Akina mama play your part,it can be done

Njowepo

JF-Expert Member
Feb 26, 2008
9,710
2,226
MT.jpg MWANAMKE ni kiumbe wa jinsia ya watu wanaoonekana wazuri wa sura na maumbo, wenye maumbo laini na teketeke na waliojaa uoga mwingi na aibu tele.
Sifa hizo za maumbile yake ni za kiasilia za kumfanya mwanaume avutiwe naye ili aombe kutengeneza ujamaa utakaofanikisha kupatikana kwa watoto na maisha ya binadamu yaendelee kuwapo.
Kwa hiyo, uzuri usio wa kawaida, uteketeke, ulaini, upole na uoga wa wanawake unatokana na sababu za kimaumbile asilia na wala si wanyonge kama wengi tunavyowachukulia.
Ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba yote ambayo jinsia ya kiume inajaribu kuyahozi kama yake, jinsia ya kike inapojaribu kuyafanya, inayafanya vizuri zaidi na kwa uadilifu sana.
Angalia mifano hii: Zamani, kazi ya ualimu ilionekana kuwa ya wanaume zaidi lakini leo hii zaidi ni ya wanawake na tena ni walimu wazuri mno waliowaleta wataalaam wengi wa taaluma mbalimbali tulionao sasa.
Zamani ilikuwa ajabu kubwa kumuona mwanamke akiendesha gari lakini leo wao ndiyo madereva wazuri na makini mno.
Hata kusoma taarifa za habari redioni, si RTD, Sauti ya Tanzania Zanzibar na Sauti ya Kenya, wakati huo VOK tu bali hata BBC London na Sauti ya Ujerumani wanawake hawakupewa nafasi lakini leo hii ni wasomaji wazuri wa taarifa za habari redioni.
Kubwa zaidi, zamani ilikuwa vigumu sana kwa wanawake kupewa nyadhifa nyeti za kisiasa na kiutawala lakini leo hii wapo wengi katika nyadhifa nyeti na kubwa ambapo uongozi wao hauna kashfa kashfa na wanaongoza vizuri tu.

Kimsingi, mwanamke ni hodari zaidi katika mambo mengi kuliko mwanaume kama atapewa nafasi ya kuonyesha ujuzi wake.
Angalia idadi ya madereva wanaohusika na ajali za kizembe barabarani, ni vigumu kumkuta mwanamke. Fuatilia popote penye mashindano ya kulenga shabaha, wanawake wana shabaha zaidi kuliko wanaume.
Nenda kawaanzishe wanawake na wanaume mafunzo ya kumpyuta, baada ya muda ukifanya tathmini utagundua wanawake wengi wameshakuwa mbali kiuelewa kuliko wanaume!
Kimaumbile asilia mwanamke ni muoga, mpole na ana aibu lakini anapolazimishwa apambane, mwanamke ana nguvu za ajabu.
Niliwahi kushuhudia miaka kadhaa iliyopita Mwananyamala, Dar es Salaam mbabe mmoja akigombana na dada mmoja kwenye foleni ya maji.
Aliitoa ndoo ya dada huyo kwenye foleni akaweka yake. Kila huyo dada alipoirudisha, yule mbabe aliitupa mbali. Yule dada akauliza endapo mbabe yule alifanya hivyo kwa sababu yeye alikuwa mwanamke, yule mbabe akamwita yule dada ‘malaya.’ Hapo ndipo alipofanya kosa kubwa.
Uvumilivu ukamshinda yule dada "aliyekwenda hewani" zaidi kidogo ya yule mbabe,akaamua kupigana na mwanamume yule. Nguvu aliyokuwa nayo, akimshambulia yule mbabe kwa ngumi na vichwa, ilikuwa ya kushangaza sana. Mbabe alipigwa vibaya katika pambano hilo kali la kikwelikweli!
Hasira nyingine niliishuhudia miaka hiyo hiyo kwenye kituo cha mabasi cha Polisi Ufundi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, wakati wengi wetu tulikuwa bado washamba dhidi ya uonevu wa kijinsia, pale kondakta wa daladala alipomshika, bila uhalali, msichana mmoja eneo la mwili la msichana huyo lililotuna sana la nyuma juu ya mapaja na chini ya mgongo.
Msichana huyo aliyevaa sare za shule moja ya Sekondari ya jijini na aliyekuwa na umbo kubwa kidogo kuliko kondakta huyo mnyanyasaji alikuwa akishuka kwenye basi hilo.
Alichofanya yule binti ni kumvuta chini kondakta huyo na kumpa kipigo cha kushangaza katika pambano kali lingine la kikweli kweli!
Hiyo si ajabu. Kwani hatujasikia mama alikuwa apokonywe pesa akitoka benki lakini alipambana mpaka kuwanyang'anya bastola majambazi na kuokoa pesa yake?
Au hatukuwahi kusikia majambazi wamevamia kwenye nyumba ya mtu, mzee amejificha kwa uoga lakini mama akachukua bunduki ya mzee na kupambana nao hadi kufanikiwa kuwaondoa?
Kweli,wanawake wanaweza kila kinachofanywa na wanaume ili mradi waamue tu, wapewe nafasi au walazimishwe kufanya.
Angalia hata katika soka, timu za wanawake za nchi kama Brazil, Marekani, Ujerumani, China na kadhalika zinacheza mpira wa ‘kiume’ kabisa ukiondoa kutojumuisha rafu za kijinga kijinga na ukiondoa pia tabia ya kumdanganya mwamuzi kwenye eneo la penalti.
Extracted from;Raia Mwema toleo no 20
 
Back
Top Bottom