Afunguliwa kesi kwa kumuuliza swali Waziri Mkuu Lowassa

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,873
1,894
Na Reuben Kagaruki

STAILI ya Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa anapokuwa katika ziara mikoani ya kuruhusu wenye kero waulize maswali sasa imezidi kuwa mzigo kwa wananchi, uchunguzi wa kina wa gazeti hili umebaini.

Uchunguzi huo katika ziara kadhaa za Waziri Mkuu umebaini kuwa wananchi wengi wanaomuuliza maswali hasa yanayoonekana kuwa na changamoto za msingi kwa viongozi, wamekuwa wakikumbana na madhila mbalimbali baada ya hapo.

Wakati Watanzania wakiwa hawajasahau sakata la mwanafunzi Allan Shella wa wilayani Ukerewe, Mwanza aliyemhoji Bw. Lowassa juu ya viongozi kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja na Waziri Mkuu kuahirisha kumjibu na ikaripotiwa kuwa baada ya hapo mwanafunzi huyo alisumbuliwa sana na watu wa Usalama wa Taifa, mwananchi mwingine amejikuta katika hali tete zaidi kiasi cha kuburutwa kortini huku mlalamikaji akiwa kiongozi mwandamizi Serikalini na mteule wa Rais.

Aliyekumbana na balaa hilo safari hii ni mkazi wa Mbeya Bw. Ilonga Elonga (56) ambaye chanzo cha matatizo yake kinaanzia katika ziara ya Bw. Lowassa jijini Mbeya iliyofanyika Oktoba mwaka jana.

Chanzo cha yote

Akieleza kilichotokea, Bw. Elonga aliyeonekana kuwa na simanzi, aliliambia gazeti hili Dar es Salaam wiki hii kuwa anakumbuka ilikuwa ni Oktoba 17 mwaka jana, wakati Bw. Lowassa akiwa ziarani mkoani Mbeya, yeye na wananchi wengine walihudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Makongosi ambapo Waziri Mkuu alihutubia.

Bw. Elonga anaeleza zaidi kuwa kabla ya Bw. Lowassa kuhutubia alitoa nafasi kwa wananchi wenye kero au swali kujitokeza mbele na kutoa dukuduku lao.

Anasema yeye pamoja na wananchi wengine walipopewa nafasi hiyo kila mmoja alihoji juu ya kero aliyoona inawasumbua. Anakumbuka kuwa yeye alihoji ni kwa nini kwa kipindi cha miaka minne tangu 2004 wananchi wa kata hiyo hawakuwa wameomewa mapato na matumizi ya fedha za ujenzi wa sekondari yao ya Kata ya Makongorosi.

Baada ya kuuliza swali hilo, Waziri Mkuu Lowassa alitoa nafasi kwa viongozi husika kujibu swali hilo lakini waliposimama walishindwa kutoa majibu ya kumridhisha Waziri Mkuu kiasi cha kumfanya atoe maagizo ya haraka.

Anasema mwananchi huyo kuwa Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile kwenda kijijini hapo Novemba 6, 2007 ili kuhakikisha wananchi wanasomewa mapato na matumizi na kusikiliza kero zao kwa undani zaidi.

Bw. Elonga anakumbuka kuwa hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alifika kijijini hapo mwezi Desemba mwaka jana na kabla ya kuitisha mkutano wa hadhara alianza na kikao cha ndani kilichowashirikisha viongozi wenzake akiwemo Mkuu wa Wilaya.

Matatizo yaanza

Anasema kuwa bila kujua kilichojadiliwa na uamuzi uliofikiwa, akiwa kwenye shughuli zake, siku moja alifuatwa na gari la Mkuu wa Wilaya likiwa na askari watatu na kuamrishwa afuatane nao kwani alikuwa akitakiwa kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa.

"Nilipofika waliniuliza kama mimi ndiye Bw. Ilonga Elonga, nikajibu ndiye mimi," alisema na kuongeza kuwa walimuuliza pia kama ni yeye aliyeandika barua ya wasomaji katika gazeti la Majira akilalamikia wananchi kutosomewa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za ujenzi wa shule.

Bw. Elonga anaeleza kuwa baada ya kuoneshwa nakala ya gazeti hilo alikiri. "Nilikiri kuandika barua hiyo na nikawaambia pia kuwa hicho ndicho nilichohoji mbele ya Waziri Mkuu," aliongeza.

Baada ya kuwaeleza hivyo alisema Mkuu wa Wilaya alimuuliza iwapo anafahamu alichokiandika au anajikaanga mwenyewe?

"Aliniuliza ni wapi nilipata takwimu hizo na kama ninaweza kuzithibitisha," anaeleza Bw. Elonga na kuongeza kuwa alianza kupata vitisho kwa kueleza kuwa atafungwa. "Niliwaambia kuwa nipo tayari kufungwa lakini haki ya wananchi itajulikana," alisisitiza.

Mbele ya wananchi

Baada ya kutoa msimamo wake huo waliondoka kwenye kikao hicho na kwenda kwenye mkutano wa hadhara huku akishinikizwa na baadhi ya viongozi hao akiri kuwa maelezo aliyoyatoa mbele ya Waziri Mkuu yalikuwa ni ya uongo na kuwaomba radhi wananchi lakini, Bw. Elonga anadokeza kuwa alikataa.

Hata hivyo anasema badala ya kufuata maelekezo waliyokuwa wakimshinikiza yeye alipopanda jukwaani aliwahoji wananchi waliohudhuria mkutano huo kama waliwahi kusomewa mapato na matumizi na wakajibu hapana hivyo akaamua kuendelea na msimamo wake wa kutokuomba radhi huku wananchi wakiamua kususia mkutano baada ya kuona wanazidi kulazimishwa.

Desemba 12, 2007

Siku hii, Bw. Elonga ansema ndipo alipofuatwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Makongorosi aliyemtaja kwa jina moja tu la Bw. Deus na kumweleza kuwa anatakiwa ofisini kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chunya, naye akitajwa kwa jina moja tu la Bw. Kombo.Alipofika huko alikuta ameshafunguliwa jalada la kesi ya jinai ya kutoa taarifa za uongo.

Kesho yake alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Chunya na kusomewa shitaka hilo. Anasema alikana shitaka na kwa sasa yuko nje kwa dhamana lakini anaendelea kupokea vitisho kuwa lazima afungwe.Alisema kuwa baadaye alibaini kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Bibi Fatuma Kimario.

RC: Sijamfungulia mtu kesi

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Mwakipesile alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu sakata la mwananchi huyo alisema yeye aliitisha mkutano baada ya kero hiyo kutolewa kama alivyokuwa ameagizwa na Bw. Lowassa na akasema wananchi walisomewa taarifa waliyokuwa wakiilalamikia. Hata hivyo hakuwa tayari kuzungumzia zaidi kesi aliyofunguliwa mwananchi huyo.

"Mpigie simu mama Fatuma (Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni mlalamikaji) umuulize jambo hilo mimi sijawahi kumfungulia mtu mashitaka," alisema.

DC:Kesi ipo ila awaeleze ukweli

Naye DC Fatuma alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya mwananchi huyo alijibu:

"Mwambie akueleze ukweli wa mambo, mtu hawezi kufunguliwa kesi kwa kuhoji ukweli...muulize akueleze vizuri, mbane hakuna mtu anayeweza kuuliza swali akapelekwa mahakamani hii nchi iko huru hakuna Mtanzania anayeweza kuuliza swali akafikishwa mahakamani."

Alipoelezwa kuwa Bw. Elonga alipoona wananchi hawasomewi mapato na matumizi ndipo alipoandika barua ya wasomaji akikumbushia yale aliyoyaeleza mbele ya Bw. Lowassa DC Fatuma alisisistiza:

"Mwambie akupe barua hiyo utaelewa matatizo yake...muulize ni kwa nini ashitakiwe? Mtanzania aliye huru hawezi kuuliza swali akafunguliwa mashitaka."

DC Fatuma pia akahoji kitendo cha mwnanchi huyo kuzungumza na waandishi akiwa Dar es Salaam badala ya Mbeya lilikotokea tukio.

"Ilikuwaje afunge safari hadi huko kwenu (Dar es Salaam)? Hivi huku Mbeya hakuna waandishi wa habari hadi atoke Chunya hadi Dar es Salaam" Kwa nini hakufuata taratibu zinazohusika," alihoji DC huyo na kumshauri mkazi huyo kama kuna vitisho anavipata akatoe taarifa polisi au aende mahakamani.

"Hakuna anayemtisha, kama anapata vitisho afungue kesi nyingine ya kumshitaki huyo anayemtisha," alisema na kuongeza:

"Kama kesi ipo mahakamani yeye anaogopa nini? Mahakama haiongozwi na mtu, inasimamia haki...Tungoje sheria ichukue mkondo wake." Hata hivyo DC huyo alishindwa kuweka bayana iwapo yeye ni mlalamikaji katika kesi hiyo na ni suala gani hasa lililomfanya ahusike katika kumfungulia mashtaka mwananchi huyo.
 
Si unaona wanavyojifanya wana majibu ya mkato wakitakiwa kujibu maswali yanawasumbua watu. Mwisho wao utafika tu. Suala la mtuhumiwa huyu kuongea akiwa dar,eti hakufuata sheria? inaonyesha jinsi huyu mama alivyo na uwezo mdogo wa kufikiri. Nchi huru unaongea popote ulipo, taratibu zipi anataka afuate huyu mtu
 
Hawa wakuu wasijifanye kukanusha, haya masuala yapo sana huko vijijini na ni ya kawaida sana. Mtu ukihoji kitu ambacho wakubwa wanakuwa na maslahi nacho lazima wakusumbue tu.
Namuomba Ilonga akomae nao tu, kitaeleweka.
 
Taabu serikali inapenda tu kupigiwa makofi saa zote , na ukiwa na maoni tofauti ndo wanakusumbua!

May be kuna zaidi- au lililofichika ambalo huyu jamaa hajasema!
 
Jk na Lowasa hawapendi challenge na wanadhani wao wana usahihi zaidi ndiyo maana hata Lowasa hutumia nguvu nyingi kuzima hoja za Bunge . Jamani wafike mahali waelewe kwamba wadanganyika wanaamka sasa na hawapenda kuendelea kuwa wasikilizaji na kusifu pekee .Ilonga ukitaka msaada tupo tuchange upate wakili .JF tunapambana na ubadhirifu na Ufisadi wa aina hii .
 
majibu yako sawa kabisa au ww ulitaka ajibu vp?

yeye alikwisha auliza na mkuu alishaagiza wasomewe na tatizo linashughulikiwa anakitia umwamba wa kuandika barua kwenye magazeti na kutoa madata ambyo yy mwenyewe anajua kayapata wapi sasa anapelekwa mahakamani kuthibitisha hizo data zake na hapo hajaonewa angefungwa au kuwekwa ndani bila ya kupelekwa mahakamani hapo ndipo sawa

sasa kama yy mwamba na mkweli aende tu huko mahakamani na atoe ushahidi wake si aombe huruma magazetini na kusema uongo ukweli ni kuwa hakushtakiwa kwa kuuliza swali ukweli auseme
 
Jk na Lowasa hawapendi challenge na wanadhani wao wana usahihi zaidi ndiyo maana hata Lowasa hutumia nguvu nyingi kuzima hoja za Bunge . Jamani wafike mahali waelewe kwamba wadanganyika wanaamka sasa na hawapenda kuendelea kuwa wasikilizaji na kusifu pekee .Ilonga ukitaka msaada tupo tuchange upate wakili .JF tunapambana na ubadhirifu na Ufisadi wa aina hii .


Hakuna uhuru usio na mipaka ata baba yako akikupa ruhusa ya kumuuliza maswali lazima kuwe na kiwango huwezi kumuuliza ata maswali ya kishabiki na kijinga.mimi naamini muwafunde vijana wajue maneno ya kuongea na wazazi wao na wakubwa wao kiumri.kama lowasa anatumia nguvu kubwa kujibu hoja za wabunge na wao wakanyamaza huo ni ujinga wao na si ubabe wa lowasa kwani wao hawamwakilishi lowasa bungeni.
 
majibu yako sawa kabisa au ww ulitaka ajibu vp?

yeye alikwisha auliza na mkuu alishaagiza wasomewe na tatizo linashughulikiwa anakitia umwamba wa kuandika barua kwenye magazeti na kutoa madata ambyo yy mwenyewe anajua kayapata wapi sasa anapelekwa mahakamani kuthibitisha hizo data zake na hapo hajaonewa angefungwa au kuwekwa ndani bila ya kupelekwa mahakamani hapo ndipo sawa

sasa kama yy mwamba na mkweli aende tu huko mahakamani na atoe ushahidi wake si aombe huruma magazetini na kusema uongo ukweli ni kuwa hakushtakiwa kwa kuuliza swali ukweli auseme

Kwi kwi kwi

Hili neno mwamba unalitumia hapa limenikumbusha kabila moja kanda ya ziwa watu hujisifia kuwa wao ni miamba! Poor this guy ingebidi azaliwe kanda ya ziwa or samthin
 
Hapa ngoja siku ujikute uko situation room ndipo utajua .Kwa sasa huwezi kumwelewa mzee yule .Mzee yule hawezi kuzaliwa na mamvi.
 
Saravoice tumesha mpa ujumbe kwamba kama anahitaji msada tupo ama akimbie aende Chadema akamuone Halima Mdee yeye atajua ampe kazi wakili gani ampe msaada wa kisheria .Ndiyo njia pekee ya kupambana na wahalifu hawa
 
Tanzania tuna watu wengi wenye kupenda kujikweza na kutaka kuwa kama Mungu, muumba wa mbingu na Dunia.

Wako akina mungu mdogo mtakatifu Lowassa, ambao wengependa kuona watu wanaanguka hadi nchi na kusujudu.
Huko mikoani kuna miungu wengi sana ambao hujipendekeza kwa mungu lowassa.
mungu rc
mungu rpc
mungu ocd
mungu dc
mungu mp
mungu katikbu kata
mungu katibu tarafa
mungu mwenyekiti wa kijiji
mungu balozi wa nyumba 10

Halafu viko vimungu uchwara kutoka usalama wa taifa hivi vinasumbua kama nini, umbufu wao ni kama kutembea peku kwenye nyika yenye mibigili, ile miiba yenye umbo la nyota.

Kuishi wilayani na vijijini huko Tanzania ni sawa na kuishi kwenye jehanamu ndogo hasa pale ukutanapo na msuri wa hawa miungu.

Dawa yao inachemka mekoni. Siku ikifika kikombe cha ghadhabu ya maovu yao watajaziwa mara mbili na kushurutishwa kunywa ghadhabu yote.

Wewe Lowassa tutakujazia mara 3.
 
Tanzania tuna watu wengi wenye kupenda kujikweza na kutaka kuwa kama Mungu, muumba wa mbingu na Dunia.

Wako akina mungu mdogo mtakatifu Lowassa, ambao wengependa kuona watu wanaanguka hadi nchi na kusujudu.
Huko mikoani kuna miungu wengi sana ambao hujipendekeza kwa mungu lowassa.
mungu rc
mungu rpc
mungu ocd
mungu dc
mungu mp
mungu katikbu kata
mungu katibu tarafa
mungu mwenyekiti wa kijiji
mungu balozi wa nyumba 10

Halafu viko vimungu uchwara kutoka usalama wa taifa hivi vinasumbua kama nini, umbufu wao ni kama kutembea peku kwenye nyika yenye mibigili, ile miiba yenye umbo la nyota.

Kuishi wilayani na vijijini huko Tanzania ni sawa na kuishi kwenye jehanamu ndogo hasa pale ukutanapo na msuri wa hawa miungu.

Dawa yao inachemka mekoni. Siku ikifika kikombe cha ghadhabu ya maovu yao watajaziwa mara mbili na kushurutishwa kunywa ghadhabu yote.

Wewe Lowassa tutakujazia mara 3.
Madela upo wapi? Nimekukumbuka!
 
Back
Top Bottom