Afunguliwa kesi kwa kumuuliza Swali Waziri Mkuu..

Samvulachole

JF-Expert Member
Oct 22, 2006
413
117
Afunguliwa kesi kwa kumuuliza
Swali Waziri Mkuu..
STAILI ya Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa anapokuwa katika ziara mikoani ya kuruhusu wenye kero waulize maswali sasa imezidi kuwa mzigo kwa wananchi, uchunguzi wa kina wa gazeti hili umebaini. Uchunguzi huo katika ziara kadhaa za Waziri Mkuu umebaini kuwa wananchi wengi wanaomuuliza maswali hasa yanayoonekana kuwa na changamoto za msingi kwa viongozi, wamekuwa wakikumbana na madhila mbalimbali baada ya hapo.
Wakati Watanzania wakiwa hawajasahau sakata la mwanafunzi Allan Shella wa wilayani Ukerewe, Mwanza aliyemhoji Bw. Lowassa juu ya viongozi kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja na Waziri Mkuu kuahirisha kumjibu na ikaripotiwa kuwa baada ya hapo mwanafunzi huyo alisumbuliwa sana na watu wa Usalama wa Taifa, mwananchi mwingine amejikuta katika hali tete zaidi kiasi cha kuburutwa kortini huku mlalamikaji akiwa kiongozi mwandamizi Serikalini na mteule wa Rais.
Aliyekumbana na balaa hilo safari hii ni mkazi wa Mbeya Bw. Ilonga Elonga (56) ambaye chanzo cha matatizo yake kinaanzia katika ziara ya Bw. Lowassa jijini Mbeya iliyofanyika Oktoba mwaka jana. Chanzo cha yote Akieleza kilichotokea, Bw. Elonga aliyeonekana kuwa na simanzi, aliliambia gazeti hili Dar es Salaam wiki hii kuwa anakumbuka ilikuwa ni Oktoba 17 mwaka jana, wakati Bw. Lowassa akiwa ziarani mkoani Mbeya, yeye na wananchi wengine walihudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Makongosi ambapo Waziri Mkuu alihutubia. Bw. Elonga anaeleza zaidi kuwa kabla ya Bw. Lowassa kuhutubia alitoa nafasi kwa wananchi wenye kero au swali kujitokeza mbele na kutoa dukuduku lao.
Anasema yeye pamoja na wananchi wengine walipopewa nafasi hiyo kila mmoja alihoji juu ya kero aliyoona inawasumbua. Anakumbuka kuwa yeye alihoji ni kwa nini kwa kipindi cha miaka minne tangu 2004 wananchi wa kata hiyo hawakuwa wameomewa mapato na matumizi ya fedha za ujenzi wa sekondari yao ya Kata ya Makongorosi. Baada ya kuuliza swali hilo, Waziri Mkuu Lowassa alitoa nafasi kwa viongozi husika kujibu swali hilo lakini waliposimama walishindwa kutoa majibu ya kumridhisha Waziri Mkuu kiasi cha kumfanya atoe maagizo ya haraka.
Anasema mwananchi huyo kuwa Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile kwenda kijijini hapo Novemba 6, 2007 ili kuhakikisha wananchi wanasomewa mapato na matumizi na kusikiliza kero zao kwa undani zaidi. Bw. Elonga anakumbuka kuwa hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alifika kijijini hapo mwezi Desemba mwaka jana na kabla ya kuitisha mkutano wa hadhara alianza na kikao cha ndani kilichowashirikisha viongozi wenzake akiwemo Mkuu wa Wilaya.
Matatizo yaanza Anasema kuwa bila kujua kilichojadiliwa na uamuzi uliofikiwa, akiwa kwenye shughuli zake, siku moja alifuatwa na gari la Mkuu wa Wilaya likiwa na askari watatu na kuamrishwa afuatane nao kwani alikuwa akitakiwa kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa. "Nilipofika waliniuliza kama mimi ndiye Bw. Ilonga Elonga, nikajibu ndiye mimi," alisema na kuongeza kuwa walimuuliza pia kama ni yeye aliyeandika barua ya wasomaji katika gazeti la Majira akilalamikia wananchi kutosomewa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za ujenzi wa shule. Bw. Elonga anaeleza kuwa baada ya kuoneshwa nakala ya gazeti hilo alikiri.
"Nilikiri kuandika barua hiyo na nikawaambia pia kuwa hicho ndicho nilichohoji mbele ya Waziri Mkuu," aliongeza. Baada ya kuwaeleza hivyo alisema Mkuu wa Wilaya alimuuliza iwapo anafahamu alichokiandika au anajikaanga mwenyewe? "Aliniuliza ni wapi nilipata takwimu hizo na kama ninaweza kuzithibitisha," anaeleza Bw. Elonga na kuongeza kuwa alianza kupata vitisho kwa kueleza kuwa atafungwa.
"Niliwaambia kuwa nipo tayari kufungwa lakini haki ya wananchi itajulikana," alisisitiza. Mbele ya wananchi Baada ya kutoa msimamo wake huo waliondoka kwenye kikao hicho na kwenda kwenye mkutano wa hadhara huku akishinikizwa na baadhi ya viongozi hao akiri kuwa maelezo aliyoyatoa mbele ya Waziri Mkuu yalikuwa ni ya uongo na kuwaomba radhi wananchi lakini, Bw. Elonga anadokeza kuwa alikataa.
Hata hivyo anasema badala ya kufuata maelekezo waliyokuwa wakimshinikiza yeye alipopanda jukwaani aliwahoji wananchi waliohudhuria mkutano huo kama waliwahi kusomewa mapato na matumizi na wakajibu hapana hivyo akaamua kuendelea na msimamo wake wa kutokuomba radhi huku wananchi wakiamua kususia mkutano baada ya kuona wanazidi kulazimishwa. Desemba 12, 2007 Siku hii, Bw. Elonga ansema ndipo alipofuatwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Makongorosi aliyemtaja kwa jina moja tu la Bw. Deus na kumweleza kuwa anatakiwa ofisini kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chunya, naye akitajwa kwa jina moja tu la Bw. Kombo.Alipofika huko alikuta ameshafunguliwa jalada la kesi ya jinai ya kutoa taarifa za uongo.
Kesho yake alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Chunya na kusomewa shitaka hilo. Anasema alikana shitaka na kwa sasa yuko nje kwa dhamana lakini anaendelea kupokea vitisho kuwa lazima afungwe.Alisema kuwa baadaye alibaini kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Bibi Fatuma Kimario.
RC: Sijamfungulia mtu kesi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Mwakipesile alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu sakata la mwananchi huyo alisema yeye aliitisha mkutano baada ya kero hiyo kutolewa kama alivyokuwa ameagizwa na Bw. Lowassa na akasema wananchi walisomewa taarifa waliyokuwa wakiilalamikia. Hata hivyo hakuwa tayari kuzungumzia zaidi kesi aliyofunguliwa mwananchi huyo.
"Mpigie simu mama Fatuma (Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni mlalamikaji) umuulize jambo hilo mimi sijawahi kumfungulia mtu mashitaka," alisema.
DC:Kesi ipo ila awaeleze ukweli Naye DC Fatuma alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya mwananchi huyo alijibu: "Mwambie akueleze ukweli wa mambo, mtu hawezi kufunguliwa kesi kwa kuhoji ukweli...muulize akueleze vizuri, mbane hakuna mtu anayeweza kuuliza swali akapelekwa mahakamani hii nchi iko huru hakuna Mtanzania anayeweza kuuliza swali akafikishwa mahakamani.
" Alipoelezwa kuwa Bw. Elonga alipoona wananchi hawasomewi mapato na matumizi ndipo alipoandika barua ya wasomaji akikumbushia yale aliyoyaeleza mbele ya Bw. Lowassa DC Fatuma alisisistiza: "Mwambie akupe barua hiyo utaelewa matatizo yake...muulize ni kwa nini ashitakiwe? Mtanzania aliye huru hawezi kuuliza swali akafunguliwa mashitaka." DC Fatuma pia akahoji kitendo cha mwnanchi huyo kuzungumza na waandishi akiwa Dar es Salaam badala ya Mbeya lilikotokea tukio.
"Ilikuwaje afunge safari hadi huko kwenu (Dar es Salaam)? Hivi huku Mbeya hakuna waandishi wa habari hadi atoke Chunya hadi Dar es Salaam" Kwa nini hakufuata taratibu zinazohusika," alihoji DC huyo na kumshauri mkazi huyo kama kuna vitisho anavipata akatoe taarifa polisi au aende mahakamani. "Hakuna anayemtisha, kama anapata vitisho afungue kesi nyingine ya kumshitaki huyo anayemtisha,"
alisema na kuongeza: "Kama kesi ipo mahakamani yeye anaogopa nini? Mahakama haiongozwi na mtu, inasimamia haki...Tungoje sheria ichukue mkondo wake." Hata hivyo DC huyo alishindwa kuweka bayana iwapo yeye ni mlalamikaji katika kesi hiyo na ni suala gani hasa lililomfanya ahusike katika kumfungulia mashtaka mwananchi huyo. Habari hii na Reuben Kagaruki.
 
Sanvulachole:
Hii habari haijakaa sawa!
Huyo mwandishi wa habari hii aliwahi kuisoma barua iliyopo kwenye gazeti la majira, na inayoonekana kuwa na utata hadi huyu bwana kufunguliwa mashitaka?

Watu wa Haki za Binaadam, na wanasheria wamtete huyu ndugu asinyamazishwe bure kwa kutoa mawazo yake, (kama hakukiuka sheria?) Siijui hiyo sheria inayowafunga watu midomo kiasi hicho!
Au aliwachochea wananchi wapindue serikali ya ccm kwa kuwaua viongozi wote mafisadi? Hata hili nadhani linaweza kuwa na kinga mbele ya sheria ya haki.
 
Back
Top Bottom