Arusha: elimu yenu itaathirika kwa ujinga wa viongozi wetu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Arusha: elimu yenu itaathirika kwa ujinga wa viongozi wetu

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by bhikola, Oct 31, 2012.

 1. bhikola

  bhikola JF-Expert Member

  #1
  Oct 31, 2012
  Joined: Apr 2, 2012
  Messages: 457
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 45
  Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewapiga mabomu mamia ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimnyaki iliyopo wilayani Arumeru walioandama kwenda katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

  Pamoja na kwenda kutoa malalamiko yao, Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, aliagiza polisi kuwatia mbaroni wanafunzi wawili waliotoa maelezo mbele yake kuhusiana na sababu za wao kuandamana.

  Wanafunzi hao walifanya maandamano hayo jana wakishinikiza Mkuu wa Shule hiyo, Mariam Chamle, afukuzwe kwa tuhuma za kusababisha wanafunzi wa kidato cha nne kuwachelewesha kuingia katika chumba cha mitihani.

  Wanafunzi hao zaidi ya 200, walianza maandamano yao katika barabara ya Ngaramtoni, nje kidogo ya Jiji la Arusha na wakiwa njiani kuelekea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, walikumbana na nguvu ya dola baada ya polisi kuanza kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi.

  Hata hivyo, pamoja na kupigwa mabomu hayo, wanafunzi hao walivumilia kwa kunawa maji usoni hadi walipofanikiwa kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

  MWANAFUNZI AOKOTA BOMU

  Mmoja wa wanafunzi hao aliokota bomu lililorushwa na polisi kabla halijalipuka akidhani kuwa ni ganda la bomu na kumuonyesha Mkuu wa Mkoa huo kama ushaidi wa jinsi walivyopigwa mabomu na polisi.

  Baada ya kulionyesha bomu hilo kwa Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Operesheni Maalum, Peter Mvulla, alimnyang'anya haraka kabla halijalipuka na kuleta madhara.

  Kamanda Mvulla alijitetea mbele ya Mkuu wa Mkoa na wanafunzi hao kuwa bomu hilo lilianguka kwa bahati mbaya wakati wa vurugu za kuwatuliza wasiandamane, lakini walikaidi na kuanza kuwapopa polisi kwa mawe hivyo kulazimisha kutumia nguvu ndogo kuwatuliza.

  Wanafunzi hao walilishutumu Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuwapiga mabomu wakati hawakuwa na lengo baya kwa kuandamana badala ya askari wake kusikiliza kilio chao.

  Mesharck Lomnyaki, akizungumza kwa niaba ya wanafuzi wenzake, alidai kuwa mkuu wa shule amesababisha baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne kuchelewa kufanya mitihani yao ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kuzuia kuingia katika chumba cha mitihani toka saa 2:00 hadi saa 4:30 alipowaruhusu kuingia.

  Alidai aliwazuia wanafunzi hao wasiingie kwenye chumba cha mitihani kwa madai kuwa walichelewa kuchanga michango ya shule na wengine walikuwa hawakujaza fomu za idadi ya masomo (selforms) na badala yake akawataka wazijaze siku hiyo ya mitihani huku wenzao wakiendelea kufanya mitihani.

  Aliongeza kuwa Oktoba 16, mwaka huu walinyimwa mwongozo wa kujibu swali la tano, lenye alama kumi kwenye somo la Kemia ambalo hawakupata kulingana na muda na kusababisha usumbufu ndani ya chumba cha mtihani na kusababisha kukata tamaa kwenye somo la Fizikia.

  Pia, alidai tatizo la kufanana na hilo limejitokeza kwa wanafunzi wa kidato cha pili kwenye mtihani wa Moko, na kuwa aliwafukuza wanafunzi hao kutomaliza mtihani huo kwa sababu ya kutolipa michango na kusababisha wanafunzi 46 kutofanya mtihani huo.

  Alisema matokeo ya kuzuia wanafunzi hao yalisababisha kushuka kwa kiwango cha ufaulu, hali iliyosababisha mwalimu huyo kutoa lugha za kashfa na kujenga woga kwa wanafunzi hao wanaotarajia kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili, utakaofanyika mwaka huu.

  Mwanafunzi mwingine, Ezekiel Memiri, alitaja kero nyingine wanazokumbana nazo kuwa ni pamoja na unyanyasaji wa wanafunzi na kuwa wengi hufukuzwa kwa makosa madogo madogo bila udhibitisho wa bodi ya shule.

  Wanafunzi hao walimuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati kwa kumuondoa mkuu huyo wa shule kutokana na matatizo hayo ambayo yanasababisha kushuka kwa kiwango cha elimu shuleni hapo.

  RC AWA MBOGO

  Akizungumza na wanafunzi hao, Mulongo aliwasikilia huku akigeuka kuwa mbogo na kuamuru polisi kukamata wawili waliokuwa wakitoa maelezo kwa niaba ya wenzao ambao ni Meshack Lomnyaki na Daudi kwa madai kuwa walikuwa viongozi wa maandamano hayo .

  Alisema kumezuka tabia ya wanafunzi wa shule mbalimbali za mkoani Arusha kuandamana hata kwa makosa yasiyo na sababu hadi ofisini kwake na kwamba ameshatoa onyo kwa shule zote kuacha tabia hiyo vinginevyo atazifunga.

  "Shule zitakazoandamana kuanzia leo (jana) nitazifunga ili mkose kabisha masomo, maana hamtaki kusoma na leo ningefanya hivi, lakini nimeonea huruma watoto wa kike walio wengi ambao tunapigania wapate elimu. Ila hawa viongozi wenu wapelekwe ndani iwe fundisho la tabia hii," alisema.

  Mulongo alitoa hadi kufika saa tisa jioni ya jana, wanafunzi hao wawe wamerejea shuleni kwao, kumsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Afisa Elimu, vinginevyo atawafungia shule yao.

  "Nashangaa kupigwa mabomu, mnashangaa nini wakati mmeandamana bila kibali, mlitegemea nini mnavunja sheria na mkivunja sheria kwa kudai haki, hata haki mnayotaka hamtapata kwa sababu ya kuvunja sheria," alisema.

  Hata hivyo, ilichukua muda wanafunzi hao kutawanyika kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa, wakishinikiza kuachiwa kwa wenzao wawili waliokamatwa na Polisi, hadi pale polisi walipoamua kutoweka kwa gari namba PT. 1834 na kuwaacha kwenye mataa wanafunzi hao.

  Baadaye wanafunzi hao waliondoka hadi makao Makuu ya polisi kusubiri wenzao waachiwe huru. source: nipashe

  mtazamo wangu: kwa ujeuri huu wa viongozi tutegemee elimu yetu keundelea kuathirika, maana badala ya kuwasikiliza wanafunzi na kuchunguza madai yao unawatisha na kuwakamata au kuwafunga, huu ni ukatili na unyanyasaji juu ya wanafunzi hawa, na zaidi ni kuwajengea nithamu ya woga katika kuhoji. mtindo huu unaua ubunifu na utafiti wa watoto kwani unawajengea nithamu ya woga katika kuhoji, tukumbuke taaluma yoyote au ujuzi wowote na ugunduzi huanza na kuhoji kwanini? kwanini? kwanini?
   
Loading...