanza kujitetea kesho Ijumaa Agosti 13, 2021.

Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine katika shauri hilo la jinai namba 105 ni Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura, wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Odira Amworo, alisema washtakiwa wote watatu wana kesi ya kujibu katika mahakama hiyo. Hakimu alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na kuwasilishwa mahakamani huko, washtakiwa wote wana kesi ya kujibu, hivyo kila mmoja anatakiwa kujitetea.

“Washtakiwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na kuwasilishwa mahakamani mna kesi ya kujibu na kuna njia mbili za kujitetea ambazo ni chini ya kiapo au kuwa na mashahidi," alisema.

Wakili wa Mshtakiwa wa Kwanza, Dancan Oola, alidai mahakamani huko kwamba Ole Sabaya atajitetea mwenyewe chini ya kiapo na tangu alipozungumza naye mara ya mwisho, alimweleza kwamba ana shahidi mmoja.

Hata hivyo, wakili huyo alidai mahakamani huko kwamba watakuwa na mashahidi wasiozidi wawili.

Wakili wa mshtakiwa wa pili, Edmund Ngemela, alidai mahakamani huko kwamba mteja wake, Nyegu, atajitetea kwa njia ya kiapo na atakuwa na shahidi mmoja.

Fridolin Gwemelo, Wakili wa mshtakiwa wa tatu, Mbura, alidai mteja wake atajitetea chini ya kiapo na atakuwa na baadhi ya vielelezo ambavyo ataviwasilisha mahakamani huko.

Awali akiwasomea mashtaka washtakiwa hao, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, alidai shtaka la kwanza ni la unyanganyi wa kutumia silaha linalowakabili washtakiwa hao.

Wakili Chavula alidai washtakiwa hao Februari 9 mwaka huu, wakiwa Mtaa wa Bondeni jijini Arusha, waliiba fedha kiasi cha Sh. milioni 2.769, mali ya Mohamed Saad na baada ya wizi huo, walitumia silaha ya bunduki kuwatisha waliokuwa kwenye duka hilo.

Shtaka la pili ni la unyanganyi wa kutumia silaha, ikidaiwa mahakamani huko kwamba washtakiwa hao kwa pamoja, wakiwa Mtaa wa Bondeni jijini Arusha, waliiba fedha kiasi cha Sh. 390,000 mali ya Bakari Msangi na baada ya wizi huo walimfunga kwa pingu, kumpiga makofi, mateke, ngumi na wakatumia silaha ya bunduki kumtisha ili wabaki na fedha walizochukua kwake.

Shtaka la tatu ni la wizi wa kutumia silaha, ikidaiwa mahakamani huko kwamba Ole Sabaya na washtakiwa wenzake hao, Februari 9 mwaka huu, katika Mtaa wa Bondeni jijini Arusha, waliiba simu moja aina Tekno Pop na fedha kiasi cha Sh. 35,000, mali ya Ramadhani Rashid na baada ya kufanya uhalifu huo, walimpiga mhusika makofi, ngumi, mateke na walitumia silaha kumtisha ili wapatiwe fedha na mali walizoiba.

Katika kuijenga kesi hiyo, Upande wa Jamhuri ulipeleka mahakamani mashahidi 11 na kuwasilisha nyaraka mbalimbali za ushahidi ikiwamo picha za mnato na barua za ushahidi zinazoonyesha mchakato wa upelelezi wa shauri hilo ulivyofanyika.

Hakimu Amworo aliahirisha shauri hilo hadi leo, washtakiwa hao watakapoanza kujitetea mahakamani huko.
 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewakuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, na wenzake wawili Sylevester Nyegu, Daniel Mbura, hivyo wanatakiwa kuanza kujitetea kesho Ijumaa Agosti 13, 2021. Sabaya na wenzake wawili wanatuhumiwa kutenda makosa matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Sabaya na wenzake, wanatuhumiwa kutenda makosa hayo katika duka la Mohamed Saad huko eneo la Bondeni jijini Arusha, Februari 9 mwaka huu.

Soma zaidi:Mke wa diwani aangua kilio mahakamani akitoa ushahidi kesi ya Sabaya
 
Baadhi ya watu
JamiiForums1285530671.jpg
 
Back
Top Bottom