Abiy Ahmed akiri kwa mara ya kwanza uwezekano wa uhalifu dhidi ya binadamu katika mapigano ya Tigray

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Waziri Mkuu wa Ethiopia amekiri uwezekano wa kuwepo kwa matendo ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mapigano katika eneo la Tigray mwezi Novemba mwaka jana.

Abiy Ahmed amekiri pia kwa mara ya kwanza, baada ya mamlaka kukanusha mara zote, kuwa vikosi vya Eritrea vimeingia nchini humo na kusababisha maafa kwa wakazi wa eneo la Tigray. Abiy amekiri hayo alipokuwa akijibu maswali ya wabunge jijini Addis Ababa.

"Ripoti zinaonesha kuwa kuna uhalifu umefanyika katika eneo la Tigray. Tunafahamu uharibifu uliotokana na mapigano hayo. Vita ni jambo baya," alisema Abiy kwa lugha ya Kiamhara.

Abiy amesema wanajeshi watakaobainika kufanya uhalifu dhidi ya binadamu watachukuliwa hatua kali. Hata hivyo, amesema kuwa kuna propaganda za kutia chumvi kuhusu maafa ya mapigano hayo zinazofanywa na kundi la Tigray la TPLF ambalo linalaumiwa na Abiy kwa kushambulia vikosi vya jeshi la Ethiopia.

Ethiopia imesema inafanya uchunguzi wa matendo ya uhalifu yaliyofanyika wakati wa mapigano hayo, lakini Jamii ya Kimataifa ikiwamo Umoja wa Mataifa inasisitiza kuwa uchunguzi ndani ya Ethiopia unaoongozwa na serikali ya Ethiopia hauwezi kuwa wazi na wa haki, ikitaka kuruhusiwa kwa mashirika ya haki ya kimataifa kufanya uchunguzi.

Ripoti zinaonesha kuwa zaidi ya watu 50,000 wameuawa katika mapigano yaliyoanza mwezi Novemba mwaka jana. Eneo hilo ni makazi kwa zaidi ya watu milioni 6 kati ya zaidi ya wakazi milioni 110 wa Ethiopia.

Chanzo: CBS
 
Back
Top Bottom