Abbas Sykes (1929 - ) Sehemu ya tatu: King's college budo shule moja na kabaka edward mutesa wa Uganda 1940s

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,912
30,253
Siku moja katika mazungumzo na Balozi Sykes akaniambia kuwa yeye baba yake alimtoa Kitchwelle Boys Government School na kumpeleka Kampala Uganda kwa ajili ya kupata elimu.

Balozi anasema yeye hakuwa anajua ni shule gani baba yake alikuwa anataka kumpeleka lakini walipokuwa Nairobi wakiwa pale hotelini wakisubiri safari ya kwenda Kampala baba yake akakutana na jamaa wa Kinubi na katika maongezi baba yake akawaeleza kuwa alikuwa katika safari anaelekea Uganda kumpeleka kijana wake shule.

Basi mmoja wao katika wale jamaa wa Kinubi akamwambia Kleist kuwa shule nzuri sana ni King's College Budo kama ana uwezo na itakuwa vyema kama anatampeleka mtoto wake shule hiyo.

Hapo King's |College Budo ndipo Abbas Sykes ailipokuja kusoma na Freddie Mutesa ambae baadae akajakuwa Kabaka wa Buganda na Rais wa Uganda mwaka 1962 Uganda ilipopata uhuru.

Balozi Sykes anakumbuka kumuona mama yake Freddie Mutesa akiwa kavaa yale magauni ya Kiganda akija shule kumtembelea mwanae na jinsi shule nzima ilivyokuwa ikitetemeka kwa ujio wa bi. mkubwa yule kwani Freddie ndiye aliyekuwa akitegemewa kuwa Kabaka wa Uganda.

Wote Abbas Sykes na Freddie Mutesa katika utawala wa kikoloni wakahusika kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi zao.

Inasikitisha kuwa kutoka miaka ile ya 1940 wazalendo hawa hawakupata tena kuonana wakati nchi zao washazikombboa kutoka kwa Muingereza na labda kwa kuwa Kabaka Mutesa alipunduliwa mwaka wa 1966 na kwenda kuishi uhamishoni Uingereza ambako alifariki mwaka wa 1969.

Miaka hiyo Abbas Sykes tayari alikuwa kwenye ubalozi wa Tanzania Ufaransa na Canada.

Hii shule King's College Budo ina sifa ya pekee katika shule za Afrika ya Mashariki kwani viongozi wengi na watu mashuhuri wamesoma hapo kutoka Uganda kwenyewe, Kenya hadi Nyasaland na wenyewe wanajiita Budoians.

Hii ni ''club,'' pekee ya wasomi kama Yusuf Lule, Godfrey Binaisa na Charles Njonjo kwa kutaja majina maarufu katika siasa za Afrika ya Mashariki.

Balozi Sykes anamkumbuka baba yake kwa mapenzi makubwa sana.

Balozi mara nyingi akinambia kuwa, ''Sisi baba yetu alitujengea msingi mzuri sana wa maisha na alipofariki aliacha jina kubwa la ukoo wetu. Hakuna mahali ambako baba yetu hakuacha alama yake kuanzia kwenye siasa, biashara na katika dini ya Kiislam hasa katika kuwasomesha watoto wa Kiislam wake kwa waume. Yeye na wenzake akina Ali Jumbe Kiro walijenga ile shule ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika. Mungu akajaalia kuwa Bwana Abdul baada ya kifo cha baba yetu mwaka wa 1949 yeye akavaa viatu vya baba na vikamuenea vizuri sana ndani ya TAA hadi kuasisi TANU mwaka wa 1954. Hapa ikawa tumekuwapo katika African Association mwaka wa 1929 na tukawepo katika kuunda TANU mwaka wa 1954. Balozi akipenda sana kunitania kwa kuniita, ''Yaa Mohamed, unaiona Sykes dynasty?''

Nakumbuka siku nilipomtembelea baada ya Kleist Abdul Sykes kuchaguliwa kuwa Mayor wa Dar es Salaam.

''Unajua Mohamed somo yake alikuwa Mwafrika wa pili kuchaguliwa katika board ya Dar es Salaam Municipal Council kwa hiyo Kleist kafuata nyayo za babu yake,'' Balozi aliniambia kwa furaha.

Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa katika board hiyo alikuwa Juma Mwindadi.

Balozi Abbas Sykes alipata siku moja kunihadithia kisa cha picha aliyopiga na masheikh wakubwa wa Afrika ya Mashariki nyumbani kwake Shaaban Robert.

Picha hii ipo kwenye Maktaba yake,

Nyumba hii ya Shaaban Robert ilikuwa ndiyo makazi ya Regional Commissioner wa Coast Region ambae yeye ndiye alikuwa kateuliwa na Nyerere na kumfanya kuwa Mwafrika wa kwanza kushika nafasi hiyo kwa Dar es Salaam.

Anasema siku hiyo ilikuwa mchana na yeye alikuwa yuko nyumbani hana hili wala lile.

Mara anashtukia mlango unagongwa na Zuberi Mtemvu kasimama anamwambia kuwa amekuja na ugeni mkubwa wa masheikh wanataka kumuombea dua.

Abbas anasema haraka akakimbilia chumbani kwake akavaa kanzu, koti na kofia kutoka nje kuwalaki masheikh wale na kuwakaribisha ndani.

Balozi Sykes anasema ilipigwa dua nzito hapo ya kumuombea mafanikio katika kazi na maisha yake.

Mwaka ule wa 1962 anasema ndiyo kwanza alikuwa kachaguliwa na Julius Nyerere kuwa Regional Commissioner wa kwanza Mwafrika wa Jimbo la Mashariki.

Abbas Sykes na Mtemvu walikuwa watu waliokuwa wakielewana sana toka utoto wao na nyumba zao zilikuwa jirani licha ya Mtemvu kujiondoa TANU 1958 kufungua chama chake African National Congress (ANC) kufuatia uamuzi wa TANU kuingia katika uchaguzi wa Kura Tatu ambao Waingereza waliweka masharti magumu ya kibaguzi.

Abbas Sykes akiishi Mtaa wa Kipata (Sasa Mtaa wa Kleist Sykes) na Zuberi Mremvu Mtaa wa Somali (Sasa Mtaa wa Omari Londo).

Sijapata kuchoka kumsikiliza Abbas Sykes.

Alipostaafu utumishi aliongeza chumba katika nyumba yake ya kifahari iliyoko Sea View ikiangalia bahari ya Hindi.

Hapa Balozi aliweka Maktaba yake na katika vitabu vilivyokuwapo pale ni kitabu cha marehemu kaka yake.

Upande huu wa bahari ndipo ilipo Majlis yetu tukikaa muda mwingi tukizungumza na kwa kweli yeye ndiye alikuwa mzungumzaji mimi ni masikio tu.

Siku moja nilimuuliza kuhusu yeye kuandika kumbukumbu zake.

''Nimeshaanza.''

Hili ndilo lilikuwa jibu lake kwangu.
Itaendelea...

1567999148364.png

Kabaka Edward Mutesa

1567999248417.png

Picha: Kabaka Edward Mutesa, Balozi Abbas Sykes akiwa katika Maktaba yake, Abbas Sykes akiwa amesimama katika ya Sheikh Ahmad bin Husayn Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (kulia) na kushoto kwake Sheikh Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt picha ya mwisho ni masheikh maarufu wa nyakati zile:

Habib Umar bin Sumayt na Habib Ahmad bin Hussayn Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim walipomtembelea Balozi Abbas Sykes, nyumbani kwake, Mtaa wa Shaaban Robert 1962.

Baadhi ya majina ya waliomo katika picha hii ni kama ifuatavyo:

1. Shareef Abdulkader al-Juinaydi (DSM),
2.al-'Allamah al-'Arif Billah Habib Ahmad bin Husayn Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (znz); 3. Balozi Abbas Syks (DSM);
4. al-Allamah al-'Arif Billah Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt (znz);
5. al-'Allamah al-Fadhil Shaykh Hassan bi 'Amier (znz) Mufti wa Tanganyika;
6. al-'Allamah Habib Hamid Mansab Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (znz);
7; al-'Allamah Sayyid Ali Badawi (Lamu-znz);
8. al-'Allamah Maallim Sa'id bin Ahmad (Mombasa);
9. al-Akh Muhammad 'Alwi Bu Numay (znz);
10. al-Akh Abdulwahhab (DSM) presidant of Arab Association Tanganyika;
11. Shaykh al-Fadhil Abdulkader Ba'Abbad (DSM).
12. Shaykh Qasim bin Jum'a Darwesh (DSM).

Nyuma al-Allamah al-'Arif Billah Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt ni Ali Mwinyi Tambwe katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na mstari wa mbele waliochuchumaa wa tatu ni Zuberi Mtemvu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom