Alikiba anakutaka usiwe na wivu

Kitumba_

Member
Aug 21, 2018
29
20
Screenshot_20210924-073526.png
Wivu ni hisia zinazotokana na mapenzi na zinazalishwa haswa na uoga wa kwamba mtu anayempenda anapenda zaidi kwingine.
.
"We ndo my pain killer kushinda hata panadol umejaa mapenzi mashetani wanakaa kando, Oooh Shushu you for me, from Zero to Hero, bado tuko pamoja why you getting jealous?"- @officialalikiba JELOUS Ft Mayorkun, 2021.

Wahenga wanasema kwamba wivu katika mapenzi ni sawa na chumvi katika mboga, wapenzi ambao wanaopendana kutokuoneana wivu _ ni sawa na mboga iliyokosa chumvi, hata kama imepikwa vizuri kiasi gani, haitakuwa na ladha nzuri mdomoni. Vilevile chumvi inapozidi kwenye mboga, ipo wazi kwamba hata kama imepikwa vizuri kiasi gani, haitalika.

Kama tunakubaliana katika dhana hii, ni vizuri tukakubaliana kwamba wivu ni hisia muhimu katika mapenzi lakini unapozidi, huwa na madhara makubwa kwa wapendanao. Upo ushahidi wa matukio mengi ya kutisha katika mapenzi, ambayo yamefanywa kwa sababu ya wivu. Wapenzi wanauwana, wanajinyonga, wanawekana majeraha na vilema.

Ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya wivu wa kimapenzi! Wapo waliopigana na kuumizana vibaya na watu wengine kisa kikiwa ni wivu wa mapenzi. Wapo watu wengi tu wanaoendelea kusota kwenye kuta za magereza kwa sababu ya wivu wa kimapenzi. Bila shaka hata wewe kichwani mwako pengine unazo kumbukumbu za matukio mengi, mabaya yaliyokutokea wewe au yaliyowatokea watu unaowajua, kisa kikiwa ni wivu wa mapenzi.

Ushahidi huu unaonyesha kwamba kumbe wivu wa kimapenzi si hisia za kawaida zinazopaswa kupuuzwa kwani madhara yake ni makubwa, kwa hiyo ni vizuri kila mmoja akajua namna ya kuudhibiti wivu au namna ya kuishi kwa amani na mtu mwenye wivu uliopitiliza.

Hili ndilo lililopelekea msanii @officialalikiba kumtafuta mtayarishaji wa muziki hapa nchini Yogo Beats ambaye pia amehusika kutayarisha nyimbo kadhaa za Alikiba kama "Infedele" pamoja na "Salute". Alikiba kwenye wimbo huu anamthibitishia mpenzi wake kuwa anampenda na kumthamini hivyo asione wivu.

Kwenye kusisitizia zaidi verse ya pili anamkabidhi msanii Mayorkun ambaye anazidi kunogesha kibao hiki kwa kuimba kiingereza chenye lafudhi ya Nigeria. "Plenty girls on my matter but i no dey shake cassava. Girl I'm for you only you. I'm trying to please you now, you still getting jealous?.."

Ukweli haupingiki kwamba mtu hawezi kukuonea wivu kama hakupendi na hili ni kwa pande zote mbili. Ukiona mwenza wako anaondoka nyumbani, anachelewa kurudi, hujui alipo na wala hujishughulishi naye, ujue kuna walakini kwenye mapenzi yenu.

Ukiona mwenzi wako yuko bize na simu yake mpaka usiku, hujui anachati na nani au anaongea na nani na hutaki kabisa kujishughulisha naye, moyo haukuumi wala hujisikii vibaya, ujue kuna walakini katika penzi lenu.

Hisia za mapenzi zinapokolea, zina kawaida ya kuwafanya wahusika waoneane wivu,
yaani hata mwanamke akitoka kwenda dukani, akachelewa kurudi, lazima huku nyuma mwanaume kiroho kiwe kinamdunda, moyoni anawaza pengine amesimamishwa na njemba mwingine anamtongoza!
Hali kadhalika kwa mwanamke, mumewe akirudi jioni atataka kujua siku yake imekuwaje, amekutana na nani, amezungumza na nani kwenye simu, ametumiana meseji na nani na mambo mengine mengi! Ni wivu wa kimapenzi ndiyo unaomsukuma kufanya hivyo.

Uchunguzi wa saikolojia ya mapenzi unaonyesha kwamba mtu ambaye anamuonea wivu sana mpenzi wake, anayeonewa wivu akijua mbinu sahihi za kumtuliza, uhusiano huo utadumu milele. Hata hivyo, anayeonewa wivu akishindwa kujua mbinu za kushughulikia tatizo hilo, uhusiano huo hauwezi kufika popote na kitakachotokea, ni maafa na madhara makubwa.

Hata hivyo binafsi nakubaliana ya kwamba wivu ni matokeo ya imani batili kuhusu mapenzi na mahusiano. Wivu ni imani. Umewahi kusikia watu wanasema, "Hakuna mwanaume anaweza kuwa mwaminifu! Hawa wanaume waangalie tu!" "Hawa wanawake waone hivi...hata ufanyeje hawawezi kutulia kwenye ndoa!" Haya ni matokeo ya imani zilizojikita kwenye akili ya mtu na ndizo zinazopalilia hisia za kutokujiamini, na hivyo kujenga taswira isiyokuwepo.

Ukweli ni kwamba unapoamini hakuna mtu anaweza kuwa mwaminifu kwenye ndoa hata ufanyeje, unajenga matarajio yanayoweza kutengeneza uhalisia usiokuwepo.

Imani kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa mwaminifu huathiri mtazamo wako na hivyo huwezi kumwamini mpenzi wako anaposafiri kikazi kwa siku kadhaa. Unajenga hofu unaposikia mumeo anakwenda kazini kwa zamu ya usiku. Na ubaya wa imani hizi zinazojengeka kwenye ufahamu humtafuna mtu ndani kwa ndani hivyo hata usiposema ulivyo na wasiwasi, lakini unajua unavyopata tabu moyoni kwa kujua lolote linawezekana kutokea.

Hakuna uhusiano wowote unaweza kuleta utimilifu wa furaha inayotarajiwa katika mazingira haya ya hofu na mashaka.

Hisia za wivu zikishakomaa ndani kwa ndani huhamia kwenye hatua inayoweza kuonekana wazi. Hapa ndio pale hisia zinahama kutoka kuwa mtazamo na imani hasi na kuwa tabia. Katika hatua hii mtu huanza kuchukua hatua za kujihami katika kukabiliana na tishio linalohisiwa.

Ni kweli kuwa wakati mwingine hisia za wivu huwa hisia za hali iliyopo. Kwamba ni kweli yupo mtu wa tatu katika mahusiano yenu. Kama mwanadamu unajisikia vibaya. Lakini dawa si wivu wa kiwango cha kupambana na mshindani wako. Katika mazingira hayo, wakati mwingine tatizo huwa ni wewe.

Ndio. Huenda hujalipa gharama ya kumfanha mpenzi wako ajisikie kupendwa na kuthaminiwa. Huenda umemfanya ajisikie kutumika kama daraja la mtu kufikia malengo mengine ya kimaisha. Badilisha mtazamo wako. Tafuta msaada wa kukufanya ujisikie mwenye wajibu wa kuleta mabadiliko kwenye mahusiano yako. Wivu haukusaidii kutatua matatizo yako.

Wivu usikufanye upambane na mtu asiyehusika. Hasira ni kiburi. Hasira, tunaambiwa haijawahi kutenda haki. Itakugharimu kukarabati mahusiano kwa kuongeza duara la mapambano na mtu wa tatu. Pambana na mwenzi wako kwa kumpa haki yake. Kama una hakika analo tatizo la kuvutwa na vya nje, kabiliana naye abadilike. Tafuteni msaada wa kitaalam kushughulikia mahusiano yenu. Hamna haja ya kupambana na mtu wa tatu ambaye kimsingi mmemkaribisha wenyewe.

Vijana wivu ni sumu mbaya katika mahusiano. Unapojisikia hatari ya kumpoteza mpenzi wako, unapojisikia unatumia nguvu nyingi kuliko anazotumia yeye, maana yake ni kwamba bado hujampenda.

Ni hatari ya hisia zako, na za mwenzako. Unajeruhi hisia zao mara nyingi kwa jambo lisilokuwepo. Unajikuta unachukua hatua zinazoongeza majeraha hata baada ya kushughulikia tatizo lenu. Upendo wa kweli hauhesabu gharama. Upendo hauna masharti. Unapompenda mtu, hufikirii yeye anafanya nini. Na unapofanya hivyo, mara nyingi, unamsababisha kubadilika.

Kabla hujafanya maamuzi ya kuhusiana na mtu, jitathimini. Jichunguze mwenyewe kwanza. Je, unajiamini? Unaamini wengine? Unafikiri nini kuhusu kupenda na kupendwa? Je, mahusiano ni kulipa gharama au kutarajia kutendewa? Kama huna hakika, tafuta msaada ndipo uweze kuingia kwenye mahusiano. Vinginevyo, utamjeruhi huyo unayetaka kuhusiana nae, utajijeruhi mwenyewe, na zaidi, utajeruhi wengine. Kwa sababu wivu, imethibitika, ni jaribio la kumtumia umpendaye kudhihirisha ulivyo na mtazamo hasi nafsi yako mwenyewe. Ishughulikie.

Mashabiki wameonekana kupenda na kufurahi kazi hii mpya ya Alikiba iliyotoka week nyuma sasa, kwani wengi wao kupitia akaunti ya Youtube ya Alikiba wametoa maoni chanya kuhusu wimbo huu

Mmoja wa wachangiaji aliandika "Dah this is more than music I mean this is music plus coz everyday when I wake up must to listen this song,, I say Alikiba (King Kiba) you know how to sanitize our soul you are the bestie of bongofleva".

Mchangiaji mwingine alimpongeza Alikiba kwa kufanya muziki mzuri aliandika "Alikiba ukimya wake ulikuwa na siri kubwa ndani yake, King Kiba kweli unafanya muziki"

Wiki chache zilizopita Kiba aliweka wazi kuwa mpaka pale albam yake inayosubiriwa kwa hamu sana na mashabiki zake itapotoka, atakuwa anatoa nyimbo mfululizo kama sehemu ya maandalizi ya kuachia albam.

Pamoja na yote video ya Jealous ya Alikiba imefikishwa views 6.5M ndani ya week mbili tu!.

Alikiba katoa funzo kubwa kwa wapenzi, haswa vijana wanayoyaanza maisha ya ndoa. LOVE IS SACRIFICE.
 
Back
Top Bottom