Adui wa Kikwete si Karume

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
129
“SASA imedhihirika kwamba jamaa huyu hawezi kushughulikia lolote; na hawezi kupambana na mikikimikiki. Anaweza tu kuzunguka huku na kule, akisukumwa na kuelekezwa kama kipofu.


“Ndivyo alivyojishughulisha na mwafaka wa Kibaki na Odinga...Ukimwacha tu aende peke yake mitaani, ndio anagongwa na magari (Richmond), pikipiki (dili za madini)... sasa zikija FUSO zilizojaa mizigo; au mabasi yanayokimbiza si ndio atakufa kabisa!...Amejiweka katika kona mbaya, sijui kama CUF watamuachia...Ngoja tuone.”

Nukuu hiyo hapo juu imetoka kwa Mtanzania mmoja akichambua hatima ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM vilivyofanyika Butiama wiki iliyopita, kwa kushindwa kufanya maamuzi mazito kama ilivyotarajiwa, hasa kwa kukataa kubariki utekelezaji wa mwafaka kati ya CCM na CUF.

Kama nilivyoandika Jumapili iliyopita, kwamba hakuna kubwa lililokuwa linatarajiwa kutoka Butiama kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, wajumbe wa vikao hivyo, wamethibitisha hilo. Walibishana sana vikaoni, lakini walishindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi wa EPA na Richmond; na walishindwa kubariki makubaliano yao na CUF juu ya mwafaka wa Zanzibar.

Washindi wa ubishi huo ni wengi, lakini hapa nitamtaja mmoja tu – Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Amemshinda kaka yake na rafiki yake, Rais wa Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete.

Zipo hoja mbili. Ya kwanza inasema Karume na Kikwete wako kundi moja kuhusu hatima ya Zanzibar, na kwamba wanapingana na wahafidhina ndani ya chama wasiopenda kuona mgogoro wa Zanzibar ukimalizika. Ya pili inasema Karume na Kikwete si wamoja, na kwamba Karume ni mhafidhina anayepambana na nguvu za Kikwete za kutaka kuibadili Zanzibar.

Hoja ya kwanza inatumiwa na watetezi wa Kikwete na Karume. Wanataka tuendelee kuwaona kuwa wana msimamo mmoja, na nia njema ya kuijenga na kuibadilisha Tanzania, na kwamba wanakwamishwa na wasaidizi wao.

Hoja ya pili inatumiwa na wale wanaomuona Karume kama kikwazo cha mwafaka, na hawataki Kikwete aonekane dhaifu katika hili.

Lakini ipo hoja ya tatu inayounganisha hizo mbili. Hii inasema kwamba wawili hawa lao ni moja, na kwamba nia yao ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar ni ile ile, kwamba isiwe kabla ya 2010. Sababu? Wote ni wahafidhina, na wanataka mambo haya yatekelezwe baada ya Karume kumaliza kipindi chake cha urais.

Ni suala la historia au urafiki wao, ambalo linafunika uzalendo wao kwa taifa. Tangu awali tulijua kwamba Rais Karume ni mmoja wa wahafidhina ndani ya CCM; watu wasiotaka kuona mabadiliko ya utawala wa kisiasa. Karume alirithi mgogoro wa kisiasa Zanzibar kutoka kwa watangulizi wake. Kama asingekuwa mhafidhina, angekuwa ameumaliza. Badala yake ameukuza, tena kwa damu ya Wazanzibari wenzake waliompinga.

Kamati ya mwafaka inayojadiliwa sasa iliundwa baada ya mgogoro uliotokana na ushindi wenye utata aliopewa mwaka 2005, akatangazwa na kuapishwa haraka haraka. Karume haoni kwamba nje ya CCM kuna mema wanayostahili Wazanzibari, na kwamba ndani ya CCM yapo baadhi ya mabaya wasiyostahili Wazanzibari.

Kwa sababu hiyo, Zanzibar inaendelea kukwama. Na kwa kinywa chake mwenyewe, Karume amekiri kwamba siasa za vyama vingi ‘zimekwamisha maendeleo ya Zanzibar.’ Hii ni kauli ya kihafidhina. Kwa hiyo, wanaotaka kumwondoa Karume kutoka kundi la wahafidhina ni wahafidhina wale wale katika kundi jipya linalomuunga mkono.

Vinginevyo, wangemwambia ukweli kwamba ametumia vibaya imani waliyompatia wakidhani si mhafidhina kama waliomtangulia. Hata kama aliingia kwa wizi wa kura, bado angeweza kujitofautisha na wahafidhina na kujenga misingi mipya.

Ndivyo alivyofanya Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi. Aliingia madarakani kwa kubebwa na watangulizi wake; alipofika Ikulu akasema: ‘Sitaki ushirika na wezi wa kura!’ Akaunda chama chake na kujitenga nao. Wananchi wale wale waliokuwa wanamkataa kwa sababu ya Bakili Muluzi (mtangulizi wake, ambaye walimuona fisadi mkuu), wakamuunga mkono hadi leo.

Bado kuna magumu yanamsibu, lakini dhamira yake imeonekana katika vitendo. Hawa wenzetu wanasema wana dhamira, lakini zinabaki katika hotuba. Hata inapopatikana fursa ya kutenda – kama hii ya mwafaka – hawajui namna ya kuitumia.

Kwa hiyo, wale wanaotambua uhafidhina wa Karume, walikuwa na matumaini na Rais Kikwete (kwani, kwa baadhi yao, naye alidhaniwa si mhafidhina). Kabla ya udhaifu wa Rais Kikwete kuanza kudhihirika, pale alipolihutubia taifa kupitia bungeni Dodoma mwaka 2005, akasema kwa mbwembwe kuhusu dhamira yake ya kutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar, walidhani sasa ameamua kupambana na kukomesha ubabe wa Karume na wahafidhina wenzake.

Walioitilia shaka kauli ya Kikwete walikuwa wachache, lakini walizingatia historia ya mgogoro wenyewe, harakati zilizokwisha fanyika zikagonga mwamba, hulka za watawala wa sasa wa Zanzibar; na uwezo na nia halisi ya Rais Kikwete.

Yote hayo yangemsaidia au kumkwamisha, lakini zaidi uwezo wake na nia yake. Waliomtilia shaka walizingatia mambo kadhaa. Kwanza, walijua kuwa Rais Kikwete hawezi kufanya lolote ambalo Rais Karume hataki. Walijua urafiki wao utaathiri nia ya Kikwete.

Wamekuwa na urafiki wa kikazi ambao ulijengwa katika ushindani dhidi ya kizazi kilichowatangulia cha kina Dk. Salmin Amour, Dk. Mohammed Gharib Bilal, John Malecela, Dk. Salim Ahmed Salim, Benjamin Mkapa na wenzao.

Kwa miaka 10 na ushehe ya utafutaji wa Kikwete na Karume, kundi lao lilijulikana kama kundi la ‘vijana’ ndani ya CCM. Walijitambulisha kama watu wanaopingana na wahafidhina wasiopenda mabadiliko. Walitaka kusisitiza, na waliweza, kwamba zamu yao ya kushika usukani wa nchi imewadia; wazee wapumzike.

Wakafanya mikakati, na wakafanikiwa, kupenyezana katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, na ilipofika zamu ya uteuzi wa mgombea urais wa Zanzibar, kundi la Kikwete lilitumia nguvu zote kuwashinda ‘wahafidhina’.

Nguvu yao iliweza kushinda hata hoja iliyotumiwa na wazee hao kwamba Karume hajasoma shule (alikuwa anashindana na Dk. Bilal mwenye shahada ya uzamivu); kina Kikwete wakasema uzoefu wake katika serikali unatosha kuwa ‘digrii’ ya kuwaongoza Wazanzibari kueleka Zanzibar mpya.

Miaka mitano ya awali ya uongozi wa Rais Karume ilidhihirisha kwamba hakuwa tofauti na hao wahafidhina, isipokuwa alikuwa mhafidhina kwenye kundi jipya.

Pili, waliotilia shaka kauli ya Kikwete walizingatia ukweli kwamba hayupo tayari kugusa jambo ambalo litamrudia yeye na kumnyima fursa ya kuwania tena kiti hicho mwaka 2010. Kukosana na Karume ni kujitafutia washindani wapya walio karibu naye. Na kwa kuwa Karume hatarajiwi kugombea urais mwaka 2010, Kikwete anamhitaji zaidi Karume kuliko Karume anavyomhitaji Kikwete sasa.

Kwa hiyo, walijua kwamba Kikwete ni bingwa wa kuahirisha masuala. Hata hili litasubiri hadi ngwe ya pili ya utawala wake, ili lisimdhuru rafiki yake, na lisimdhuru yeye mwenyewe, maana naye hatarajiwi kugombea urais baada ya mwaka 2010.

Tayari Karume amekwishalipa fadhila ya kwanza kwa Kikwete ilipofika zamu ya kugombea urais wa Tanzania. Ni kujidanganya leo kudhani kwamba Kikwete ameingia kupambana na wahafidhina. Ile dhana kwamba yeye ni ‘mpinzani ndani ya CCM’ ilikuwa hoja ya kupatia kura kutoka kwa wapinzani wa wakongwe ndani ya CCM.

Ndiyo maana sasa wanagawanyika baada ya kugundua Kikwete huyo huyo anawategemea wakongwe kufanya yale yale aliyokuwa anayapinga kabla hajawa rais na mwenyekiti.

Wanaoendelea kudhani kwamba Kikwete si mhafidhina, ndiyo wanazungumzia ‘ndoto yake’ juu ya Zanzibar. Lakini wanaojua uhusiano wa Kikwete, Karume, Edward Lowassa na wengine, wamekuwa wakionya juu ya nchi kutawaliwa na marafiki.

Na sasa katika mazingira ambayo Lowassa ameshaondoka katika utawala wa nchi, si rahisi kwa Kikwete kupoteza wote katika muda mfupi hivyo. Miaka miwili ya utawala wa Kikwete, imedhihirisha kwamba naye hawezi kuwa Bingu wa Mutharika.

Kama ‘ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya’ vimeshindwa kuleta lolote jipya katika miaka miwili ya awali, chochote kitakachokuja katika miaka mitatu ijayo hakiwezi kufananishwa na uwezo aliodaiwa anao.

Na kwa katiba tuliyo nayo, rais ana madaraka makubwa ya kufanya atakalo – baya na zuri. Kama Kikwete ameshindwa kutumia fursa hiyo hadi wananchi wakaamka na kuanza kumzomea, ni ushahidi kwamba amekumbatia uhafidhina ule ule, ambao wananchi walidhani angeupiga vita.

Kwa hiyo, katika masuala ya msingi ya utawala wa nchi, Kikwete hana jipya; na kuhusu Zanzibar, lao ni moja. Ni kweli, ukimsikiliza Kikwete utaona kuwa anayo dhamira safi, maana anazungumza mambo ambayo Karume hawezi kuyasema.

Lakini kinachogomba ni uwezo wake wa kuiweka dhamira hiyo katika vitendo. Ana woga wa kisiasa ndani mwake. Na Karume ni mmoja wa wanaojua udhaifu huo wa Kikwete. Ndiyo maana ametumia vema vikao vya Butiama kugeuza hoja.

Kikwete angependa mwafaka wa CCM na CUF utekelezwe hata leo. Lakini anaogopa kukosana na Karume. Bado anamlilia Lowassa, hayupo tayari kujiingiza katika mtego ambao utamfanya akose hata imani ya Karume.

Nguvu ya Kikwete kufanya uamuzi na kuchukua hatua kali inaweza kuonekana baada ya mwaka 2010, kama atakuwa amepita na kuwa rais tena. Kwa hiyo, jambo hili halisogezwi mbele kwa bahati mbaya. Ni mkakati wa kuwalinda Karume na Kikwete na kuwatesa Wazanzibari.

Ni mkakati wa kihafidhina unaokuza urafiki na kupuuza uzalendo. Ni kumbukumbu ya aibu kwa Rais Kikwete, ambaye kwa wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alionekana katika vimulimuli vya shamrashamra za mwafaka wa mahasimu wa kisiasa nchini Kenya, wiki chache zilizopita.

Tusubiri ya Zimbabwe; Kikwete anaweza kwenda kusuluhisha ZANU-PF na MDC, bila kulazimisha kura ya maoni kama ambavyo chama chake kinataka ifanyike Zanzibar.

Na hiki ndicho kielelezo cha utovu wa busara ya kawaida, ambayo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ameizungumzia – kwamba ndiyo ilitumika kudai kura ya maoni!

Kwanza, wote tunajua fika kwamba Wazanzibar hao ndio waliopiga kura zilizosababisha mgogoro huo. Pili, tunajua kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni sehemu ya mgogoro huo. Inakuwaje busara za kawaida za viongozi wa CCM haziwawezeshi kuona kwamba kura ya maoni wanayotaka ni njia ya kufumua upya mgogoro huo?

Lakini lipo suala la pili, tunapojadili njama za Karume na Kikwete kuhusu mgogoro wa Zanzibar. Karume ni makamu wa pili wa mwenyekiti wa CCM. Naamini kwamba viongozi wakuu wanakutana kabla ya vikao, na wanakuwa na ajenda za vikao, na wanakuwa na mwelekeo au msimamo wa pamoja katika masuala mazito kama haya – huko wanakotaka kuwaongoza na kuwapeleka wajumbe wao.

Sitaki kuamini kwamba katika hili – tena lililo nyeti hivi – Karume na Kikwete hawakuteta kabla ya kulifikisha kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Maana haiwezekani kwamba Katibu Mkuu Yusuph Makamba alipeleka ajenda kwenye kamati bila kushauriana na mwenyekiti wake.

Sidhani kama Kikwete alishtukizwa tu na hoja za Karume kupinga utekelezaji wa mwafaka. Vinginevyo, alishindwa kuongoza kikao.

Na kama Kikwete na Karume hawakuteta kabisa na kuwa na msimamo wa pamoja kabla ya vikao, basi Karume amempiku Kikwete. Lakini kwa CCM tunayoijua, mambo hayaendi hivyo. La Karume ndilo lilikuwa la Kikwete. Walichokubaliana ni mbinu ya kutumia kuwavuruga wajumbe na kuwachochea mashabiki wao. Hatima ya yote ni kwamba, walikubaliana kuendekeza uhafidhina.

Laiti Karume na Kikwete wasingekuwa pamoja katika hili, Kikwete ndiye angekuwa mshindi. Nachelea kusema kwamba adui wa Kikwete si Karume, ni yeye mwenyewe; na ‘huruma’ yake imemfanya Karume aibuke dume!

+447847922762
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
 
Jk kakumbwa na dharuba jamani, muhurumieni jamani,aliposhika tuu nchi, aaa!!! Umeme, OOOOO!!!! Kiangazi----- mara njaaa, uuuiii!! mara muafaka , duu !! sijui ashike wapi, Kikwete amepagawa, naomba tusilie naye sasa nguvu ya umma iamue
 
kaka kweli huyu jamaa ni msaa the way alivyoingia madarakani hizo sera zake yaani chai tupu in short hazitekelezeki ooh maisha bora kwa kila mtanzania,is it possible kupata maisha bora kwa kila mtanzania kweli sisi wabofongo ni wazembe tunaamini kila kitu sasa si afadhali angesema nitapunguza ugumu wa maisha tungemuelewa
 
“SASA imedhihirika kwamba jamaa huyu hawezi kushughulikia lolote; na hawezi kupambana na mikikimikiki. Anaweza tu kuzunguka huku na kule, akisukumwa na kuelekezwa kama kipofu.


Hiyo hapo juu ni makala ya Ngurumo aliyoiandika mwezi march mwaka huu watu hawakuamini hayo maneno yaliyo katika aya ya mwanzo kabisa wakadai kikwete apewe muda amepewa lakini juzi bungeni amedhihirisha hayo maneno kuwa hawezi kitu na hana jipya!
 
Jk kakumbwa na dharuba jamani, muhurumieni jamani,aliposhika tuu nchi, aaa!!! Umeme, OOOOO!!!! Kiangazi----- mara njaaa, uuuiii!! mara muafaka , duu !! sijui ashike wapi, Kikwete amepagawa, naomba tusilie naye sasa nguvu ya umma iamue
 
Back
Top Bottom