Alilotaka Mwalimu halikuwa, lakini laja

Kubwajinga

JF-Expert Member
Jan 23, 2008
2,194
297
Wakuu,
Ingekuwa jambo jema kwa nchi kama wale wana CCM wote wanaotishiwa nafasi zao na wana-mtandao wakajiunga pamoja na kujenga timu ya upinzani ndani ya CCM. Kwa mazingira ya sasa hivi ambapo rushwa imekithiri ndani ya CCM, nina uhakika mkubwa kuwa atakayeanzisha huu upinzani atakuwa na nafasi kubwa hata ya kumpiku JK mwaka 2010, akiamua kula naye sambamba, kwani ni wazi kuwa wana CCM walio wengi wamepoteza imani kwake na ameonekana kuwa kazi haiwezi. Wake up wana CCM halisi, chukueni chama chenu msikiache kikaendelea kupotezwa.
Alilotaka Mwalimu halikuwa, lakini laja

Jenerali Ulimwengu Machi 12, 2008NI dhahiri kwamba Mwalimu Nyerere, kama nilivyosema huko nyuma, alitaka Chama cha Mapinduzi kigawanyike ili kitokee chama kingine na upinzani uwe na maana katika siasa za Tanzania. Hili alilisema hadharani, lakini kuna mengine ambayo hakuyatamka hadharani na mengine aliyoyafanya lakini hayakujulikana kwa wengi.

Bunge la Jamhuri ya Muungano chini ya chama kimoja, lilikuwa ni Bunge la aina yake. Kutokana na misingi ya kinadharia aliyokuwa ameijenga Mwalimu, “upinzani” ulibidi utoke ndani ya chama chenyewe kutokana na kwamba ilikwisha kuamuliwa siasa za ushindani hazikulifaa taifa changa lenye haraka ya kuleta maendeleo ya watu wake.

Lakini hata huo “upinzani” alioutaka Mwalimu wakati wa chama kimoja ulikuwa teke mno kutokana na mantiki yenyewe ya chama kimoja. Katika hali ya kawaida haiwezekani kupiga marufuku vyama vya upinzani halafu ukajenga upinzani ndani ya chama kimoja kilichosalia.

Ile adha ya upinzani, ambayo tuliambiwa ingechelewesha maendeleo, ingeepukwa vipi? Ni wazi kwamba utawala wa kiimla, hata kama ulikuwa na nia njema, ulikuwa umejichimbia.

Mfano unaodhihirisha hili ni ule niliousimulia awali, wa akina Bakampenja na Mwakitwange. Inaelekea wabunge hawa waliiamini nadharia ya “upinzani” ndani ya chama, wakaijaribu, wakaona cha mtema kuni. Tangu walipofukuzwa kutoka katika chama, na wakafa kisiasa, kwa muda mrefu haikutokea sauti nyingine ya kutaka kijaribu nadharia hiyo.

Hata hivyo, katika miaka ya 1990-1995, likazuka kundi ndani ya Bunge la Jamhuri lililoijaribu nadharia hiyo kwa mafanikio makubwa. Kundi hili, lililojulikana kama G-55, kimsingi lilifanya kazi ya kuilazimisha Serikali “kukaa chonjo” kwa jinsi lilivyokuwa linaibua mjadala kuhusu masuala makuu ya kitaifa. Likawa ni kundi la upinzani usio rasmi.

Wengi wanaolikumbuka kundi hili wanachokumbuka ni ile hoja iliyoletwa mbele ya Bunge minajili ya kutaka iundwe ile iliyoitwa “Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano”. Lakini, kabla ya hoja hiyo kuhusu Tanganyika, G-55 ilikuwa imekwisha kuwasilisha hoja mbali mbali mbele ya Bunge na kuichachafya Serikali mpaka mambo yakaeleweka. Hoja hizi zilihusu mambo kama vile ubadilishaji wa madeni, “debt conversion,” urithi wa kitaifa (national heritage) kama vile mbuga za wanyama na visiwa vilivyoko Bahari ya Hindi mkabala na Dar es Salaam, maadili ya uongozi, na kadhalika.

Kundi hili lilijengeka mithili ya chama cha upinzani kwa vile lilivyoweza kujiratibu na kupanga namna ya uwasilishaji wa hoja kiasi kwamba Serikali ikajikuta imebanwa bara bara. Lakini Mwalimu alivutiwa zaidi na kundi hili pale lilipoleta “Hoja ya Tanganyika,” kwa sababu kimsingi aliipinga hoja hiyo.

Baadhi ya waliokua ndani ya kundi hilo tulikwenda mara kwa mara nyumbani kwake Msasani na kufanya mazungumzo naye, hususan kuhusu hoja hiyo iliyokuwa inamkera.

Ni jambo ambalo labda hata kwetu sisi wenyewe halikueleweka: Sisi tulikuwa tumeleta hoja hiyo wazi wazi mbele ya Bunge na tukasimama, mmoja baada ya mwingine kuitetea. Mwalimu akasema hoja hiyo haikubaliki, na akaapa kwamba ataipinga kwa “nguvu zangu kidogo zilizosalia.” Hata hivyo, akaendelea kutualika nyumbani kwake, na tukawa na majadiliano ya kirafiki kabisa, hata kama tulikuwa tunabishana naye sana.

Tukumbuke kwamba ni wakati huo huo Mwalimu alipoandika na kuchapisha kitabu chake, “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” akiwashutumu, kwa ukali usio wa kawaida baadhi ya viongozi wa chama na Serikali kuhusu “Hoja ya Tanganyika.”

Kwa wengi haikueleweka kwamba sisi waanzilishi wa hoja tunaitwa kunywa chai Msasani, tunacheka na kutaniana naye, huku watu ambao hawana uhusiano wa moja kwa moja na hoja hiyo wanatungiwa kitabu cha kuwashambulia.

Tuliposhindwa kuafikiana naye, Mwalimu aliamua kufanya kiitishwe kikao “shangingi,” kama lilivyokiita gazeti moja wakati huo. “Shangingi” kwa sababu kikao hicho kilijumuisha asasi takriban zote za utawala na uongozi nchini: Halmashauri Kuu ya CCM, Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wakilishi Zanzibar, wakuu wa mashirika ya umma, wakuu wa vitengo vya ulinzi na usalama n.k.

Hoja kuu aliyoijenga Nyerere katika kikao hicho kilichofanyika Kilimani, Dodoma, ni kama ifuatavyo: Sera ya CCM ni kuwa na serikali mbili, moja ya Zanzibar na nyingine ya Muungano, basi. Hawa vijana wameleta hoja ya kuunda serikali tatu, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sera ya CCM. Sasa, wachague, ama kuifutilia mbali hoja yao, au waondike ndani ya chama, wakaunde cha kwao kitakachotetea sera ya serikali tatu.

Si rahisi kueleza ni jinsi gani wana-G-55 waliponapona vipi kufukuzwa CCM, hasa baada ya baadhi ya wajumbe waandamizi kutaka wahusika wote wasimame, mmoja baada ya mwingine, watangaze msimamo wao, na wale watakaotofautiana na msimamo wa Mwalimu na CCM waondoke.

Ni busara za Mzee Mwinyi, mwenyekiti wa chama wakati huo, zilizoepusha hatima hiyo. Hatimaye hoja hioyo ikafutwa katika kumbukumbu za Bunge, na mambo yakawa shwari kwa wakati huo.

Baada ya muda nilikuja kuelewa maana ya hatua za Mwalimu Nyerere, hasa baada ya kuzungumza na mmoja wa wasaidizi wake wa karibu kabisa. Sikuwa tena na shaka kwamba Mwalimu alitaka ama tuondoke ndani ya CCM, ama tufukuzwe, ili tuweze kuanzisha chama kipya ambacho kingetoa changamoto kwa CCM na kuchangamsha siasa za ushindani. Bila shaka aliamini kwamba kwa jinsi hii kingezaliwa chama chenye msimamo wa kutetea maslahi ya wananchi vyema kuliko CCM, ambayo ilikwisha kumchosha.

Ni kwa hilo tu nilielewa kauli ya kila mara ya Mwalimu alipokuwa akikutana na wawakilishi wa G-55: Hii hoja mnayoileta Bungeni ni hoja ya kuvunja nchi. Mimi nawaelewa, mnafanya hivyo kutokana na frustration, lakini nchi haijengwi kwa frustration. Nipeni hoja nitakayoweza kuiunga mkono. Hoja hiyo, bila shaka, alitaka ijielekeze katika kujenga upinzani wa kweli nchini.

Sikuwa na njia ya kumdadisi Mwalimu kabla hajapatwa na maradhi yaliyomtoa duniani, lakini nadiriki kusema kwamba alifariki akiwa ni mwenye kusononeka kwa kuona mambo hayakwenda kama alivyotaka.

Kwa wale waliomjua Nyerere, hii haikuwa mara yake ya kwanza ya kutaka jambo liwe na lisiwe. Alikuwa na ushawishi mkubwa na madaraka yake yalikuwa makubwa wakati akiwa Ikulu. Hata alipoondoka madarakani aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa kutokana na haiba aliyokuwa ameijenga miongoni mwa wananchi.

Hii ni kwa sababu alikuwa kiongozi wa kweli, aliyewajali wananchi wake, akaishi maisha ya mtu wa kawaida, akadharau mali na ukwasi, na hivyo akajiepusha kabisa na ufisadi wa kila aina. Lakini si kila kitu alichotaka kilikuwa, na hili la kugawanyika kwa chama-tawala ni mojawapo.

Lakini hakuna shaka kwamba matakwa yake yatakidhiwa siku moja, hata kama itachukua karne nzima. Hali iliyomo ndani ya chama-tawala inaashiria kwamba chama hicho kimepungukiwa mshikamano, na dalili zimeanza kujitokeza za msambaratiko wa aina moja au nyingine. Hakuna anayeweza kutabiri msambaratiko huo utachukua mkondo gani, kama ni ule alioutabiri Mwalimu au ni kutoweka kabisa katika uwanja wa siasa za Tanzania.

Hili ni suala nitakalolijadili hapo baadaye.
 
Mkuu unataka watu wengine wakufanyie wewe vipi? CCM iko sawa kabisa wala haina noma mkuu, na kama kuna mwananchi anasubiri hayo unayosema, basi huenda CCM ikatutawala mpaka mwisho wa dunia, maana toka tumeanza kusikia kuwa watameguka na bado wapo tu,

cha muhimu ni sisi wenyewe wenye uchungu na taifa kuingia huko kunakotakiwa, otherwise dua la kuku halimpati mwewe mkuu, CCM wana makundi kama vile Republican Party na Democrats walivyo na makundi, ni very healthy kuwa nayo kwa ajili ya demokrasia, eti watagombana haitakuja kutokea ndio maana, mtandao hawakupewa nafasi yoyote muhimu ndani ya CCM, na pia makund mengine yakapewa uwaziri pia, ndio demokrasia hiyo mkuu makundi mbali mbali kupigana na mwishowe kupata idea moja inayokubalika na makundi yote, CCM inasonga mbele, lakini tunajua kuwa tuna some mafisadi, wameshaanza kuondolewa na bado tunasubiri umauzi wa Waziri Mkuu kutokana na mapendekezo aliyopewa na kamati ya Mwakyembe.
 
Madaana wanakiri upinzani wa kweli utatoka CCM hilo halina shida!lakini kwa upinzani tulikuwa nao sasa hakuna kitu
 
Back
Top Bottom