The Watchman
JF-Expert Member
- Nov 7, 2023
- 1,137
- 1,928
TAARIFA KWA UMMA
Tunalani Uvamizi dhidi ya Wamachinga na Kubomolewa Vibanda vyao eneo la Mbagala Rangitatu
ACT Wazalendo tunasikitishwa na kulaani vikali tukio la kubomolewa kwa vibanda na kuporwa bidhaa za wafanyabiashara wadogo eneo la Mbagala Rangitatu, Temeke Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana, Novemba 2, 2024. Kitendo hiki kimewaacha zaidi ya wafanyabiashara 200 na hasara kubwa na kuwaweka kwenye hatari ya kutumbukia katika hali ya umaskini.
Ni jambo la kusikitisha kwamba tukio hili limefanyika kwa maagizo ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke bila kuwashirikisha Wafanyabiashara hao wala kutoa notisi ya kutosha. Hii ni kinyume na haki za binadamu, utu wa wafanyabiashara wadogo na misingi ya utawala bora.
Tukio hili dhidi ya wamachinga wa Mbagala ni mwendelezo wa madhila wanayokutana nayo wamachinga nchini ikiwemo kubomolewa, kuvamiwa na kuporwa mali zao na Halmashauri kuvamiwa (kuondolewa kwa nguvu) usiku wa manane ili kuwaacha wakididimia kwenye ufukara.
Wafanyabiashara wadogo ni uti wa mgongo wa uchumi wa mijini katika nchi yetu. Wanapasa kuheshimiwa na kusaidiwa badala ya kufanyiwa vitendo vya ukatili vinavyowadidimiza kiuchumi na kijamii.
ACT Wazalendo tunapinga kwa nguvu zote vitendo vya uvamizi na bomoa bomoa vya mara kwa mara vinavyofanywa na Serikali dhidi ya Wamachinga. Tunaitaka Serikali kuchukua hatua zifuatazo mara moja:
i. Tunaitaka Serikali iwalipe fidia wafanyabiashara wote walioathiriwa na unyama huu wa kuharibiwa biashara na kupoteza mitaji yao.
ii. Tunaitaka Serikali kuhakikisha wanapatiwa wafanyabishara hawa maeneo yao ya biashara ili waendelee kufanya kazi zao.
iii. Tunaitaka wizara za Uwekezaji pamoja na Viwanda na Biashara kushughulikia masuala yanayohusu ustawi wa wafanyabiashara wadogo kwani nao wanahitaji mazingira mazuri ya kufanya biashara zao hapa nchini.
iv. Serikali iwachukulie hatua za kisheria na kinidhamu wale wote waliohusika katika tukio hili ili kuhakikisha haki inatendeka na matukio kama haya hayajirudii
ACT Wazalendo tutaendelea kuwa upande wa wananchi, kupaza sauti dhidi ya dhuluma na kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa kila Mtanzania. Tunawasihi wafanyabiashara waendelee kusimama imara kudai haki zao.
Imetolewa na;
Ndg. Mwanaisha Zuberi Mndeme Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara
ACT Wazalendo.
03 Desemba, 2024