Anna Mghwira: Mapendekezo ya Maboresho ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)

Anna Mghwira

R I P
Mar 9, 2012
206
362
627e71e912ede8aeb918434947d57854.jpg


Kufuatia dhamira ya serikali ya kutaka kuboresha usafiri wa anga, kuongeza idadi ya ndege za abiria na mizigo na kuimarisha utalii wa ndani na nje, Chama cha ACT Wazalendo kinapenda kutoa maoni yake kama ifuatavyo:

Lengo la maboresho katika sekta hii liwe kuirudishia ATCL mamlaka ya kumiliki huduma zote muhimu za chini za uendeshaji wa viwanja vya ndege (Ground Handling). Hivi ni pamoja na viwanja vyote vikubwa kama vile Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ulioko jijini Dar es salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, pamoja na Viwanja vya ndege vya Mwanza, Kigoma, Songwe, Mtwara, Dodoma na Mbeya.

Huduma muhimu tunazozizungumzia ni pamoja na hizi:-

Kuhudumia abiria, kuhudumia mizigo yote ya ndege, kuhudumia vyakula ndani ya ndege na kumbi (Lounge) zote za daraja la kwanza (first class) na huduma ya ukatishaji wa Tiketi (Booking) za ndege (Galileo).

Ili kumudu jukumu hili tunaiomba serikali iunde kitengo cha uwezeshaji wa huduma za chini (Air Tanzania Ground Support Company) ambacho kitagawanyika katika sehemu zifuatazo kwa kutumia lugha ya tasnia ya usafiri wa anga:

• Cargo Handling (utunzaji wa mizigo)
• Ramp - Handling
• Passengers Handling (utunzaji wa abiria)
• Computer Reservation Systems (Galileo)
• Clearing & Forwarding (usafirishaji na upokeaji mizigo)
• Airport Shuttle Buses (Usafiri wa Mabasi wa kwenda na kutoka kwenye viwanja vya ndege)
• Security (Mfumo wa usalama wa viwanja)
• Travel Agency kama vile STS ya zamani
• Kitengo cha uhandisi kwa ajili ya kutengeneza ndege zinazoharibika zikiwa zimetua katika viwanja vyetu (Kitengo hiki kinaweza kuzalisha mapato kwa kutengeneza ndege za kigeni zinazopata matatizo katika viwanja vya Tanzania).

• Huduma ya kuuza mafuta ya ndege T3

Kimsingi maeneo haya ya uendeshaji pia ndiyo vitega uchumi vya mashirika ya ndege duniani. Kwa kutoa huduma hizi, shirika letu litaweza kuzalisha fedha (nyingi ikifanywa kwa umakini) za kulisaidia shirika kufanya vizuri katika kutoa huduma na kutoa ajira kwa watanzania, na itaimarisha usalama katika viwanja vyetu vya ndege.

Haina maslahi kwa shirika letu la ndege kwenda kinyume na utaratibu wa mataifa mengine katika usimamizi wa utoaji huduma hizi wenye faida kwa mashirika ya ndege.

Nchi zote jirani na zenye mafanikio katika sekta hii zinafanya hivyo pia. Hizi ni pamoja na Kenya, Ethiopia, Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Misiri, Sudan, n.k. Kimataifa nchi wanachama wa ICAO, CAA, na FAA zote zinazingatia utaratibu huu na imekuwa faida kwao.

Viwanja vya ndege ni lazima humilikishwa wananchi wazalendo ambao huajiriwa na shirika la ndege la Taifa husika (National Flag Carrier). Kwa muda mrefu sasa Tanzania tumekwenda kinyume na utaratibu huu unaotumiwa na mataifa mengi ya Ulaya na Marekani ambao ndiyo waanzilishi wa taratibu zote za mambo ya ndege za abiria hapa duniani kama vile ICAO, CAA, FAA.

Biashara ya shirika la ndege si kurusha ndege tu yaani kufanya ile biashara ya msingi (core business). Utaratibu tunaopendekeza unalenga kuleta ufanisi wa uendeshaji biashara hii. Kinyume na hapo itakuwa ni mbinu za kuinyakulia ATCL rasilimali zake.

Utaratibu wa kimataifa umetaka mamlaka ya usimamizi wa uwanja wa ndege umilikiwe na (Airport Authority) na wazalendo halisi wa Taifa husika na wawe waaminifu, waadilifu na wazalendo kwa Taifa na shirika lao, kwa ajili ya kuimarisha Usalama wa viongozi wetu, viongozi wengine na raia kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya ziara za aina mbalimbali nchini kwetu (kiserikali, binafsi, kibiashara na kitalii).

Historia ya viwanja vya Tanzania inaonesha kuwa udhaifu huu ulianza miaka ya 1990.

Hiki ni kipindi ambacho uzalendo ulianza kupungua na viongozi wakaanza kujihusisha na ufisadi wa kuuza mali za Umma kwa wageni bila ya kujali usalama wa nchi. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa hai aliwahi kukemea ubinafsishaji huu aliouita kuvuka mipaka.

Mwalimu alionya kuwa tukiendelea hivyo tungebinafsisha na magereza.

Leo tunavyoongea mashirika yasiyositahili kubinafsishwa kama vile NBC, NASACO, ATC, TANESCO, TTCL nk tayari yamebinafsishwa kwa wageni.

Ubinafsishaji haukufanyika kwa lengo la kuinua ufanisi na kuongeza faida kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizi, lakini hasa ilichangiwa na tabia ya rushwa ya kupata 10% (ten Percent) ya faida kutoka kwa mashirika yaliyobinafsishwa!

Hii ni aibu ya kudumu ya taifa letu kuwa na viongozi wanaoongoza kwa rushwa za kulididimiza taifa!

Katika mfuatano huu tumeona pia uuzaji wa viwanda na mashirika ya Umma, mengi yakitolewa katika usimamizi wa umma kwa faida binafsi za viongozi waliohusika na udalali wa kuuza mali za umma kwa hasara.

Ni katika kipindi hiki shirika letu la ndege la Taifa lilipoanza kuyumba. Katika kipindi hiki tulishuhudia viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na uchukuzi katika kitengo cha usafiri wa anga walianza kuuza njia (Routes) za Air Tanzania kwa mashirika mengine ya ndege na kuilazimisha AIR TANZANIA kuingia kwenye mikataba mibovu ya ushirikiano (joint venture) wa kulifilisi shirika letu.

Tuna mifano ya mikataba hii kama ifuatavyo:-

Mkataba wa AJAS/ALLIANCE/SOUTH AFRICAN AIRWAYS
GULF AIR/ EMIRATES/OMAN AIR na kuiongezea Routes Kenya Airways za kuja DSM/NBO- wakawa wanaendesha njia hizi (Operate) kama shirika la taifa la Tanzania (National Flag Carrier ya Tanzania) AIR TANZANIA ikanyang’anywa moja ya vitega uchumi vyake, DAHACO –Dar es salaam Air port handling Company ambayo ATC ilikuwa inamiliki asilimia 65% na shirika la SAS (SCANDINAVIAN AIRLINES SYSTEM) walikuwa wanamiliki asilimia 35%.

Kwa ujanja kampuni mpya ya Swissport ilianzishwa na kulinyang’anya Shirika la ndege la Taifa majukumu yake.

Shirika hili lilipewa Raia wa nje wakishirikiana na moja kati ya wakurugenzi wa kampuni mama ya ATC (DAHACO).

Tunakumbuka kuwa wafanyakazi wote waliokuwa DAHACO walilazimishwa kuanza ajira mpya na Swissport bila kulipwa mafao yao ya kuitumikia DAHACO kwa zaidi ya miaka 10.

Uchunguzi unaonesha kuwa Mkurugenzi mkuu wa DAHACO wakati ule ambaye alianzisha Swissport (Bwana Gaudence Kilasara Temu) aliwatishia wafanyakazi wa DAHACO kuwa yeyote atakayekaidi amri hii angefukuzwa kazi.

Wafanyakazi hao walisaini kuingia Swissport kwa shingo upande kwa vile serikali iliyokuwepo madarakani ilikuwa na uhusiano wa karibu na viongozi wa ngazi za juu wa serikali kwa wakati huo (miaka ya 2000) na mkurugenzi wa utawala alikuwa mdogo wake mama ANNA MKAPA kwa jina ESTHER MARO. Wafanyakazi hawakuwa na la kufanya. Bodi na menejimenti ya Air Tazania ikanyamaza, ikakosa la kufanya baada ya kujua kuwa kuna mikono ya wakubwa.

Hii ndiyo Tanzania tuliokuwa nayo katika awamu zilizopita na hasa awamu ya tatu na awamu ya nne mara baada ya ATC kunyang’anywa Ground handling na kulazimishwa kuingia ubia na South African Airways ikawa ndiyo kifo cha ATC.

Makaburu wa SAA waliilazimisha menejiment na bodi ya ATC kupunguza MARUBANI 15 na ma- Engineer 30 na kuwadanganya kuuza ndege hizi kwa madai kuwa ni ndege za kizamani aina ya B737-200 japokuwa zilikuwa zinaruka vizuri kwa safari za ndani na za nje mpaka Europe/USA pamoja na kwao afrika ya Kusini.

Ndege zilizouzwa zilitumiwa na makampuni mengi ya ndege kwa ahadi kuwa tumeshaingia ubia na nyie tutaleta ndege za kisasa ambazo zitafanya safari ndefu kama B767-300 au AIR BUS 300-200/MD 11.

Huo ndiyo utapeli tuliofanyiwa na makaburu na kwenye mmoja ya mikataba yetu na Alliance Air wakatuletea ndege aina ya B747 SP (special performance) ndege ambazo walikuwa wanazitumia wakati wa siasa za ubaguzi zilikuwa zikiruka kutoka Johannesburg kuelekea London (NON-STOP) kwa kuwa hazikuruhusiwa kutua katika miji iliyokuwa chini ya OAU (Organisation of African Union).

Jambo la kushangaza ni kwamba baadaye Makaburu waliirubuni ATC kuuza ndege zake B737-200 walileta ndege mbili mbadala na ambazo zilikuwa B737-200 ambazo zilikuwa zimechoka zaidi ya zile za kwetu walizotulazimisha tuziuze kwa bei ya kutupa.

Itakumbukwa kuwa Makaburu hao hao walimrubuni mmoja kati ya mawaziri wetu wa mawasiliano na uchukuzi Mhe, William Kusila akasaini andiko (Document)/ mkataba kati ya mikataba ya Alliance Air/ATC karatasi likiwa na nembo ya wizara (letter headed) bila ya maandishi yeyote akaweka sahihi yake mkataba huo na kuwapatia makaburu waende wakajaze maelezo wanayotaka wao nchini kwao Afrika ya Kusini.

Jambo hili ndilo linachangia kuitesa AIR TANZANIA mpaka leo.

Kwa kuwa serikali imeamua kuimarisha sekta na idara hii, basi ifanye maamuzi sahihi ya kumiliki asilimia mia moja (100%) za hudumazote kama tulivyoziainisha hapa. (Total Ground handling, CATERING, GALILEO nk).

Mhe, Rais biashara ya ndege haitegemei ndege peke yake kupata faida kama tulivyajaribu kunyambua hapo juu. Itakuwa vema maandalizi haya yaanze mara moja ili ndege zitakapowasili zikute mfumo wa uzalishaji ukiwa umekaa vizuri kibiashara.

Huu si wakati tena wa shirika la kibiashara kujiendesha kwa ruzuku wakati vitega uchumi vyake vipo.

Tunaamini kuwa wafanyakazi na wataalamu wa ndege katika fani mbalimbali wanakubaliana na maoni haya na kuwa dhamira ya sasa ya serikali kulifufua shirika la taifa la ndege ni motisha tosha kwao kujituma kiutu, kiuadilifu na kizalendo,na kulirejeshea taifa fahari yake katika tasnia hii.

Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilithamini jambo hili ikatoa mafunzo ya gharama kubwa kwa marubani na wahandisi kwa ajili ya uendeshaji kamili wa viwanja na mnyororo wa biashara hii, si nusu nusu. Litakuwa jambo la heshima angalau mara hii tuthamini gharama hizi na kuzirejesha kuzalishia shirika na taifa faida.

MISINGI MUHIMU YA MAFANIKIO YA ATC MPYA
UTAALAMU WA KWELI KATIKA FANI MBALIMBALI
UADILIFU,UZALENDO NA UTU KATIKA UTENDAJI KAZI
WAFANYAKAZI KUPEANA USHIRIKIANO WA KUTOSHA
WAFANYAKAZI KUEPUKANA NA MIGOGORO YA KIKAZI
WAFANYAKAZI KUWA WABUNIFU KATIKA KILA ENEO
WAFANYAKAZI KUTHAMINI NA KUTUNZA NDEGE HIZI KAMA MBONI YA MACHO YA TAIFA.
NDEGE NDIYO KIWANDA CHA BIASHARA YA ANGA KWA HUDUMA YA ABIRIA NA MIZIGO. IKIFANYWA KWA UMAKINI BIASHARA HII INA FAIDA KUBWA KWA SHIRIKA NA TAIFA.

Kwa kuwa ndege ni chombo nyeti na mahususi katika usafri wa anga, na kwa kuwa wanaozijua vizuri ni marubani na wahandisi, tunaamini wanashirikishwa kikamilifu katika ununuzi wa ndege unaoendelea sasa hivi, licha ya ukweli kuwa ndege nne za Dash8-Q400 zilikuwepo katika mpango wa kununuliwa na ATCL kama inavyoonekana kwenye mpango wao wa kazi wa mwaka 2014 ( Business Plan).

Serikali iliangalie swala hili kwa macho mapana ya uzalendo na kwa kuzingatia usalama wa Taifa letu. Kwa kuwa uwanja wa ndege ni mahala nyeti, maadui wa Taifa wanaweza kutumia udhaifu wa watendaji wa kigeni wasiokuwa na uchungu na nchi yetu kuruhusu vitendo visivyo vya kizalendo kutokea.

Tulizuie hili mapema.
Mapungufu ya awamu za nyuma yamechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa uzalendo na maadili kwa viongozi mbalimbali wa serikali walioendekeza kupata asilimia 10% bila kujali maslahi ya Taifa.

Ni lazima sasa tujikie katika kulirejesha taifa katika misingi, turejeshe rasilimali za nchi katika mikono ya wananchi, tuendeshe ubinafsishaji wa faida pale inapokuwa ni lazima na kwa masilahi ya taifa.

Licha ya uboreshaji wa shirika la ndege kwa taratibu zinazoendelea na kwa maoni tunayotoa hapa,

ACT WAZALENDO tunapenda kukaza kuwa mkombozi halisi wa maendeleo ya kichumi wa nchi yetu ni uwezo wa kiuchumi wa wananchi wenyewe. Hata matumizi ya usafiri wa anga, wa reli na barabara na suala zima la utalii ni lazima ulenge soko la ndani kwanza.

Hili ndilo soko sahihi na la uhakika kwa mashirika yote ya biashara na ya huduma.

Kwa hiyo changamoto kubwa kwa sasa si watalii wa nje, ama idadi ya ndege tunazoweza kuingiza ama la, bali ni umiliki wa rasilimali hizi kama tulivyoeleza hapo juu na idadi ya watanzania wanaopata maisha kutokana na utendaji wa huduma hizi na idadi ya wananchi wanaotumia huduma hizi.

Serikali ijikite na iangalie kwa makini sana suala la kuweka mazingira bora ya kukuza uchumi wa raia wetu, kwanza, kisha uwekezaji wa nje baadae.

Tusipofanya hivi katika kipindi hiki cha awali, tunaweza kujikuta tumegawa rasilimali zetu zote kwa wageni na kuwasahau wazawa, na hili likitokea ndipo anguko la taifa hili litakapotokea kwa kasi ya uasi.

TUMEAMUA KUJENGA: TUWEKE MISINGI IMARA, TUREJESHE MNYORORO WA BIASHARA YA ANGA MIKONONI MWA ATCL.

Asanteni sana.

Mama Anna Mghwira
Mwenyekiti wa ACT – WAZALENDO
 
Hapo umemtaja Esther Maro -> Anna Mkapa -> Mkapa, sidhani kama JPM atakusikiliza..
 
Itakumbukwa kuwa Makaburu hao hao walimrubuni mmoja kati ya mawaziri wetu wa mawasiliano na uchukuzi Mhe, William Kusila akasaini andiko (Document)/ mkataba kati ya mikataba ya Alliance Air/ATC karatasi likiwa na nembo ya wizara (letter headed) bila ya maandishi yeyote akaweka sahihi yake mkataba huo na kuwapatia makaburu waende wakajaze maelezo wanayotaka wao nchini kwao Afrika ya Kusini.
Mawazo ni mazuri sana nafikiri yanaweza kufanyiwa kazi.

Kwenye red,sidhani hata Mangungo ambaye tunafanya reference kwake kama SI unit ya mikataba ya hovyo aliyowahi kuingia lakini huyo Mangungo atasubiri kwa Kusila na nafikiri ni vyema hiyo SI unit ikabadilika.

kituko hicho kimeniacha hoi, hakika bila kurekebisha mambo yetu hasa sheria,Katiba na taratibu za maamuzi yasiwe kwa mtu mmoja kama Rais au waziri basi haya mambo yatajirudia mbeleni na hilo ndo TATIZO la msingi tulilonalo na si sehemu nyingine. Naamini tunajielewa ila ni binadamu wachache wanaotumia loophole za udhaifu wa Katiba yetu pamoja na sheria zetu kujinufaisha wao lakini bado tunaona hakuna tatizo hapo. Hakika nimeghairi, HATUJIELEWI!
 
Hoja nzuri sana ya ACT-Wazalendo. Pia kwa kuongezea ATCL wafanye kazi kwa karibu na mawakala wa tiketi mahiri wenye weledi wa sekta hii ya anga inakwenda vipi kimataifa ili ATCL iweze kuunganishwa ktk mnyororo (chain) ya mahoteli, usafiri wa majini, mbuga za wanyama n.k nitafafanua
  • Safari za kimataifa za kuleta watalii ATCL waunganishe tiketi zao za ndege, usafiri wa baharini (Azam Marine) na Mahoteli ya Z'Bar ili mtalii anayetaka ''package holidays What are package tours, How to organise package tours '' nzima basi analipia vitu vyote hivyo ktk mnyororo wa safari ya kitalii sehemu moja. Mtalii aliyetumia ATCL anakuwa anapokelewa airport JKNIA anapanda shuttle bus mpaka bandarini kupanda boti ya kazi ya Azam Marine na kufika Z'bar ktk hoteli iliyokwisha pangiwa. Hii itafanya mtalii kupata huduma bora bila usumbufu wa kutafuta teksi, kufika bandarini kuanza kutafuta tiketi ya boti na akifika Z'bar aanze kukata kiguu na njia kutafuta hoteli. Wenzetu Kenya, South Africa na Ethiopia n.k tayari huduma ya namna hii yenye kuhakikisha ''mnyororo wa huduma'' haukatiki huwasaidia sana kupata watalii wengi maana analipa pesa kwa huduma zote hizi. Na siyo Afrika tu nchi nyingi za Ulaya na Visiwa vya Karibi, Marekani n.k huduma hii ipo na inafahamika kuwavutia watalii na kupunguza usumbufu ugenini.
  • Mnyororo wa huduma kwa mtalii hiu pia unaweza kutumika kanda ya kaskazini ya utalii Tanzania ATCL inaunganishwa na bus shuttle services/hoteli/4x4 drive car hire/ malipo ya kupanda mlima Kilimanjaro, malipo ya kuingia Ngorongoro Crater/Serengeti/Manyara/Wapangazi n.k
  • Isifikiriwe kuwa ''mnyororo wa huduma a.k.a package holidays What are package tours, How to organise package tours '' kwa watalii kuanzia tiketi ya ndege na huduma zingine zinastahiki kwa '''watalii matajiri tu'' bali hata wale watalii wa bajeti ndogo pia huvutiwa na aina hii ya ''muunganisho wa huduma zote kulipia'' sehemu moja na ATCL, Azam Marine, Ngorongoro Crater, Mbuga zingine, mahoteli, wapagazi, tour operators n.k watatafuta mfumo wa namna gani watagawana pesa kwa kumhudumia mtalii kupitia mfumo huo wa one pay point.
 
Makala ya ukweli, kwa upande wangu yangu ni haya:

1. Air Tanzania waboreshe website yao, website ya sasa iko too local (haivutii). Biashara ya ndege inaenda na mambo ya mvuto mvuto.

2. Nilisikia huko mbeleni wanataka kuanzisha route za moja kwa moja hadi USA, nawashauli wazidishe usalama kwenye viwanja vya ndege maana kule US wanabagua sana-sio kila nchi inaweza kuwa na direct fright link. Mkitaka kujua vizuri hili jambo fuatilieni yaliyo wakutaga WAKENYA na shirika lao.

3. Halafu wazo la kuwa na ndege nne aina ya Q 400 nimelipenda, kwasababu route wanazotaka kwenda ni nyingi so ndege tatu au mbili nahisi hazitatosha na zitachoka mapema.

4. Rais, Waziri mwenye dhamana, na bodi mnafanya kazi nzuri so kazeni buti.
 
Back
Top Bottom