Ajenda ya vijana katika bajeti ya Serikali iangazwe sekta zote

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,886
939


AJENDA YA VIJANA KATIKA BAJETI YA SERIKALI IANGAZWE SEKTA ZOTE

Na; Victoria Charles Mwanziva: (Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Taifa)

Vijana ndio dira ya maendeleo kwa Taifa lolote lile linaloendelea ulimwenguni, huwezi kuyapata maendeleo ya kweli na yenye tija kwa Taifa bila kuwekeza na kutambua mchango wa vijana katika maendeleo. Tanzania kama Taifa lenye dira ya maendeleo na kwa kuzingatia idadi kubwa ya wananchi wake ambao ni vijana halitakiwi kubaki nyuma katika nyanja zote za kiuchumi kuwekeza katika maeneo ambayo sio rafiki kwa kizazi hiki adhimu na chenye tija kubwa kwa Taifa lao.

Tupo kwenye msimu mpya wa Bajeti Kuu ya Serikali 2022/2023, ni wakati sasa kwa Serikali kuangalia ni kwa namna gani kila Wizara ndani yake inakuwa na ajenda ya kuwainua vijana na kuwapa fursa mbalimbali na kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa ndio kiini cha uzalishaji na maendeleo katika Wizara husika. Inakuwa ni vigumu kuwepo kwa Wizara ya kimaendeleo ambayo bajeti yake itakosa kuwa na maeneo mahsusi kwa ajili ya vijana wa kitanzania.

Ilani ya uchaguzi ya CCM, 2020/2025 Sura ya 1 Ibara ya (9) kifungu (f) kipengele cha (i-iv) inafafanua kwa undani nini Chama cha Mapinduzi kitafanya kwa ajili ya vijana ambapo ilani imeanisha “Kutengeneza ajira zisizopungua 7,000,000 (milioni saba) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana”. Haya ni maelekezo ambayo Chama cha Mapinduzi kinaielekeza Serikali kutekeleza kwa ajili ya vijana, ambapo imeainisha maeneo mahsusi kabisa yatakayowezesha upatikanaji wa ajira au fursa hizi kwa vijana kama ifuatavyo;

(i) Kuchochea ukuaji wa uchumi, hususani katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi pamoja na utalii;

(ii) Kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu;

(iii) Kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na sanaa kwa ajili ya afya bora na burudani na pia kuongeza fursa za ajira na kipato; na

(iv) Kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania. Mbali na maelekezo hayo mujarubu ya Ilani ya Uchaguzi pia adhma na dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ipo wazi na imedhihirika katika maeneo mbalimbali alipopata fursa ya kuzungumza na wananchi hususani akizungumzia ajenda na fursa za Vijana kwa nyakati tofauti ameonyesha ni kwa jinsi gani amelibeba kwa uzito suala la Vijana. Mfano; Alipokuwa Arusha tarehe 17 Oktoba, 2021 alisema “Vijana, Mama yenu silali nahangaika wapi nitapata pesa ya kuwatengenezea ajira vijana wangu”. Kwa kauli hii inadhihirisha ni kwa kiasi gani Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaguswa na ameibeba ajenda ya vijana kwa ukubwa gani.

Ni jukumu la Wizara kupitia mawaziri wake kwenye Bajeti zao za kisekta wanazoziwakilisha bungeni kuhakikisha ajenda ya vijana inakuwa ni kipaumbele namba moja ili kutimiza malengo na matarajio yaliyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025 ili kuifikia kiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyonayo kwa Vijana. Kuna baadhi ya sekta kwa upekee wake ningependa kuzizungumzia kwa undani kwa jinsi gani wanaweza kuwa mfano kwa sekta nyingine katika kuhakikisha ajenda ya Vijana inapewa kipaumbele katika bajeti zao za 2022/2023.

Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Wizara hii ndio Wizara Mama inayobeba misingi ya maendeleo yanayowagusa wananchi moja kwa moja, kupitia Wizara hii mapato ya Halmashauri zote nchini 4% inatengwa kama mikopo isiyokua na riba kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri; lakini cha kushangaza kumekuwa na mlolongo wa masharti ambayo yanawafanya vijana kukosa vigezo vya kukopesheka kupitia fedha hizi na mwishowe kuangukia kwa watu wasiostahili fedha hizi na kusababisha upotevu wa mapato haya kwa wanasiasa na baadhi ya viongozi wasio wazalendo kwa Taifa na kusababisha Vijana kuendelea kuumia bila kuzipata fursa hizi. TAMISEMI inapaswa kuandaa na kusimamia vyema Sera mahsusi itakayokwenda kusimamia fedha hizi kwa ajili ya Vijana na kuhakikisha kunakuwa na Sheria madhubiti ambayo italinda fedha hizi ili kuhakikisha zinawafikia walengwa ambao ni vijana. Kupitia TAMISEMI pia utekelezaji na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya maendeleo kama shule, Vituo vya afya, hospitali na barabara inafanyika hivyo ni jukumu la Wizara kuhakikisha kuwa Vijana ndio wanapewa vipaumbele kupewa tenda za ujenzi na kupata ajira maeneo haya.

Wizara ya Kilimo; Waswahili husema “Kilimo ni uti wa mgongo” lakini kwangu mimi kilimo sio uti wa mgongo pekee bali pia ni “Moyo au hewa ya Oksijeni” kwa maana ya kwamba mwanadamu anaweza kukosa uti wa mgongo na akaishi, lakini huwezi kuishi bila Moyo au hewa ya oksijeni. Wizara ya Kilimo ina nafasi kubwa sana ya kuhakikisha ajenda ya vijana inakuwa kipaumbele kwani Tanzania tuna maeneo makubwa ya wazi na yenye rutuba yanayofaa kwa ajili ya kilimo, kulingana na mazao yanayoweza kusitawi maeneo husika. Kilimo ni dira ya maendeleo katika Taifa letu, kilimo kinazalisha chakula, kilimo kinazalisha malighafi za viwandani,
kilimo kinazalisha mazao mahsusi ya biashara.

Hivyo, vijana kama injini ya maendeleo katika Taifa hili kama alivyosema Mhe. Rais lazima ajenda yao iwe kipaumbele namba moja. Wizara ya kilimo, bajeti yake natarajia kuona itajikita katika Pembejeo, Viwatilifu, kuwawezesha wataalumu n.k. Pia, natamani kuona ni kwa namna gani Wizara ambayo ni Moyo wa maendeleo katika Taifa letu inabeba ajenda ya kuwawezesha vijana kuingia kwenye kilimo na kujiari kujipatia kipato kupitia kilimo na kupunguza mzigo mkubwa kwa serikali kutafuta ajira kwa vijana.

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara; Mhe. Rais anafanya jitihada kubwa kuhakikisha anavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Je, Ni kwa jinsi gani wizara hii kubwa na iliyobeba dira na matumaini ya kuzalisha ajira kwa vijana imejipanga kuhakikisha kuwa ajenda ya vijana inapewa kipaumbele katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023? Ni lazima Wizara hii kuwa na mpango mahususi kwa Vijana. Mfano, upande wa viwanda ni lazima Wizara ijipange kupitia SIDO kuhakikisha kuwa inawashika mkono vijana wanaofanya ubunifu na kuuanzisha viwanda vya uzalishaji mdogo ili kuwaongezea tija na kukuwa katika uwanja wa kibiashara, lakini pia kwenye upande wa uwekezaji ni lazima kuwe na sheria na muongozo unaowabana wawekezaji kuhakikisha kuwa vijana ndio wanakuwa kipaumbele katika maeneo ambayo wanaenda kuwekeza.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Asilimia kubwa ya vijana wanaoishi maeneo ya Pwani na maeneo yanayozunguka Maziwa, Bahari na Mito Mikubwa wanajihusisha na Uvuvi na Kilimo cha Umwagiliaji. Wizara hii haiwezi kuzungumzia kupata tija kwenye uvuvi bila kuwa na ajenda ya kuwawezesha vijana katika bajeti ya 2022/2023. Wizara lazima iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha ajenda ya kuwawezesha vijana kwenye sekta ya uvuvi inatiliwa mkazo. Mfano, kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa bora vya uvuvi na kuwapata Vijana, kutoa elimu juu ya uvuvi wa kisasa ili kutengeneza tija katika shughuli zao ili waweze kujitengenezea vipato na kujikwamua kiuchumi, halikadhalika kweye Ufugaji ni lazima wizara ijikite katika utoaji wa elimu ili kuwavutia vijana wengi kujishughlisha na ufugaji wa mifigo mbalimbali kwa njia sahihi na za kisasa ili ufugaji uwe wa kitaalamu na kuzalisha tija kwa Vijana.

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi; hii ni wizara iliyobeba miradi mingi ya maendeleo ambayo kwa asilimia kubwa inazalisha ajira kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, swali linaokuja ni, Je, Vijana wana nafasi gani katika ugawaji wa tenda za ujenzi wa miradi hiyo inayoendelea nchini na inayotarajiwa kutekelezwa katika bajeti ya 2022/2023? Ni lazima wizara ya ujenzi ihakikishe kuwa vijana wasomi wa kitanzania kutoka katika kada za uhandisi wanapata fursa za kupewa tenda za ujenzi ili kuwainua na kuwajengea uzoefu katika nyanja hiyo, lakini pia Vijana wetu wengine katika fani ya uhandisi wameanzisha makampuni yao ya ujenzi, hivyo wizara inapaswa kuzilea kampuni hizi kwa kuwapa tenda mbalimbali za ujenzi kwani kupitia makampuni haya, wazawa wanaweza kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa vijana wenzao pamoja na kuipunguzia serikali gharama ya kutoa tenda hizo kwa makampuni ya nje.

Sekta ya Teknolojia; Dunia kwa sasa imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya TEHAMA, kama Taifa hatuwezi kubaki nyuma kwani Mapinduzi ya 4 ya viwanda duniani yamejikita na kujitambulisha katika sayansi na teknolojia. Katika bajeti ya serikali 2022/2023 ni lazima kuwepo na bajeti maalumu kupitia Vyuo vya COSTEC, DIT, MUST na ATC ya kuwekeza katika TEHAMA ili kuawawezesha vijana wa kitanzania kuendana na kasi ya ulimwengu katika teknolojia na kutoa elimu mashuleni kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari, hii itasaidia kukuza uwezo wa wanafunzi kufikiria zaidi na kuwa wabunifu. Hivyo, Wizara ya elimu kupitia Vyuo vya ufundi bajeti zao zijikite katika uwekezaji wa TEHAMA kama njia mahususi ya kuwainua vijana katika ulingo wa Teknolojia Ulimwenguni.

Mwisho Japo Siyo kwa Umuhimu

Ni Imani yangu kwamba Wizara zote ambazo nimezitaja na ambazo sikuzitaja zitaangazia ajenda ya Vijana kwa mapana yake katika Bajeti zao ili kuyafikia malengo ya Ilani ya CCM kwa Vijana, lakini pia adhma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan. Natambaua kuwa kuna Wizara maalumu ya vijana lakini Wizara hii haina fursa za moja kwa moja kwa vijana kama ilivyo kwa sekta za kimaendeleo, hivyo mbali na Wizara ya vijana iliyobeba jukumu la kuwasemea vijana ni lazima kila wizara kwenye bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023 iangaze kwa uzito ajenda ya vijana ili tuweze kufikia ajira 7,000,000 (milioni saba) zilizoainishwa kwanye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025 kwa ajili ya Vijana.


Ndugu Victoria C. Mwanziva
Katibu Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Taifa
Instagram: @victoria.mwanziva
Twitter: @victoriacharlz

IMG-20220518-WA0006.jpg


FS98VQyWIAADOD5.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom