TANZIA Ambilikile Mwasapile, maarufu 'Babu wa Loliondo' afariki Dunia


Ambilikile Mwasapile maarufu kama Babu wa Loliondo amefariki dunia akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha Digodigo baada ya kuzidiwa gafla leo Mchana. Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro, Waso.

Babu wa Loliondo aliugua muda mrefu na kujitibu kwa miti shamba, alipoenda hospitali akiwa amechelewa.

Babu wa Loliondo alipata umaarufu kwa dawa yake aliyodai inatibu magonjwa yote.

=======
UPDATE: July 30, 2021

Chanzo cha kifo cha Mchungaji Ambilikile Mwasapile (86) kimetajwa aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha kupata tatizo la upumuaji na homa.

Tangu afariki wasaidizi wake na majirani wamekuwa wakieleza kushtushwa na kifo hicho ambacho kimetokea akiwa anaendelea kutoa huduma ya tiba ya kikombe aliyoanza tangu mwaka 2011.

Mchungaji Ambilikile ambaye ataendelea kukumbukwa kwa kuvutia maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kati ya mwaka 2011 hadi 2013 kutokana na tiba yake ya kikombe alifariki jana saa 9:45 jioni.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala amesema kuwa taarifa za awali za madaktari zinaeleza chanzo cha kifo ni nimonia ambapo kwa takriban siku tano alikuwa anaumwa na kupata sindano za masaa.

"Jana asubuhi aliamka vizuri akiendelea na matibabu lakini majira ya saa nane alianza kujisikia vibaya ndipo ilitafutwa gari kutaka kumpeleka hospitali ya Wasso ambaye alitaka,"amesema

Hata hivyo amesema wakiwa wanampandisha gari alijisikia vibaya na kuanza kutapika ndipo walimkimbiza kituo cha afya Chadigodigo na alifika akiwa tayari amefariki.

Baadhi ya wasaidizi wa mchungaji Mwasapile walisema kabla ya kuzidiwa na ugonjwa alikuwa akiendelea kutoa tiba ya kikombe kwa wagonjwa kadhaa ikiwepo wa corona.

Hivi karibuni akizugumza na vyombo vya habari Mwasapile aliomba kupelekewa wagonjwa wa corona kupata tiba kwani hakuna ugonjwa ambao Mungu unamshinda.

"Wiki mbili zilizopita alikuwa vizuri anatoa tiba japo kwa watu mmoja mmoja waliokuwa wanakuja lakini hali yake iliendelea kubadilika," amesema.

James Richard jirani wa Mchungaji huyo amesema hadi anafariki hakuwa na hali mbaya na ameacha mali kadhaa ikiwepo magari, nyumba na kiwanja ambacho alikuwa anaandaa kwa kutolea tiba

"Babu bado alikuwa anasema watu watakuja Samunge maelfu kupata tiba na alipata eneo kubwa ambalo alikuwa anaendelea kuliandaa,"amesema.

Mmoja wa waliowahi kuwa wasaidizi wababu wake Poul Dudui amesema taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa kwa uratibu wa Serikali na wanasubiriwa ndugu na watoto wake kujua atazikwa wapi na lini.

James Leyani mkazi wa Loliondo, amesema msiba umetokea wakati kuna janga la corona na kuna chanjo imeanza kutolewa hivyo muhimu watu kusikiliza maelezo ya wataalam wa afya na Serikali.

"Tunakubaliana na tiba za asili na imani lakini sasa muhimu kufuata maelezo zaidi ya wataalam wa afya na Serikali ili kukabiliana na janga hili,"amesema.
Corona imebeba! haina mchezo kwa wapuuzi
 
Back
Top Bottom