SoC01 Alama 10 za kumtambua mtoto si wako

Stories of Change - 2021 Competition

Ambakucha

JF-Expert Member
Aug 16, 2019
277
445
*Hii ni mbali na DNA....

Miaka ya karibuni, kumekuwepo na madai kwamba, asilimia kubwa ya wanaume (na wanawake kwa uchache) wanalea watoto wasiyokuwa damu yao (biological father).

Iliwahi kudaiwa kuwa, takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini 'Rita' (Registration Insolvency and Trusteeship Agency) wamewahi kusema kwamba, wanaume wengi (karibu 49%) wanalea watoto wasiyo wao. Hii ni hatari sana kama ndivyo.

Lakini kuna wanawake pia wanaolea watoto wasiyokuwa wa kuwazaa wao bila kujua, wakiamini wamewazaa. Japokuwa ni mara chache. Na hii hutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya wauguzi, kubadilisha watoto kwa akina mama wanapokwenda kujifungua. Hata hivyo, inaelezwa miaka ya hivi karibuni, hali hii imethibitiwa.

Sasa zipo alama 10 za kumjua mtoto unayemlea siyo wa kwako. Iwe kwa kubambikizwa au kwa mwanamke kubadilishiwa na wauguzi kwa uzembe.

ALAMA YA KWANZA; UTAMBUZI WA KIMILA KAMA WANGONI

Mara nyingi alama hii hutumika kimila. Baadhi ya makabila hutumia alama za kitamaduni kumjua mtoto asiye wa ndoa au wa baba husika.

Mfano Kabila la Wangoni; mwanamke akiwa na ujauzito, kuna siku hutengwa ambapo mjamzito huyo huingizwa chumba maalum ambamo watakuwepo mabibi au watu wazima wengine. Mjamzito hulazwa chali chini kwenye mkeka akiwa nusu mavazi. Tumbo likiwa wazi.

Huchukuliwa unga na kuwekwa kwenye kishimo cha kitovu na kutengeneza
kichuguu kidogo. Kisha, mabibi au watu wazima hao huimba nyimbo za kiasili (kilugha). Mtoto tumboni akiwa ni wa mwanaume mhusika, inaaminika kichanga tumboni hucheza kwa kurusha mateke na hivyo, kile kichuguu cha unga humwagika kwa kutawanyika. Kama mimba si ya mwanaume huyo, kichanga tumboni hutulia na kukifanya kile kichuguu kubaki kama kilivyo.

Hapo Sasa, mabibi au watu wazima hao huweza kuamua kukaa kimya asiambiwe mwanaume hivyo kulea mtoto asiye wake au humwambia ili maamuzi yawe kwake. Kila kabila lina njia yake.

ALAMA YA PILI; MTOTO KWA BABA HAYUPO, KWA MAMA HAYUPO!

Alama ya pili ambayo hutumiwa kumtambua mtoto kama ni damu husika au siyo ni mwonekano. Hapa namaanisha kufanana kwa sura, mwendo, sauti na namna ya kuumba matamshi wakati wa kuongea na namna ya uchekaji.

Wanaume wengi hutumia njia mojawapo ya hizo ili kujiridhisha. Kwa kawaida, kama mtoto ni damu moja na baba, lazima afanane naye hata kwa jambo moja. Kama siyo sura, Basi mwendo. Kama siyo mwendo, basi sauti au namna midomo inavyoumba maneno wakati wa kuongea au namna ya uchekaji.

Wanaume wengi huwa hawapendi kusikia kauli hii; 'mtoto huyu yaani marehemu babu yake mtupu' (babu mwenyewe mzaa mama alikufaga zamani). Halafu yeye asifanane naye hata kwa kitu kimoja.

Afadhali hata asifanane na yeye baba, akafanana na mkewe. Lakini siyo kwa mke hayupo, kwa mume hayupo halafu aambiwe babu yake marehemu. Wanaume huwa wanaingiwa na wasiwasi ingawa huenda hata mama alibadilishiwa mtoto na wauguzi wakati wa kujifungua.

ALAMA YA TATU; MAMA KUTOPENDA MTOTO AADHIBIWE NA BABA YAKE

Wako akina mama wamekuwa wakilionesha hili waziwazi. Mtoto ndani ya nyumba akikosea, kimalezi hustahili adhabu kidogo, hata viboko kama siyo fimbo.

Sasa, wapo wamama ambao, mtoto ndani ya nyumba akikosea, yeye huweza kushika fimbo na kumwadhibu mpaka mtoto akalia kilio kikuu. Lakini fimbo hiyohiyo ikishikwa na baba na kumwadhibu mtoto, mama huja juu akitetea asipigwe au kipigo kinatosha. Kama baba hataacha kumpiga, mama hufoka na kusema maneno mengi.

Wengi hutafsiri kwamba, tabia za wamama hao zinatokana na maumivu ya moyo wakijua siri nzito kwamba, baba anayempiga ni sawa tu na mwanaume yeyote wa mtaani kwa vile si damu yake.

Tabia hii imekuwa ikianzisha migogoro ndani ya familia japokuwa wababa wengi huwa hawasemi hisia zao.

ALAMA YA NNE; MTOTO KUWA MWIZI AU TABIA MBAYA ISIYOKUWEPO KOKOTE

Miaka ya zamani, kijijini iko familia ilikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Pasco. Pasco alikuwa mwizi balaa, vitu alivyokuwa akiiba ni kuku, bata, njiwa, viatu na vingine vingi ambavyo hupatikana nje ya nyumba.

Kesi kwa wazazi wake zilikuwa hazikauki. Kwa siku hata kesi tatu, kwamba Pasco ameiba kwa watu mbalimbali mitaani. Watoto wengine watano wa familia hiyo, walisifiwa kwa uadilifu.

Mbaya zaidi, Pasco alikuwa hafanani na baba yake wala mama yake. Hafanani na dada zake wala Kaka zake. Hana aliyefanana naye hata ujombani wala ushangazini.

Siku moja, baada ya jirani kupeleka mashtaka kwamba, Pasco alikamata kuku wake, ndipo baba mtu akamrushia maneno makali sana mkewe akitaka kujua, baba halali wa Pasco ni nani!! Mzozo ulikuwa mkubwa na kumalizwa na wazee wenye busara za Mungu.

Lakini baadaye ilikuja kuibuka tetesi kwamba, Pasco alikuwa mtoto wa mzee Linusi. Huyo mzee Linusi alishafariki dunia lakini alifia jela alikokuwa akitumikia kufungo baada ya kutiwa hatiani kwa wizi wa mbuzi wa mtu mmoja kijijini. Kifo chake kilipokelewa kwa furaha na wamama kwa sababu alikuwa na tabia ya kuwabaka wakienda kuchota maji ziwani mbali na kijiji.

Kwa hiyo, wazee wa zamani waliamini kuwa, mtoto akiwa na tabia mbaya isiyofanana na watoto wake wengine katika familia au ujombani na ushangazini basi huenda alibambikwa. Ingawa pia inawezekana mama alibadilishiwa mtoto na wauguzi wazembe.

ALAMA YA TANO; MTOTO, HASA BINTI 'KUTEMBEA' NA BABA YAKE

Hii imekuwa ikisikika kwenye jamii kwamba, 'yule binti anatembea na baba yake mzazi'. Tena hufikia mahali, mapenzi huwalevya wote kiasi cha kushindwa kuficha tena. Jamii imekuwa ikilaani sana matukio hayo.

Wazee wa Kimila waliyoongea na Mwandishi wa makala haya wanakataa wakisema kuwa, maumbile yameumbwa na aibu! Wanasema kuwa, haiwezekani baba akafanya mapenzi na binti yake wa kumzaa zaidi ya Lutu na binti zake ndani ya Biblia ambao ilikuwa maalum ili Mungu asimamishe uzao uliyokaribia kufutika.

"Ukiona au ukisikia kuna baba analala na bintiye wa kumzaa, basi mke alibeba mimba ya mwanaume mwingine. Na ukitaka kujua ukweli huu, wamama wengi wanapogundua mumewe katembea na binti yao, hawapati viharusi (stroke), kwa sababu wanajua si damu yake," anasema mzee Jumanne Matele, mkazi wa Muheza, Tanga.

Mzee Matele anamaliza kwa kusema: "Na hili lipo sana. Ndiyo maana wababa siku hizi hawana tena nguvu ya laana au baraka kwa watoto wao kwa sababu wengi wanalea watoto si damu yao. Unakuta baba anamlaani au abambariki mtoto lakini vyote vinadunda, maana hana koneksheni ya damu."

ALAMA YA SITA; MTOTO KUPENDA SANA UJOMBANI

Wapo watoto wanakuwa karibu na watu wa upande wa kwa wajomba zake, yaani kwa ndugu wa mama kuliko upande wa ndugu wa baba hata bila kusimamiwa, kulazimishwa wala si kwa sababu kwamba, ndugu hao wa mama wanaishi karibu zaidi.

Wazee wa Kimila wanasema hili nalo walikuwa wakilifuatilia kwa karibu sana. Wanasema kuwa, damu huvuta pia damu hukataa. Wanasema mtoto akibobea upande mmoja bila kuwepo kwa sababu inayosababisha, huko ndiko kwenye damu yake.

ALAMA YA SABA; WATOTO WA BABA MMOJA KUWA NA UHUSIANO WA KIMAPENZI

Inasemekana kwamba, mbali na utoto wa kutojitambua, watoto waliozaliwa kwa damu ya baba mmoja, mama awe mmoja au mama mbali, hawawezi kujenga uhusiano wa kimapenzi iwe kwa kujua au kutokujua.

Yaani iko hivi; mfano mzee Hamis anaishi Dar, ana mke na watoto, wakiwemo wavulana. Halafu akaenda kufanya kazi Lindi kwa muda. Kule akapata mwanamke, akampa mimba, kisha mzee Hamis akarejea Dar na kuendelea na familia yake. Kule Lindi yule mwanamke akazaa binti, akakua bila kumjua baba yake mzazi ni nani na hakuna mawasiliano.

Sasa mfano, mvulana mmoja wa mzee Hamis, Dar, amekua, akapata kazi Lindi ambako akakutana na yule binti ambaye alizaliwa kwa damu ya baba yake (kimsingi ni mdogo wake) akampenda kiasi cha kutaka kuoana au kuwa na uhusiano wa kimapenzi, wazee wa Kimila wanasema haitakuja kutokea wakakamilisha azma yao bila kujulikana kuwa wao ni kaka na dada.

Na ikitokea hivyo, basi mama wa Lindi, binti si wa mzee Hamis au mvulana si kijana wa mzee huyo kwa vile maumbile yana aibu. Japokuwa inawezekana mama mmojawapo alibadilishiwa mtoto na baadhi ya wauguzi wazembe.

ALAMA YA NANE; MTOTO KUTISHIA KUMLAANI BABA YAKE

Ninewahi kumsikia binti mmoja anazozana na baba yake mzazi. Ikafika mahali, (eti) kwa hasira, binti akatishia kumvulia nguo baba yake ili auone utupu wake kama ishara ya kumlaani. Wazee waliingilia kati na kusuluhisha mzozo huo.

Lakini wachambuzi wa maswala ya kijamij, wanasema kuwa, kitendo kama hicho hakiwezi kufanywa na mtoto aliyetoka kwenye kiuno cha baba huyo bali mkewe ndiyo anajua ukweli wake.

Wachambuzi hao wanaungwa mkono wa moja kwa moja na wazee wa Kimila, kwamba, mtoto kumtishia mzazi wake yeyote, awe mama au baba, kwamba atamlaani ni majibu kwamba, si damu yake.

"Siyo mtoto kutishia kulaani tu, hata kumwambia baba yake au mama yake kwamba, angechelewa yeye angemzaa, ni ishara kwamba, damu siyo halisi," anasema mzee mmoja wa Kimila.

ALAMA YA TISA; MTOTO KUJITENGA NA WENZAKE

Wewe baba, inapotokea mtoto wako anapenda sana kujitengatenga na nduguze ambao wote kwa ujumla ni damu yako, jaribu kufuatilia kwa undani. Huenda hospitali alikojifungulia mkeo alichezewa mchezo wa kubadilishiwa au mama aliteleza kidogo kwa mwanaume mwingine.

Watafiti wanasema kuwa, mtoto anayependa kujitenga na au kujionea huruma, mara nyingi kiroho anakuwa anafukuzwa na nguvu za damu za wenzake. Haya mambo yapo kiroho zaidi na mtoto mwenyewe anaweza au mara zote hawezi kujua.

ALAMA YA KUMI; MTOTO KUFANANA 100% NA MWANAUME AMBAYE BABA ALIKUWA AKIMTILIA SHAKA KUTEMBEA NA MKEWE

Hii sasa ni alama ya mwisho lakini ndiyo alama kubwa sana na ipo wazi kimadai. Yaani alama zote tisa, akina baba huweza kuzivumilia au kuzimezea, ukiachana na ile ya akina mama kubadilishiwa watoto na wauguzi wazembe.

Hutokea, baba akatokea kumhisi mkewe kuwa na mahusiano na mwanaume fulani, pengine mtaani kwake au nyumba waliyopanga.

Hisia hizo huenda amewahi kuzitoa kwa mkewe zikapingwa au zikakubaliwa na kuombana msamaha. Sasa kama mke atabeba mimba, akaja kujifungua mtoto ambaye amefanana na mwanaume huyo kwa asilimia mia moja, basi hakuna shaka kwamba huyo ndiye baba mzazi.

Hata hivyo, pamoja na yote, kipimo cha vinasaba kiitwacho kitaalamu Deoxyribonucleic Acid (DNA) ndicho chenye uwezo mkubwa wa kutambua ukweli kuhusu baba wa mtoto husika. Wataalamu wanashauri wanaume wenye shaka waende huko.






blue-helix-human-dna-structure-260nw-1669326868.jpg
 
Back
Top Bottom