Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,086
- 13,929
Maazimio ya Halmashauri Kuu
Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imekutana kwenye kikao chake cha kawaida jana tarehe 23 Februari 2025 katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo katika Jengo la Maalim Seif (Makao Makuu ya Chama).
Kikao hicho kilipokea na kujadili Taarifa ya Uvurugaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, Hali ya Kisiasa Nchini na Mwelekeo wa Chama katika Kukabiliana na Mazingira mabovu ya Chaguzi nchini.
Baada ya mjadala wa kina, Halmashauri Kuu iliazimia kama ifuatavyo;
1. Kwamba kipaumbele cha Chama kwa sasa ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini utakaohakikisha HAKI na kuheshimiwa maamuzi na matakwa ya wananchi. Halmashauri Kuu imeelekeza kwamba suala la kushiriki ama kutoshiriki Uchaguzi kabla ya kufanyika marekebisho yanayotakiwa litaamuliwa na Kamati ya Uongozi ya Taifa katika wakati muafaka.
2. Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo imejiridhisha kuwa maridhiano yaliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamesambaratika na falsafa yake ya 4R imeota mbawa.
Ikumbukwe kwamba Chama cha ACT Wazalendo, vyama vingine vya upinzani na wadau wengine wa demokrasia nchini walimuunga mkono Rais Samia kutokana na ahadi yake ya kuboresha mazingira ya kisiasa nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba chaguzi zinakuwa huru, za haki na za kuaminika. Halmashauri Kuu imejiridhisha kuwa hakukuwa na utashi wa kisiasa kutekeleza ahadi hii.
Hivyo basi, Halmashauri Kuu inamtaka Rais Samia kujitathmini juu ya tofauti iliopo baina ya ahadi anazotoa kwa maneno na kukosekana kwa vitendo katika kutekeleza ahadi hizo. Mh. Rais ajiulize swali muhimu: Yanapojengwa mazingira ya ahadi za Rais kutoaminika, wananchi wamuamini nani?
4. Kwa upande wa Zanzibar, ACT Wazalendo kinayo ripoti ya kina juu ya mauaji ya raia 21 na matukio mengine ya ukatili wa kutisha yaliyofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. Pia, chama kimekusanya vitendo vyote vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu Zanzibar tangu mwaka 2020-2025.
Halmashauri Kuu imeelekeza Ripoti hizo zichapishwe na kupelekwa kwa wadau wa demokrasia nchini pamoja na jumuiya ya kimataifa ikiwemo taasisi za fedha za kimataifa na pia kushirikiana na taasisi hizo kufikisha kesi katika Mahakama za Kimataifa.
5. Halmashauri Kuu imeelekeza kuwa Chama cha ACT Wazalendo kiendeleze ushirikiano na vyama vingine makini vya upinzani na wadau wengine muhimu wa demokrasia ikiwemo Asasi za Kiraia na viongozi wa dini katika kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini.
6. Halmashauri Kuu imeelekeza Chama kiandae operesheni kubwa ya kulinda demokrasia nchini Tanzania itakayojulikana kama OPERESHENI LINDA DEMOKRASIA. Lengo la operesheni hiyo ni kuhamasisha umma wa Watanzania kupigania haki zao na kutokubali kuwa wanyonge.
7. Halmashauri Kuu imeelekeza Chama kijikite katika kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini ikiwemo kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba (minimum constitutional reforms), kuundwa kwa Tume Huru za Uchaguzi (NEC na ZEC kwa upande wa Zanzibar) na kupinga kwa nguvu zote kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar.
HITIMISHO:
Wanachama na viongozi kwenye ngazi zote wanaelekezwa kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya kuilinda na kuitetea demokrasia nchini Tanzania ili kura ya kila mwananchi iweze kuwa na thamani. Muda wa kubembeleza mageuzi umekwisha sasa ni muda wa mapambano!
Ado Shaibu,
Katibu Mkuu.
Feb 24, 2025