Ahadi ya JK yachakachuliwa; HALI ya mambo si shwari katika Kijiji cha Butiama

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

Na Mwandishi Wetu, Butiama

HALI ya mambo si shwari katika Kijiji cha Butiama baada ya Serikali kuhamishia makao makuu ya Wilaya mpya ya Butiama katika eneo la Nyamisisi, Kiabakari mkoani Mara.


Hivi karibuni Serikali ilitangaza majina ya mikoa na wilaya mpya, huku makao makuu ya Wilaya ya Butiama yakiondolewa kijijini Butiama tofauti na ahadi mbili zilizowahi kutolewa na Rais JakayaKikwete, mwaka 2008 na baadaye mwaka 2010.


Wapo wanaosema kwamba huenda Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imejichanganya kwa kudhani kuwa Nyamisisi ni miongoni mwa vitongoji vya Kijiji cha Butiama, jambo ambalo si sahihi.


Ahadi ya mwaka 2008, Rais Kikwete aliitoa wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kilichofanyika kijijini hapo.


Mara ya pili alirejea ahadi hiyo Juni 5, mwaka jana wakati aliposimama kwa muda kijijini Butiama akiwa safarini kwenda kufungua Bwawa la Kisangwa.


Aliposimama alimtaka Mwenyekiti wa Kijiji aombe lolote lililo juu ya uwezo wake, na Mwenyekiti akamjibu kwa kumkumbusha kwamba anasubiri makao makuu ya wilaya kuwa Butiama. Rais alikaririwa akisema, "Hiyo mmeshapata".


Mamia ya wananchi wa Butiama wakionyesha hasira za waziwazi, juzi walishiriki katika mkutano mkubwa uliofanyika nje ya Ukumbi wa Jumba la Maendeleo kijijini hapa na kumshirikisha Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.


Lawama za awali anarushiwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, kwamba ndiye aliyeongoza mkakati wa kuhakikisha Butiama inapokwa heshima ya kuwa makao makuu ya wilaya hiyo mpya.


Baadhi ya wananchi walizungumza kwa hasira, na mmoja akafikia hatua ya kupendekeza hata ikiwezekana Butiku achukuliwe hatua zaidi kwa madai kwamba amewasaliti Wanabutiama wenzake.


Mwenyekiti mstaafu wa Butiama, Marwa Magesa, alisema, "Butiku asiwe msemaji wa kijiji, hatumtaki, ahame."

Naye, Mwalimu Kyasi alisema; "Siku walipotangaza mikoa na wilaya mpya mimi nilikuwa nasikiliza redio. Walipotangaza Nyamisisi nilizima redio, Mbunge wetu tunakuunga mkono, lakini ujue kwamba wilaya inapaswa ijengwe Butiama."


Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama, Zacharia Wambura, ambaye ndiye aliyeongoza mkutano huo, aliungwa mkono na wananchi kwa msimamo wake wa kutaka jina la Wilaya ya Butiama libadilishwe, ili ikiwezekana iitiwe Wilaya ya Nyamisisi au Kiabakari.


"Kama wameona haiwezekani kuweka makao makuu Butiama, basi wafute jina hilo, wasilitumie, watumie jina tofauti," alisema na kuungwa mkono na hadhira.


Kwa upande wake, Mbunge Mkono, akizungumza kwa tahadhari kubwa, alisema amefuatilia suala la mahali yalipohamishiwa makao makuu na kubaini kuwa kuna uchakachuaji.


"Wananchi mimi ni Mbunge wenu, Butiama ni wapigakura wangu, Nyamisisi ni wapigakura wangu, kwa hiyo naomba nieleweke kuwa siegemei upande wowote.


"Lakini kwa suala hili la Makao Makuu ya Wilaya ya Butiama ieleweke kuwa si mimi niliyesema au kupendekeza yawe Butiama. Hii ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Rais
Jakaya Kikwete.


"Kama aliahidi kuwa makao makuu yatakuwa hapa, sasa tuelezwe ni nani aliyetengua kauli yake, maana hapa katikati hajatoa kauli ya kufuta kuwa Butiama isiwe makao makuu. Hao waliochakachua ndiyo tunaotaka kuwajua," alisema na kuongeza:


"Mimi nalinda kauli ya Rais, sisi hatukuomba, ni yeye aliyetuambia…sasa tumjue huyo anayetoa tonge domoni…nalinda kauli ya Rais.


"Hapa kuna maneno makali makali na mazito, lakini nawaambia kuwa Rais hajafuta kauli yake kwa hiyo wananchi kuweni na subira, lazima kieleweke."


Mwenyekiti wa Kijiji, Wambura, akihitimisha mkutano huo, alitoa mambo kadhaa aliyosema kuwa ndiyo msimamo wa wana Butiama.


Alisema, "Wana Butiama Waziri Mkuu anakuja hapa, aje na jibu la kueleweka, aeleze ni kwa namna gani ahadi ya Mheshimiwa Rais imefutwa, na kama si yeye Rais aliyeifuta, waliohusika kufanya hivyo ni kina nani?


"Wananchi wanasema kama msimamo ni Nyamisisi kuwa makao makuu ya Wilaya ya Butiama, basi jina la wilaya libadilishwe ili tubaki na Kijiji chatu cha Butiama kama kijiji.


"Wananchi wanasema kama hakuna uwezekano wa kuifanya Butiama kuwa makao makuu, basi hata sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru kijijini Butiama zitahudhuriwa na viongozi wa wilaya, mkoa na Taifa tu. Tena wanataka watoto wao wasiendelee kufanya mazoezi ya halaiki maana wanashinda njaa."


Juzi, wananchi zaidi ya 1,000 wa Kijiji cha Butiama walikuwa wametia saini kwenye karatasi za pingamizi la kunyang'anywa makao makuu ya wilaya.


Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Geofrey Ngatuni, amekaririwa akisema hata yeye hajui imekuwaje Nyamisisi imekuwa makao makuu.


Alisema hana taarifa za eneo hilo kuwa makao makuu ya Wilaya ya Butiama ambayo imetokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Musoma.


Mkurugenzi wa Maendeleo Wilaya ya Musoma, Dk. Karaine ole Kunei, yeye amesema kwamba anachojua ni kwamba eneo la Nyamisisi lilipimwa kwa ajili ya kuwa mji mdogo, na si vinginevyo.


Eneo la Nyamisisi ambako kunaweza kuwa makao makuu ya wilaya ya Butiama hakuna jengo lolote la huduma za kijamii. Butiama ina majengo na huduma karibu zote,
zikiwamo shule, hospitali ya Wilaya, Kituo cha Polisi chenye hadhi, umeme, miundombinu ya maji (ingawa haina maji), na ofisi za Posta.


Wakati hali ikiwa hivyo kijijini Butiama, kwa wakazi wa Nyamisisi na Kiabakari, ni shangwe na vigelegele.


Wanatumia kigezo kwamba tangu zamani hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alipinga wilaya kujengwa Butiama, badala yake akawa akitaka ijengwe Kiabakari.


Wanasema kama kweli ni kumuenzi Mwalimu, basi uamuzi wa Serikali kuweka makao hayo Nyamisisi ni wa busara.

 
Laiti mwalimu angekuwa hai mpaka leo, JK asingekuwa Rais wa hii nchi, na yeye (JK) analitambua hilo, usisahau ni JK ni mtu wa visasi.
 
Back
Top Bottom