ACT Wazalendo: CCM malaghai, Bunge liagize ukaguzi maalumu juu ya matumizi ya Shilingi Trilioni 1.5 za Watanzania

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Hoja 5 za Ufafanuzi wa ACT Wazalendo Kuzima Upotoshaji wa CCM Juu ya Trilioni 1.5 Zisizojulikana Ziliko.

Bunge Liagize Ukaguzi Maalum Juu ya Matumizi ya Shilingi Trilioni 1.5 za Watanzania

Imetolewa na Ndg. Ado Shaibu, Katibu Uenezi ACT Wazalendo

Ndugu Wanahabari

Juzi jumapili, Aprili 15, 2018, sisi ACT Wazalendo tulifanya uchambuzi wa awali wa ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka 2016/17. Tunafurahi kuwa uchambuzi wetu juu ya masuala 8 ya hatari kwenye taarifa ya CAG umepokelewa vyema, na umekuwa ni mjadala wa kitaifa.

Katika masuala hayo 8 ya hatari tuliyoyaibua, suala la shilingi 1.5 trilioni kutokujulikana zimetumikaje ndilo ambalo limegusa hisia za watanzania. Kwa ujumla sehemu kubwa ya ufafanuzi wetu utajikita kwenye hoja hii, kwa sababu ndiyo hoja iliyogusa zaidi hisia za watu, hivyo hata upotoshaji na uzushi umefanyika zaidi kwenye hoja hii.

Aprili 15, ACT Wazalendo tulisema yafuatayo kuhusu jambo hili,

“6% ya Fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilizokwenda. Katika ukaguzi wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kuwa kati ya Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi 25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.

Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4.2 trilioni, sawa na 15% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Jambo la kushtusha na linalohitaji majibu ya Serikali ni kwamba, CAG amegundua kuwa katika fedha zote zilizokusanywa, shilingi 25.3 trilioni, ni shilingi 23.8 trilioni tu ndio zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za serikali na riba, shilingi 1.5 trilioni zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi.

Fedha hii ambayo matumizi yake hayajulikani ni sawa na 6% ya Fedha zote zilizokusanywa mwaka huo. Matrilioni haya ambayo Serikali imeyapoteza ni zaidi ya mara mbili ya Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka husika (672 bilioni)”.

Jana, Katibu Mwenezi wa CCM alizungumza nanyi wanahabari, ambapo ukiacha matusi, kejeli, vitisho na kashfa, sehemu kubwa ya mkutano wake ulijikita kwenye hoja hii. Maelezo yake ni kuwa shilingi 25.3 trilioni ni mapato ghafi ya Serikali, yakiwa na fedha za Zanzibar shilingi 203.92 bilioni, pamoja na Hela Tarajiwa (Receivables) shilingi 687.3 bilioni.

Na hivyo basi, mapato halisi ya Serikali yalikuwa ni shilingi 24.4 trilioni. Zaidi akifafanua kuwa CAG alikuta matumizi ya shilingi 23.79 kwa sababu Serikali haikuwa imepokea fedha zake za hati fungani iliyoiva, kiasi cha shilingi 697.85 bilioni.

Mahesabu haya yaliyotolewa na msemaji wa CCM ndio msimamo rasmi wa chama hicho, na hivyo ndio msimamo rasmi wa Serikali ya chama hicho. Na hivyo basi ni dhahiri kuwa chama hicho kinaikataa taarifa ya CAG, kimeamua kufanya upotoshaji mkubwa, na kuwahadaa watanzania juu ya ziliko shilingi 1.5 trilioni zao.

Hoja 6 za Ufafanuzi juu ya Upotoshaji wa CCM:

1. Chama Kidogo kama ACT Wazalendo Kinaweza Kufanya Uchambuzi wa Ripoti ya CAG?

Mwenezi wa CCM ameeleza kuwa ACT Wazalendo ni chama kidogo, chenye mbunge mmoja, hivyo hakina uwezo wa kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG. Hoja hii ni dhaifu, ni dhihaka ya kututoa kwenye mstari, maana pia haelezi kuwa ili chama cha siasa kichambue ripoti ya CAG kinapaswa kiwe na ukubwa kiasi gani na kiwe na wabunge wangapi, na hasemi kwamba masharti hayo anayoyaweka ni kwa mujibu wa sheria gani ya nchi?

Uchambuzi wa ripoti za CAG ni suala la kitaalam zaidi, hauna mahusiano kabisa na udogo au ukubwa wa chama cha siasa, au hata idadi ya wabunge wake. Ili Mtu, au kikundi cha watu (Chama cha Siasa) afanye/kifanye uchambuzi wa ripoti ya CAG, yanahitajika mambo matatu muhimu, mosi ni Weledi (Proffesionalism), pili ni Ujuzi (Skills), na tatu ni Uzoefu (Experience). Hivyo uchambuzi wa ripoti hii si zao la ukubwa wa chama wala idadi ya wabunge.

ACT Wazalendo tumekuwa chama pekee nchini, chenye utamaduni wa kuchambua Bajeti Kuu ya Taifa pamoja na kutoa mapendekezo ya maboresho yake, tumefanya uchambuzi wa bajeti kuu zote mbili za Serikali ya awamu ya 5. kiasi cha Serikali (kwa khofu) tu mwaka jana kuvamia na kupiga marufuku mkutano wetu wa uchambuzi wa Bajeti. Hivyo ni dhahiri kuwa tunao uwezo wa kuchambua ripoti hii ya CAG, kiasi cha kukhofiwa na Serikali, na sasa kukhofiwa na chama kinachoongoza Serikali (kikiomba Polisi waje kutukamata).

Kiongozi wa Chama chetu, ndugu Zitto, ambaye aliongoza timu iliyofanya uchambuzi wetu juu ya ripoti ya CAG, ni Mchumi Mweledi kitaaluma, ana Ujuzi wa kutosha juu ya masuala ya Uchumi na Ukaguzi kutoka kwenye vyuo mbalimbali nchini na vya nje ya nchi, na ana uzoefu wa miaka 8 wa kuchambua taarifa za CAG kwa kuwa ameongoza Kamati za Bunge za usimamizi wa hesabu za Serikali za POAC na PAC kwa miaka hiyo 8. Sifa zote hizo zinatupa hadhi na heshima stahili sisi ACT Wazalendo, pamoja na kuwa chama kidogo tu chenye mbunge mmoja, kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG.

2. Ukaguzi wa CAG ulihusu fedha ZILIZOKUSANYWA. Si Mapato Ghafi wala Fedha Tarajiwa (Receivables).

Katika Kitabu cha Hesabu za Serikali Kuu, CAG ameonyesha kuwa amekagua fedha za Makusanyo ZILIZOKUSANYWA na Serikali, na sio Fedha zilizotarajiwa kukusanywa na Serikali, au Mapato GHAFI kama alivyodai mwenezi wa CCM. CAG ameonyesha kuwa kwa mwaka 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya shilingi 29.5 trilioni kutoka kwenye vyanzo vya mapato yote; ya kodi, yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani, pamoja na mikopo ya nje na misaada ya wahisani (Ukurasa na 29 - Jedwali Na. 12: Mchanganuo wa Bajeti ya Makusanyo).

CAG ameonyesha kuwa Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni, na kushindwa kukusanya shilingi 4.2 trilioni, sawa na 14.33% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. (Uk. wa 30 na 31: Muhtasari wa Ukusanyaji wa Mapato ya Fedha Zilizotolewa). Fedha hizi zilizokusanywa (shilingi 25.3 trilioni), CAG aliziona, kwa kuwa ziliingia kwenye Hesabu Jumuifu za Taifa (Consolidated Accounts).

CAG ameonyesha kuwa Serikali iliweza kukusanya shilingi 25.3 trilioni kutoka vyanzo na mchanganuo ufuatao; vyanzo vya kodi (14.27 trilioni) vyanzo visivyo vya kodi (2.072 trilioni), mikopo ya ndani (5.916 trilioni) na mikopo nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo (3.047 trilioni). Hayo yapo Ukurasa wa 32 (Kielelezo Na. 6: Mwenendo wa Mapato ya Serikali kwa miaka minne).

Kwa ushahidi huo, utaona kuwa hakuna Fedha Ghafi kama ilivyo propaganda ya mwenezi wa CCM, bali CAG alikagua fedha ambazo Serikali imeshazikusanya. Na Serikali yenyewe imetoa ushahidi wa nyaraka juu ya namna ilivyozikusanya fedha hizo, na CAG ameziona katika hesabu jumuifu. Hivyo basi, katika shilingi 25.3 trilioni zilizokusanywa hakuna fedha tarajiwa (receivables), na pia hakuna fedha ghafi.

3. Hakuna Fedha za Serikali ya Zanzibar, Zingekuwepo Zingeripotiwa.

Mwaka wa fedha wa 2016/17 ulianza Julai 1, 2016 na kuisha Juni 30, 2017. CAG hutoa muda wa miezi mitatu kwa taasisi zinazokaguliwa, ili ziweze kurekebisha vitabu vyake vya hesabu na kuviandaa vyema kabla hajaanza kuvikagua. Serikali Kuu iliwasilisha hesabu zake kwa CAG mwishoni mwa Septemba, 2017, miezi mitatu tangu mwaka wa fedha wa 2016/17 uishe, ikionyesha namna ilivyokusanya fedha, kiasi cha fedha zilichokusanywa, kiasi cha fedha zilichotumika, na namna fedha hizo zilivyotumika.

CAG alifanya ukaguzi wake kuanzia mwezi Oktoba, 2017, na alifanya kikao na taasisi alizozikagua (exit meeting), ili kufafanua hoja zilizoibuliwa kwenye ukaguzi husika, Januari, 2018. Katika nyakati zote hizo, Serikali Kuu, kwa barua na kwa nyaraka, haikuonyesha kuwa kuna fedha zozote za Zanzibar ambazo imezikusanya na hivyo hazipaswi kuwemo katika makusanyo ya shilingi 25.3 trilioni.

Kama kuna fedha za Zanzibar, Serikali ilikuwa na miezi mitatu ya kuzionyesha (Julai - Septemba, 2017), na pia ilipata wasaa wa kukutana na CAG kwenye kikao cha kujadili hoja alizoziibua (Exit Meeting), mwezi Januari, 2018. Nyakati zote hizo, Serikali imeonyesha namna imezikusanya shilingi 25.3 trilioni, kwa uwazi, na hakuna mahali imesema kuwa kuna fedha za Zanzibar. Mwenezi wa CCM anapingana na Serikali yake?

4. Hati Fungani za Serikali zimekaguliwa na CAG

CAG ameeleza yafuatayo katika ripoti yake; “Kati ya shilingi 23.5 trilioni zilizokusanywa, shilingi 23.79 trilioni ndizo zilizotolewa kwaajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja na riba”. (Uk. wa 34: Uchanganuzi wa Makadirio ya Mapato ya Kugharamia Matumizi).

Kwa mujibu wa CAG, Serikali imeonyesha nyaraka za hati fungani zote ilizouza (katika eneo la mikopo ya ndani, ambapo Serikali ilikopa bilioni 500 zaidi ya fedha ilizoomba kukopa na kuidhinishiwa na Bunge), shilingi 5.9 trilioni (ikiwa imeomba ruhusa ya kukopa shilingi 5.4 trilioni), na pia Serikali ameonyesha kiasi cha madeni ya amana na riba ambacho imelipia kwenye hati fungani hizo (Uk. 34 Ripoti ya CAG juu ya Serikali Kuu).

Labda tu mwenezi wa CCM haelewi ‘Hati Fungani’ ni nini. Ndio maana anaropoka tu kuwa Serikali inasubiri hati fungani zake ziive ili iweze kulipwa shilingi 697.85 bilioni zake. Kwanza Serikali ndio huuza hati fungani, watu, makampuni, mabenki, taasisi na asasi ndio hununua hati fungani, na zinapoiva hizo hati fungani, Serikali ndio hulipa amana na riba za iliowauzia hati fungani. Sasa mwenezi wa CCM hajui hata jambo hili rahisi kuhusu masuala ya kibenki?

Serikali hupata sehemu kubwa ya mikopo ya ndani kwa utaratibu wa kuuza hati fungani, na hulipia hati fungani hizo (zilizoiva) kwa utaratibu wa kulipa amana na riba. CAG ameonyesha namna mikopo ya ndani ilivypatikana kupitia hati fungani, na pia amefafanua namna madeni ya riba na amana za hati fungani zilizoiva yalivyolipwa.

5. CCM na Serikali yake Hawaaminiki

Kutokana na ufafanuzi huo tulioutoa, mtaona kuwa CCM, kama ilivyo kwa CAG, nao wanakiri kuwa Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni, na ikatumia shilingi 23.8 trilioni, na kuonyesha kuwa, kama ilivyo kwa CAG, nao wanakiri pia kuwa shilingi 1.5 trilioni hazionekani ziliko. Wao wamekwenda mbele zaidi tu kwa kuamua kufanya propaganda zenye lengo la kuuhadaa umma kwa kutengeneza sababu na matumizi hewa juu ya fedha hizo (Fedha za Zanzibar, Receivables na Hati Fungani). Wao na Serikali yao wametuhadaa mno, hawapaswi kuaminiwa tena na Watanzania.

Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya CAG uliibua masuala 48, tuliamua kwanza kuyaainisha yale masuala 8 ya hatari tuliyoyasema Aprili 15, 2018 kwa sababu ya unyeti wake dhidi ya haya masuala mengine 40 yaliyobakia. Masuala hayo 48 yatokanayo na ripoti hii ya CAG ni taswira juu ya udhaifu wa Serikali ya awamu ya 5 katika kuongoza nchi yetu.

CAG ametuonyesha mapungufu makubwa mno ya Serikali, ameonyesha hadaa za hali ya juu za Serikali, kufikia kiasi cha cha kupika takwimu na kutangaza mapato feki ya kodi yanayokusanywa na TRA ili ipate sifa tu kuwa inakusanya mapato zaidi, wakati ni kinyume na ukweli. Zaidi ripoti ya CAG imetuonyesha namna maamuzi ya kukurupuka ya Serikali yanavyolitia hasara Taifa.

Nitatoa mfano mmoja kwenye eneo hili, kwa mwaka mmoja tu wa Serikali ya awamu ya 5, hasara linayoipata Shirika la Umeme nchini, TANESCO imepanda kwa zaidi ya mara 2, ukuaji wa hasara kwa mwaka mmoja tu ni zaidi ya 175%, kutoka hasara ya shilingi 124.46 bilioni, chini ya Serikali ya awamu ya 4, mpaka hasara ya shilingi 346.40 bilioni za Serikali hii ya awamu ya 5.

Mapendekezo ya ACT Wazalendo ni yapi?


-Tumemwandikia Barua Spika wa Bunge, Kuomba Uchunguzi Maalum wa Jambo hili

Sasa ni dhahiri kuwa fedha za watanzania, shilingi 1.5 trilioni, hazijulikani ziliko, CAG ameonyesha jambo hilo kupitia ripoti yake, CCM, chama kinachoongoza Serikali, nacho kimeonyesha hilo kupitia taarifa yake, zaidi kimeonyesha hakina uwezo tena wa kuisimamia Serikali yake, kimeamua kushiriki hadaa ili fedha zenu Watanzania zipotee, hivyo basi vyama vya Upinzani tunao wajibu wa kuhakikisha watanzania wanajua fedha zao zimekwenda wapi.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama chetu, ndugu Yeremia Kulwa Maganja, amemuandikia barua Spika wa Bunge, ndugu Job Ndugai, kumuomba atoe kibali kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC, ili ikutane, na imuagize CAG afanye ukaguzi maalum juu ya zilikopelekwa fedha hizi. Ni matarajio yetu kuwa Spika atazingatia ombi letu kwake, kwa sababu ya unyeti wake kwa nchi yetu.

Tunatoa wito kwa watanzania wote, watokanao na vyama vyote vya siasa, tuungane pamoja kupaza sauti juu ya jambo hili. Fedha hizi, shilingi 1.5 trilioni ni nyingi mno, zingeweza kutumika kukopesha shilingi 100 milioni kwa kila kijiji katika vijiji 15,000 nchi nzima, na kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na kinamama, zingeweza kujenga hospitali 10 zenye hadhi kama ya Mlingazila, na kutatua changamoto za sekta ya afya nchini, zingeweza pia kuwasomesha bure chuo kikuu, vijana wote wa Kitanzania wanaomba mikopo kwa sasa, kwa muda wa miaka minne mfululizo. Ni fedha nyingi mno, tuungane kuhakikisha tunajua ziliko.

Ahsanteni Sana

Ado Shaibu
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo
Aprili 19, 2018
Dar es Salaam
 
Ingekuwa inahusu Hamissa Mobeto kuliwa denda Na Domo ungepambana kupata bundle Hata Kwa Mkopo ufungue uone
Au Shilole Kiuno achezesha Msambwanda wake live usingeikosa
Na asilimia kubwa ya watz ndio hivyo wao mambo ya kipuuzi watayashikia bango, wakati wenzao hao wanatengeneza pesa, ila kwenye vitu vya muhimu, wala, ndio maana huwa ni wepesi kuhamishwa kutoka kwenye reli
 
Nashangaa hii ripoti ya 1.5 kufafanuliwa na wanasiasa badala ya wataalamu wa uchumi
Wrong. Kufumuliwa na mwanasiasa ambayo pia ni mtaalamu wa kila field: Aviation expert, financial expert, Renowned economist, ecological and environmental expert, Criminal and Civil lawyer. Simply, The genius.
 
Wrong. Kufumuliwa na mwanasiasa ambayo pia ni mtaalamu wa kila field: Aviation expert, financial expert, Renowned economist, ecological and environmental expert, Criminal and Civil lawyer. Simply, The genius.
Hapa unamzungumzia Polepole au Zitto?
 
Back
Top Bottom