Ado Shaibu amshtaki Rais Magufuli Mahakama Kuu kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Salary Slip

JF-Expert Member
Apr 3, 2012
46,998
144,329
Mimi @AdoShaibu nimemwelekeza wakili wangu Fatma Karume ambaye ni wakili wa mahakama kuu, kufungua kesi mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kumshtaki Rais @MagufuliJP na Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya kupinga uteuzi wa AG usiofuata masharti ya Katiba.

Capture.PNG

-----
KWANINI NIMEMSHTAKI RAIS MAGUFULI MAHAKAMA KUU KUPINGA UTEUZI WA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI?

Na Ado Shaibu

Jana tarehe 12 Desemba 2018 nilimwelekeza Mwanasheria Fatma Karume ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Lugango Kilangi.

Kwenye kesi hiyo, nimemwelekeza Wakili wangu kuwa Mdaiwa awe Ndugu John Pombe Magufuli na Ndugu Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aunganishwe.

Kwa vile Wakili wangu amekwishaliingiza suala hili kwenye mchakato wa kimahakama, sitaingia kwenye kiini cha kesi na badala yake nitafafaua mambo mawili; msukumo uliosababisha kesi hii kufunguliwa na mbili, sababu za kumuunganisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Joseph Pombe Magufuli.

Nitayashughulikia masuala yote mawili kwa pamoja.

Kabla ya kuyashughulikia masuala hayo kwanza tutazame usuli wa suala lenyewe.

USULI (BACKGROUND) WA SUALA HILI

Tangu Dk. Kilangi ateuliwe na Rais kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwezi Februari 2018, kumekuwepo na madai kwamba hayatimiza masharti ya kikatiba ya kushika nafasi hiyo.

Binafsi, kwa kutambua unyeti wa nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sikuyachukulia madai hayo kuwa porojo linalostahili kupuuzwa au habari ya kawaida inayoweza kupita bila hatua yoyote kuchukuliwa. Niliamua kufanya utafiti wa kina kujiridhisha na madai hayo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempa Mwanasheria Mkuu wa Serikali madaraka makubwa. Yeye ndiye mshauri mkuu wa serikali kwenye masuala ya kisheria.

Hii ndio sababu katiba imeweka masharti maalum ya uteuzi wa mtu wa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ibara ya 59 (2) imeweka masharti kuwa mtu anayeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu ni lazima awe mtumishi wa umma mwenye sifa za kuwa wakili kwa miaka 15 mfululizo.

Utafiti wangu umebaini kuwa Dk. Kilangi amekuwa na sifa ya kuwa wakili kwa miaka saba tuu, chini ya hata nusu ya miaka iliyowekwa na katiba. Hana pia sifa ya kuwa mtumishi wa umma kwa miaka hiyo (
Rejea kiapo changu nilichoambatanisha kwenye andiko hili kujisomea zaidi)

MSUKUMO WA KESI

Binafsi, masuala matatu ndiyo yaliyonisukuma kwanza kupinga uteuzi wa Dk. Kilangi na pili kumjumuisha Rais Magufuli kwenye kesi hii.

1. Rais si Mfalme.

Zipo hisia potofu kwa baadhi ya watu kudhani kwamba Rais ni Mfalme. Watu wenye hisia hizi potofu hudhani kwamba Rais yupo juu ya sheria, hakosei na hapaswi kukosolewa.

Hisia hizi potofu zina mzizi wake wa kihistoria. Huko Ulaya enzi wa tawala za kifalme, iliaminika kwamba Mfalme ni mteule wa Mungu asiyeweza kufanya makosa. Hata Afrika ya kabla ya ukoloni, machifu walikuwa Alfa na Omega; mwanzo na mwisho.

Wakati wa ukoloni, Afrika ilikuwa chini ya udhibiti kijeshi, kisheria, kiuchumi na kisheria wa wakoloni walikuwa nchi za ng'ambo.

Mathalani, wakati wa ukoloni wa Uongereza, Tanganyika na Zanzibar yalikuwa makapu ya Malkia wa Uingereza kuchuma malighafi na rasilimali mbalimbali.

Mustakabali wa Afrika uliamuliwa ng'ambo. Kauli ya Malkia na serikali yake ilikuwa sawa na amri takatifu isiyoweza kupingwa.

Baada ya uhuru, Rais kwa katiba au utamaduni tuliourithi kutoka katika ukoloni, alikuwa na madaraka ya kifalme. Mwalimu Nyerere ameshawahi kusema katiba imempa madaraka yaliyopindukia.

Kwa yale madaraka ya kifame yanayotolewa na Katiba dawa yake ni kuendelea na mapambano ya kudai katiba mpya. Kwa yale ya utamaduni potofu, tunapaswa kuyaondoa kwa kuchukua hatua.

Kesi hii inalenga katika hilo la pili. Tunapaswa kuondosha utamaduni wa kufikiri kuwa Rais hawezi kugusika. Katiba ipo wazi kuwa Rais ni Mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa serikali.

Kwa maoni yangu, Katiba imempa kinga Rais dhidi ya masuala ya jinai na masuala ya madai ya kibinafsi. Kwa masuala mengine anayoyafanya kama Rais anaweza kuchukuliwa hatua. Kwa vile suala hili tunalifungua mahakamani, Mahakama yenyewe itaamua juu ya uhalali wake kisheria.

Iwapo suala lenyewe litafanikiwa, itamfanya Rais wa sasa na wa baadaye kuchukua kufanya teuzi na maamuzi mengine kwa umakini na kwa kuzingatia sheria kwa hofu ya masuala hayo kupingwa Mahakama.

2. Utii wa Katiba ni Wajibu wa Wote.

Ibara ya 26 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa wajibu kwa kila mtu kuheshimu katiba. Viongozi na wananchi sote tuna wajibu wa kuiheshimu na kuitii katiba.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeweka masharti kwenye uteuzi wa watu wa kushika baadhi ya ofisi nyeti. Kwa mfano, Rais hawezi kumteua mtu apendavyo kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali au Jaji bila kuzingatia masharti ya katiba.

Hivyobasi, Rais hakupaswa kumteua Ndugu Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akifahamu kuwa mtu huyo hana sifa zilizowekwa na Katiba.

Dk. Kilangi naye hakupaswa pia kukubali kuteuliwa kushika nafasi ambayo hana sifa nayo. Alichopaswa kufanya ni kumshukuru Rais, kumweleza kuwa hawezi kushika nafasi hiyo kwa vile hana sifa na kumuomba Rais kumteua mtu mwingine. Hili lingemjengea heshima.

Haiwezekani mtu anayepaswa kuishauri serikali kufanya maamuzi yake kwa kuzingatia katiba huku yeye mwenyewe ameteuliwa kwa kuvunja katiba. HAIWEZEKANI.

Wakati tunaendelea na michakato ya kimahakama, Dk. Kilangi anaweza kulinda heshima yake kwa KUJIUZULU. Kwa kukosa sifa hawezi kumshauri Rais na Serikali kwa kujiamini huku akijua yeye mwenyewe hana sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu.

3. Katiba ni Mali na Zao la Wananchi, Italindwa na Wananchi.

Kwenye petition yangu nimeeeka wazi kwamba mimi ni mwananchi na Kiongozi wa ACT Wazalendo. Kama mwananchi nina wajibu wa kuilinda na kuitetea katiba. Kama kiongozi wa chama cha siasa ninao wajibu wa kuitumia mahakama kama uwanja wa mapambano ya wanyonge na kupigania haki za binadamu na utawala wa sheria. Shauri hili linalenga kutekeleza wajibu wangu kama mwananchi na kama kiongozi wa chama.

Mahakama huamua kwa kupelekewa jambo. Nimechukua hatua hii kuitikia wito wa watetezi wa haki za binadamu kwa viongozi wa kisiasa kuitumia mahakama kupigania haki kwa kufanya mashtaka ya kimkakati (Strategic litigation).

Ado Shaibu,

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi,
ACT Wazalendo.

IMG-20181213-WA0072.jpeg
IMG-20181213-WA0078.jpeg
IMG-20181213-WA0077.jpeg
IMG-20181213-WA0074.jpeg
IMG-20181213-WA0075.jpeg
IMG-20181213-WA0079.jpeg
IMG-20181213-WA0077.jpeg
IMG-20181213-WA0080.jpeg
IMG-20181213-WA0081.jpeg
IMG-20181213-WA0073.jpeg

 
Hii nzuri regardless of outcome, kama kuna jambo lina ukakasi ni bora kuchukua hatua stahiki kuliko kuishia tu kupiga kelele twitter na JF, ili hata kama wenye dhamana wakiboronga ktk maamuzi yao historia itakuja kuwahukumu tu siku moja.
 
Back
Top Bottom