Aliyoyazungumza msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari leo jumamosi septemba 04, 2021

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,893
940
ALIYOYAZUNGUMZA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI NDUGU GERSON MSIGWA WAKATI AKIZUNGUMZA NA WANAHABARI LEO JUMAMOSI SEPTEMBA 04, 2021.

1. BEI YA MAFUTA.

Palitokea taarifa mbili, EWURA walitoa taarifa ya kupanda kwa bei ya mafuta na baadae kusitisha bei hizo. Ufafanuzi wa Serikali ni kwamba baada ya bei kupanda, Waziri Mkuu Mhe Kasim Majaliwa aliona kuna haja ya kuziangalia bei hizi na kuagiza bei zilizotumika Mwezi uliopita yani Agosti ndizo ziendelee. Kwahiyo bei zilezile za Agosti zinaendelea na zile zilizotangazwa za Septemba zimesitishwa na wananchi wanaendelea kutumia za Mwezi Agosti na Kamati ya kuchunguza bei hizi imeshakutana na imeanza kazi rasmi na imepewa muda wa wiki mbili na lengo la Serikali ni kuhakikisha bei za mafuta zinakuwa nafuu.

2. KUHUSU CORONA.

Nchi yetu ni moja ya nchi zilizoathirika na ugonjwa huu, wapo wagonjwa na wapo Watanzania ambao wamepoteza maisha. Serikali inaendelea kusisitiza Watanzania kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Wataalamu ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kukaa umbali usiopungua mita 1, kuepuka mikusanyiko, kutumia barakoa, vitakasa mikono, kufanya mazoezi na zaidi kutumia afuu iliyoletwa ambayo ni chanjo. Watanzania wote waliozidi miaka 18 wanahimizwa kwenda kwenye vituo mbalimbali kote nchini ili kupokea chanjo kwasababu ukichanja unajiepusha na hatari ya kifo au hatari ya kuugua sana na kupata ugonjwa mkali. Eneo hili Serikali inasisitiza Wataalamu ndiyo wasikilizwe.

Kwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan tulifanikiwa kupata dozi 1,058,400 ambazo mpaka sasa jumla ya Watanzania 325,000 sawa na asilimia 31.5 ya chanjo zilizoletwa wameshapokea chanjo na zoezi linakwenda vizuri katika vituo mbalimbali na Watanzania wengi wanaendelea kujitokeza kupokea chanjo na Serikali ingependa kuhimiza hasa yale makundi ya hatari kama watu wenye umri zaidi ya miaka 50, wenye magonjwa sugu, wanaofanya kazi katika maeneo yanayowakutanisha na watu wengi, madaktari, wauguzi, askari n.k ni vizuri kuchangamka kupata chanjo tujikinge.

3. KUHUSU TOZO.

Kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Samia Suluhu Hassan kufanyia kazi madai na malalamiko yote ya wananchi kuhusu tozo, Agosti 31, 2021 Serikali imetoa taarifa na imeamua kupunguza tozo za miamala ya simu kwa asilimia 30 na kwa watu wanaotuma kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine, Serikali imefanya mazungumzo na watoa huduma (makampuni ya simu) na wamekubali kupunguza kwa asilimia 10. Chini ya elfu 1 yaani kuanzia 0 hadi elfu 1 hakuna tozo yoyote na tunaamini sasa italeta nafuu baada ya Watanzania kulalamikia kwamba ni mzigo na Serikali imeona. Tozo hizi zinafanyika kwa nia njema na tumepata mafanikio makubwa kwa muda wa mwezi mmoja na nusu. Tumekusanya jumla ya bilioni 63 na kipindi hiki tu tumepata uwezo wa kujenga vituo vya afya 150 na vingine 70 vinakuja kwahiyo tutakua na vituo vya afya kwa ngazi ya tarafa 220 na maboma ya madarasa takribani 560 yanakwenda kumalizwa.

Kumekuwa na maneno kwamba mbona huko nyuma tozo hazikuwepo na tulikuwa tunajenga, Serikali sasa imeamua kuongeza kasi ya kuimarisha huduma hizi kwa wananchi. Kama madarasa haya 560 yalitakiwa yajengwe kwa miaka minne, sasa Serikali imeona iweke hii tozo ili Watanzania watatuliwe matatizo haya ya madawati, madarasa, vituo vya afya, barabara ambazo hazipitiki basi yatatuliwe haraka na tuwe na kasi. Kuna watu huko vijijini anasikia kuna lami mpaka anazeeka lami haijafika. Sasa Serikali imeona kasi hii tuiongeze ndo maana inakuja na vyanzo hivi vya mapato.

4. SUALA LA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA).

Watanzania wanalalamika, vitambulisho hatujapata, nitoe taarifa kwamba Serikali kupitia NIDA inaendelea na mchakato huu wa kutoa vitambulisho. Mpaka sasa NIDA wametoa vitambulisho milioni 9 na laki 4 na vitambulisho milioni 8 na laki 5 vimehakikiwa vyema kimajina, umri n.k na vimepelekwa kwa wahusika. Katika vitambulisho hivyo milioni 8 na laki 5 vilivyohakikiwa, tayari Watanzania milioni 7 na laki 2 wameshachukua vitambulisho vyao. Kuna vitambulisho milioni 1 na laki 3 bado viko kwenye ofisi ya wasajili, sasa Watanzania wanaolalamika hawajapata vitambulisho vyao ni hao ambao hawajaenda kwenye ofisi za wasajili kwenda kuchukua. Serikali inatoa wito kwa Watanzania wote ambao wamejisajili mwende kwenye vituo vyenu vya usajili mkachukue vitambulisho vyenu.

Ziko changamoto zingine, wako baadhi ya Watanzania waliomba vitambulisho, wamezalishiwa lakini vilipokuja wakabaini vina kasoro. Vitambulisho vile vimerudishwa NIDA kwa ajili ya kurekebishwa na mchakato huo unachukua muda mrefu kwasababu eneo hili la vitambulisho ni nyeti kidogo Kwahiyo ni lazima NIDA ijiridhishe juu ya mtu anayebadirisha kitambulisho chake isije akawa anachukua taarifa za mtu mwingine au anafanya hivyo kwa nia ovu na kama kuna Mtanzania anapata changamoto basi afike ofisi za Wasajili watapata maelezo na utatuzi wa shida yake.

5. UPATIKANAJI WA SUKARI.

Kumekuwa na mjadala juu ya upatikanaji wa sukari. Hali ya upatikanaji wa sukari kwenye nchi yetu ni mzuri na tunayo sukari ya kutosha. Tulipata upungufu kidogo kati ya Mwezi Aprili na Juni na hii inatokana na kwamba wakati huo viwanda vyetu vinakuwa havizalishi kwasababu ya mvua ko Wataalamu wetu wa uzalishaji wa sukari wanatuambia muda huo miwa ukiivuna na kuipeleka kwenye kiwanda inakua na kiwango kidogo cha sukari ko si kipindi kizuri cha kuzalisha sukari. Wastani wa uzalishaji wa sukari kwa mwaka katika nchi yetu ni tani 367,000 na mahitaji ya nchi yetu ni kama tani laki 420,000 hivyo tuna upungufu kati ya tani 40,000 na 50,000 lakini pamoja na kuwepo kwa upungufu huu Serikali iliamua kuweka utaratibu wa hawa wazalishaji wa sukari wawe wanapewa vibari kwa ajili ya kuagiza sukari nje inayopungua na zoezi linafanyika vizuri na wanaendelea kuleta.

Kumekuwa na wafanyabiashara ambao wanataka kulazimisha kuleta sukari nje ya utaratibu huu, lakini Serikali imefanya hivi kwa nia njema kwa kukubaliana na hawa wamiliki wa viwanda waongeze uzalishaji hatua kwa hatua na zoezi linakwenda vizuri na hawa hawa ndio wabebe jukumu la kuleta sukari inayopungua. Wale wanaojaribu kuhangaika kwa maslahi yao, Serikali iko macho na inafuatilia. Serikali inafanya hivi kwa sababu kuu mbili, moja kuhakikisha Watanzania wanapata sukari na wanapata kwa bei nzuri japo tunatambua bei kwasasa zimepanda kidogo na zaidi kuhakikisha Watanzania wanapata sukari salama. Tukiachia kila mtu anaingiza, wapo watu wataleta sukari iliyopitwa na wakati na kuwaletea Watanzania madhara. Yote kwa yote Serikali imeendelea kufanya juhudi kubwa kuhakikisha uzalishaji wa sukari unaongezeka katika nchi yetu.

Kwa ujumla wa viwanda vyetu vitatu nchini kuanzia cha Kagera, Mtibwa na Kilombero kwa miaka mitatu ijayo vinatarajia kuongeza uzalishaji kwa kiwango cha tani 265,000 zitaungana na tani 367,000 za sasa na hivyo nchi yetu itakuwa na tani 660,000 na wakati huo tutakuwa hatuzungumzi upungufu wa sukari na kazi kubwa inafanyika katika viwanda vyote kuongeza uzalishaji ili tusiende kwenye upungufu wa sukari. Yote kwa yote Serikali inaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya sukari na viwanda vipya vya kuzalisha sukari ikiwemo kiwanda cha Bagamoyo Sugar cha Mzee Salim Bakhresa na mradi wa kuzalisha sukari unaotekelezwa kwa ushirikiano wa NSSF na Magereza na wana shamba wanalima kule Mbigili na tayari wamelima shamba zaidi ya hekari 2760.

NB: Yote kwa yote shughuli zote za Serikali zinaendelea vizuri, Serikali inaendelea kugharamia shughuli mbalimbali za kuhudumia Watanzania, miradi inaendelea vyema.

Wiki hii Serikali imefanya malipo ya awali ya bilioni 212.959 kwa ajili ya ndege zingine 5 ambazo Serikali imeagiza. Serikali imefanya malipo ya bilioni 50 wiki hii kwa ajili ya mradi wa reli, malipo mengine ya bilioni 50 kwa mradi wetu wa kufua umeme kule Julius Nyerere, imetoa bilioni 20 kwa ajili ya elimu bure, kwenye mfuko wa barabara wiki hii Serikali imetoa bilioni 55.4 kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa barabara. Umeme vijijini mpaka mwezi Disemba 2022 tunataka tumalize kabisa kila Kijiji kiwe na umeme na tayari wiki hii Serikali imetoa bilioni 25 kwenda REA kwenye mradi wa umeme vijijini na mijini, ununuzi wa nafaka kwenye mahindi na mazao mengine. Serikali imetoa bilioni 14 kwa NFRA kwa wakala wa hifadhi ya chakula na bilioni 5 kwa Bodi ya mazao mchanganyiko ili kununua mazao ya Tanzania.

Zaidi Serikali iliahidi, badala ya madiwani kulipwa posho zao kupitia Halmashauri, sasa zitalipwa kutoka hazina na tayari Serikali imetoa bilioni 1.686 kwa ajili ya kulipa posho na mishahara ya madiwani. Kwahiyo mambo yanakwenda na hakuna kilichoharibika na Watanzania tuendelee kuunga mkono Serikali yetu mambo yanakwenda vizuri msiwe na wasiwasi na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan anawahakikishia kwamba mambo yanakwenda vizuri. Tuchape kazi, tujenge nchi yetu na tulipe kodi.

#KaziInaendelea.


E-brmdRWEAE4ENo.jpg


E-bsCeuWYAMFp41.jpg
 
Pia kwa sasa tunaelezwa wazi kwamba Serikali ndiyo iliyotoa fedha hizo na kufanya manunizi hayo na si vinginevyo.
 
Back
Top Bottom