Aliyeanza kutikisa mnara wa Babel asaidiwe kuuangusha

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Posted Date::4/28/2008
Aliyeanza kutikisa mnara wa Babel asaidiwe kuuangusha
Na Hemed Kivuyo
Mwananchi

KATIKA kila uongozi wa nchi kuna miiko, mojawapo ya miiko ya uongozi ni kiongozi kutokuwa fisadi, kutohujumu nchi na kuwajali wananchi anaowaoongaza.

Tanzania ya sasa inataka kuazimia kumfanya kiongozi wa kisiasa kuwa tajiri mwenye biashara kubwa aliyowakabidi watu wamwendeshee. Ile miiko ya kiongozi kutokuwa bepari na kutokujilimbikizia mali, sasa imeshapitwa na wakati.

Kabla ya sijazama kinagaubaga naomba nivute kumbukumbu na kumkumbuka Rais wetu wa awamu ya tatu mzee Benjamin Mkapa. Mzee Mkapa alipokea kijiti kutoka kwa Mzee Mwinyi kwa `madaha na kutoa kauli kali sana dhidi ya wala rushwa, alisema kuwa tetesi za rushwa zitatosha kumuondoa kiongozi aliyeko katika ofisi ya umma, Mkapa alisisitiza maadili mazuri ya uongozi kwa viongozi wa chini yake.

Mmoja wa mawaziri wake aliupamba uamuzi wa kununua ndege `mbovu ya Rais kwa kuwaambia Watanzania kuwa ndege ni lazima inunuliwe hata kama itabidi Watanzania kula majani.

Kwa kile kilichoitwa kuwa ni `funika kombe mwanaharamu apite`Mkapa aliwafikisha kortini mawaziri wake wawili kwa madai ya ufisadi, wengine wakatafsiri kuwa ameamua kuwatoa kafara ili Watanzania wadadisi wapoteze mwelekeo kifikra.

Pamoja na kuunda kamati za kuibua rushwa lakini wananchi walipoteza imani na juhudi za serikali katika kupambana na rushwa kwani zaidi serikali ilibuni mianya mingine ya kuwanufaisha viongozi kutokana na kuingia mikataba isiyo na maslahi kwa Watanzania.

Mkapa pamoja na mmoja wa mawaziri wake walidaiwa kujinunulia kampuni bila kuwepo na ushindani wa zabuni, achili ambali kusajili kampuni yeye na mkewe.

Kumekuwapo na vyanzo mbalimbali vya habari zinazothibitisha kuwa Mkapa alijilimbikizia nyumba nyingi za umma bila kufuata taratibu na mikataba mingi mibovu inayosakama roho ya serikali ya awamu ya nne sasa ilipita wakati yeye akiwa Ikulu, isisahaulike kuwa baadhi ya watu walipokwa uraia wao wakati wa uongozi wake, watu walijaribu kumkosoa pale walipoona kakosea lakini alitia pamba masikioni na zaidi aliwabedua kwa kiburi wale waliothubutu kumkosoa kwa kuwaambia kuwa wana wivu wa kike.

Kuna wakati Mkapa aliulizwa kuhusiana na baadhi ya tuhuma alisema kuwa hawezi kujibu chochote kwa kuwa ameshastaafu siasa. Je, Mkapa anaweza kutuonyesha kifungu cha katiba kinachosema kiongozi akistaafu haruhusiwi kuongea chochote kiwe kizuri au kibaya kilichokuwa kikimuhusu wakati akiwa Ikulu?

Katika sakata la Richmond lililoitikisa nchi, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ilipewa jukumu la kufuatilia suala hilo, wakafanya hivyo, wakaleta taarifa kuwa Richmond ni safi ingawa kulikuwa na mapungufu kidogo tu ya kibinadamu.

Haihitaji kuwa na elimu ya juu sana kutambua udhaifu wa taasisi hiyo na nitashangaa endapo hawatowajibishwa. Kwa mtazamo wangu ni vyema taasisi hiyo ikavunjwa na kuundwa upya kwa kuwa haikuanza kushindwa kazi juzi.

Suala zito linalohusu maslahi ya Taifa linahitaji busara za hali ya juu sana, Watanzania wa sasa si wale wa zidumu fikra za mwenyekiti, ni Watanzania wenye uwezo wa kudadavua mambo na kuyaweka bayana. Hivi sasa ni wazi kwamba ni kelele za mlango zinamnyima usingizi mwenye nyumba.

Kuwepo kwa mikataba yenye mapungufu, ufisadi katika ofisi za umma ni mbiu ambayo ilianza kupigwa wakati Mkapa akiwa Ikulu na ni dhahiri alifumba masikio na kama alikuwa akisikia basi alihisi ni kelele za chura hazimzuii mwenye kisima kuteka maji. Madhara mengi yanayoonekana hivi sasa na kuisakama roho ya serikali ya awamu ya nne yalipikwa wakati wa utawala wa awamu ya tatu.

Kwamba Tanzania ni nchi masikini hilo si kweli kwa sababu nyingi na mojawapo ni hili la rasilimali inazomiliki Tanzania, baadhi ya watendaji wasio waaminifu ndio walioambukiza ukimwi, uchumi wa Tanzania.

Tuchukulie kwa makadirio ya chini sana, yaani zile fedha zinazodaiwa kufujwa katika Benki Kuu (B.O.T.) na hizi za Richmond zingetumika kufufua viwanda vya serikali vilivyokufa miaka mingi iliyopita, kila mkoa ungekuwa na viwanda visivyopungua vitano na pia kila mkoa kwa viwanda hivyo vingeajiri Watanzania wasiopungua laki sita ambao wangeinua vipato vyao na maisha bora kwa kila mtanzania yasingeleta ubishani.

Hayo ni kwa yale mapungufu yaliyojulikana je kwa yale ambayo bado kufahamika ama yanafahamika lakini yanazimwa? Tanzania ni masikini kwa sababu zipi? Inavyoonekana ni kama mafisadi walianza kujenga mnara kama wa Babel na sasa umetikiswa kama sio kuvunjwa kabisa na ndoto zao za kumfikia Mungu kuyeyuka!

Mnara wa Babel haukujengwa na mtu mmoja ama wawili au watatu,ulijengwa na watu wengi na kwa siku isiyo moja. Walioshiriki kujenga mnara wa kifisadi hapa Tanzania hawakuanza kazi hiyo jana wala juzi na wala sio watu wachache kiasi hicho. Ulijengwa na timu kubwa kwakuwa sio kazi rahisi. Wasitolewe kafara wachache, ikiwezekana wote washughulikiwe!

Tatizo la utafunaji wa mabilioni ya Watanzania ni kama ka mtindo kalikozoeleka na tabia hii tayari viongozi wadogo wameshaambukizwa. Mnara wa ufisadi ulianza kujengwa na timu kubwa chini ya nahodha wao Mkapa.

Kama kweli kilio cha Watanzania kimaeanza kusikilizwa, basi aliyeanza kutikisa mnara wa Babel na asaidiwe ili uangushwe!

Sitaki kuamini kama waliohusika kutumia mabilioni ya umma kwa manufaa yao wataachiwa bila kushtakiwa kwa madhila waliyowasababishia Watanzania ya kuzama katika lindi la umasikini.

Batuapepe: Medkivuyo11@yahoo.com

Simu: 0752 250157
 
Mkapa is a proof that the Late JK Nyerere was wrong in some of his decisions after he choose him for a presidential position and here he is seen to be the most corrupt president in history of Tanzania.

Huyu jamaa anamwaibisha hata Baba wa Taifa huko alipo sasa hivi.
 
Ile kauli ya JK kuwa tuwaache wastaafu wetu wapumzike kwa amani nadhani angeanza kwa kuwashauri wao kuwa wapumzike kutuibia mali zetu ya Umma ndipo wananchi tungewaacha wapumzike. Vinginevyo hatuna budi kuwaandama kwa kuwa wao pia hawajaamua kupumzika.
 
Back
Top Bottom