Afrika yatokomeza ugonjwa wa polio

mkiluvya

JF-Expert Member
May 23, 2019
802
725
Hatimaye nchi za Afrika zilizo kwenye ukanda wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO kwa kanda ya Afrika zimefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Polio.

Taarifa hizo za leo ni kwa mujibu wa kamisheni huru ya kanda ya Afrika ya uthibitisho kutokomeza polio, ARCC iliyotangaza rasmi hii leo kwamba virusi vya polio havipo tena kwenye nchi hizo kwa sasa.

Tangazo la leo la kutokomeza virusi ni la pili tangu kutangazwa kutokomezwa kwa ugonjwa wa ndui miaka 40 iliyopita.

“Leo ni siku ya kihistoria kwa Afrika. ARCC inafurahia kutangaa kuwa ukanda huo wa Afrika umefanikiwa kukidhi masharti na kupatiwa cheti cha uthibitisho wa kutokomeza Polio mwitu, kwa kuwa hakuna mgojwa yeyote aliyeripotiwa katika kipindi cha miaka minne sasa,” amesema Profesa Rose Gana Fomban Leke, Mwenyekiti wa ARCC.

Katika nchi zote 54 za Afrika, nchi ambazo si wanachama wa WHO kanda ya Afrika ni Somalia, Sudan, Eritrea, Misri, Libya na Tunisia.

Nini kilifanyika?

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika iliyotolewa kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazaville imesema kuwa uamuzi wa kamisheni hiyo unafuatia mchakato wa kina na wa miongo kadhaa ukichambua ufuatiliaji wa polio, chanjo na uwezo wa maabara kupima ugonjwa huo, katika mataifa 47 wanachama wa WHO kanda ya Afrika, chambuzi ambazo zilihusisha pia ziara za uthibitisho katika kila nchi.

Mwaka 1996, wakuu wa nchi hizo za Afrika wakati wakiwa kwenye mkutano wa 32 wa uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU, huko Yaoundé, Cameroon waliazimia kutokomeza polio ugonjwa ambao wakati huo ulikuwa unasababisha watoto 75,000 kupooza kila mwaka barani Afrika.

Mwaka huo huo, Nelson Mandela, Rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini kwa usaidizi wa klabu ya Rotary walianzisha azma ya Afrika kutokomeza polio kwa kuzindua Tokomeza Polio Afrika ambapo Hayati Mandela alihamasisha nchi za Afrika na viongozi wake kuongeza juhudi za kumfikia kila mtoto na chanjo dhidi ya Polio.

Mgonjwa wa mwisho wa polio kwenye ukanda huo alibainika mwaka 2016 nchini Nigeria.

Tangu mwaka 1996, juhudi za kutokomeza Polio zimeepusha watoto milioni 1.8 kupata ugonjwa wa kupooza na kuokoa maisha ya watu 180,000.

“Hii ni historia kwa Afrika. Vizazi vijavyo vya watoto wa Afrika vitakuwa havina kabisa polio,” amesema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, akiongeza kuwa, “mafanikio haya ya kihistoria yamewezekana tu kutokana na uogozi na azma za serikali, jamii na wadau wa kutokomeza polio duniani na watu wakarimu. Natoa shukrani zangu sana kwa wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele, watoa chanjo na baadhi yao ambao hata wamepoteza maisha wakitekeleza jukumu hili muhimu.”

Hata hivyo amesema lazima kuwa macho na kuendelea na viwango vya utoaji chanjo ili kuepusha kuibuka tena kwa polio.
Mratibu wa utokomezaji wa polio kwa kanda ya WHO barani Afrika, Dkt. Pascal Mkanda amesema, “Afrika licha ya mifumo dhaifu ya afya, imeonesha, uhaba wa miundombinu, imeweza kushirikiana kwa ufanisi na kutokomeza Polio.”

Dkt. Moeti amesisitiza kuwa utaalamu uliotumika katika kutokomeza polio, utaendelea kusaidia ukanda wa Afrika kushughulikia COVID-19 na matatizo mengine ya kiafya ambayo yameghubika bara hilo wakati huu ambao hoja sasa hivi ni kuwa na huduma za afya kwa wote.

Ugonjwa wa polio husababishwa na virusi na huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kula kinyesi au mara chache kula chakula au kunywa maji yenye kinyesi.

Ingawa hakuna tiba ya polio, ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa kupatiwa chanjo na ndio maana WHO inataka juhudi zaidi ziendelezwe kuongeza kinga ya watoto kupitia chanjo.

Chanzo: Afrika yatokomeza Polio
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom