Angel: Niliteseka mno nikiwa teja, natamani kurudi darasani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Angel: Niliteseka mno nikiwa teja, natamani kurudi darasani

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 19, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 19, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Angel Bonconsil​

  Na Habel Chidawali, Dodoma
  WASWAHILI husema, maisha ni safari ndefu na kuongeza kwamba katika maisha kuna milima na mabonde ambayo binadamu huyapitia kabla ya kuyafikia mafanikio.

  Japo siyo binadamu wote wanaoweza kufika katika mafanikio, yumkini kila mtu amepangiwa mafanikio ya namna moja au nyingine na kwa njia yake kulingana na gawio lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye mara zote ndiye mgawaji.

  Licha ya kwamba wapo waliofanikiwa wakiwa bado vijana, lakini wapo pia ambao wamefanikiwa katika umri mkubwa wa uzee wao na hata wakati mwingine kuna watu wanakufa bila ya kufikia mafanikio, hivyo wanakufa na ndoto zao.

  Ni ukweli usiopingika kuwa njia za kutafuta mafanikio kwa kila mtu zipo nyingi ikiwa ni halali na nyingine huwa si za halali jambo linalofanya kuwepo na changamoto nyingi za kimaisha juu ya namna watu wanavyoweza kutumia njia zinazokubarika katika kuhalarisha mapato yao.

  Lakini, simulizi ya Angel Bonconsil, msichana mbichi kiumri ni ya aina yake ambayo kila mwenye macho na masikio asingetaka apitwe nayo kutokana na ukweli kuwa simulizi yake ni kama ndoto ya mchana, lakini kubwa ni kuwa anaapa kupigana kwa nguvu, akili na utashi wake wote kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya katika jamii.

  Katika umri wake mdogo binti huyu anakiri kuwa bingwa wa kutumia dawa za kulevya kiasi cha kuweza kuingia katika orodha ya watumiaji mabingwa (mateja) katika namna ya kutumia dawa hizo lengo likiw ani kupita njia ya mkato baada ya kuelezwa kuwa ingemfikisha katika mafanikio ya haraka.

  Angel anaanza historia ya maisha yake amayo inaogopesha na hasa katika maeneo ambayo amepitia hadi hapo alipo na namna ambavyo anakabiliwa na changamoto kubwa kuliko umri wake wa miaka 20, lakini kikubwa anataka kurudi shule akasome kwani ametambua kuwa elimu ndiyo pekee itakayomuondolea adha ya maisha.

  Angel ni nani
  Kiumri, ana miaka 20 , ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya Mzee Bonconsil yenye jumla ya watoto sita inayoishi eneo la Area D katika Manispaa ya Dodoma ambaye alitokea kuwa kituko katika familia yao na kuishia kufukuzwa nyumbani kwa baba yake mzazi.

  Maisha yake yamekuwa hatarini kwa zaidi ya miaka minne tangu alipoanza kujihusisha na dawa za kulevya, jambo hilo limemsababishia hata kuacha masomo yake akiwa kidato cha tatu licha ya sasa kuujutia uamuzi wake huo.

  Kwa maneno yake mwenyewe anasema, “Sikuona kama kulikuwa na dunia nyingine zaidi ya kutumia unga na kama ilikuwepo kwangu ilikuwa ni giza jambo ambalo nalijutia maisha yangu yote na kikubwa najuta kuacha shule nikiwa kidato cha tatu.’’

  Msichana huyo mwenye uso wa aibu mbele za watu anaweka bayana kuwa ametumia dawa hizo kwa zaidi ya miaka minne mfululizo na katika muda huo hakuwa na kauli ya hapana kwa watu waliomhitaji katika ushirikiano wa kimapenzi, kitu kilichokuwa kikihatarisha maisha yake.

  Lini alianza kutumia mihadarati
  Anasema akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kiwanja Cha Ndege Manispaa ya Dodoma mwaka 2009, alianza kutumia dawa za kulevya baada ya kudanganywa na mvulana ambaye hakupenda kumtaja kwa jina ambaye anasema walikuwana uhusiano wa kimapenzi.

  “Sipendi hata kulisikia jina lake maana aliniponza hata kufukuzwa na baba yangu nyumbani na akaufanya mwili wangu kuwa ni mali ya kila mtu,………….,’’anasimulia huku akibubujikwa na machozi.

  Anasema kuwa alipoanza kutumia dawa hizo ilimlazimu mara nyingi kuiba fedha kutoka kwa wazazi wake ambapo anakiri kuwa kupitia mkono wake alimsababishia hasara kubwa baba yake kwani ilikuwa ni lazima mpenzi wake anapokosa fedha, basi yeye (Angel) achakarike na kupata pesa na njia pekee ilikuwa ni kuiba.

  Vipi aliingia mitaani
  Muda mfupi baada ya kuanza kutumia dawa hizo, anasema hali yake ilibadilika ikiwa ni pamoja na kushuka ghafla kwa uwezo wake kimasomo darasani na vitendo vya udokozi, jambo lililomfanya baba yake kumfukuza nyumbani baada ya kumuonya mara kadhaa bila mafanikio hivyo akakimbilia mitaani ambako ameishi kwa zaidi ya miaka mitatu.

  Tangu wakati huo hadi mwishoni mwa mwezi Machi alipopata bahati ya mtende baada ya kuombewa msamaha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen na baba yake kumkubali alipobaini kuwa binti huyo amejitambua na kujutia makosa yake.

  Binti huyu anasema mara kadhaa alikuwa akipata misukosuko mikubwa kutokana na umri wake, lakini anaeleza kuwa hakuona kitu cha hatari mbele yake kwani ulikuwa ni wakati wa yeye kutumia kila kilichopatikana mbele yake jambo lililomsababishia kuchoka na hata mwili wake kudhoofu kwa kiasi kikubwa.

  Mara kadhaa alipelekwa katika hospitali ya watu wenye matatizo ya akili katika Taasisi ya Mirembe, lakini aliporudishwa kasi ya kutumia dawa hizo iliongezeka zaidi.

  Changamoto anazopata
  Licha ya kusamehewa na kurudi kwa wazazi, anasema bado vijana wengi wanamtafuta na mara kadhaa wanamdhihaki kwa kumpa dawa hizo huku wakihoji kama kweli ameacha kutumia kabisa.

  Anasema anapambana na vikwazo hata kwa wauzaji ambako alizoea kupita kwa kununua ambao wamekuwa na shaka naye huku akiwa na hofu kutokana na maovu mengi aliyofanya katika kipindi cha utumiaji wake na hofu yake kubwa ni kwa wanaume ambao wakati wote anaamini kuwa ndio chanzo cha yeye kufikia hatua hiyo.

  “Kwa sasa nimerudi kwa wazazi wangu na baba amenipokea japo nahisi bado ana shaka kidogo nami na wakati mwingine hata majirani, lakini si unajua kuharibu kitu ni rahisi, lakini kukitengeneza itachukua muda mrefu,’’ anaeleza.

  Baba yake anena
  Baba mzazi wa binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Bonconsil Olomi amesema kuwa hali ya binti yake kwa sasa ni nzuri na kwamba kuna tofauti kubwa kati ya kipindi cha kabla ya kujiunga na Saada na wakati huu ambapo mara zote amekuwa mtu wa majuto na msahama zaidi.

  “Ukweli huyu mtoto nilishakata tamaa kabisa maana sikutegemea kwamba angeweza kuwa mtu kama walivyo watoto wengine, lakini nawashukuru Jeshi la Polisi, hasa RPC sina cha kuwapa ila nawaombea kwa Mungu,’’anasema Mzee Olomi.

  Hata hivyo, Mzee Olomi analiomba jeshi hilo kuangalia muda wa mazoezi kwa vijana hao ili wautenge na kwamba inampa wasiwasi pale wanaporudi usiku kutoka katika uelimishaji wao kwani anasema kama mtu aliumwa na nyoka wakati wote anakuwa na shaka.

  Kwa nini yupo hadharani
  Anakitaja kikundi cha SAADA kuwa ndicho kilichomuwezesha yeye kufikia hatua ya kuona kile alichokuwa akikitumia hakikuwa sahihi baada ya kupata elimu ya kutosha kutoka kwa wanakikundi wenzake (mateja wastaafu).

  Anasimulia kuwa kikundi hicho kilimkuta katika Mitaa ya Hazina mjini Dodoma mahali ambako ni maarufu kwa watumiaji wa dawa za kulevya na mara kadhaa walijaribu kuzungumza naye ndipo ulipofika wakati wa yeye kuamua kuwa ni wakati muafaka wa kuachana na madawa hayo.

  Saada ni nini
  The Small Axe Against Drugs Abuse (Saada) ni mtandao ulioanzwishwa na Kamanda Zelothe Stephen ambacho kilizinduliwa Oktoba 23,2009 kwa ajili ya kuwakusanya watu wanaotumia dawa za kulevya na kuwapatia elimu badala ya kuwapeleka mahakamani.

  Kauli ya Kamanda Zelothe
  Kamanda Zelothe anasema kazi ya kupambana na watumiaji wa dawa za kulevya mkoani dodoma imekuwani ngumu lakini kwa kuwatumia vijana wa Saada wameweza kupata mafanikio makubwa kiasi kwamba mtandao wa watumiaji hao sasa umekuwa ni mdogo.

  Anasema kuwa amekuwa akipata ushirikiano wa karibu kutoka kwa taasisi mbalimbali ikiwemo Manispaa ya Dodoma, Hospitali ya Mirembe, Hospitali ya DCMC pamoja na Tume ya Taifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya.

  Kwa mujibu wa Zelothe, mashirika hayo pia yanategemea kwa kiasi kikubwa nguvu kutoka kwa watumiaji wenyewe yaa saada kutoka na kuwa wanazifahamu njia zote zinazotumiwa na watu katika kuingiza madawa pamoja na masoko kwa watumiaji wao.

  “Sisi tumeanzisha mfumo wa urafiki na hawa watu sio kuwatenga bali ni kutaka kujua historia yao pamoja na kutafuta namna bora ya kuwasaidia kwani tukisema kwamba wafikishwe mahakamani tutajaza gereza ndio maana tunaangalia nam,nay a kuwafanya wawe wajasiliamali,’’anasema Zelothe.

  Anayataja mafanikio ya Saada kuw ani pamoja na kuwarudisha shule vijana wawili, akiwemo James Komanya ambaye yuko mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye hapo awali alishaharibika, lakini baada ya kuacha amekuwa raia mwema na anayetumia muda wake kwa ajili ya kuelimisha wengine.

  Kamanda huyo anasema kuwa katika mapambano hayo, wanayo changangamoto pia ikiwemo kuwa na kituo maalumu cha vijana hao kwa ajili ya kupata elimu (sober house) ambacho kinaweza kuwa ni sehemu ya kutolea darasa kwa waathirika badara ya kuwafuata mmoja mmoja.

  Ofisa msimamizi wa masuala ya afya katika Hospitali ya Dodoma Christian Medical Centre (DCMC), Katrin Boehl anabainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa katika mapambano hayo kwnai wako vijana ambao wanahitaji kuelimishwa zaidi.
  Angel: Niliteseka mno nikiwa teja, natamani kurudi darasani
  Boehl anasema njia iliyotumiwa na polisi ni njia ya kisasa zaidi inayofaa kuigwa maana sio kila wakati kuwakamata watu na kuwajaa magerezani bila ya kuangalia chanzo chanzo na akasema (DCMC) itaendelea kutoa msaada kwa kadri inavyowezekana katika mapambano hayo.

  Mwisho
   
 2. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #2
  May 19, 2012
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 9,223
  Likes Received: 1,412
  Trophy Points: 280
  Huyu RPC hana maisha marefu kwenye cheo hicho kwani aanataka kuwashika wakubwa wake mahali pabaya, atawekwa benchi sasahivi.
   
 3. N

  Nguto JF-Expert Member

  #3
  May 21, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 2,654
  Likes Received: 629
  Trophy Points: 280
  Kama mtu anamjua Angel amwambie au ampeleke tu kanisani akaombewe. Asiishie kutamani aende akakutane na Bwana Yesu.
   
Loading...