Abdul Nondo ajibu upotoshaji wa Kafulila dhidi ya hoja za Zitto Kabwe

Abdul Nondo

JF-Expert Member
Oct 28, 2016
515
2,874
Kwanza nimpongeze David Kafulila kwa kuona umuhimu wa kujaribu kujibu hoja za Mh.Zitto juu ya uchambuzi wa ripoti za CAG. Ingawa hajafikia lengo la matarajio yake kwani amechagua maeneo ambayo kwake ni mepesi na kukwepa hoja kubwa na za msingi kama ile ya serikali kuzuia Makampuni makubwa ya ukaguzi kutoka nje kukagua Benki kuu (BOT). Mbali na kwamba alichagua maeneo aliyoyaona anayaumudu ila bado amedanganya na kupotosha waziwazi.

Mimi binafsi simshangai juu ya huu upotoshaji wake.Kwani kuna msemo unasema,

"People of integrity don't hide their reactions or opinions ,they don't manipulate others through deception and they don't pretend".

Kutokuwa na uwadilifu Kafulila ameficha rangi yake na kuongea unafiki, anapotosha na kudanganya umma, anajifanya kujua pasi kujua kitu. Majibu ya Kafuli dhidi ya hoja za Mh. Zitto ni mepesi mno na maneno matupu kuliko hoja, majibu ya Kafulila yanaweza kujibiwa na mtu yeyote mwenye akili ya kawaida tuu.

Nimejitolea kujibu maelelezo kadhaa ya Kafulila kwani najua hawezi kujibiwa na Mh. Zitto. Mh.Zitto atamjibu Mh. Rais Magufuli ndio hadhi yake. Kafulila ni hadhi yetu sisi vijana.

#Mh. Kafulila alijaribu kujibu hoja ya Mh. Zitto juu ya makusanyo ya mapato.

Mh. Zitto alionesha serikali imeshindwa kukusanya mapato ukilinganisha na malengo yake iliyojiwekea, hivyo imeshindwa kufikia lengo lake la makusanyo kwa mwaka husika, hivyo alijaribu kulinganisha na serikali ya awamu ya nne namna ilivyoweza kufikia malengo yake ya makusanyo ya mapato. Huu mlinganisho ni pamoja na Tax collections variance ya awamu zote hizi mbili, natumia lugha ya kawaida ili kueleweka.

Kufikia au kutofikia lengo la makusanyo ya mapato haijalishi malengo yako ya makusanyo ni madogo au makubwa ila inategemea na namna ulivyopanga malengo ya makusanyo uliyojiwekea. Unaweza panga kukusanya Milion 10 ila ukakusanya milion 12 hapa umevuka lengo(Realistic). Ila kama umepanga kukusanya Milion 16 ukakusanya milion 13 hapo hujafikia lengo(Over-estimation/unrealistic).

Hii ndio ilikuwa hoja ya Mh. Zitto kwa serikali ya awamu ya tano kwamba haifikii malengo katika makusanyo yake halisi (Actual collections) ukilinganisha na makadirio yake (estimates), hapa ulinganisho ni kati ya makadirio (estimates) na uhalisia (actuality) na sio ukubwa au udogo wa kiasi kilichokusanywa kwani hii ni hoja nyingine tofauti.

Ndio maana Mh. Zitto alisema 2016/2017 serikali ilipanga kukusanya trilioni 29.5 (estimates), ila makusanyo halisi ilikusanya 25.3 trilioni hivyo haikufikia lengo kwa asilimia 14.33% na mwaka 2018/2019 ilipanga kukusanya trilioni 32.5, Ila uhalisia ilikusanya trilioni 25.8 haikufikia lengo kwa asilimia 21%.

Ila Serikali ya awamu ya nne iliweza kufikia lengo la makadirio ya makusanyo (estimated collections) kwa asilimia kubwa bila kujali makusanyo yake yalikuwa madogo kiasi gani ukilinganisha na kipindi cha JPM. Ukubwa na udogo wa makusanyo ni hoja nyingine, awamu ya nne waliyopanga kukusanya ni kwa asilimia ndogo sana hawakufikia lengo; 2013/2014 hawakufikia lengo kwa 9%,2014/2015 hawakufikia kwa 4% na ,2015/2016 hawakufikia kwa 6% .

Ila awamu ya tano asilimia za kutofikia lengo ni kubwa bila kujali ukubwa wa makusanyo yake ambayo ni hoja nyingine kabisa ,mfanol; 2018/2019 haijafikia malengo yake kwa asilimia 21%.

Hoja hii Kafulila aliijibu kitoto sana kwa kurahisisha akahama kutoka katika suala la kufikia lengo la makusanyo, akahamia kwa jambo lingine kabisa kwa kuzungumzia ukubwa wa makusanyo ya mapato kwa kulinganisha na awamu ya nne na ya tano.

Akafanya kujumlisha (+) mapato ya 2012/2013 trilion 8 + trilion 9.28 ya 2013/2014 + trilion 10.77 ya 2014/2015 =akapata trilioni 28, akaja na hoja ya kwamba ni sawa na makusanyo ya trilioni 27.7 ya 2017/2018 kipindi cha awamu ya tano. Hesabu za kitoto kweli.

Kafulila hakujali kabisa wala kuwaza juu ya determinants za utofauti wa makusanyo Kati ya miaka na miaka (Determinants for revenue collections variance).

Hakujali factor ya Idadi ya watu (Population) na wala hakujali factor ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu kati ya miaka hiyo aliyolinganisha makusanyo.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2012 Tanzania ilikuwa na watu milion 44.9 hivyo makusanyo yake ya mapato huwezi linganisha na makusanyo ya 2018 ambapo idadi ya watu kwa mujibu wa WorldOmeter (UN Data) ilikuwa milion 56. Ongezeko la watu milion 11.Sawa na idadi ya watu wote wa nchi ya Rwanda.

Hakujali juu ya kushuka kwa thamani ya fedha yetu yeye alikurupuka tuu akajumlisha ,Simple!!! , wakati mwaka 2012 USD 1 ilikuwa sawa na Tsh.1583 ukilinganisha na 2018 na kuendelea ambapo USD 1 imekuwa ni zaidi Tsh. 2300 sawa kama na ongezeko la zaidi ya Tsh.800. Hivyo ni wazi Trilion 1 ya 2012,2013,2014 sio trilion 1 ya 2020.

Mfano, mwaka 2004 February 14, Rais Mkapa akitoa hatuba bungeni Dodoma alitoa hongera kwa TRA kwa kuvuka lengo la makusanyo ya Bilion 788.3 kwa miezi saba ikiwa lengo lao ilikuwa Bilion 757 kwa miezi saba hivyo kulikuwa na ongezeko la Bil.30.9 .Kwa akili za Kafulila anaweza kupinga mafanikio haya ya kuvuka malengo, kwa hoja kwamba sasa hivi mbona TRA chini ya Magufuli inakusanya Trilion 1 kwa mwezi ambayo ni sawa na makusanyo ya Bilion 788.3 kwa miezi saba wakati wa Mkapa.

Hizi ni akili za kujumlisha na kutoa kutoka kwa Kafulila, bila kuwaza kwamba 2004 Mkapa alikuwa na idadi ya watu milion 37 tuu, leo hii tuna milion 59 sawa na ongezeko la watu milion 22 kwa mujibu wa WorldOmeter 2020 (UN Data). Na makusanyo ya mapato huakisiwa sana na idadi ya watu.

Hoja ya Mh. Zitto ya makusanyo ya mapato aliizungumza sawa na hoja ya utekelezaji wa bajeti za serikali ya awamu ya tano na awamu ya nne. Awamu ya nne asilimia kubwa sana ya bajeti zilikuwa zinatekelezeka, mwaka 2014/2015 ilitekelezeka kwa 84.9% na 2015/2016 ilitekelezeka kwa 91.5%

Ikiwa kipindi cha Rais Magufuli awamu ya tano, Bajeti zinatekelezwa kwa asilimia ndogo, yaani (Budget Implementation Gap is higher) 2016/2017 ilitekelezeka kwa 66.5%, 2017/2018 kwa 64.5% ,2018/2019 kwa 68.6% ,2019/2020 kwa 56% hii yote ni kwasababu ya serikali kufanya makadirio makubwa (over estimation) pasi na misuli ya utekelezaji. Wataalamu wanasema Over-estimated budget ni bajeti ambayo haina vigezo vya kuwa bajeti bora. Hoja hii ukimpa Kafulila aijibu ataanza kujumlisha na kutoa.

#Hoja nyingine ya Kafulila anatetea kwamba Serikali kuwa na kesi nje ni matokeo ya mikataba mibovu.

Kafulila asiwe muongo, ukweli ni kwamba Tanzania kuwa na kesi nyingi nje ni matokeo ya ubabe wa serikali ya awamu ya tano kuvunja mikataba hovyo hovyo bila kufuata taratibu, Jambo ambalo linaendelea kuingiza Taifa hasara na madeni hivyo ndege zetu kuwindwa mara zote. Kafulila ameishia kutaja tuu kampuni moja Symbion kwa hoja ya Capacity charges, anasahau kwamba tarehe 10 Novemba 2018 Kabudi akijibu swali la Mh.Zitto Bungeni juu ya idadi ya kesi tulizofunguliwa katika mahakama za kimataifa alijibu kwamba "Tangu Novemba 2015 tuna kesi 13 zilizofunguliwa mahakama tofauti tofauti za kimataifa dhidi ya Tanzania ,ikiwemo PCA,LCIA,ICSID na UNICTRAL " .Pia 2019 April 16 tulifunguliwa kesi nyingine na Ayoub Farid Saab wa FBME kesi zote hizi ni za kuvunja mikataba kinyume na sheria ambapo jumla ya madai katika kesi hizi zote ni dola za kimarekani milion 185.58 sawa na Tsh Bilion 400.

Kafulila haumii juu ya hasara zote hizi ambazo tutaingia ,Kasomeni hukumu ya 16/October 2019 iliyotolewa na ICSID ikiitaka serikali ya Tanzania iilipe Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) USD milion 185 serikali kupitia msemaji Abbas ilipotosha kwamba hatulipi sisi ila IPTL ikiwa hukumu ilitaja serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kulipa, soma award ya Kampuni ya Japan Kanoike Construction company iliyotolewa mwaka 2016 na International chamber of Commerce in London ambapo 2017 Kanoike walipeleka award mahakamani ili iwe enforced dhidi ya serikali ya Tanzania kuilipa Kanoike Bilion 130 Tzsh.

Kafulila sasa hivi ni kipofu na kiziwi hasikii wala haoni athari juu ya kesi hizi. Mambo haya yanafanya tuingie hasara kwa ndege zetu kukamatwa na kutishiwa kukamatwa sababu tu ya maamuzi ya mtu mmoja ambaye hafuati sheria. Nani anajua suala Hermanus Phillipus Steyn yule mzungu aliyekamata ndege yetu limeishiaje? Je serikali ilishinda kesi au ilimlipa ? nani anajua usalama wa ndege na mali zetu huko nje kesho? haya yote Taifa linaingia hasara kwa maamuzi ya mtu mmoja tuu.

#Hoja ya Kafulila nyingine Mapinduzi katika Sekta ya afya na elimu akigusia mikopo elimu ya juu.

Sekta ya afya bado ina changamoto chungu nzima ila Kafulila sasa ni kipofu hawezi ona, uhaba wa vifaa tiba, uhaba wa wafanyakazi bado ni changamoto kubwa haya sio maneno yangu ni maneno kutoka katika Ripoti za CAG kila mwaka Pia hata Ripoti hii ya 2018/2019 Uk.wa 162 inaonesha katika hospital 18 za rufaa Kuna uhaba wa wafanyakazi 5047 ,vifaa tiba upungufu 312. Changamoto hizi zipo katika vituo vingi vya afya nchini .

Mikopo elimu ya juu, Kafulila asipende kujibu jibu ataendelea kujidharaulisha, katika utoaji wa mikopo elimu ya juu serikali ya awamu ya 5 imekuwa ikiwadidimiza wanafunzi kuanzia upatikanaji wa mikopo hiyo hadi marejesho yake.

Kafulila anasema serikali imeongeza kiwango hadi kufikia Bil.360 cha utolewaji mikopo ,Ila nataka kumwambia awamu ya nne 2013/2014 , Serikali ilitenga Bil.306 zikitolewa kwa ufanisi kuliko awamu ya tano.

Ufanisi wake, 2014 kurudi nyuma serikali ilikuwa inatoa fedha kwa wanafunzi kwa kufuata categori hii , Chakula na malazi 8500 kwa siku, siku 60 sawa na 510000,hela mafunzo kwa vitendo elf 10 kwa siku ,siku 56 za mafunzo 560000 ,fedha ya viandikwa laki mbili kwa mwaka. Baada ya serikali ya Magufuli kuingia madarakani 2016/2017 serikali ikapunguza fedha ya vitabu na viandikwa sio laki mbili sasa kila mwanafunzi kwa mwaka bali wengine wanapewa elf 50, wengine elf 80, wengine laki, wengine hawapati kabisa. Bado serikali ya Magufuli inakata wanafunzi fedha ya mafunzo kwa vitendo badala ya kupewa 560000 kwa siku 56 ya mafunzo,sasa hivi kila mwanafunzi anapewa namna yake, wengine laki moja kwa siku 56, wengine elf 80, wengine laki 2, kwa siku 56 za mafunzo na wengine hawapati kabisa kutokana utaratibu mpya wa MT(Means Testing) ambao huko mwanzo ulikuwa kwenye categori ya Tuition Feess tuu (Ada).

Utolewaji wa mikopo mwaka 2017/2018 wanafunzi wa mwaka wa kwanza walioomba mkopo walikuwa 61,000 Ila Serikali ilipanga kutoa kwa wanafunzi 30,000 tuu hivyo nusu 31,000 kukosa. Hii huwezi kusifu kwamba Serikali ya Magufuli imeongeza utolewaji wa mikopo wakati 2014/2015 awamu ya nne walioomba mkopo mwaka wa kwanza ni 57,860 ila waliopewa ni 30,654 kwahiyo waliokosa ni 27,206 ila wakati wa Magufuli 2017/2018 waliokosa ni 30,000.

Katika marejesho, serikali ya Magufuli ilifanya marekebisho ya sheria ya Bodi ya mikopo mwaka 2016 na kuongeza asilimia ya makato ya deni la mkopo wa bodi katika mshahara ghafi kufikia 15% kutoka 8% 2015,2014,2013 kushuka chini.

Makato haya yaliwahi kupingwa vikali na CAG Mussa Assad katika Ripoti yake ya 2016/2017 kwani alisema wafanyakazi 4,830 wa halmshauri 58 wanapata mishahara chini ya theluthi moja baada ya makato. Pia katika sheria hiyo ya bodi kuna makato ya 6% tozo ya kulinda thaman ya fedha (rention fee) kila mwaka, pia makato ya adhabu ya 10% ukichelewa kulipa deni miezi 24 baada ya kuhitimu chuo. Hii Kafulila haoni amevaa miwani ya mbao, wala hasikii ameweka nta masikioni. Wafanyakazi na wahitimu wanalia yeye anaimba mapambio ya kusifu.

#Hoja nyingine ya Kafulila ni kutaka wananchi waendelee kuiamini CCM .

Kwa kuonesha miradi mikubwa inayojengwa nchini.Miradi mikubwa kama hiyo aliyoitaja Kafulila ujenzi wa reli (SGR) na Stiglers gorge ilipaswa kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini na kuakisi ongezeko la ajira nchini na sio ukosefu wa ajira wala kusinyaisha uchumi.

Mfano,tarehe 18 Disemba 2018 serikali kupitia Sekretariat ya ajira kuanzia mwaka 2015 hadi kufikia 2018 walitoa nafasi ya ajira kwa watu 6554 ila walioomba ni 594,300 hivyo waliokosa ni 587,746 .(chanzo Katibu wa Sekretariat ya ajira ndugu Xaviar Daudi).

Pia ukisoma Ripoti ya African Development Bank ya 2019 (Tanzania economic Outlook) inasema ukosefu wa ajira kwa vijana umezidi kuongezeka kutoka 5.7% 2012 hadi 7.3% 2016 na hadi sasa hali bado ni mbaya. Serikali inajisifu kuwa na miradi mikubwa isiyozalisha ajira. Hivyo wananchi hawapaswi kuiamini tena serikali ya CCM sababu imeahidi katika ilani yake 2015/2020 kutoa ajira kwa vijana katika vipengele karibu zaidi ya 14 , kipengele cha 8,9,10,22f,25d,27,29g,44g,51,56(b),57(d) Ila haijatekeleza chochote hadi leo 2020.

Kafulila anawezaje kushawishi vijana na watanzania waendelee kuiamini serikali ya CCM ? ,Kafulila anapotosha kwa kusema Tanzania inaelekea kwa kasi kama uchumi wa Vietnam. Sielewi huyu Kaka yangu anawaza nini. Ukisoma taarifa iliyotolewa na worldatlas mwaka 2017 "The Economy of Vietnam" utaona trend ya ukuaji wa uchumi wa nchi ya Vietnam ilianzia katika kilimo ambapo idadi ya watu milion 54.61 wa Vietnam karibu asilimia 44% ya idadi ya watu hao walianza kujikita katika kilimo baadaye ndio transition ya kuingia katika manufacturing (viwandani). Ni muulize Kafulila mzee wa kujumlisha na kutoa hali ya kilimo nchini kwetu ipoje?

Kwa mujibu wa ADB (African Development bank 2019)"Tanzania economic Outlook" inasema ajira katika kilimo imeporomoka kutoka 71.4% 2008 hadi 66.3% 2018 .

Alafu mnatuambia mipango ya miaka mitano awamu ya pili, 2016/2017-2020/2021 ni kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu kwa viwanda vipi na mikakati ipi ?

Mnatuambia kufikia 2025/2026 tuwe nchi ya uchumi wa kati (Middle income country) kwa mikakati gani ya kuwa na export economy?

Hoja zingine kama za Rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma,madeni,maisha magumu siwezi jisumbua kumjibu sababu hali inaonekana wazi labda sababu yeye sasa hivi haoni wala kusikia hawezi jua wala kuona uhalisia.Zitto alitoa hoja kupitia ripoti za CAG kuanzia 2015-2019 ila Kafulila hajagusa Ripoti hata moja ya CAG amegusa ripoti zake za World Economic Forum, Executive opinions Survey ,bila kugusa Ripoti hata moja ya Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali CAG,huu ni udhaifu mkubwa sana na hali ya kutafuta kichaka cha kujifichia.

Kafulila atulie asijivishe ngozi ya kuwa mtetezi mpotoshaji. Maana hata Saga ya trilion 1.5 Kafulila alijitokeza kujibu akidhani Zitto angemjibu, Mh. Zitto hawezi kumjibu Kafulila sio hadhi yake hadhi ya Mh.Zitto ni Mh. Rais Magufuli.


Abdul Nondo.

Mwenyekiti Ngome ya Vijana Act wazalendo.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hii nondo ya Abdu Nondo imeshiba mno

Kwa hesabu za kujumlisha na kutoa za Kafulila anaweza kudai kuwa Makusanyo ya Miaka mitano ya serikali ya Mzee Mwinyi yanazidiwa na Makusanyo ya mwaka mmoja tu wa Magufuli bila kuzingatia idadi ya watu, mchango wa tekinohama katika makusanyo, miundo mbinu uliyowekewa na waliokutangulia na kuchukua pesa za halmashauri kama vile mabango, majengo, huduma mbalimbali na kuziingiza kwenye fuko la TRA kama alivuofanya Magufuli badala ya kuziacha huko kwenye halmashauri husika
 
Kuhusu CAG kuondoa utegemezi wa ukaguzi wa taasisi za ndani kwa makampuni ya nje namuunga mkono CAG, hakuna sababu ya kutumia wakaguzi wa kujitegemea kwenye kila idara yetu ya serikali.

Ofisi ya CAG inapaswa iwezeshwe wataalam wa idara zote ili iweze kufanya ukaguzi yenyewe kwa sehemu kubwa. Sio kila ukisoma report ya ukaguzi utaona kpmg, ey, deloitte, pwc hasa kwenye mashirika na taasisi za umma, cag yeye ni halmashauri tu.

Tumuunge mkono cag kupata man power tupunguze utegemezi wa ukaguzi wa taasisi binafsi.
 
Kuhusu CAG kuondoa utegemezi wa ukaguzi wa taasisi za ndani kwa makampuni ya nje namuunga mkono CAG, hakuna sababu ya kutumia wakaguzi wa kujitegemea kwenye kila idara yetu ya serikali.

Ofisi ya CAG inapaswa iwezeshwe wataalam wa idara zote ili iweze kufanya ukaguzi yenyewe kwa sehemu kubwa. Sio kila ukisoma report ya ukaguzi utaona kpmg, ey, deloitte, pwc hasa kwenye mashirika na taasisi za umma, cag yeye ni halmashauri tu.

Tumuunge mkono cag kupata man power tupunguze utegemezi wa ukaguzi wa taasisi binafsi.
Heri tutumie gharama hata binafsi wa nje wasionunulika tupate usahihi wa Kodi zetu,Kama twaweza nunua ndege cash nn kuwalipa wakaguzi binafsi wakashirikiana na wa nje tuondoe Querres.Kama tumeamua kupambana na ufisadi linapokuja suala la gharama ili kulinda Kodi zetu si kitu
 
Njaa kiboko ya matatizo. Utafanywa choccho
Nondo stop jumping whenever Zitto is mentioned, inakufanya ionekane kama kibaraka au mlinzi asiye na busara. Kafulila amejibu hoja vizuri sana, japokuwa haimaanishi he is absolutely right and he is neither totally wrong

Sent using Jamii Forums mobile app
Njaa ni kiboko ya matatizo. Utafanywa lolote kwa sababu ya njaa
te kwa sababu ya njaa. Njaa haina sheria, kanuni wala taratibu. Njaa haina dini
 
Kafulila kwa ujumla hakujibu chochote kuhusiana na hoja za Zito zilizokuwa zimeegemea ripoti ya CAG. Kafulila alitumia muda mwingi kunukuu taarifa za forums badala ya report ya kina ya CAG.

Nilimwona mtu ambaye very uprofessional alipokataa kutumia asilimia, anataka kutumia absolute figures. Nikaona sasa JF imeingiliwa na watu wenye upeo mdogo. Katika vipimo vya uchumi, ni lazima utumie asilimia na siyo figures. Asilimia hubeba maana ile ile wakati wote lakini namba kama sh 10m, uhalisia wake unabadilika kila siku.

Majibu yale ya Kafulila, ilikuwa ni kujiaibisha. Kuna wakati ukikaa kimya watu hawawezi kujua huelewi nini. Utakapotamka, ndipo watu watajua unapungukiwa nini katika uelewa wako.
 
Back
Top Bottom