Aibu ya Tanzania katika Olimpiki hii hapa...

Kibunango

JF-Expert Member
Aug 29, 2006
8,394
2,221
WAKATI michezo mikongwe ya kihistoria ya Olimpiki iliyoasisiwa na wazee wa Kigiriki inatimiza karne moja na miaka 10, Tanzania ina miaka 44 katika ushiriki wake.

Lakini tangu Tanzania ianze kushiriki Olimpiki ya Kimataifa kwa miaka hiyo, kwa takwimu hakuna kikubwa cha kujivunia kwani mafanikio yake ni hafifu.

Katika miaka yote hiyo ya ushiriki wa Tanzania, tumekuwa tukishiriki katika michezo ya aina nne tu, ingawaje mashindano hayo hushindanisha michezo mingi.

Jinamizi hili la Tanzania kushiriki michezo michache, linazidi kuiandama tena mwaka huu, kwani ingawa muda wa mwisho wa kuthibitisha bado, lakini kuna kila dalili kwa mwaka huu tena kuwakilishwa na michezo michache.

Hadi sasa ni takribani wanariadha watano pekee ambao ndio tayari wamefikia viwango vya kushiriki Olimpiki, huku mchezo wa ngumi ukiwa unahaha nao kuhakikisha mabondia wao wanafikia viwango.

Michezo ambayo tumewahi kushiriki ni riadha, ngumi, baiskeli na magongo katika miaka yote hiyo ya ushiriki, na hii inatokana na michezo mingine kushindwa kufikia viwango ambavyo ndio vigezo vinavyowezesha kushiriki.

Mpira wa magongo na baiskeli, Tanzania ilishiriki mara moja tu mwaka 1980 katika mashindano yaliyofanyika katika Jiji la Moscow, Urusi ya zamani huku ngumi ikishiriki mara sita na riadha ikiongoza kwa kushiriki mashindano yote ya Olimpiki iliyoshiriki ndani ya miaka hiyo 44.

Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambayo ni mwanachama wa kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) yenye makao yake makuu jijini Athens, Ugiriki, ndiyo mratibu mkuu wa michezo hiyo hapa nyumbani.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilitinga katika Olimpiki mwaka 1964, katika mashindano ambayo yalifanyika katika Jiji la Tokyo, Japan ambako iliwakilishwa na mchezo wa riadha pekee.

Timu iliwakilishwa na wanariadha sita katika mbio za mita 400, 800, 1,500 na 10,000 sambamba na kiongozi mmoja na matokeo iliambulia patupu na kurejea bila medali.

Kwa mara ya pili, Tanzania ilitinga mashindano hayo 1968 katika michezo iliyofanyika Mexico City nchini Mexico na kwa mara ya kwanza ngumi ilishiriki.

Timu iliundwa na wachezaji watatu ikiwa ni wanariadha wawili na bondia mmoja, huku viongozi wakiwa wawili, ambako pia iliambulia patupu.

Katika michuano hiyo ya Mexico, ngumi haikushiriki licha ya mchezaji kwenda huko, huku wanariadha wakishiriki katika riadha mita 400 na marathoni.

Hata hivyo, mmoja wa wanariadha wa Tanzania, John Steven Akhwari alimaliza mbio hizo akiwa wa mwisho na alipoulizwa, alisema: “Nimetumwa na Tanzania kumaliza mbio na si kuishia njiani.”

Hiyo ilimpa heshima na katika michezo ya Olimpiki ya Sydney, Tanzania ilipata tuzo maalum ya Olimpiki ya Akhwari, ambayo IOC iliahidi kujenga kituo cha michezo kama kumbukumbu yake na kutambuliwa na kamati hiyo.

Mwaka 1972, timu za ngumi na riadha ziliiwakilisha tena nchi katika michezo iliyofanyika Munich, Ujerumani Magharibi ya wakati huo, ikiwa na kikosi cha wachezaji saba na viongozi watatu, ambako ngumi walishiriki katika uzito wa Light Middle na Bantam na kurudi bila medali.

Tanzania tangu ianze kushiriki Olimpiki mwaka huo wa 1964 hadi mwaka huu, 2008 imeikosa michezo hiyo mara moja tu, mwaka 1976 huko Montreal nchini Canada, kutokana na sababu za kisiasa.
Serikali haikuruhusu kupeleka timu huko, sababu kubwa ilikuwa kupinga hatua ya IOC, kuiruhusu timu ya rugby ya New Zealand kwenda Afrika Kusini, ambayo tayari ilikuwa imetengwa kisiasa kutokana na ubaguzi wa rangi.

Baada ya kuikosa michezo ya Montreal, ilijitosa katika Olimpiki ya Moscow, USSR (Urusi ya zamani) 1980 ambako ilishiriki katika michezo ya riadha, magongo, ngumi na baiskeli.

Mashindano hayo ya Moscow ni ya kihistoria, kwani kwa mara ya kwanza ndipo jina la Tanzania lilipoingia katika rekodi ya nchi zilizowahi kunyakua medali katika historia ya mashindano hayo.

Katika mashindano hayo, Tanzania kwa mara ya kwanza na ya mwisho hadi hii leo, iliibuka na medali mbili za fedha, kupitia kwa wanariadha wake Filbert Bayi na Suleiman Nyambui katika mbio za mita 3,000.

Mashindano ya Moscow yalifuatiwa na yale ya Los Angeles, Marekani mwaka 1984 ambako tuliwakilishwa na wachezaji wawili bila kiongozi katika michezo ya ngumi na riadha na kurudi kwenye uvurundaji na kurejea mikono mitupu.

Riadha na ngumi ziliibeba Tanzania tena, katika michezo ya mwaka 1988 huko Seoul, Korea Kusini na kuwakilishwa na kikosi cha wachezaji 17 na viongozi saba katika ngumi na riadha na kumaliza bila medali.

Jinamizi la kuwa ‘watalii’ katika kinyang’anyiro cha Olimpiki ya Kimataifa, liliendelea kuikumba Tanzania tena katika mashindano ya Barcelona, Hispania mwaka 1992 tulikowakilishwa na timu ya riadha pekee iliyokuwa na wachezaji 15 na viongozi saba.

Mwaka 1996, Tanzania iliwakilishwa na mchezaji wa kike kwa mara ya kwanza katika michezo ya Olimpiki huko Atlanta, Marekani.

Timu iliundwa na wachezaji 11 na viongozi watano. Michezo ilikuwa ni riadha na ngumi. Katika riadha ilishiriki mita 800 wanawake na wanaume, mita 10,000 na marathon na kutoka tena kapa.

Tanzania ilishiriki tena michezo ya Olimpiki mwaka 2000, jijini Sydney, Australia na kuwakilishwa na wachezaji watatu katika riadha pekee, ambako walishiriki katika mbio za mita 10,000, 5,000 na marathon.

Baada ya Olimpiki ya Australia, iliyofuata mwaka 2004 ilikuwa ni Athens Ugiriki Athens, yalikoasisiwa na kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1894. Tanzania iliwakilishwa na riadha pekee, wakiwemo wanariadha wawili wa kike; Restituta Joseph katika mita 1,500 na 5,000 na Banuelia Brighton ‘Mrashani’ kwenye Marathon, ambako pia iliambulia patupu.

Agosti mwaka huu, Tanzania inatimiza miaka 44 ndani ya Olimpiki ya Kimataifa na mashindano yake ya kumi, yanafanyika katika Jiji la Beijing China.

Hadi sasa wenye tiketi mkononi na kuwa na uhakika wa kushiriki ni takribani wanariadha sita tu wakiwamo Dickson Marwa, Samson Ramadhani na Msenduki Mohammed, huku mchezo wa ngumi wakihaha wachezaji wao wafikie viwango, ambako umebaki mtihani wa mwisho katika mashindano ya kufuzu yatakayofanyika Namibia, Machi, mwaka huu.

Mbali ya ushiriki wa Tanzania katika michezo ya mwaka huu, pia imebahatika kuwa na tukio la kihistoria duniani linalokwenda sambamba na michezo hiyo, nalo ni Mwenge wa Olimpiki ambao utakimbizwa jijini Dar es Salaam, Machi, mwaka huu.

Mwenge huo ambao utakimbizwa miji takribani 59, Dar es Salaam ndilo jiji pekee katika bara la Afrika kupewa hadhi hiyo.

Kasumba ya Tanzania kuwakilishwa na michezo michache inayojirudiarudia, imeendelea tena mwaka huu na kuacha maswali miongoni mwa wapenda michezo na taifa kwa ujumla. Je, kupitia riadha pekee, au na ngumi endapo nao watafanikiwa kupenya, tunaweza kuandika historia tena na kutukumbusha yale yaliyofanywa na Bayi na Nyambui 1980 kule Moscow?

Hii ni changamoto kubwa kwa serikali, TOC na wanariadha wanaounda timu ya taifa kwa vigezo vya kihistoria. Riadha ndiyo inayotuweka katika ramani na rekodi za medali katika michuano hii.

Mtanzania wa kwanza kuleta medali nchini, mwaka 1980, Meja mstaafu Filbert Bayi, ndiye kinara wa TOC, ambaye ndiye katibu wa TOC na mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF). Nini tutarajie huko Beijing, je historia itaandikwa?

Hilo ni swali ambalo ni gumu kulijibu, lakini ukweli kwa takwimu, ni vigumu kuleta medali kwa uchache wa michezo ambayo Tanzania inashiriki, hali iliyosababishwa na kutojipanga na kukosa maandalizi ya muda mrefu katika michezo mbalimbali.

Source:TZ Daima
 
Mwaka 2012: Tanzania imeshiriki katika uogeleaji kwa mara ya kwanza! Hata hivyo maji ya London yameonekana ni mazito sana kwa washiriki wa Tanzania.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom