Afrika Kusini ya jana (1950s) na ya leo (2000s) kumbukumbu

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,900
30,235
AFRIKA KUSINI YA JANA (1950s) NA YA LEO (2000s)

KUMBUKUMBU…

Jana usiku nimefanya mahojiano na Salim Kikeke wa BBC Dira ya Dunia kuadhimisha Miaka 100 toka Nelson Mandela azaliwe. Katika mahojiano yale kuna picha kanipiga mpiga picha wa BBC, Dar es Salaam kijana Mtenga, inamwonyesha Nelson Mandela kulia, Barack Obama, katikati na mimi nahojiwa.

Nimeipenda sana picha hii.

Nataka msomaji nikurudishe nyuma Dar es Salaam ya mwaka wa 1957 nina umri wa miaka mitano nyumbani kwa mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed, Mtaa wa Kiungani. Mama yangu alikuwa na nakala nyingi za gazeti la DRUM.

Hili lilikuwa gazeti likichapwa Johannesburg na lilikuwa maarufu sana kwa watu weusi kwanza kwenyewe Afrika Kusini kisha nchi zote za Afrika ambako Waingereza walitawala, kama Ghana, Nigeria, Northern na Southern Rhodesia, Kenya Uganda na kwengine kwingi. Aliyekuwa ana miliki gazeti hili alikuwa Jim Bailey, Mzungu ambae alikuwa na mapenzi na watu weusi juu ya kuwa ubaguzi ulikuwa umeshamiri Afrika ya Kusini.

Allah ni muweza.

Miaka mingi baadae, sasa mimi mtu mzima nilikuja kukutana na Jim Bailey mwenyewe uso kwa uso na aiyetukutanisha ni Ally Sykes ofisini kwake. Lakini hiki ni kisa kingine In Shaa Alah siku ikipatikana fursa nitakihadithia.

Nilikuwa nikipenda kufungua gazeti hili na kuangalia picha zilizomo ndani yake kwani DRUM lilikuwa na picha nyingi katika makala zake lakini kwa kuwa mimi sikuwa najua kusoma achilia mbali kuwa lilikuwa gazeti la Kiingereza nilitosheka na kule kuangalia zile picha za Waafrika wa Johannesburg waliovalia suti na kofia za ‘’hat,’’ kichwani na wanawake waliovaa magauni marefu waliyofunga kwa mikanda mipana kiunoni na magauni kuchanua chini kama mwamvuli na wamevaa viatu virefu vya mchongoko. Sikuishia hapo bali nilichukua penseli na nikawa nawachora kwenye karatasi.

Mwaka wa 1990 nilikwenda Maputo, Msumbiji na hapa ndipo niipopata harufu ya Afrika ya Kusini.

Niliondoka na Royal Swazi hadi Mbabane, Swaziland, ndege ikatuacha hapo ikapeleka abiria wa Johannesburg kisha ikaturudia na kutuchukua hadi Maputo. Wakati niko uwanja wa ndege Mbabane chumba cha abiria wanaosubiri kuunganisha ndege nilitoa radio yangu, ‘’World Receiver,’’ miaka ile ambayo mitandao ilikuwa bado, hizi radio zilikuwa maarufu sana kwani zilikuwa zina uwezo wa kukamata stesheni nyingi sana duniani ingawa kwa ‘’Short Wave.’’

Mimi niliweka FM nikiwa pale uwanjani na kwa mshangao mkubwa stesheni iiyoingia kwa haraka ilikuwa Radio Bloemfontein, Afrika Kusini, mtangazaji akitangaza kwa Kiingereza mambo kadhaa kisha akaweka muziki na nyimbo aliyoweka ilikuwa ya Nat King Cole, mwimbaji mahiri mweusi kutoka Marekani aliyefariki kwa saratani ya koo mwaka wa 1965.

Hili lilinishangaza sana kwani nikijua Afrika ya Kusini ni wabaguzi wa kutupwa iweje leo wapige muziki wa mtu mweusi? Hapa ndipo ulipoanza mshangao wangu na labda niseme pia uhusiano wangu wa kutaka kuijua Afrika Kusini kwa undani.

Nilishangaa nilipokuwa Maputo nilipokwenda benki siku ya pili kuvunja Thomas Cooke Travelers Cheque nikitegemea kupewa Dola za Kimarekani badala yake nikaambiwa kuwa Msumbiji watu wanalipwa Rand za Afrika ya Kusini. Tanzania ya miaka ile dola ilikuwa inaogopewa ukiwanayo na ikiwa umeipata kienyeji lazima uifiche kwa kuwa ikiwa utakamatwa una dola hata ikiwa ni dola moja kesi yake ni mbaya sana. Sasa ukiwa na dola ulikuwa wewe bwana.

Rand nilikuwa nazivunja mtaani napata Meticais, fedha za Msumbiji. Inabidi uwe na mfuko wa kutosha kubebea hizo fedha kwani fedha utakazopata kwa kuvunja dola mia moja ulikuwa mzigo wa haja.

Ajabu haikuishia kwenye fedha na nilipokwenda madukani bidhaa nyingi sana zilizokuwa zinauzwa zilikuwa zinatoka Afrika ya Kusini na zikiuzwa waziwazi bila kificho ilhali Afrika Kusini kwa ajili ya siasa zake za kibaguzi wakati ule ilikuwa imepigwa, ‘’trade embargo,’’ haifanyi biashara na nchi nyingi achilia mabali nchi za Afrika ambazo ziliichukulia nchi hiyo kama adui mkubwa sana.

Kuwa Msumbiji inafanya biashara na Makaburu kwangu mimi hili lilifurtu ada.

Haya hakika yalinishangaza sana kwani nilikuwa najua vipi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anapiga kelele dunia nzima kuhusu kuigomea Afrika ya Kusini. Sasa kufika Msumbiji na kukuta hali hii ajabu yangu haikuwa ndogo.

Kila siku nikawa napita Super Market iliyokuwa jirani na hoteli yangu kununua vitu viwili, gazeti la Johannesburg Star na zabibu zisizokuwa na mbegu vyote kutoka Afrika Kusini.

Nikifika hotelini baada ya kujinadhifisha na kubadili nguo nafungua radio yangu kusikiliza FM Stesheni, nyingi kutoka Johannesburg huku nikitumbukiza zabibu moja moja mdomoni.

Katika safari hii wakati narejea Dar es Salaam nilivunja safari Mbabane nilipotua na ndege nikaenda Manzini kwa siku chache kupumzika. Wenyeji waliniambia hakuna basi linaokwenda Manzini usafiri ni wa teksi.

Yale niliyoyaona Maputo nikayakuta Manzini lakini angalau kuna baadhi ya vitu walikuwa wanaficha wanakuonyesha sampuli ukipenda mnakwenda nyuma ya duka kwenye ghala anakuuzia kwa kificho kama vile mnauziana bangi. Hivi ndivyo nilivyonunua TV yangu ya kwanza ya ukubwa wa nchi 11 na video player, siku hizo hivi vitu adimu sana Tanzania.

Sina haja ya kueleza shida iliyonikuta kuvikomboa Customs, Dar es Salaam. Ilikuwa kama vile wananiambia ukome kuleta vitu kama hivi Tanzania.

Baada ya miaka kumi kupita mwaka wa 2000 nilikwenda Afrika Kusini nikitokea Mbabane.

Nikiwa ndani ya ndege nikitokea Dar es Salaam niliingia katika mazungumzo na Mzungu mmoja tuliokuwa tumekaa pamoja. Akanambia kuwa anatoka Serengeti na yeye ni mkazi wa Johannesburg. Nikamwambia kuwa mimi nikimaliza shughuli zangu Mbabane nategemea kwenda Johannesburg.

Yule bwana akaniuliza nakwenda Johannesburg kufanya nini? Nikamwambia sijapata kufika na ningependa kwenda kuona mji. Yule bwana akacheka akaniuliza kama nimepata kusafiri na kipi cha kuona Johannesburg. Ile saruji nzito katika majengo marefu ya mjini? Maneno aliyosema yalikuwa, ‘’Heavy concrete buildings?’’ Akanishauri kuwa nisipoteze fursa ya kuona mandhari nzuri ya Afrika Kusini, ikiwa nitakwenda Johannesburg nipande mabasi madogo yanayoitwa, ‘’Kubi,’’ nipite Kwa Zulu Natal hadi Durban kisha niende Johannesburg.’’

Hakika ulikuwa ushauri mzuri sana kwangu.

Basi katika mazungumzo na huyo jamaa niliyejenganae urafiki ndani ya ndege nikamwambia kuwa nakwenda Johannesburg pia nimpitie rafiki yangu mmoja anaitwa Jim Bailey. Jamaa alishtuka akakunja kidogo kipaji cha uso wake akaniuiza nimemjuaje Jim Bailey.

Nilimfahamisha kuwa ni rafiki ya baba yangu (nikiwa na maana ya Ally Sykes) na tulifanya kazi moja pamoja Dar es Salaam. Huyu rafiki yangu akanipa pole akanambia, ‘’Jim Bailey mimi ni jirani yangu na tumemzika mwezi uliopita.’’ Jim Bailey ni mtu muhimu sana katika historia ya Afrika ya Kusini kiasi imetengenezwa senema ya maisha yake na imepewa jina la gazeti lake, DRUM.

Hakika dunia ni ndogo sana na Allah ana njia nyingi za kutushangaza ikiwa utazingatia.

Nikiwa Johannesburg nikitembea katika mitaa yake nilileta hisia za picha nilizokuwa naziangalia za Johannesburg katika gazeti la DRUM nikiwa mtoto mdogo nakua katika mitaa ya Gerezani, Dar es Salaam, lakini sikuona zile suti za miaka ya 1950 ndani ya DRUM, badala yake niliona, ‘’jeans,’’ nyingi kwa wanaune na wanawake.

Picha nyingine niliyokuwa nayo ya Johannesburg ni ile niliyoiona katika senema, ‘’Cry the Beloved Country,’’ Black and White ya miaka ya 1950 aliyocheza Sidney Poitier. Hiki kitabu kiliandikwa na Allan Paton na ni moja ya vitabu mashuhuri duniani kwa nyakati zote. Mwandishi katika njia ya hadithi kaeleza jinsi ubaguzi unavyoweza kuvuruga na kuangamiza maisha ya watu- dhalimu na yule anaedhulumiwa.

Johannesburg niliyoikuta haikuwa na tofauti na miji niliyokuwa nimeizoea Uingereza. Hata katika maduka ya kuuza muziki sikusikia muziki ambao nilikuwa ninaujua kuwa ni muziki wa Afrika Kusini. Miziki niliyosikia ya Afrika Kusini ilikuwa na tofauti ndogo sana na midundo niliyokuwa nasikia Uingereza.

Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa hodari sana wa kupiga filimbi na nikiiga nyimbo nyingi za muziki wa Kwela ambao bingwa wake alikuwa Spokes Mashiyane kutoka Afrika Kusini na muziki huu ulikuwa mashuhuri pia Tanganyika na nyimbo zake zikipigwa sana Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) katika miaka ya 1950 hadi 1960 pamoja na ‘’Jive,’’ mtindo maarufu wa dansi kutoka Afrika Kusini.

Miaka mingi ilikuwa imepita Johannesburg ya 1957 niliyokuwa naiangalia katika kurasa za DRUM ilikuwa tofauti na ile niliyokuwa naikanyaga kwa miguu yangu.

Nikarudi tena Afrika Kusini mwaka wa 2006 na safari hii nilifika hadi Cape Town na kutembelea, Soweto na Robben Island na kuangalia kwa jicho langu kizimba alichofungwa Nelson Mandela ambae jana BBC walinihoji na nikamzungumza.

Mahojiano yale ya BBC na hiyo picha hapo juu yanenirudisha mbali sana.

Mohamed Said
19 July, 2018
 
Attachments

  • upload_2018-7-19_9-32-1.png
    upload_2018-7-19_9-32-1.png
    163.4 KB · Views: 136
Ahsante mkuu Mohamed Said kwa uzi huu murua kabisa..! Lakini hujatwambia kuhusu maoni yako ya hali ya kisiasa na uchumi ya watu weusi wa kipindi kile na sasa... lakini pia maoni yako kuhusu kupandishwa thamani kwa Nelson Mandela na wazungu wakati Nyerere akionekana wa kawaida ambapo kiukweli kazi ya kuipa uhuru afrika ilifanywa zaidi na Nyerere kuliko Mandela.
 
Ubavu,
Mimi kusudio langu lilikuwa ni kuleta kumbukumbu zangu.
Ikiwa unataka kujua hali ya siasa za Afrika ya Kusini ndiyo
tayari mada ushaifungua naamini watu watachangia.
 
Kadri unavyoijongelea Afrika ya Kusini, ndivyo utakavyogundua jinsi nchi zinazoizunguka zilivyo na utegemezi kwa Afrika ya Kusini. Nchi zinazopakana na Afrika ya Kusini zinaitegemea sana, hasa kwenye bidhaa za viwandani na kilimo. Zambia wakati wa miaka ya vita vya ukombozi walijitahidi sana kuzuia bidhaa za Afrika ya Kusini lakini ilikuwa ni taaabu sana kudhibiti uingizwaji wake.
Tatizo lillilopo Afrika ya Kusini ni siasa zisizo na muelekeo wa kuwakwamua waafrika ili kukipata kile walichokipigania. Hivi sasa viongozi wa ANC ni kama waigizaji. Hebu angalia Zuma alichokifanya, ni aibu! Lakini Zuma anaakisi ubinafsi wa viongozi tulionao katika bara la Afrika.
 
Ahsante sana kwa mada nzuri iliyoielezea experience yako katika kutembelea nchi mbalimbali hasa hizi za SADC,SIASA ya SA imepindishwa mno na wanasiasa wetu kwa faida moja au nyingine ni ukweli usiopingika kuwa pressure iliyowekwa na Baba wetu wa Taifa akishirikiana na viongozi wengine ilisaidia kuondolewa kwa siasa ya kibaguzi hapo SA,ILA hii ilikuwa sehemu ndogo tu ya juhudi zote,ukomo wa siasa hii ya kibaguzi ulichangiwa zaidi na msukumo ndani ya nchi yenyewe hasa baada ya maandamano ya wanafunzi kupinga kutumika kwa lugha ya Africaans katika masomo yao(1976),pia msukumo mkubwa uliletwa na mkusanyiko chini ya UDF ambao ndio walichangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya kisiasa ndani ya SA,Uchumi wa SA uliyumba sana miaka ya 1980s ukawa dhaifu na pressure kubwa kutoka mataifa ya Ulaya na USA,tuelewe kuwa hakuna popote ambapo jeshi la makaburu lilipambana uso kwa uso na wapigania uhuru(katika medani hii ya kivita hakuna nchi yeyote kusini wa Africa ambayo ilikuwa na uwezo wa kusimama kivita na jeshi hili)yaliyotokea Angola its a debate of another day ila elewa CUBA na URUSI hawakushinda ile vita ni propaganda tu tulizolishwa kuhusu real what happened katika medani ya kivita pale;always time na history ni mwalimu mkweli.
 
nilipoona avatar yako nikaenda kuingalia hadithi maana ww hakika ni gwiji wa kusimulia,isitoshe wakati salimu anakuhoji nilikuwa niko mbele ya tv yangu nilishuhudia majibu yako mjarabu kulingana na maswali uliyoulizwa,hongera sana bw mkubwa.
 
AFRIKA KUSINI YA JANA (1950s) NA YA LEO (2000s)

KUMBUKUMBU…

Jana usiku nimefanya mahojiano na Salim Kikeke wa BBC Dira ya Dunia kuadhimisha Miaka 100 toka Nelson Mandela azaliwe. Katika mahojiano yale kuna picha kanipiga mpiga picha wa BBC, Dar es Salaam kijana Mtenga, inamwonyesha Nelson Mandela kulia, Barack Obama, katikati na mimi nahojiwa.

Nimeipenda sana picha hii.

Nataka msomaji nikurudishe nyuma Dar es Salaam ya mwaka wa 1957 nina umri wa miaka mitano nyumbani kwa mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed, Mtaa wa Kiungani. Mama yangu alikuwa na nakala nyingi za gazeti la DRUM.

Hili lilikuwa gazeti likichapwa Johannesburg na lilikuwa maarufu sana kwa watu weusi kwanza kwenyewe Afrika Kusini kisha nchi zote za Afrika ambako Waingereza walitawala, kama Ghana, Nigeria, Northern na Southern Rhodesia, Kenya Uganda na kwengine kwingi. Aliyekuwa ana miliki gazeti hili alikuwa Jim Bailey, Mzungu ambae alikuwa na mapenzi na watu weusi juu ya kuwa ubaguzi ulikuwa umeshamiri Afrika ya Kusini.

Allah ni muweza.

Miaka mingi baadae, sasa mimi mtu mzima nilikuja kukutana na Jim Bailey mwenyewe uso kwa uso na aiyetukutanisha ni Ally Sykes ofisini kwake. Lakini hiki ni kisa kingine In Shaa Alah siku ikipatikana fursa nitakihadithia.

Nilikuwa nikipenda kufungua gazeti hili na kuangalia picha zilizomo ndani yake kwani DRUM lilikuwa na picha nyingi katika makala zake lakini kwa kuwa mimi sikuwa najua kusoma achilia mbali kuwa lilikuwa gazeti la Kiingereza nilitosheka na kule kuangalia zile picha za Waafrika wa Johannesburg waliovalia suti na kofia za ‘’hat,’’ kichwani na wanawake waliovaa magauni marefu waliyofunga kwa mikanda mipana kiunoni na magauni kuchanua chini kama mwamvuli na wamevaa viatu virefu vya mchongoko. Sikuishia hapo bali nilichukua penseli na nikawa nawachora kwenye karatasi.

Mwaka wa 1990 nilikwenda Maputo, Msumbiji na hapa ndipo niipopata harufu ya Afrika ya Kusini.

Niliondoka na Royal Swazi hadi Mbabane, Swaziland, ndege ikatuacha hapo ikapeleka abiria wa Johannesburg kisha ikaturudia na kutuchukua hadi Maputo. Wakati niko uwanja wa ndege Mbabane chumba cha abiria wanaosubiri kuunganisha ndege nilitoa radio yangu, ‘’World Receiver,’’ miaka ile ambayo mitandao ilikuwa bado, hizi radio zilikuwa maarufu sana kwani zilikuwa zina uwezo wa kukamata stesheni nyingi sana duniani ingawa kwa ‘’Short Wave.’’

Mimi niliweka FM nikiwa pale uwanjani na kwa mshangao mkubwa stesheni iiyoingia kwa haraka ilikuwa Radio Bloemfontein, Afrika Kusini, mtangazaji akitangaza kwa Kiingereza mambo kadhaa kisha akaweka muziki na nyimbo aliyoweka ilikuwa ya Nat King Cole, mwimbaji mahiri mweusi kutoka Marekani aliyefariki kwa saratani ya koo mwaka wa 1965.

Hili lilinishangaza sana kwani nikijua Afrika ya Kusini ni wabaguzi wa kutupwa iweje leo wapige muziki wa mtu mweusi? Hapa ndipo ulipoanza mshangao wangu na labda niseme pia uhusiano wangu wa kutaka kuijua Afrika Kusini kwa undani.

Nilishangaa nilipokuwa Maputo nilipokwenda benki siku ya pili kuvunja Thomas Cooke Travelers Cheque nikitegemea kupewa Dola za Kimarekani badala yake nikaambiwa kuwa Msumbiji watu wanalipwa Rand za Afrika ya Kusini. Tanzania ya miaka ile dola ilikuwa inaogopewa ukiwanayo na ikiwa umeipata kienyeji lazima uifiche kwa kuwa ikiwa utakamatwa una dola hata ikiwa ni dola moja kesi yake ni mbaya sana. Sasa ukiwa na dola ulikuwa wewe bwana.

Rand nilikuwa nazivunja mtaani napata Meticais, fedha za Msumbiji. Inabidi uwe na mfuko wa kutosha kubebea hizo fedha kwani fedha utakazopata kwa kuvunja dola mia moja ulikuwa mzigo wa haja.

Ajabu haikuishia kwenye fedha na nilipokwenda madukani bidhaa nyingi sana zilizokuwa zinauzwa zilikuwa zinatoka Afrika ya Kusini na zikiuzwa waziwazi bila kificho ilhali Afrika Kusini kwa ajili ya siasa zake za kibaguzi wakati ule ilikuwa imepigwa, ‘’trade embargo,’’ haifanyi biashara na nchi nyingi achilia mabali nchi za Afrika ambazo ziliichukulia nchi hiyo kama adui mkubwa sana.

Kuwa Msumbiji inafanya biashara na Makaburu kwangu mimi hili lilifurtu ada.

Haya hakika yalinishangaza sana kwani nilikuwa najua vipi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anapiga kelele dunia nzima kuhusu kuigomea Afrika ya Kusini. Sasa kufika Msumbiji na kukuta hali hii ajabu yangu haikuwa ndogo.

Kila siku nikawa napita Super Market iliyokuwa jirani na hoteli yangu kununua vitu viwili, gazeti la Johannesburg Star na zabibu zisizokuwa na mbegu vyote kutoka Afrika Kusini.

Nikifika hotelini baada ya kujinadhifisha na kubadili nguo nafungua radio yangu kusikiliza FM Stesheni, nyingi kutoka Johannesburg huku nikitumbukiza zabibu moja moja mdomoni.

Katika safari hii wakati narejea Dar es Salaam nilivunja safari Mbabane nilipotua na ndege nikaenda Manzini kwa siku chache kupumzika. Wenyeji waliniambia hakuna basi linaokwenda Manzini usafiri ni wa teksi.

Yale niliyoyaona Maputo nikayakuta Manzini lakini angalau kuna baadhi ya vitu walikuwa wanaficha wanakuonyesha sampuli ukipenda mnakwenda nyuma ya duka kwenye ghala anakuuzia kwa kificho kama vile mnauziana bangi. Hivi ndivyo nilivyonunua TV yangu ya kwanza ya ukubwa wa nchi 11 na video player, siku hizo hivi vitu adimu sana Tanzania.

Sina haja ya kueleza shida iliyonikuta kuvikomboa Customs, Dar es Salaam. Ilikuwa kama vile wananiambia ukome kuleta vitu kama hivi Tanzania.

Baada ya miaka kumi kupita mwaka wa 2000 nilikwenda Afrika Kusini nikitokea Mbabane.

Nikiwa ndani ya ndege nikitokea Dar es Salaam niliingia katika mazungumzo na Mzungu mmoja tuliokuwa tumekaa pamoja. Akanambia kuwa anatoka Serengeti na yeye ni mkazi wa Johannesburg. Nikamwambia kuwa mimi nikimaliza shughuli zangu Mbabane nategemea kwenda Johannesburg.

Yule bwana akaniuliza nakwenda Johannesburg kufanya nini? Nikamwambia sijapata kufika na ningependa kwenda kuona mji. Yule bwana akacheka akaniuliza kama nimepata kusafiri na kipi cha kuona Johannesburg. Ile saruji nzito katika majengo marefu ya mjini? Maneno aliyosema yalikuwa, ‘’Heavy concrete buildings?’’ Akanishauri kuwa nisipoteze fursa ya kuona mandhari nzuri ya Afrika Kusini, ikiwa nitakwenda Johannesburg nipande mabasi madogo yanayoitwa, ‘’Kubi,’’ nipite Kwa Zulu Natal hadi Durban kisha niende Johannesburg.’’

Hakika ulikuwa ushauri mzuri sana kwangu.

Basi katika mazungumzo na huyo jamaa niliyejenganae urafiki ndani ya ndege nikamwambia kuwa nakwenda Johannesburg pia nimpitie rafiki yangu mmoja anaitwa Jim Bailey. Jamaa alishtuka akakunja kidogo kipaji cha uso wake akaniuiza nimemjuaje Jim Bailey.

Nilimfahamisha kuwa ni rafiki ya baba yangu (nikiwa na maana ya Ally Sykes) na tulifanya kazi moja pamoja Dar es Salaam. Huyu rafiki yangu akanipa pole akanambia, ‘’Jim Bailey mimi ni jirani yangu na tumemzika mwezi uliopita.’’ Jim Bailey ni mtu muhimu sana katika historia ya Afrika ya Kusini kiasi imetengenezwa senema ya maisha yake na imepewa jina la gazeti lake, DRUM.

Hakika dunia ni ndogo sana na Allah ana njia nyingi za kutushangaza ikiwa utazingatia.

Nikiwa Johannesburg nikitembea katika mitaa yake nilileta hisia za picha nilizokuwa naziangalia za Johannesburg katika gazeti la DRUM nikiwa mtoto mdogo nakua katika mitaa ya Gerezani, Dar es Salaam, lakini sikuona zile suti za miaka ya 1950 ndani ya DRUM, badala yake niliona, ‘’jeans,’’ nyingi kwa wanaune na wanawake.

Picha nyingine niliyokuwa nayo ya Johannesburg ni ile niliyoiona katika senema, ‘’Cry the Beloved Country,’’ Black and White ya miaka ya 1950 aliyocheza Sidney Poitier. Hiki kitabu kiliandikwa na Allan Paton na ni moja ya vitabu mashuhuri duniani kwa nyakati zote. Mwandishi katika njia ya hadithi kaeleza jinsi ubaguzi unavyoweza kuvuruga na kuangamiza maisha ya watu- dhalimu na yule anaedhulumiwa.

Johannesburg niliyoikuta haikuwa na tofauti na miji niliyokuwa nimeizoea Uingereza. Hata katika maduka ya kuuza muziki sikusikia muziki ambao nilikuwa ninaujua kuwa ni muziki wa Afrika Kusini. Miziki niliyosikia ya Afrika Kusini ilikuwa na tofauti ndogo sana na midundo niliyokuwa nasikia Uingereza.

Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa hodari sana wa kupiga filimbi na nikiiga nyimbo nyingi za muziki wa Kwela ambao bingwa wake alikuwa Spokes Mashiyane kutoka Afrika Kusini na muziki huu ulikuwa mashuhuri pia Tanganyika na nyimbo zake zikipigwa sana Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) katika miaka ya 1950 hadi 1960 pamoja na ‘’Jive,’’ mtindo maarufu wa dansi kutoka Afrika Kusini.

Miaka mingi ilikuwa imepita Johannesburg ya 1957 niliyokuwa naiangalia katika kurasa za DRUM ilikuwa tofauti na ile niliyokuwa naikanyaga kwa miguu yangu.

Nikarudi tena Afrika Kusini mwaka wa 2006 na safari hii nilifika hadi Cape Town na kutembelea, Soweto na Robben Island na kuangalia kwa jicho langu kizimba alichofungwa Nelson Mandela ambae jana BBC walinihoji na nikamzungumza.

Mahojiana yale ya BBC na hiyo picha hapo juu yanenirudisha mbali sana.

Mohamed Said
19 July, 2018
Maandishi murua sana haya mkuu.. Muhimu watu wayasome na kuyatafakari.

Nimefurahia!
 
nilipoona avatar yako nikaenda kuingalia hadithi maana ww hakika ni gwiji wa kusimulia,isitoshe wakati salimu anakuhoji nilikuwa niko mbele ya tv yangu nilishuhudia majibu yako mjarabu kulingana na maswali uliyoulizwa,hongera sana bw mkubwa.
Nnangale,
Ahsante ndugu yangu.
 
Mzee huwa ninazipenda makala zako. Asante sana na nimejifunza jambo. Umenikumbusha radio yangu ya kwanza ya kupandisha eria niloinunua 1996. Nilikuwa mzuri kwenye kuandika na nilishinda mashindano ya uandishi wa insha, ila siku hizi nimekifukia kipaji hiki. Nikiona waandishi wazuri kama wewe nafarijika haswa!

Asante.
 
Jumong,
Rudia kuandika tukusome.
 
Back
Top Bottom