Ahadi za mawaziri zageuka shubiri

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Ahadi za mawaziri zageuka shubiri

Baadhi ya ahadi hizo ni pamoja na ile ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Vijana na Ajira, Jenista Muhagama, ambaye baada ya kuapishwa, aliahidi kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana kuhakikisha wanapata.

Pia Mhagama aliahidi kulifanya Bunge kuwa la wananchi na kuwaunganisha vijana na wafanyakazi katika sekta zote zinazosimamiwa na wizara yake.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, kwa upande wake, Desemba 24, mwaka jana, alipiga marufuku matangazo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Pamoja na kataza hilo, matangazo hayo bado yanaendelea kwenye kusikika au kusomwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya jamii.

Naye Waziri wake, Ummy Mwalimu, muda mfupi baada ya kuapishwa, aliahidi kuhakikisha anapata fedha ili kupunguza tatizo la dawa hospitalini na kuhakikisha wauguzi, madaktari na wataalamu wa afya wanakuwapo wa kutosha.

Sambamba na ahadi hiyo, Desemba 16, mwaka jana, alipiga marufuku uuzaji wa vyakula na matunda yaliyomenywa kwenye maeneo ya wazi na barabarani. Agizo hilo linaonekana kugonga mwamba kwani matunda yaliyomenywa yanaendelea kuuzwa sambamba na vyakula kwenye maeneo ya wazi.

Ahadi nyingine ni ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stellah Manyanya. Desemba 16, mwaka jana, Manyanya alisema atawasimamisha kazi walimu wakuu wa shule ambao wanafunzi watafika darasa la tatu bila kujua kusoma na kuandika.

Manyanya alitoa agizo hilo, akiwa wilayani Bagamoyo alipokuwa akipokea msaada wa madawati, huku akisema wanafunzi wanafeli kwa sababu mbalimbali ikiwamo mfumo wa ufundishaji, jambo ambalo wadau wa elimu wamesema halitekelezeki na haiwezekani walimu kuadhibiwa kwa sababu hiyo.

Mwingine ambaye ahadi zake hazijatekelezwa ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akitoa matamko yakiwamo kugawa mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD). Ahadi hiyo haijatekelezwa kama alivyosema.

Ahadi hiyo kwa mara ya kwanza aliitoa Desemba 12, mwaka jana, kabla hata ya kuwa waziri, wakati huo akiwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Aliahidi kugawa mashine 200,000 kwa nchi nzima.

Baada ya kuteuliwa kuwa waziri, aliahadi kupunguza utegemezi wa serikali kwa wahisani, akisema kufanya hivyo katika bajeti ya serikali ni kujidhalilisha.

Hata hivyo, katika bajeti ya mwaka 2016/17 aliyoisoma bungeni, inaonyesha bado utegemezi wa serikali uko pale pale. Bajeti hiyo ni tegemezi kwa takribani asilimia 20.

Kwa mujibu wa bajeti hiyo ya Sh trilioni 29.5, TRA inatarajiwa kukusanya Sh. trilioni 17.8, mikopo ya kibiashara Sh. trilioni 7.5, misaada ya wafadhili ni Sh. trilioni 3.6.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, naye mara baada ya kuapishwa alisema ili kuondoka kwenye umasikini ni lazima kuwe na umeme wa uhakika na usio katikakatika.

Pamoja na kuahidi kutekeleza hilo, alizungumzia suala la kuzalisha umeme wa kutosha kati megawati 10,000 mpaka 15,000 hivyo kufanya bei ya nishati hiyo kushuka.

Baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo kwa muda mfupi, nishati hiyo ilishuka kwa asilimia moja, ingawa kwa sasa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeomba kupandisha bei kwa asilimia 18.

Hatua hiyo inaonyesha, ndoto ya kushuka bei ya umeme kuwa ngumu kwani licha ya gharama ya ‘service line’ kuondolewa, watumiaji kila wakinunua umeme, hukatwa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT.

WADAU WATOA NENO

Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, shirika lisilo la kiserikali linalohusika na masuala ya afya nchini, alisema upatikanaji wa dawa bado ni tatizo kubwa katika hospitali nchini. Alisema utafiti wao umebaini wagonjwa wengi hulazimika kununua dawa katika maduka binafsi.

Alisema watumishi wa afya wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na uhaba wa vifaa tiba ambavyo wakati mwingine vinakosekana au kuwa vichache na kuweka mrundikano wa wagonjwa hospitalini.

“Setka ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi mno. Madaktari bado ni wachache, lakini pia hawana dawa na vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa. Ukienda Muhimbili utakuta mashine ya ‘CT Scan’ ni mbovu kama kuna wagonjwa unadhani watapata huduma wapi?” alihoji.

Aliongeza kuwa kwa sasa taifa linahitaji nusu ya wataalamu walioko kazini na kwamba kuna wasomi wa vyuo vikuu waliohitimu miaka mitatu mfululizo na hawakuajiriwa, ambao wangeweza kutosheleza katika hospitali za serikali.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Billy Haonga, alisema sekta hiyo kwa sasa bado ina changomoto nyingi na kwamba kama serikali haitazifanyia kazi kama ilivyoahidi, itakosa wataalamu wengi.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uhaba wa dawa na wataalam na vifaa vya kufanyia kazi. Pia alisema serikali inachelewesha kufikisha fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hizo.

“Tanzania tuna uhaba wa madaktari bingwa katika hospitali za serikali, tuna uhaba wa dawa na vifaa. Hivi karibuni tulisikia pesa zitapatikana kutatua changamoto hizo lakini zinakuwa na mlolongo mrefu, zitoke Hazina hadi kufika mahala husika inachukua muda.

“Naomba serikali ikumbuke muda pesa hiyo ikifanyiwa kazi lakini wagonjwa wanaendelea kuteseka na kuna uwezekano wa kupoteza nguvu kazi ya taifa,” alisema Dk. Haonga.

Pia Makamu wa MAT, Dk. Obadia Nyongela, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwa sasa kuna madaktari 1,700 mtaani ambao wana sifa lakini hawajaajiriwa. Alisema kama mwaka huu utaisha bila vibali vya ajira kutoka, hivyo mpaka mwakani kutakuwa na madaktari 2,866 wasio na ajira licha ya kuwapo upungufu wa wataalamu hao.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Ephata Kaaya, alisema wanaendelea kuzalisha wataalamu hao kwa sababu wanajua bado Tanzania ina upungufu wa madaktari.

CWT YAIBUKA

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch, aliieleza Nipashe kuwa kuwawajibisha walimu kwa sababu ya watoto kutojua kusoma na kundika ni jambo lisiloingia akilini kwa kuwa uhaba wa wataalamu hao unajulikana.

Alisema hali hiyo iko hivyo licha ya kuwapo kwa walimu 30,000 nchini ambao hawana ajira licha ya kuhitimu masomo yao. Alisema hao ni wale waliomaliza masomo mwaka jana na kwamba wataongezeka baada wengine kuhitimu mwaka huu.

Oluoch alisema upungufu wa walimu shuleni ni kwa masomo yote na kwamba serikali inavyoendelea kutotoa ajira kwa walimu idadi inaongezeka.

Pia alisema mfumo wa ufundishaji wa walimu vyuoni haumwezeshi mwalimu kumudu kufundisha wanafunzi wa chekechea na wale wa darasa la kwanza. Alisema wanafunzi wa chekechea wanahitajika wanafunzi 25 darasani lakini shule nyingi wanawekwa zaidi ya idadi hiyo huku wa darasa la kwanza wakiwa 40.

“Kwa wanafunzi hawa ni lazima tufuate utaratibu ili wajue Kusoma, Kuandika na kuhesabu vinginevyo watafeli… Wanasiasa wamekuwa wakizungumza kisiasa lakini si jambo rahisi kama wanavyosema, suala la mwalimu kufaulu linatokana pia na mazingira,” alisema.

TRA yafunguka

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alisema mpaka sasa TRA imeshagawa mashine za EFD kwa baadhi ya wafanyabiashara walioko jijini Dar es Salaam peke yake kuanzia Juni hadi Septemba, mwaka huu.
“Kwa wafanyabiashara wenye sifa na vigezo vya kupata mashine hizo tulishawapatia.

Hili tulianza na mkoa wa Dar es Salaam na baadaye tunapanga kufanya katika mikoa mingine kwa sababu lengo ni kuwafikia wafanyabiashara wote nchi nzima, ambao wana sifa za kupata mashine hizo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alikiri kugawiwa mashine hizo kwa wafanyabiashara wa Dar es Salaama pekee na kuitaka serikali kukamilisha kazi hiyo kwa nchi nzima kama ilivyoahidi tangu awamu ya tano ilipoingia madarakani mwaka jana.

“Ni kweli kuwa hapa Dar es Salaam wafanyabiashara wanaopaswa kugawiwa bure wote walipata ingawa kuna wengine ambao hawakuwa na sifa nao walikuja na tuliwaelewesha na kwa bahati nzuri walielewa.

“Kuna wafanyabiashara ambao walikuwa wamesajiliwa kwa VAT, ambao wana uwezo wa kukusanya hesabu ya kuanzia Sh. milioni 100 na kuendelea. Hawa waliambiwa wajinunulie mashine hizo. Pia kuna wale ambao wamesajiliwa kwa kufanya hesabu ya mwaka kuanzia Sh. milioni 20 hadi Sh. milioni 100 nao waliambiwa watakopeshwa na baadaye watakatwa katika hesabu zao za mwaka.

“Lakini kuna wale wasiozidi Sh. milioni 20, hawa ndio wanapaswa kupewa bure hizo EFD na ndio ambao serikali iliahidi na imeanza na Dar es Salaam,” alisema.

Hoja za Mhagama

Akizungumzia ahadi ya Waziri Mhagama, mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Kitila Mkumbo, alisema dhana ya bunge kuwa la wananchi haipo tena hasa baada ya serikali kutangaza kutolionyesha bunge hilo mubashara kupitia runinga na kulionyesha kwa masaa machache ama kwa vipindi maalum vyilivyohaririwa.

“Bunge halionyeshwi live, hivyo haliwezi kuwa la wananchi bali ni bunge la serikali. Bunge la wananchi ni lile ambalo wananchi wanashuhudia wawakilishi wao wakitoa hoja za msingi kama walivyowatuma lakini hawaoni kinachoendelea. Badala yake wanaangalia vipindi vilivyohaririwa,” alisema.

Profesa Mkumbo ambaye ni mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mmoja wa viongozi waandamizi wa chama cha ACT-

Wazalendo, alisema Bunge la sasa ni la kibaguzi na si la wananchi. Alisema wabunge kutoka vyama vya upinzani, ambao pia ni wawakilishi wa wananchi, hawasikilizwi hoja zao kama walivyotumwa na wananchi wanaowawakilisha.

Aidha Nipashe ilimhoji mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Bungeni, Owen Mwandumbya, kuona ni jinsi gani Bunge hilo ni la wananchi kama Mhagama alivyoahidi.

Mwandumbya alisema ahadi hiyo ilianza kutekelezwa baada ya maofisa wa bunge kuanza kutoa elimu kwa wananchi hasa katika maonyesho ya sabasaba kuhusu bunge linavyofanya kazi na wananchi hutoa maoni yao na kufanyiwa kazi.

Aliongeza kuwa bunge limetoa fursa kwa wadau mbalimbali kujadili miswada inayopelekwa bungeni na hoja hizo hupelekwa katika kamati husika na kuona ni namna gani maoni hayo yanaweza kuwa msaada.

“Tunayo sera ya bunge ambayo inalenga kulifanya bunge kuwa la wananchi. Tunatoa elimu kwa wananchi kulijua bunge lao lakini pia tunahakikisha miswada mbalimbali kabla ya kuwa sheria inapitia kwa wadau ambao hutoa maoni yao na yanafanyiwa kazi.” Alisema.

Aliongeza kuwa mijadala pamoja na kumbukumbu rasmi za bunge huwekwa katika tovuti ya bunge na wananchi wanapata fursa ya kuangalia kilichojiri bungeni kila siku nyakati za mikutano ya chombo hicho.

“Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja haimaanishi kwamba si la wananchi. Kilichotokea ni kubadilisha mfumo lakini matangazo haya hurushwa na Bunge lenyewe na ni jukumu la wenye runinga kurusha live (mubashara) au kurekodi,” alisema.

Chanzo: Habari Leo
 
Story hii nitaisoma yote kesho aisee, hiki ndo nimekuwa nikiyalalamikia magazeti na vyombo vyetu vya habari, viko mstari wa mbele kuandika maagizo, matamko na ahadi za wanasiasa lakini hawatupi mrejesho wa ahadi, makatazo na maagizo ndani ya muda husika.

Mfano, Kigwangala aliwahi kumwagiza Mganga Mkuu wa Hospital ya Rufaa Mbeya kwamba ndani ya mwezi mmoja awe amepata Machine/Mtambo wa MRI vinginevyo kazi hana, mpaka sasa ni zaidi ya miezi 7 sasa, nilitegemea magazeti yaliyoiandika habari watoe mrejesho ndani ya muda husika lakini sikuona kitu hiko.
 
Back
Top Bottom