Afukuzwa kazi kwa kughushi mishahara 21

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,441
7,780
MFANYAKAZI wa Idara ya Fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, amefukuzwa kazi kwa madai ya kughushi nyaraka za mishahara 21, kwa lengo la kujipatia mamilioni ya fedha.

Mhasibu huyo (jina linahifadhiwa), ni miongoni mwa wafanyakazi 19 waliofukuzwa kazi na halmashauri hiyo.

Azimio la kuwaachisha kazi watumishi hao lilifikiwa juzi kwenye baraza la madiwani lililokutana katika kata ya Kinyeto, tarafa ya Ilongero wilayani Singida, baada ya awali kukaa kama kamati kisha kupitisha uamuzi huo.

Waliofukuzwa kazi ni pamoja na watumishi wawili wa idara ya afya na wengine 17 kutoka kada mbalimbali za utumishi katika halmashauri hiyo iliyogawanywa na kuanzisha halmashauri mpya ya wilaya Ikungi.

Licha ya mtumishi huyo kuhusika na wizi wa fedha zinazofikia zaidi ya Sh. milioni 25, wafanyakazi wengine walibainika kuwa na vyeti feki, utoro na uzembe kazini hali iliyolazimu baraza hilo kufikia uamuzi wa kuwaachisha kazi.

Baadhi ya madiwani wakiwamo Omari Mande na Bilali Yusufu, walipongeza hatua hiyo na kuwaonya watumishi wengine wenye mienendo isiyoridhisha katika utumishi wao kuhakikisha wanarejea kwenye msingi ili kurejesha maadili na nidhamu ya kazi.

Aidha, Diwani wa Kinyagigi, Magdalena Mangu, pamoja na kupongeza hatua hiyo, aliiomba idara ya utumishi kupeleka haraka watumishi wengine mbadala kwenye zahanati ya kijiji cha Kinyagigi baada ya wauguzi wote wawili kufukuzwa kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rashid Mandoa, aliliomba baraza hilo kuendelea kuwasimamia katika nidhamu ili kila mtumishi atekeleze majukumu yake kwa ufanisi.

Ufisadi, utoro na uzembe kazini ni kati ya sababu zinazopigwa vita na Serikali kutokana na kugharimu hasara kubwa hali ambayo imeanza kuungwa mkono na baadhi ya taasisi, kama ambavyo halmashauri ya Wilaya ya Singida imefanya.
 
Back
Top Bottom