30 waomba kumrithi Mrema Tanroads........................

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,172
30 waomba kumrithi Mrema Tanroads

Imeandikwa na Frank Leonard, Iringa; Tarehe: 8th December 2010 @ 06:11

WIKI moja baada ya serikali kusitisha ajira ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Ephraim Mrema, nafasi yake hiyo imewatamanisha zaidi ya watu 30 na itajazwa ndani ya miezi miwili ijayo.

Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuunda Baraza la Mawaziri na kuwateua Dk. John Magufuli na Dk. Harrison Mwakyembe kuongoza Wizara ya Ujenzi, ajira ya Mrema aliyekuwa akidaiwa kukingiwa kifua na baadhi ya watendaji wa serikali katika nafasi hiyo, aling’olewa Tanroads.

Lakini sasa, Naibu Waziri Dk. Mwakyembe ameweka wazi kuwa baada ya ajira ya Mrema kusitishwa katika muda usiozidi juma moja, nafasi hiyo imewavutia watu zaidi ya 30.

“Tumeambiwa walioomba nafasi hiyo wako zaidi ya 30, tumejipanga vizuri, mchujo utabakisha watatu kati yao na hatimaye atapatikana mmoja kutoka miongoni mwao,” alisema Dk. Mwakyembe jana alipozungumza na watumishi wa wizara yake mkoani hapa, baada ya kupokea taarifa ya jumla ya Tanroads Mkoa.

Wakati mchakato wa kumpata mtendaji mkuu mpya, Dk. Mwakyembe alisema nafasi hiyo inashikiliwa kwa muda na aliyekuwa Mkurugenzi wa Barabara za Vijijini, Patrick Mfugale, na aliwataka mameneja wa mikoa kuongeza ufanisi kwa kuchapa kazi zao kwa nguvu.

Akiahidi kuyashughulikia matatizo mengine katika wizara hiyo, Dk. Mwakyembe alisema vitu vyote vitakavyobainika kukwamisha utendaji, vitafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

“Tunajua tunayo matatizo, na matatizo yaliyopo hayahitaji fedha za kigeni kuyatatua, tutayashughulikia yote kwa nguvu zetu wenyewe,” alisisitiza na kuongeza kuwa katika miaka mitatu ijayo, wizara yake imejiwekea ahadi ya kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta hiyo.

Alisema, mambo yanayoonekana ya kawaida katika wizara hiyo yatashughulikiwa kwa kasi kubwa na alitoa mfano wa umuhimu wa kuwepo kwa sheria itakayowataka watu au wamiliki wa magari yanayoharibu barabara au alama zake kutokana na ajali au wizi, kulipa fidia.

“Lazima wahusika wa uharibifu wa barabara zetu na alama zake watafutwe na kulipa fidia kwa mujibu wa sheria badala ya mzigo wa gharama za ukarabati wake kuachwa kwa Tanroads,” alisema.

Awali, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Iringa, Paulo Lyakurwa alisema matukio yanayohusisha wizi wa alama za barabarani yanazidi kuongezeka mkoani humo na kulitia hasara taifa na makandarasi wanaopewa kazi.

Lyakurwa alisema baadhi ya alama za barabara zilizotengenezwa kwa chuma zimekuwa zikinyofolewa na kuuzwa kama vyuma chakavu na watu wasioona madhara ya kufanya hivyo.

Aliwakumbusha viongozi katika ngazi zote kushirikiana na mamlaka zingine ikiwemo Polisi kuwafichua watu wanaojishusisha na vitendo hivyo.
 
Back
Top Bottom