Alfu lela u lela: Kisa cha punda, fahari na mkulima

Ushimen

JF-Expert Member
Oct 24, 2012
38,232
88,988
HAPO kale, akaanza Waziri Mkuu, paliondokea mkulima mmoja tajiri aliyekuwa na kundi la wanyma wa kila namna na
aliyejaaliwa kujua lugha zao. Hakuna aliyejua siri hiyo kwani ali￾yemfundisha alimwonya asiitoe ama sivyo atakufa!
Basi katika banda moja mkulima huyo aliwaweka wanyama wawili: punda ampandaye aendapo safarini, na fahari amlimiaye shamba lake.

Ikawa kila jioni, baada ya kazi, fahali humwendea punda aliyewekwa mahali pazuri penye nafaka nyingi na maji safi
ya kutosha, ili aongee naye. Kwa kuwa yule mkulima hakuwa na safari nyingi, ikawa kazi ya yule punda ni kula na kupumzika tu mle bandani wakati mwenzake fahali anababuka kwa kazi ngumu ya kukokota jembe
zito kule shambani!

Siku moja yule mkulima alimsikia fahali wake akimwambia punda, “Bahati ilioje hiyo uliyo nayo mwenzangu! Mimi humenyeka kutwa shambani ilhali wewe mwenzangu wapumzika kutwa humu bandani ukilishwa na ukinyweshwa vizuri bila hata kupandwa na bwana wetu!”

Punda akamwambia fahali, “Tumia akili, rafiki yangu; bila kutumia akili mambo hayaendi. Kwa hiyo, nakushauri ufanye hivi: kesho utakapotiwa hatamu kwa madhumuni ya kupelekwa shamba, jibwage chini ujifanye mgonjwa! Usinyanyuke hata kama watakutandika mijeledi mia! Ukinyanyuka, jibwage tena chini; na watakapokurudisha hapa na kukuletea nyasi, susa kabisa kuzila! Fanya hivyo kwa muda wa siku mbili tatu upate kupumzika!”

Mfanyakazi alipompeleka shamba asubuhi ya pili, yule fahali akajifanya mgonjwa wa kufa! Na aliporudishwa bandani
na kuletewa nyasi, akafuata ushauri wa mwenzake punda. Ndipo mkulima akamwambia mfanyakazi wake, “Leo mwache fahali apumzike, mchukue punda akafanye kazi yake!”

Jioni, baada ya kufanyishwa kazi kweli kweli, yule punda akarudishwa bandani yu hoi taabani! Alipoingia ndani, yule fahali akamshukuru punda kwa ule ushauri wake mwema uliomfaa sana; lakini punda hakujibu kitu ila alijuta kimoyomoyo kwa kumshauri haraka mwenzake bila kufikiri matokeo yake yatakuwaje!

Siku ya pili mfanyakazi akaja tena, akamchukua punda, akaenda akamfanyisha tena kazi kutwa mpaka jioni. Aliporudishwa hoi, yule fahali akamshukuru tena mwenzake. “Laiti nisingemshauri!” Punda akajuta kimoyomoyo; hapo
akamgeukia mwenzake akamwambia, “Sahib yangu, nilipokuwa nikirudi, nilimsikia bwana wetu akimwambia mfanyakazi: ‘kama fahali hakupona, kesho mpeleke machinjoni akachinjwe!’

Kwa kuwa u rafiki yangu mpenzi, nimeona ni kkheri nikuarifu mapema upate kujua mambo yalivyo!“” Fahali kusikia vile, akamshukuru tena mwenzake, akamwam￾bia, “Kesho nitajitolea mwenyewe kwenda kazini!” Asubuhi ya pili mkulima na mkewe wakenda kule bandani kumwangalia fahali huku wakiongozana na mfanyakazi. Wal￾ipofika, wakamwona fahali anatimka mbio mle bandani huku akitoa mashuzi kuthibitisha kuwa yu mzimwa wa kigongo! Hapo mkulima akaanguka kicheko akacheka sana!

“Una cheka nini, mume wangu?” Akataka kujua mkewe. Mume akamjibu, “Linalonichekesha halifai kuambiwa mtu; si
wewe wala si mwingine.” Mke akashikilia lazima aambiwe; mume akakataa katakata mpaka kule nyumbani kwao kukawa hakuna tena furaha isipokuwa bughudha, manung’uniko na kununa kwa mke aliyedai sharti aam￾biwe lililomchekesha mumewe siku ile.

Alipoona hali ya nyumbani mwake imekuwa mbaya, siku moja mume akamwambia mkewe, “Nitilie maji nikaoge nivae nguo tohara nisali ndipo nitakapokuambia kile kilichonichekesha siku ile; lakini ujue kuwa mimi si mumeo tena maana nikikuambia, nitakufa!”

Mke asijali; mradi atimiziwe lile alilolitaka. Basi akafanya kama vile alivyoambiwa na mumewe. Alipokwisha sali, mume akamwambia mkewe, “Kwanza nakwenda kuwaaga wazee wangu, ndugu zangu, na jamaa zangu. Nitakaporudi, nitakuambia kilichonichekesha siku ile.” Wakati alipokuwa akielekea kwa wazazi wake, njiani mkulima akamkuta jogoo wake amewakusanya makoo hamsini akiwabe￾beza huku wote wakiwa katika hali ya furaha na ya maridhawa.

Lakini mbwa wake aliyekuwa karibu na aliyekuwa amejikunyata kwa huzuni na majonzi, akamwambia jogoo, “Mbona mwenzetu huna huzuni?” “Kwa nini niwe na huzuni?” Jogoo akataka kujua. “Unacheka na kufurahi na makoo wako ilhali unajua kuwa bwana wetu atakufa leo; huna hata huruma?” Akasema mbwa kwa huzuni. “Nini kitakachomwua bwana wetu? Mbona namwona yu mzima wa kigongo tena anaonekana ana afya nzuri?” Akauliza tena jogoo.

“Sababu,” akajibu mbwa, “ni mkewe ashikiliaye kuambiwa neno ambalo bwana wetu akimwambia, atakufa!” Jogoo kusikia vile akasema, “Basi bwana wetu ndiye mjinga wa mwisho! Hebu nitazame mimi; nina makoo hamsini wanitiio
wote kwani nawafurahisha na nawaridhisha vilivyo bila tatizo lolote ilhali bwana wetu ana mke mmoja tu amsumbuaye na kumwumiza kichwa kutwa kucha! Kama mkewe hasikii maneno yake, basi aende dukani akanunue hainzarani amtandike mikwaju mpaka mke ashike adabu na akome kuulizauliza mambo yasiyomhusu!”

Yule bwana kusikia maneno ya jogoo, akaenda zake moja kwa moja mpaka dukani, akanunua bakora nyembamba ya mtobwe, akarudi nayo nyumbani kwake. Alipoingia ndani, akamwita mkewe chumbani. Alipokuwa ndani, akaubana mlango vizuri, akamtandika mkewe bakora za kutosha mpaka mke akakoma kuzaliwa! Mke akataka kujua sababu ya kupigwa vile; ndipo mumewe akamjibu, “Lililonichekesha siku ile na ulilialo sikuzote ndilo hili; na kama unataka zaidi sema!”

“Toba ya Rabbi!” akalia mke kwa maumivu makali huku akipiga mayowe, “Nimekoma, mume wangu, wala sitaki tena kulijua lile lililokuchekesha siku ile!”

* * *

BAADA YA Waziri Mkuu kusimulia kisa hiki, Shahrazad akasema, “Hakuna chochote kitakachonibadili nia katika jitihada
yangu niliyoikusudia kuitekeleza.” Basi Waziri Mkuu ikawa hana budi kumpamba bintiye kwa lebasi za hariri na vito vya tunu kabla hajampeleka kwa Sultani.

Lakini kabla hajaondoka, Shahrazad akamwambia Dunyazad, “Mdogo wangu, nitakapopelekwa kwa Sultani, nitakuagiza uje. Usiku, kabla hakujapambazuka, uniamshe, useme, ‘Dada yangu, tafadhali nakusihi unisimulie moja ya hadithi zako tamu za kusi￾simua ili nipate kuipitisha sehemu iliyobaki ya usiku huu tutaka￾okuwa pamoja kwa mara ya mwisho.’

Halafu nitakusimulia visa ambavyo, Inshaallah, natumaini vitakuwa ni chanzo cha mwisho wa msiba uukabilio umati wa mji huu.” Basi Waziri akamchukua Shahrazad mpaka kwa Sultani. Sultan Shahriyar alipoufunua ushungi wa Shahrazad, akastaajabu sana kuona uzuri wake usio kifani.

Basi usiku wa manane, baada ya starehe na maburudiko, Shahrazad akamwambia Sultani kwa unyenyekevu, “Ewe Seyyid yangu, nina mdogo wangu nimpendaye kuliko mboni za macho yangu; nataka kumuaga kabla hakuja kucha. Nakusihi niidhinie aje niagane naye kwa mara ya mwisho.”

Mara ileile Sultani akatoa amri Dunyazad akaletwe. Alipofika, akamkumbatia dada yake na kabla hakujapambazuka, akasema, “Dada yangu mpenzi, tafadhali nakusihi unisimulie moja ya hadithi zako nzuri ili tuipitishe sehemu ya usiku huu tutakaokuwa pamoja kwa mara ya mwisho.” Hapo Shahrazad akamgeukia Sultan Shahriyar, akasema, “Itakuwa ni furaha kwangu iwapo Sultani ataniridhia.” Sultani, ambaye hakuwa na usingizi wakati ule, akakubali na kumsikiliza Shahrazad akasimulia.
 
siku alfu na moja... Boss usisahau kuleta na Adili na nduguze

Jr
Unenikumbusha jinsi ambavyo Adili, kijanamwenye roho na tabia njema, alihusudiwa na ndugu zake (Hasidi na Mwivu), walimchukia na kumpatia mateso na kumweka katika hali ngumu katika nyakati tofauti.

Hao walimtesa kiasi cha kutosha na kama malipo ya makosa yao wakageuzwa manyani na jini liitwalo Huria. Lakini kwa moyo wake mwema Adili akayaombea msamaha baada ya miaka mingi yakitunzwa naye kwa mateso ya kuyapiga kiboko kila usiku na kuyapa posho.

Baada ya hapo Huria alikubali pendekezo la Adili wakarejea katika utu tena. Mara baada ya baba yao kufariki dunia Adili na nduguze waligawana mali sawa kwa sawa katika sehemu tatu.

Ebu subiri pakuche chief.....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom