Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,004
- 13,773
TUNAITAKA SERIKALI YA JMT, KUWACHA MARA MOJA UTOWAJI WA LESENI KWA ENEO LA FUNGU MBARAKA NA BAHARI KUU UPANDE WA ZANZIBAR
Tokea mwaka (2009) ambapo Baraza la Wawakilishi na Serekali ya awamu ya sita ya Dr. Abedi Amani Karume na aliekua Waziri wa sekta hiyo ndugu Mansour Yussuf Himid, kuweka msingi wa wazi na kishujaa wa kulinganganua suala la mafuta na gesi asilia kutoka makucha ya Tanganyika. Awamu zote zilizofuata hazijachukua hatua madhubuti na zilizo wazi kuona sekta hii inaelekea kutoa mchango uliotarajiwa katika uchumi wa Zanzibar, badala yake zipo taarifa zenye kuaminika zakuturejesha tulikotoka.
Jambo ambalo Serekali ya Zanzibar haipaswi kuona aibu kuficha wala kulifumbia macho juu ya khatma ya utafutaji wa mafuta na gesi katika eneo la Fungu Mbaraka na Bahari Kuu upande wa Zanzibar. Fungu Mbaraka au Fungu Kizimkazi au Kisiwa cha Latham, Kisiwa ambacho masafa kutoka rasi ya Kizimkazi hadi katika Kisiwa hicho ni mail 36 (Kilomita 57.9). Kisiwa hicho kina urefu wa mita 320 na upana wa mita 164.5 kwa vipimo vya mwaka 1898. Kisiwa hicho kilitangazwa rasmi kuwa mali ya Zanzibar saa 12 asubuhi ya tarehe 10 october 1898.
ACT Wazalendo tunazo taarifa zenye kuaminika kwamba Serekali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, ipo katika maandalizi ya kutangaza utowaji mpya wa leseni kwa vitalu vipya kwa awamu ya tano (5th licencing round) katika eneo la ziwa Tanganyika na bahari ya hindi ikiwemo eneo la Fungu Mbaraka na eneo la bahari kuu upande wa Zanzibar, uzinduzi ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 05/3/2025 huku mgeni rasmi akitegemewa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, kufanya hivo ni kuingilia mipaka ya Zanzibar jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Ukimya huu kwa Serekali zote mbilli ile ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na hii ya Zanzibar pamoja na Taasisi zao zote zinazohusika na masuala ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta unatia mashaka na kuibua maswali mengi kwa wananchi.
Hivyo basi ACT Wazalendo tunaitaka Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyo chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, kufanya yafuatayo:
1. Kuweka wazi mipaka ya kitaalam (Geological coordinates) baina ya vitalu vya Zanzibar vilivotangazwa (Block 1_A, 1_B, 1_C, 1_D, 1_E, 1_F, na 1_G) na vile vya Tanganyika vinavotegemewa kutangazwa March 2025 (Block 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12).
2. Kueleza umma juu ya mkanganyiko wa ramani za marejeo (Reference map) za Tanganyika za mwaka 2024 kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ambayo zimeiweka eneo lote la Zanzibar katika mpango kazi wao wa baadae.
3. Kueleza umma ni upi mpango wa Serekali ya Zanzibar kwa utafataji na uchimbaji wa mafuta na gesi katika eneo la Fungu Mbaraka.
4. Kuuleza umma kwa kina namna Zanzibar itakavofaidika na utoaji wa leseni kwa eneo la bahari kuu ambalo ni eneo la Zanzibar.
5. Serekali ya Zanzibar itoke hadharani na kueleza umma kwa tamko rasmi la serekali kwamba eneo la Fungu Mmbaraka ni eneo la Zanzibar na haipaswi kwa mamlaka nyengine yoyote kufanya shuhuli yoyote bila ya ridhaa ya Serekali ya Zanzibar.
6. Tunaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwacha mara moja mpango wake wa utowaji wa leseni kwa eneo la la Fungu Mbaraka eneo ambalo ni mali ya Zanzibar na kuindoa mara moja eneo lote la Zanzibar katika mpango wao wa baadae wa uchimbaji wa mafuta na gesi ili kuondoa migogoro inayoweza kutokea.
Chama cha ACT Wazalendo, Tunamtaka Raisi Samia Suluhu Hassan asikukubali kutumika kuiziba mdomo Zanzibar kwa kushiriki katika ufunguaji huu wa leseni mpya za vitalu vya mafuta na gesi kwa Tanganyika bila yakutatua mkanganyiko uliopo sasa. Hata hivyo Chama chetu, hakitasita na kuendelea kua sauti ya Wazanzibari kwa kusimamia Serekali juu ya masuala yote yanayohusu rasilimali za Zanzibar kwa maslahi ya wanachi wa Zanzibar.
Imetolewa leo, tarehe 03/01/2025 na,
Ndg. Said Ali Mbarouk
Msemaji wa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar
0779955778