Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Abiria 80 wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), waliokuwa wakielekea visiwani Comoro wamekwama kwa takriban wiki moja baada ya ndege kuharibika.
Abiria hao waliwaeleza wanahabari jana kuwa wamekwama tangu Alhamisi iliyopita na kwamba wamechoka kukaa mbali na familia zao hivyo kuiomba Serikali ifanye jitihada za kuwarudisha kwao. Mmoja wa abiria hao, Adinani Benkharifa alisema Sh50,000 walizopata kama fedha za kujikimu kwa siku haitoshi kwa kuwa maisha ya Dar es Salaam ni tofauti na kwao.
"Maisha ya huku ni magumu sana, fedha ninayopewa kwa ajili ya matumizi haitoshelezi mahitaji yangu, nataka kurudi Comoro na si kupewa fedha ili niendelee kuwepo," alisema.
Alisema kuendelea kukaa Dar es Salaam ni tatizo kwao kutokana na kuishi bila kuzalisha chochote. Zainoudine Moilimou alisema anashangazwa na kitendo cha shirika hilo kushindwa kuwarudishia nauli ili watafute utaratibu mwingine wa kurudi kwao.
"Tuliambiwa tutaondoka jana, lakini tulishangaa kuitwa ofisini badala ya uwanja wa ndege kumbe safari siyo leo."
Abiria mwingine, Mariam Nassor alisema yeye na mwanaye walimaliza bajeti yao wiki iliyopita na hawawezi kuishi kwa kula chipsi mayai kwa kuwa si chakula walichozoea.
Akijibu Madai ya wasafiri hao, Kaimu Ofisa Uhusiano wa ATCL, Lily Fungamtama alisema ndege pekee ya shirika hilo aina ya Dash 8-Q 300 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 50 ilipata tatizo la kiufundi Alhamisi iliyopita na taratibu za matengenezo zinaendelea.
Alisema ndege hiyo ambayo kwa kawaida hufanya safari tano kwa wiki katika Visiwa vya Comoro, inaweza kuruka lakini kiusalama shirika liliona ifanyiwe marekebisho kabla ya kuendelea na safari.
"Kipuri cha tatizo lake kiliagizwa mapema ila hakikuja kwa wakati na kimefika jana na kuanza kufungwa tunatarajia kukamilika kesho (leo). Endapo matengenezo hayatakamilika, tumefanya mawasiliano na kampuni ya AB Aviation iwasafirishe," alisema.
Akizungumzia kiwango cha fedha wanachopewa abiria hao, Fungamtama alisema kinatolewa kwa mtu mmojamoja hivyo wanaamini kinawasaidia abiria hao wakati hatua nyingine zikiendelea.
Chanzo: Mwananchi