Anayedaiwa msimamizi wa mali za mke wa Balali ashtakiwa kwa utakatishaji fedha

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,490
54,884
Dar es Salaam. Elizabeth Balali (54), mfanyabiashara mkazi wa Boko Magengeni amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh25 milioni kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.

Mshtakiwa huyo anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali za mke wa gavana wa zamani wa Benki Kuu Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali, amesomewa mashtaka hayo leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 na wakili Wankyo Simon mbele ya hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina.

Wankyo amedai kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh25 milioni kwa ulaghai kutoka kwa Dk Roderick Kisenge.

Anadaiwa kumuuzia eneo la mita 900 ambalo halijapimwa lililopo Boko Dovya wilayani Kinondoni wakati akijua si lake.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wankyo amedai katika kipindi hicho mshtakiwa alipokea Sh25 milioni kutoka kwa Dk Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Elizabeth hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhujumu uchumi.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom