70% ya Wagonjwa wa Kitengo cha Fiziotherapi Hospitali ya MZRH Mbeya wana tatizo la uti wa mgongo

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,458
Asilimia 70 ya wagonjwa wanaopata matibabu katika kitengo cha Fiziotherapi Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya, wanasumbuliwa na matatizo ya uti wa mgongo huku chanzo kikubwa kikitajwa ni kukaa kwa muda kwenye viti ambavyo havina teknolojia ya kuepukana na tatizo hilo.

Vilevile, imebainishwa kuwa asilimia kubwa ya watu wanaosumbuliwa na tatizo hilo ni wafanyakazi wa benki, wafanyabiashara wanaouza madukani, watumishi katika taasisi mbalimbali na madereva ambao hukaa muda mrefu kwenye viti ambavyo havina teknolojia ya kukabiliana na tatizo hilo.

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Fiziotherapi juzi, Mkuu wa Idara ya Fiziotherapi Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH), Namnyaki Abrahamu, alibainisha kuwa kwa sasa watu wengi wanaofika hospitalini huko wanasumbuliwa na uti wa mgongo.

Alisema maadhimisho ya Siku ya Fiziotherapi yanatoa nafasi kwa wataalamu wa afya kutoa elimu kwa wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kuzingatia mazoezi na mlo sahihi ili kuzuia baadhi ya magonjwa ambayo yanaathiri mifumo ya utendaji kazi ambayo yanasababisha maumivu, athari za mjongeo na hata ulemavu.

Aliongeza kuwa taaluma ya Fiziotherapi inahusisha utendaji kazi wa mwili pamoja na mjongeo wa mwili ikiwa na lengo la kuongeza uwezo wa utendaji kazi wa viungo na mwili kwa ujumla.

Mtaalamu huyo alisema taaluma hiyo hutumia zana mbalimbali kama vile umeme, hali joto, mazoezi, elimu ya njia bora ya kuishi pamoja na uwezo wa mfiziotherapia katika matibabu kwa njia ya vitendo.

“Ni muhimu mtu mwenye magonjwa yasiyoambukizwa kumwona mfiziotherapia mapema kwa sababu moja ya kazi yetu ni kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa, kuzuia au kupunguza usugu wa dawa, huduma yetu ambayo inaambatana na mazoezi ya viungo, umeme na hali joto, huduma zetu huleta ubora wa maisha na kurejesha mjongeo ndani ya mwili wake,” alisema.

Abraham alisema wanatoa huduma ya Fiziotherapi kwa watu wenye ulemavu, wenye matatizo ya uti wa mgongo na watoto wenye mguu kifundo, lakini wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kutolea huduma kama vile mashine za kunyooshea viungo.

Pia alisema hawana eneo la kutosha kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa kuwa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kila siku ni takriban 100.

Alitoa rai kwa wananchi kwamba katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa, mfiziotherapia ndiye mtaalamu pekee aliyebobea kwenye mjongeo, shughuli za kimwili, utaalamu na ubingwa wa mazoezi tiba, pia yuko mstari wa mbele kumsaidia mgonjwa hadi anapona.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Godlove Mbwanji, aliwataka mafundi seremala kubuni teknolojia ambayo itamwezesha mtu anayeketi kwenye kiti muda mrefu kutopata madhara ya uti wa mgongo.

Alisema mafundi hao wanapaswa kuwahusisha wataalamu wa Fiziotherapi nchini ili kuwapatia ushauri wa namna gani wanaweza kutengeneza samani zitazosaidia kukabiliana na uti wa mgongo.

“Kuna watu wanauza madukani huku wameketi sehemu moja muda mrefu, kuna watumishi kama mimi ambao pia tunashinda kwenye viti, watumishi wa benki, madereva wa malori na mabasi, hawa watu wako hatarini kupata tatizo la uti wa mgongo, maana viti tunavyovitumia havina utaalamu wowote unaotusaidia kuepukana na tatizo hilo,” alionya Dk. Mbwanji.

Alex Mwalyepelo, mmoja wa wagonjwa wanaopata matibabu ya Fiziotherapia katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya, alisema huduma aliyoipata imesaidia kuleta utengamano wa mwili.

Alikumbusha kuwa mwaka 2010 alipata ajali ya gari na kusababisha majeraha kwenye viungo mbalimbali vya mwili wake, akishindwa kutembea lakini baada ya kupata matibabu katika kitengo hicho, afya yake imeimarika.

Chanzo: IPP
 
Back
Top Bottom